KIJASUSI

Ep 01: Naitwa Geza

Naitwa Geza Sehemu ya Kwanza
Naitwa Geza Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Chombezo: Naitwa Geza

Sehemu ya Kwanza (1)
_________________

Ikitokea kwa bahati mbaya katika masaa ya giza ukajikuta haujarejea nyumbani kwako, usikubali kutembea peke yako! uwe mlinzi wa mwenzako naye awe mlinzi wako.
Tamko hili la mkuu wa polisi ngazi ya wilaya lililotangazwa kila kona kwa kutumia magari na pikipiki, baada ya kuwepo na tishio la mauaji kwa raia pasi na kuibiwa mali zozote. Muuaji hasemi kwanini anatenda yale na bado anaendelea kuua tena na tena.
Awali tangazo hili lilizingatiwa kwa ukubwa sana. Walitembea wanne wanne hadi sitasita, licha ya wingi huo bado walikuwa wenye hofu katika siku za awali.
Mbona hakuna kinachotokea? Swali hili liliulizwa kwa sauti, kisha likajibiwa kwa vitendo. Waliouliza swali hili walikuwa na akili timamu, lakini waliochagua kulijibu ni wanakijiji ambao pombe ilikuwa imezagaa katika vichwa vyao.

Kwanza tangazo lile juu ya usalama wao, kwao kilikuwa ni kifungo kamili katika maisha yao ya kukutana kilabuni na kufurahia maisha yao bora kabisa wanayoyatazama baada ya kilevi kusafiri kutoka tumboni na kuweka makazi katika ubongo.
Kama ni mnywaji, tafadhali beba chupa zako ukaifanyie starehe hiyo nyumbani! Tangazo lile lilinadi huku likiongeza maneno kadha wa kadha ya kusababisha waliokuwa wanasikiliza wapige mbinja na vigelegele. Kasoro wale walevi wa pombe za kienyeji ambao waliona dhahiri kuwa wametengwa katika angalizo lile. Pombe zao zilinyweka kwa kupimiwa katika vikombe vya ujazo mbalimbali na harufu ya pombe zao ni kali kiasi kwamba kuibeba na kuitumia mbele ya familia ni sawa na kuhamishia simanzi nyumbani na vingi viulizo. Zaidi ya hayo kuna wale waliokuwa wakitumia pombe hizi kali za kienyeji kwa kificho kikubwa, wanakunywa pombe za kienyeji na kisha wanasindikizia na pombe za kimapokeo chupa kadhaa ili kuficha ile harufu kali kinywani.
Hawa wakajikuta pasi na kikao rasmi wakiamua kukiuka lile tangazo ambalo ni agizo kutoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, tangazo hili likitolewa na mkuu wa polisi katika wilaya ile.
Walikutana kilabuni majira ya saa nane mchana, akili zao zilipokuwa timamu walijadiliana juu ya mauaji ambayo yalitikisa ghafla wilaya yao, mtaa wao ukiwa haujashuhudia kifo hata kimoja lakini tahadhali kubwa ilitangazwa kwa sababu muuaji alikuwa hajakamatwa wala kujulikana nia yake. Wakiwa katika kuchangia mada hii walimsisitiza mama muuza pombe kuwa itakapojiri saa kumi kamili, aifunge ile biashara ili kila mmoja aweze kurudi nyumbani kwake kabla ya giza halijaingia ili kuyakwepa masaibu yale. Tena wakahamasishana kuwa wote kwa pamoja watasindikizana barabarani.
Hilo likawa ni agano ambalo lilizua kasheshe baada ya pombe kukorofisha bongo za wanywaji. Ilipotimu saa kumi za alasiri na mama muuza kuwakumbusha kuwa wanatakiwa kuondoka. Kikageuka kizaazaa. Ni vinywa vyao vinazungumza lakini akili haimilikiwi tena na wao.
Unatudharau sana wewe mwanamke!
Umeridhika na pesa zetu eeeh!!
Umeamua kutufukuza au sio!
Mimi siogopi kufa! Kwani nani hajui kuwa ipo siku atakufa?
Mimi hapa siondoki hata mnipige mniue!
Hayo yalikuwa majibu ya wateja mbalimbali baada ya mambo kuwa yamechanganya. Ni heri ya hao walioweza kusema lolote, wapo ambao walikuwa wamesinzia kabisa baada ya ulevi kuwazidia. Mama mwenye kilabu chake akaamua kuendelea kuchota pombe na kuhudumia. Uzuri ni kwamba nyumba yake ya kulala nd’o hicho hicho kilabu, hakuwa na safari ndefu ya kufanya iwapo litatokea lolote la kutokea.
“Mama wanzagi!” Mteja mmoja ambaye hakuonekana kulewa sana alimwita yule mama akiwa karibu yake.
“Polisi wakifika hapa, anayekamatwa ni wewe… sio wateja. Mkuu wa wilaya na mkuu wa polisi wana hasira, hautaachiwa kirahisi… tena hawakawii kusema unamjua muuaji nd’o maana hauna hofu…na unakiuka kanuni.” Mteja akaweka nukta na kubeua. Mama Wanzagi anaonekana kupagawa baada ya taarifa ile.
“Sasa mimi nafanyaje waondoke jamani eeeh! Watanipiga nikiwalazimisha si unawajua!?” Anajibu mama yule huku akiifungua na kuifunga vyema kanga yake kiunoni. Asijali lolote lililoonekana baada ya kuwa ameifunua.
“Ngoja hebu! Si unataka waondoke…”
“Ndio…”
“Kusanye hela zako kwa ambao hawajakulipa kwanza…”
“Wote wamenilipa kabla huo nd’o utaratibu.”
“Sawa! ngoja” Anajibu kisha anapiga hatua kadhaa na kuutafuta usawa ambao atatazamana na walevi wengi.
“Inasemekana muuaji leo yupo mtaani kwetu jamani!” Anaipaza sauti yake. Maneno yale hakuwa wa kwanza kuyasema, tayari wengine walikwishayazungumza hata kama hawakusimama katika urasimi aliokuwa amefanya yule mteja mwenzao. Matusi yakaanza kuporomoshwa kumuelekea, bado wanajinadi kuwa hawakiogopi kifo na zaidi wakaenda mbali na kusema kuwa mlevi hata akipigwa risasi anazimia tu wala hafi.
Mtoa angalizo yule akageuka kama anayetaka kuondoka, na mara akageuka akiwa na bunduki katika mkono wake wa kuume na hapohapo ukasikika mlipuko mkubwa, risasi ilikuwa imejikita katika kifua cha mmoja kati ya wale wateja walioshabikia kuwa mlevi hata akipigwa risasi hauwawi.
Ikawa kijiwe cha hekaheka, waliokwishalala kwa ulevi waliamka, waliokuwa wanahisi wamelewa, pombe iliwakimbia wakawa timamu na kisha ikawa ni kushindana ni nani anayeweza kukimbia kuliko mwenzake. Waliodai hawakiogopi kifo wakiwa mbele zaidi katika mbio hizo huku wakiwaita mama zao wazazi waweze kuwaepusha na dhahama ile. Mama muuza alikuwa anapumulia katika uvungu wa kitanda chake, pesa zake zikiwa salama katika pindo la kanga yake.
Haikufyatuliwa risasi nyingine licha zile hekaheka kuwa kubwa, siku ikaisha katika namna ile ya kipekee. Askari wa doria wakaipata ile taarifa na kukifikia kile kijiwe kinachouza pombe za kienyeji.
Huyu mama ndiye wa kwanza kabisa kukamatwa kwa ajili ya kujibu mashtaka kadhaa ya kuuza pombe hadi muda ambao watu wanatakiwa kurejea majumbani, na pili alitajwa kuwa mtuhumiwa ni mteja wake hivyo yumkini anatambua wapi alipojificha anatakiwa kulieleza jeshi la polisi.
Mama muuza ulabu akatupwa rumande!
Huku katika pambazuko la kijiji kingine, taarifa imewafikia na imewahamasisha zaidi kudai haki zao.
Tatizo moja likaanza kuzaa matatizo mengine. Walianza kwa kudai haki tu….
Haki yao!.
_______________

OFISI ilikuwa chungu sana kwa ndani kwa sababu ya fukuto la joto, na maumivu ya kukikalia kiti cha mbao kwa muda mrefu. Nje palikuwa pachungu zaidi ambapo watu wengi walikuwa wamepanga foleni kwa ajili ya kuingia ndani ya ofisi ile. Kila mmoja akiwa na dukuduku lake ambalo anahitaji kupewa ufafanuzi.
“Tunawafanyaje hawa watu?” Mwanaume mtu mzima makamo ya kukwangua miaka sitini na ushei ulimwenguni alimuuliza mwanamke aliyekuwa ameketi pembeni yake.
“Yaani hata sijui na wanazidi kumiminika. Na wana hasira…” Alijibu huku akigeuza jicho lake kutazama mlangoni, akainyanyua shingo yake zaidi kuutazama umati kwa mbali.
“Kwani wilayani wao wanasemaje?” Akauliza mwanamama yule, umri wake haukimbilii kuitwa bibi na hauna muda mrefu katika ubini wa mwanamama.

“Mama Kalunde! Nimepiga simu kuanzia saa moja hadi sasa hivi… saa tatu. Imepokelewa mara moja halafu mtu hata hajaongea akakata. Nyingine zote hazipokelewi….” Mzee yule anazungumza kwa vitendo huku akiwa anashirikiana na muhuri uliokuwa mkononi mwake usiwe na kazi yoyote ya kufanya. Muhuri ule uliandikwa, ‘Mwenyekiti wa kijiji’ na ulikuwa ni mali yake ndani ya ile ofisi.
“Mi nadhani uwasikilize… maana wanavyozidi kuwa wengi ni hatari sana.”
“Unavyosema niwasikilize wewe unajitoa ama? Kwenye mazuri unakuwa mwenyekiti msaidizi, kuna balaa unasema nizungumze nao au sio?” Analalama mwenyekiti huku akitumia kiganja cha mkono wake kujipangusa jasho lililokuwa linatiririka.
“Sijamaanisha hivyo mwenyekiti, tuzungumze nao. Mimi nipo nawe bega kwa bega hili ni tatizo letu sote na sio sisi tuliolisababisha. Sisi na wao wote ni wahanga…..” Mama Kalunde anamsihi mwenyekiti wake.
“Waruhusu waingie wawili kwanza….”
“Haya wawili waingie…. Jamani tusipige kelele ili tuweze kufanya zoezi letu kwa wepesi, nawaomba sana ndugu zangu.” Anasihi mwanamama yule huku akikiweka sawa kitenge chake kiunoni. Waliokuwa mbele wanazama ofisini wanamsalimia mwenyekiti na kuketi.
“Ehee nawasikiliza…..”
“Mwenyekiti, majina yangu…”
“Achana na habari za majina, tuokoe muda ndugu yangu….mimi nitalipeleka wapi jina lako sasa..”
“Sawa, mwenyekiti ni hivi. Miili mitatu haijazikwa hadi sasa, miili hiyo imeharibika katika kiwango cha kuudhihaki ubinadamu wa ndugu zetu hao. Mmoja kati ya marehemu hao ni mama mkwe wangu…. Tunataka kujua serikali inatusaidiaje katika hili suala ambalo linahatarisha afya za wanakijiji na pia linaleta hofu kwa watoto wetu.” Bwana yule asiyeruhusiwa kujitambulisha jina lake anazungumza mbele ya mwenyekiti wa serikali za mtaa.
“Na wewe….” Mwenyekiti anahamia kwa yule mwanakijiji mwingine aliyeambatana na mwenzake.
“Mwili mwingine ni wa mdogo wangu, ni siku ya sita sasa haujaweza kuzikwa. Hakuna watu wa kuchimba makaburi, hakuna vifaa vya kiusalama kuweza kuubeba mwili ule ulioharibika vibaya…… sijui tunafanya nini mwenyekiti.” Kwa huzuni kuu anajieleza.
Mwenyekiti anahangaika na muhuri wake mkononi, alitambua kuwa watu wale watakuwa na malalamiko juu ya hali ya kiusalama katika kijiji chao lakini hakuwa amejiandaa kwa majibu yoyote yale. Anahaha na muhuri pamoja na kalamu ya wino iliyokuwa ikigongagonga kichwa chake. Hakuna majibu yanayopatikana, anachukua simu yake na kubofya namba kadhaa kisha anapiga. Anaweka spika za nje na kisha anainyanyua ile simu na kuwaonyesha watu wale wawili.
“Jina linasomeka nani hapo?”
“Mkuu wa wilaya!” Wakajibu kwa pamoja.
“Akipokea hii simu nitawaomba muongee naye moja kwa moja juu ya hali halisi mliyonieleza. Huenda ninyi mtaeleweka zaidi…” Anazungumza huku ile simu ikiendelea kuita. Kama ilivyokuwa awali, iliita pasi na kupokelewa na alivyopiga mara ya pili ilipokelewa.
“Mwenyekiti, kwani ukipiga simu mara moja unahisi unapungukiwa nini, unapiga simu mara thelathini mzee wangu? Unadhani ofisi ina kazi ya kukusikiliza wewe pekee,, aaargh!” Simu inakatwa.
Mwenyekiti anashusha pumzi anatazamana na wale wanakijiji wawili wa kwanza kuingia pale ndani.
“Katika hili suala, ni kila mtu anabeba mzigo wake ndugu zangu. Kila mmoja atazame la kwake, serikali yenyewe nd’o inatujibu kama mlivyosikia.” Mwenyekiti anazungumza akiwa ameegemea meza.
“Kwa hiyo hawajafahamu nani anahusika na haya mauaji?” Swali kutoka kwa mmoja kati ya wale wanakijiji waliopata nafasi ya kuzungumza na mwenyekiti na kisha kuisikia sauti ya mkuu wa wilaya ikiunguruma katika simu.

Swali lake halikujibiwa bali aliishia kutazamwa kama mtu mzembe katika kuchagua namna njema ya kuuliza maswali. Watu wale wawili walitoka katika ofisi ya mwenyekiti wa mtaa na wakawa mabalozi kamili wakimlaumu mkuu wa wilaya jinsi anavyosababisha lawama nyingi zitupwe kwa viongozi wa chini wakati ushirikiano hafifu unatokea katika ngazi za juu.
Licha ya haya yote kuna wanakijiji kadhaa bado hawakutaka kuchukua maneno ya wawili hao kama uamuzi wa jumla. Walilazimisha mpaka wakaonana na mwenyekiti wa kijiji. Wakaomba barua zao ziidhinishwe ili waweze kwenda polisi kumshtaki mkuu wa wilaya kwa jinsi anavyocheza na maisha yao na kuwadharau. Mwenyekiti akagonga muhuri katika barua zao, mmoja baada ya kugongewa ile barua aliishirikisha familia yake ikamzuia asifanye jaribio lile hususani kwa mkuu yule wa wilaya ambaye ni jeuri na mjivuni, lakini mwingine yeye hakuwa na familia ya kuweza kuishirikisha na hakutaka kufanya jambo kisa mwenzake amefanya ama hajafanya. Yeye alikuwa na msimamo wake, akaiacha siku ile ipite, kisha siku iliyofuata mapema kwa mwendo wa taratibu kabisa akajitembeza hadi kituo cha polisi.

“Yupo bize sana hataweza kuonana nawe.” Askari akamjibu baada ya kusisitiza kuwa anayehitaji kuonana naye ni mkuu wa kituo kile.
“Nitasubiri…” Mwanakijiji akajibu.
“Nimekueleza yupo bize.”
“Kituo cha polisi kinafaya kazi masaa ishirini na nne ama utaratibu umebadilishwa?” Bwana yule mtu mzima anahoji kwa sauti tulivu.
“Kama ni masaa ishirini na nne?” Askari anajibu kwa jeuri.
“Ni haki yangu kikatiba kumsubiri mpaka atakavyopata nafasi ya kuzungumza nami.”
Askari anajishika kiuno, anataka kusema zaidi lakini ni kama hana sentensi ya kubadilisha msimamo wa yule mwanakijiji abaye hajaitamka shida yake bali ameapa kuwa atamueleza mtu mmoja tu.
“Unawezaje kuganda hapa kumsubiri mtu ambaye hauna miadi naye?” Ni baada ya dakika sita askari yule alirejea na swali hili.
“Yanayotuleta kituoni ni matatizo. Wewe umewahi kuwa na miadi na matatizo?” Anamswalika.
“Sawa kama una tatizo, utaratibu ni kwamba unamueleza askari ambaye umemkuta kituoni. Nieleze na nitafikisha ujumbe wako…. Sijui ni ujumbe sijui ni shida… vyovyote.” Anapambana kuutuliza munkari wake lakini jazba ipo bayana.
“Je? Kama shida yangu mimi ni kukushtaki wewe kwa mkuu wa kituo? Na hapo natakiwa kukutaarifu wewe halafu utajishtaki?” Hatumii nguvu katika kuuliza na uso wake ameuinamisha chini.
“Unachanganyikiwa eeh! Sasa unataka unishtaki mimi kwa kosa gani?”
“Nani anayechanganyikiwa hapa kati yangu na wewe. Yaani unataka nikutangazie hapa mashtaka yangu ili uwahi kutafuta utetezi. Wewe elewa kwamba nitamsubiri mkuu wa kituo, na ninakuhakikishia kuwa kama sijavunja sheria za nchi, iwe isiwe nitaonana naye. Huo niliokueleza ni uhakika!” Uso umenyanyuka na macho yanamtazama yule askari.
“Unaitwa nani?”
“Kwa sasa nielewe kwa jina la Mtanzania… ila mkuu wako nitamueleza zaidi ya hapo. Kama ambavyo kwa sasa mimi nakutambua kama askari ila baadaye mkuu wako atanieleza zaidi juu yako.” Ni jibu sahihi lakini linaloonekana kumkwaza yule askari, anasonya na kuondoka.
Mzee yule anaendelea kungoja.

“Mkuu jamaa amesisitiza kuwa anahitaji kuonana na wewe. Na hataondoka bila kuonana nawe.” Konstebo wa polisi alitanguliza saluti kabla hajamueleza mkuu wa kituo cha polisi, Sajenti Guilaume Hiza.

“Yeye anachotaka ni nini haswa? Kwa ufupi”

“Alifika akiwa ananung’unika kuwa amechoka kulala saa kumi na moja alasiri. Mgongo unamsumbua…”

“Sasa mimi natakiwa kufanya nini yaani. Niende kulala naye nyumbani kwake?” Sajenti Guilaume anauliza huku akiipigapiga kofia yake mezani. Ameghadhabika.

“Anadai mtukufu raisi amesema raia wana haki ya kusikilizwa na jeshi la polisi. Na amechagua kuzungumza na wewe leo.. wewe tu hataki mtu mwingine”

“Ametaja jina langu?”

“Hapana, amesema mkuu wa kituo.”

“Umesema yupo wapi?” Sauti imepoa kiasi.

“Nje mkuu!” Saluti inasindikiza jibu lake.

“Mkague kisha mlete…..si anataka kuonana na mimi, mlete nasema” Ni kama anayeikaanga shari.

“Au nimwondoe?” Konstebo anatoa kauli ya kuonyesha yupo upande wa mkuu wake.

“Umtoeje sasa… unataka kuanza kutumia nguvu mapema yote hii. Hizo nguvu si mngezitumia kulisaka hilo dubwana Eboh! Eti au nimtoe… yaani yanakutoka tu maneno… unajisikia unachozungumza kweli…. Hebu toka hapa, kamkague na aingie hapa ndani!” Ni kufokewa kisha amri.

“Sawa mkuu!” Anatoka.

Hamfikii mgeni yule moja kwa moja, anampita takribani mara mbili. Anajisikia unyonge kumpa ushindi bwana yule ambaye kwake yeye anaona bwana yule anahusika moja kwa moja na sababu za yeye kufokewa.

“Ofisi ile pale, ingia..” Anamweleza kinyonge.

Akitarajia bwana yule atauliza swali lolote ili na yeye ambwatukie. Hakuulizwa na bwana yule hakusimama. Mpaka zilivyovuka sekunde zaidi ya kumi na tano.

Akasimama na kuuendea mlango, akaingia baada ya kutimiza ustaarabu wa kubisha hodi.

__________________

“Raisi alivyosema kuwa jeshi la polisi liwasikilize raia hakumaanisha jeshi liache kazi zake na kumsikiliza kila mtu mzee wangu. Kama umetumwa kunifanyia jaribio lolote lile, umefanya kosa kubwa sana. Kama utakalozungumza halitakuwa na maana yoyote pia, utajutia kuingia katika ofisi hii? Nakusikiliza sasa….” Sjt. Guilaume alianza kuzungumza huku akiwa anaigandamiza kofia yake mezani. Shari ishaiva anajipanga kuipakua, lakini hayupo tayari kuirarua peke yake.

“Nimekuja hapa tujadiliane kuhusu dubwana linalosababisha Kevin na Salu washindwe kwenda kwenye uwanja wa mpira baada ya masomo yao.” Sentensi hii inamwingia Sajenti, anaganda na kuendelea kumsikiliza mgeni wake anayeonesha nia ya kuendelea kuzungumza, “Dubwana ambalo limesababisha hata Bi. Tatu asikutane tena na akinamama wenzake katika vikundi vyao vya kukopeshana pesa…” Akaweka pumziko la lazima baada ya askari yule kumfanyia ishara ya mkono kumzuia. Hii sentensi ambatano ni tatanishi.

“Umemfahamu vipi mke wangu na watoto?” Anauliza kwa sauti inayoelekea katika hamaniko, kisha anameza funda kubwa la mate.

“Raisi alisema uhusiano baina ya raia na polisi unapaswa kuimarishwa. Mimi sikupuuzia, nilijitahidi kuzijua familia za polisi na mojawapo ya hizo familia ni ya kwako. Je? Kuna makosa mkuu? Ama sikumuelewa raisi wa nchi yangu aliposisitiza suala la mahusiano?” Mgeni yule anajibu huku akiwa ameituliza mikono yake miwili juu ya mapaja yake kwa nidhamu kubwa. Hatoi sababu lau moja kwa Sajenti Guilaume kumshukia kwa ghadhabu.

“Who are you?… eeeh! Wewe ni nani mzee, umetumwa na nani?” Sauti ya sasa ni tulivu sana, utulivu unaoambatana na kuipachika kofia yake kichwani.

“Nilijitambulisha mkuu! Mimi ni raia ambaye nimekuja hapa kwa sababu nimechoka haya maisha ya kulala saa kumi na moja alasiri. Yaani mwanadamu anaingia ndani mapema kuliko kuku wake na bata? Hili jambo wewe linakufurahisha mkuu, yaani kuku na bata wanakuwa huru kuliko mwanadamu?” Anahoji.

“Tufanye kwamba hili suala halimfurahishi mtu yeyote. Wewe umekuja hapa ukiwa na wazo gani labda?” Sajenti hana uhakika juu ya wadhifa wa mtu aliyeketi mbele yake, anajitahidi kuyasoma macho yake lakini bado hajapata uhakika ikiwa ametumwa ama amejituma kufika pale.

“Kwa sasa sina wazo kabisa nipo katika mshangao tu. Hili dubwana kwanini linaua tu, halisemi chochote wala haliibi chochote. Linaacha alama zilezile za vidole na haziwi msaada kwa chombo kikubwa kama hiki. Kwakweli bado nashangaa….” Anatua sentensi yake.

“Alaah! Kwa hiyo muda huo wote uliongoja kukutana nami ulihitaji kuelezea kuwa una mshangao na hauna wazo? Ili tusaidiane kushangaa au sio?” Sajenti Guilaume anastaajabu, kofia inaondolewa tena kichwani.

“Mimi kwa sasa ni mzee, nimekuja hapa kulieleza jeshi la polisi kuwa daktari alinisisitiza kila jioni niwe nafanya mazoezi ya kutembea walau kilometa mbili. Huwezi kuamini ila sasa ni siku ya kumi na mbili sijafanya mazoezi hayo, hivi hapa nikifa kwa presha nani atalaumiwa? Bila shaka ni hilo dubwana….na mimi pia watu watanishangaa sana kwanini sikufanya jitihada ya kutoa ripoti kituo cha polisi kilichopo jirani na mimi. Sasa hapa nina kosa gani kuja kulishtaki hilo dude lisilokuwa na jina wala sura? Au kosa langu ni kuwa mzee?” sasa anabinua mabega yake kuzistawisha lawama zake.

“Hivi unatambua kuwa unajitafutia matatizo ambayo yanaepukika mzee? Unalijua hilo??” Sajenti anakuwa mkali.

“Mkuu unawaza kuniweka Lock up ama unataka nipelekwe gerezani kabisa? Hiyo nd’o adhabu ninayostahili?” Anauliza na pasi na kusubiri jibu anaangusha tabasamu jepesi na kuendelea, “Hadi sasa dubwana hilo lisilojulikana limeua watu ishirini na mbili, kati ya watu hao hakuna hata mmoja aliyekutana na dubwana akiwa lock up ama akiwa gerezani. Ukiniweka sehemu mojawapo kati ya hizo na kisha wewe ukarejea nyumbani kwako ni bayana kwamba wewe umenilinda mimi na kisha wewe na familia yako mnabaki kuishi kwa mashaka. Je? Hiyo bado ni adhabu stahiki unayowaza katika kichwa chako?” Mgeni yule asiyeonekana kuwa na haraka yoyote anajibu kwa utulivu. Majibu yake yanamweka Guilaume katika fikra mchanganyiko.

Huyu mtu ni nani? Na Je? Kumweka mahabusu ni adhabu ama msaada?

“Kwanini unahisi kuwa sisi tukishirikiana na wewe tunaweza kulikamata hilo unaloliita dubwana?” Akachagua kuuliza swali lile ambalo halikuwa katika orodha ya maswali yake.

“Kwa sababu mimi naitwa mzee Geza Ulole.” Akajibu kwa utulivu.

“Geza Ulole! Yaani huu upuuzi wa kujiita jina la hayati Geza Ulole nilidhani ni kwa vijana peke yao, kumbe hadi watu wazima tena wazee kabisa na wao wanaangukia katika huo upepo? Mwenzenu Geza alikuwa na akili nyingi, kalifanyia taifa mambo mengi sana, hakuwa na hizi habari za kumalizia uzee wake vituo vya polisi kuwachokoza askari kisha aadhibiwe watu walalamike kuwa jeshi la polisi linawaonea wazee” Akazungumza huku anatokwa na tabasamu la kukarahika.

“Hivi unajua kuwa hili dubwana limesababisha watanzania watambue kuwa jeshi la polisi lina idadi chache sana ya askari kuweza kuwalinda raia wake. Kwa hesabu za harakaharaka hadi sasa watu wa mahesabu wanadai kuwa jeshi la polisi lina wastani wa askari mmoja kulinda raia elfu moja….. huoni kama hilo dubwana linataka kuivua nguo nchi yetu?” Mgeni aliyejitambulisha kama Geza Ulole akatupa hoja nyingine tofauti na matarajio ya sajenti.

Sajenti akatokwa na tabasamu kisha akazungumza kwa majivuno, “Hakuna kitu unajua kuhusu jeshi letu la polisi wewe. Jeshi letu lina vijana wa kutosha kuweza kuwalinda raia na mali zao…” anajikweza.

“Ni kitu gani basi kimejitokeza kiasi kwamba jeshi hilihili limeshindwa kuwalinda raia dhidi ya hilo dubwana….. jeshi limeshindwa walau kujitokeza hadharani na kutoa japo picha tu ya dubwana hilo. Badala yake jeshi linawahamasisha raia wake waingie ndani saa tisa alasiri, na linaenda mbali likisisitiza wasiokuwa na vyoo vya ndani watumie ndoo ama chupa tupu za maji kukidhi haja zao……kuna tofauti gani kati ya gereza na maisha haya. Na bado unaamini kunipeleka mimi gerezani ni kuniadhibu? Gereza hilohilo ambalo mmefungia mama muuza pombe za kienyeji ili awasaidie upelelezi. Mbona mnalikosea heshima gereza, zamani nikiwa kijana kuna watu walikuwa hadi wanatamani kwenda jela wajue palivyo, sio kizazi chenu hiki kila mtu akiamua kwenda jela anaenda tu kirahisi. Anatukana mtu, anaiba kuku, anakojoa vichakani. Eti hizi zote ni kesi za kupeleka mtu gerezani….” Mikono juu ya meza, macho yanamtazama sajenti.

“Kwanini umechagua kuja kunitukana katika ofisi yangu?” Sajenti anauliza kwa utulivu, ile dhana ya bwana yule kuwatambua watoto na mke wake ilikuwa inamtafuna na hajaipatia ufumbuzi.

“Nadhani jeshi nd’o linatutukana sisi kwa kukusudia. Yaani jeshi linatangaza kwa raia kuwa tukimwona mtu na kumtilia mashaka tutoe taarifa kituo cha polisi, vipi kama hilo dubwana lipo ndani ya taasisi yenu?….na kuna uhakika gani kuwa hilo dubwana ni moja na sio kwamba ni taasisi.”

“Sasa naona unavuka mipaka yaani umekuja hapa kunieleza kuwa jeshi linaua wananchi wake. Naomba sasa jina lako halisi sitaki tena masikhara, muda wa masikhara umekwisha…..” Anafoka huku anachukua karatasi na kalamu.

“Mzee Guilaume, mbona wewe jina lako ni la marehemu babu yako. Ulihukumiwa miaka mingapi gerezani kwa kutumia jina la marehemu…..kama haukuhukumiwa ni kwanini mimi kuitwa Geza Ulole unatafuta namna ya kunitupa gerezani?” Sentensi ile ikaihamisha kalamu kutoka katika karatasi ikaelekea mdomoni na kuanza kutafunwa.

Sajenti alikuwa amekamatika!.

“Kwanini umekuja kwangu bwana Geza Ulole….. hukuona vituo vingine vya polisi? Umetumwa kuniharibia kazi yangu?”

“Mkeo Tatu amezaliwa tarehe ngapi?”

“Achana na habari za mke wangu nakuomba!”

“Tarehe ya mkeo kuzaliwa inahusiana nini na kuwa habari ya mkeo, kwani alizaliwa peke yake katika hiyo tarehe kumi na tisa usiyotaka kuitaja, ama katika mwezi wa sita alizaliwa yeye peke yake?” Mgeni anazungumza kwa utulivu huku anatabasamu. Sajenti anakosa utulivu, jasho linavuja katika mfereji wa mgongo wake, mgeni yule alikuwa ameitaja tarehe ya mkewe kuzaliwa. Hajaishia katika tarehe pekee ameutamka hadi mwezi.

“Mimi nakwenda Sajenti, lakini siku ukikutana na kichwa cha mke wako kikiwa kimetoroka katika kiwiliwili chake, isiwe mwanzo wa wewe kutambua nini maana ya swali langu….”

“Wewe ndiye muuaji si ndio, wewe nd’o hilo dubwana na unataka kumuua mke wangu eeeh!” Taharuki ingali juu sana wakati anahoji. Mgeni yule aliyejitambulisha kwa majina ya Geza Ulole anaingiza mkono katika koti lake chakavu, Sajenti anawahi kuchukua bastola yake na kumwelekezea akiamini kuwa bwana yule anataka kummaliza.

“Huu utaratibu wa kubambikiziwa mabunduki bila risasi nilijua ni kwa vi konstebo huko kumbe hadi wewe mkuu wa kituo kuwa na bunduki inayokosa risasi ni jambo la kawaida?…..” Bwana yule anasita kidogo anazungumza kisha anatoa bahasha, anaifungua na kutoa picha kadhaa anazirusha moja baada ya nyingine mbele ya sajenti ambaye ameitua bunduki yake mezani. Haina inachomfaa katika kumtishia mgeni yule.

“Kati ya makaburi niliyoweza kufanikisha kutembelea, marehemu wote walizaliwa tarehe kumi na tisa…… tarehe kama ileile uliyokuwa unaringa kuitaja utadhani ukiitaja mimi nitaondoka nayo ikanipe utajiri. Vipi kama mmiliki wa tarehe kumi na tisa anayefuata kuuwawa ni shemeji yangu??” Swali lile likaambatana na kuzikusanya zile picha na kuzirejesha katika bahasha. Kisha akazitumbukiza katika mfuko wa koti lake chakavu.

“Sina simu, sina barua pepe, sina pahali unaweza kunipata kwa wepesi sana maana hata nyumba yenyewe naweza kuhama. Wakati sahihi wa kuamua ni sasa… mimi naondoka hivyo!” Alizungumza akiwa ameufikia mlango wa kutokea.

“Simama ewe Geza Ulole…simama hapohapo.” Guilaume akatoa amri, sauti yake ingali bado inaelea katika hofu.

Geza Ulole akanyoosha mikono yake juu, “Nipo chini ua ulinzi ama?” Akauliza huku akiendelea kunyoosha mikono yake. Sajenti Guilaume akaruka kishupavu na kuinasa mikono ya Geza Ulole iliyolegezwa na kuizungusha nyuma kisha akaiunganisha na pingu. Geza hakujaribu kufurukuta.

“Hauwezi kuondoka hivihivi kienyeji enyeji wewe ujiitaye Geza Ulole. Unapaswa kushirikiana na jeshi la polisi kikamilifu…” Akamsemesha huku akimsukuma hadi akarejea kuketi katika kiti.

Geza Ulole anamtazama pasi na kuongeza neno lolote lile. Mzee yule anaitwaa simu yake na kuinyanyua kisha anabofya namba kadhaa.

“Fika kituoni kuna mtu unapaswa kukutana naye…” Akatoa angalizo katika simu, kisha akausikiliza upande wa pili ulivyojibu.

“Jitahidi iwe mapema…” Akaongeza msisitizo.

Geza Ulole akapekuliwa na kukutwa na senti kadhaa pamoja na barua kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa wake iliyokuwa inampa idhini ya kumfungulia mashtaka mkuu wa wilaya yake. Akatupwa rumande katika chumba cha peke yake, kabla hayajatolewa maagizo mengine ya ziada ya Geza Ulole kuhamishwa kutoka pale alipokuwa na kufikishwa katika ukumbi mwingine maalumu.

Hawakujua walichokuwa wanakikaribisha.

Hawakujua!

_________________________

ITAENDELEA…..

Naitwa Geza Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment