KIJASUSI

Ep 04: Fedheha

SIMULIZI Fedheha
Fedheha Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Fedheha

Sehemu ya Nne (4)

Tuliwasili usiku sana katika nyumba ambayo kwa nje tu ilitamanisha kujua ndani ipo vipi.

Ilikuwa inavutia sana na ilikuwa ya kisasa.

Kabla sijauliza chochote Geza alisema kama anayezungumza mwenyewe.

“Haka kajumba nilikapata walau ndo matunda yenyewe. Hajawahi kukanyaga msichana yeyote humu ndani ila kuna mwanamke mmoja ambaye atakuwa wa kwanza kukanyaga humu!!!”

Nikamuuliza ni msichana gani akaniambia niwe na subira maana hata akinitajia jina haitanisaidia kitu.

“Sasa wewe unauliza ni msichana gani nikisema Getruda uniulize Getruda yupi au? Acha mambo zako dogo” alinijibu kiukali!!

Na hapo tukawa tumeufikia mlango tayari!!

Akatoa funguo na kufungua tukaingia ndani!!

Amakweli usihukumu ladha ya kitabu kwa kutazama jalada lake.

Laiti kama ningempuuzia Geza kuanzia tulipokutana Mwanza basi hii ilikuwa aibu yangu!! Kweli nilipomuona kule mahabusu nilimuhesabia kama kijana aliyepoteza uelekeo wa maisha na hana chochote mtaani!!

Sasa mwenzangu kumbe anamiliki nyumba!!

Mimi na digrii yangu hata msingi sikuwanao mwenzangu alikuwa anaishi kwake. Tena sio ilimradi nyumba ni nyumba haswa katika maana halisi ya nyumba.

Amakweli kusoma kwingi si kufanikiwa sana!!

Geza aliingia jikoni akaandaa chakula, tukala. Na hapo nikagundua kitu kipya kabisa, Geza hakuwa kama nilivyodhania.

Hakuwa mtu wa kukurupuka na licha ya kwamba hakuwa na elimu ya chuo kikuu, yule bwana alikuwa makini sana katika kila kitu ambacho alikuwa anakifanya.

Nilimuuliza ni kwanini hakuna mwanamke ambaye amewahi kuingia katika nyumba ile alinipa jibu ambalo lilikuwa la kulalia. Na kusoma kwangu kote sikuwahi kuwaza alivyowaza Geza.

“Dogo ukisikia mtu anaitwa mwanamke usidhani ni yule tu anayebeba mimba na kuzaa, mwanamke anaweza kuwa hata wewe…yaani asione kitu lazima atasema tu kwa mashoga zake. Humu wanawake wa kuzaa walishaingia mbona sema hao walikuwa na mioyo ya kiume, na wanaume ambao wanaingia humu ndani ni wanaume haswa….. kwa hiyo jitambue kuwa hadi nimekuleta hapa wewe upo kundi gani…. Lala salama dogo tukijaaliwa kuamka kesho kuna kazi nzuri sana tutafanya. We mwenyewe utaipenda walah!!” Geza akamaliza kuzungumza akaachia tabasamu hafifu.

Na hapo nikabaki kushangaa huyu jamaa vipi? Yaani mimi mgeni katika nyumba ile halafu yeye anaenda tu kulala na kuniambia usiku mwema sasa mimi nitalala wapi.

Nikatamani kuuliza ila sasa majibu yake yalikuwa yananiogopesha jamaa alikuwa na kichwa kizuri aisee!!

Alipojifungia mimi nikabaki pale sebuleni na usingizi ulinichukua palepale!!

Alfajiri nilishtuka na kumkuta Geza akiwa macho ameketi akisoma magazeti.

“Dogo! Yaani huo nd’o ulikuwa mwisho wako wa kujiongeza!!! Ukalala sebuleni?” akaniuliza huku akiendelea kusoma magazeti.

Sikuwa na la kumjibu lile swali lilikuwa gumu.

Geza Ulole akatulia kisha akanigeukia, “Ila umefanya jambo jema sana ndo maana nakuita wewe mwanaume wa kweli, kwani umepungukiwa nini ulivyolala hapo chini.”

Nikaifikiria kauli ya Geza na kuzidi kustaajabu maisha ya huyu jamaa!!

Alfajiri hiyohiyo Geza akajianda bila kuniambia mimi nijiandae sasa sikuwa mtu wa kusubiri kuambiwa, na mimi nikajiandaa.

Nikakutana na mshangao mwingine mkubwa asubuhi ile!!

Geza alikuwa anamiliki gari!!

Na hapa sikuuliza alisema mwenyewe tena.

“Dogo hili nimenunua kwa biashara zangu, sijaibia mtu!! Yaani we unalala vibaya sana mdogo wangu. Yaani nimeishtua gari we umelala tu… jiangalie sana usingizi baba mmoja mama mmoja na kifo!!!” alizungumza yale kisha akaiondoa gari.

Sikujua hata ni wapi tulipokuwa tunaenda!!

Gari ilienda kwa mwendo wa wastani tu, hadi mwanga ulipochomoza bado tulikuwa tukiingia kona hii na kutokea ile, sikujua Geza anatafuta kitu gani na bado sikuweza kumuuliza nilichosubiri ni maagizo tu!!!

Naam! Maagizo yakaanza mnamo saa nne asubuhi ile.

Geza akaniambia nishuke nikanunue baibui. Sikuuliza swali nikaenda kununua!!

Tukazunguka huku na kule mitaa aliyoijua mwenyewe hatimaye akaniagiza tena kununua miwani nyeusi!!

Baada ya hapo gari likaondoka kwa kasi hadi nje kidogo ya mji maeneo ya koko beach!!

Huko nilibaki kumwangalia Geza akivaa lile baibui kisha akaivaa miwani. Na mwishowe akajivika juba .

“Vipi hapo nafanania na Maimuna eeh!!” Geza aliniuliza huku akinitazama….. nilitamani kucheka lakini nikajikaza.

Hakuwa Geza yule hakika!!

Akaukalia usukani tena tukatoweka!!

Tukayafikia maduka ya urembo akaniagiza kununua aina fulani ya manukato. Nikayanunua na kumpelekea akajipulizia.

Baada ya hapo ikiwa ni saa sita na dakika kadhaa tukaondoka tena.

“Dogo nimebakiza kukutuma mara moja tu ili tuimalize siku!!! Na hili agizo la mwisho kuwanalo makini sana, ukikosea kidogo tu umeharibu kila siku. Kuanzia dakika hii mimi sio Geza Ulole na wala si mwanaume bali ni mwanamke na jina langu ni KHAJAT BINTI KHALIFA… sema Khajati binti Khalifa!!” Geza akaniamuru nami nikarudia jina lile vyema.

Naam! Tukaondoka!!!

ILIKUWA ZAIDI YA FILAMU YA KISWAHILI KWA KILICHOTOKEA!!!!

Gezaaa! Mwacheni aitwe Geza!!!

Ilikuwa ni hatari lakini kwa Geza aliona ni salama tu!!

Baada ya kuwa amependeza katika lile vazi lililomfanya afananie na mwanamke huku akiwa ameniambia kuwa jina lake kuanzia muda huo ni Khajat binti Khalifa. Baada ya kimya kirefu kiasi kidogo alivunja ukimya!!!

“Dogo unajua kuendesha gari!!” aliniuliza Geza huku akiwa anatazama mbele. Sura yake ilikuwa inatazama mbele hakuonekana macho wala pua yake!!!

Nikamkubalia kuwa nilikuwa najua kuendesha lakini sikuwa na leseni!!

“Dogo nimekuuliza swali moja halafu unajibu maswali mawili labda nikikwambia huo muda uliopoteza kujibu swali la pili ambalo haujaulizwa ukiambiwa uufidishie utafanya nini? Eeh! Maana sijauliza kuhusu leseni” Geza aliniuliza huku akionekana kutilia maanani zaidi katika usukani!!

Swali lake lilikuwa gumu, sasa ikawa kama kawaida kila swali analouliza Geza kwangu linakuwa gumu sana lakini akilini nikitambua wazi kuwa alikuwa akiuliza kweli tupu!!

Matukio hayo ya kushindwa kujibu maswali ya Geza mfululizo yakanifanya nikiri kuwa Geza alikuwa na akili sana kupita mimi!!

Baada ya sekunde kadhaa Geza alisimamisha gari baada ya kukutana na taa nyekundu za kuzuia gari zisitembee!!

Palepale akaufungua mlango na kutoka nje upesi!! Akazunguka na kuja kuufungua mlango wa upande wangu, nikasahau kujiongeza kuwa alikuwa ameniuliza iwapo najua kuendesha gari. Geza akanitandika ngumi mgongoni!!

Nikahamia upesi katika kiti cha dereva na mara taa zikaruhusu nikiwa ni dereva, sasa ikawa ni neno lizae kitendo cha upesi.

Kila neno akisema Geza natakiwa kufanya kwa kitendo!!

“Kata kushoto…. Nyoosha, usimpite huyo!! Overtake hapo, haya kushoto tena nyosha moja kwa moja!!” nilizifuata sheria zote hizi!!

Hatimaye akaniamuru nisimamishe na hapo tulikuwa jirani kabisa na umati mkubwa wa watu!!

Wengi wakiwa na kanzu na mabaibui!!

Naam! Nikatambua kuwa tulikuwa eneo karibu kabisa na msikitini!!

“Nilikwambia jina langu nani?” Geza akaniuliza. Sikufikiria sana nikamjibu upesi.

“Geza ulole!!” nikajibu. Mara Geza akanishtukiza kibao kikali sana shavuni. Na hakutaka kuniambia kosa langu nikajirekebisha mwenyewe huku nikivumilia yale maumivu. Maana Geza alikuwa na mkono mzito balaa!!

“Khajat binti Khalifa!!” nililitaja jina lake na yeye akaitika kikekike, ‘Abeee dogo”….

Geza bwana!! Nikayasahau maumivu ya kutandikwa kofi, yaani yeye akanizaba kibao halafu tena analeta utani!!

Jamaa wa ajabu sana huyu!!

“Nenda hadi pale katika kile kioski, jifanye unanunua gazeti…aah! Usijifanye we nunua kweli gazeti halafu muulize huyo muuza magazeti akuonyeshe mke wa Baisar… usimtazame machoni wakati unazungumza naye. Jifanye hauna haja!! Akishakuonyesha upesi rejea garini utanikuta Khajat mimi mtoto wa Khalifa nakusubiri. Upesi!!! Kumbuka huyo ni mke wa Baisar nadhani wajua tafsiri yake” akaniamuru, nikashuka na kujichanganya hadi nikamfikia yule muuza magazeti.

Geza akabaki garini, nilikuwa natetemeka sana. Sikuwahi hapo kabla kushiriki matukio ya namna hii sasa Geza amenitupa katika domo la mamba.

Awali wakati napiga hatua uoga ulikuwa katika kiwango cha juu sana lakini kadri nilivyozidi kusogea nikayakumbuka maneno ya Geza akinisifia kuwa mimi ni mwanaume, na kisha nikayakumbuka yale maneno yake wakati naondoka aliniambia kuwa yule ni mke wa Baisar. Kauli ile kwa maksudi Geza alinieleza ili nipate hasira naam! Ile hasira ikauondoa ule uoga wangu!!

Nikamfikia yule kijana, nikafanya kama alivyoniagiza Geza. Nikanunua gazeti na kisha nikamuuliza lile swali.

“Vipi na wewe unahitaji kuonana na Baisar nini? Yaani mimi hadi nimechoka huyu mama sina hamu naye na Baisar mwenyewe na utajiri wake bado Bushoke tu yaani mtu hauonani naye eti mpaka umvizie mkewe ndo akuunganishe aaargh! Wanaume wengine… yaani mimi kaka nikija……..” akasita pale kisha kabadili mada ghafla huku akitetereka.

Na mara akanipa ishara kwa macho kuwa mke wa Baisar mwenyewe nd’o yule aliyekuwa anapita!!!

Manshalaah! Alikuwa na haki ya kutetereka yule muuza magazeti, yule mama hakuwa na haja ya kukueleza kuwa amezikalia pesa kwa sababu mwili wake wenyewe tu ulinukia pesa!! Na mimi nikajikuta namuogopa!!

Nikaondoka bila kushukuru na kwenda garini moja kwa moja.

“Usiingie ndani!!!” akanizuia Geza. Akazungumza nami nikiwa palepale dirishani.

“Wewe ni dereva wangu, mimi naitwa Khajat binti Khalifa…. Ok! Upesi sana nenda kamwambie mke wa Baisar kuwa nahitaji kumwona. Ole wako useme mimi naitwa Geza ni hapo ndo utakapokitoa cheti cha kliniki kilichoandikwa kuwa mimi naitwa Geza!! Upesi muwahi!!!” akaniamuru, nikatoweka. Yaani nilikuwa kama kichaa hakuna nilichokuwa nahofia tena.

Nikaenda kwa mwendo wa heshima kabisa!!

Nikataka kupenya pale mara wanaume wawili wakanizuai!!

Doh! Kumbe yule mama alikuwa analindwa!!

Nikatazama kule garini nikamuona Geza akiwa hana utulivu kabisa bila shaka hata yeye hakujua kama yule mama anao walinzi tena wawili. Nikaikumbuka ile kauli ya Geza aliyoniambia asubuhi kuwa kujiongeza kwangu kote nikalala sebuleni.

Sasa ulikuwa wakati wa kumwonyesha Geza kuwa hata mimi naweza kujiongeza katika dharula kama zile!!

Nikaongea kwa sauti kubwa kama ninayewaambia wale walinzi lakini lengo langu sauti ipenye katika masikio ya mke wa Baisar!!

“Mimi ni Sumri dereva wa madam Khajat Khalifa nahitaji kumuona mama!!!”

Naam! Ulimbo ukanasa ndege!! Yule mwanamama akageuka!!

“Kijana taka nini?” akaniuliza katika lafudhi yake ya kiarabu.

“Mimi dereva wa madam Khajat anahitaji kuonana nawe…” nikapaza sauti tena. Yule mama akanisogelea huku akijisemesha mwenyewe.

“Khajat naweka derefa Swahili tena?” kujiongelesha kule kukanifanya nitambue kuwa bi Khajat halisi alikuwepo kweli. Tatizo sikujua alikuwa na mahusiano gani na huyu mwanamama wa kiarabu.

“Where is she?? Aaahm! Ako wapi yeye..” akaniuliza. Nikanyoosha kidole kuelekea ilipokuwa gari ya Geza.

Na hapohapo Geza akiwa na baibui lake akatoa kichwa nje na kupunga mkono!!

Ebwana ee!! Geza sina la kusema!!!!!! Yaani tayari alikuwa amehamia siti ya nyuma!!

Yule mke wa Baisar akaondoka kuelekea ilipokuwa gari ya Geza, nami nikawa nafuata nyuma!!

Nilipofika nikajiongeza tena!!

Nikaufungua mlango wa nyuma yule mama mpenda kuabudiwa akaingia. Nami nikaingia katika usukani.

Yule mama akaanza kuongea kiarabu na mara akachanganya na Kiswahili ni hilo tu nililoweza kubahatisha kulijua.

“Hii Swahili wizi sana…. Kwanini penda wao??” hilo lilikuwa swali lake la mwisho.

Kupitia kioo cha juu pale nikamuona Geza akimfyatua yule mama ngumi moja tu!! Narudia nikiwa namaanisha jama!! Ngumi moja tu!!

Kimya kikatanda!!

“Dogo safari moja mpaka maskani hii. Najua hupakumbuki nitakuwa nakuelekeza!!!” Geza akanieleza na hapo nikajiweka vyema nikawasha gari na kutoweka kwa amani tele.

Wakati naondoka kwa mbaali niliwaona wale walinzi wa mke wa Baisar wakiitazama gari wasijue nini kinaendelea!!! Na wale watu ambao walikuwa wamemzunguka bila shaka kwa ajili ya kuomba misaada walibaki kuduwaa, inakuwaje anaondoka mama huyu bila kuaga!!

Geza alinielekeza hadi tukafika mahali ambapo si yale makazi ya awali. Huku palikuwa pengine. Ni kama alikuwa anaisoma akili yangu yaani kabla sijamuuliza yeye ni aidha anakuwa na jibu tayari ama ananipa jibu hata kabla sijauliza.

“Dogo hii gari ikirejea kule muda huu itakaririwa na kutufanya tupoteze pointi tatu muhimu hata kabla dakika tisini tu hazijakamilika.”

Akasita kidogo akatazama yale mazingira!!

“Dogo hili dude zito kweli sijui tunamtoaje humu… halafu big up sikudhani kama ungemfikisha garini. Nd’o maana nilikwambia baba yako amewahi kuwa jambazi ama mpelelezi!! Bado haujanijibu!! Anyway usinijibu tu maana haisaidii kitu ila wewe ni mwanaume!! Na vita nd’o kwanza imeanza!! Naupenda mchezo huu jamani!!!” alizungumza huku akionekana kweli kufurahia kile alichokuwa anakisema.

Jibu la tunamtoa vipi alilitatua yeye. Akafungua buti la gari na kisha akamwagia yule mama huku akimnasa vibao!!

Kweli akainuka na aliongoza njia mwenyewe hadi tukafika ndani!!

“Hivi Khajat….” Nikakosea nikamuita Geza lile jina kuna jambo nilitaka kumwambia.

Aisee huyu jamaa nadhani kuna athari zilikuwa kichwani mwake na zilikuwa zinafifia na kuibuka. Kama si matumizi ya bangi zamani basi alikuwa anaendelea kuvuta bila mimi kujua hadi wakati huo. Eti akanigeuka kisa kumuita Khajat!!

Ghafla akanirukia na kunikaba koo.

“Nani Khajat!! Dogo mi nafanania na mwanamke ama? Nasema nani Khajat..” aliniuliza maswali huku akijua fika kuwa amenikaba koo na siwezi kujibu!!

Na hapo kikatokea kitu kilichotufanya tukodoe macho!!

Mtutu wa bunduki!!

Yule mama wa kiarabu alikuwa ametuelekezea mtutu wa bunduki!!

Asalaale! Nikakiona kifo kilee!!

Nakufa kabla sijamuona Latipha wangu nakufa dakika za mwanzo kabisa za mchezo!!!

Mkojo ukabisha hodi na hapo jicho langu likashuhudia yule mama akianza kukisogeza kidole chake katika kifyatulio!!!! (Triggre)

Ni balaa jipya.. baada ya kufanikiwa kumpata mateka wao Geza anazua ugomvi kisa kuitwa Khajati. Ugomvi ambao unasababisha wamsahau mateka wao!!

Na ghafla mateka anatoa bunduki huku akiwa dhahiri shahiri tayari kuua!!!!

BADALA ya kushtuka kuwa tupo katika hatari ya kuuwawa Geza Ulole alianza kucheka. Alicheka sana na hapo nikamuona yule mama akianza kutetemeka huku akionekana dhahiri kupagawa. Wakati huo mimi hali ilikuwa tete sana na nilikuwa nakaribia kujikojolea!!

Geza akaachana na mimi na ikawa zamu ya kushuhudia maajabu mengine!! Yaani kumbe Geza wakati yule mama amepoteza fahamu alimpekua na kutoa risasi zote zilizokuwa katika ile Bunduki na kisha kwa maksudi kabisa akaiacha palepale ambapo mama yule aliamini kuwa ni sirini sana. Sasa yule mama akajiamini kabisa kuwa alikuwa na silaha na alikuwa anaenda kutumaliza.

Baada ya kucheka kwa takribani dakika moja hatimaye Geza alimvagaa yule mama, akaichukua ile bunduki kisha akampiga na kitako mdomoni yule mama akapasuka.

“Dogo piga picha!! Nasema piga picha za kutosha kabisa… na wewe mwanamke itazame kamera vizuri na ikiwezekana jitahidi utabasamu!!!” Geza alitoa maelekezo, nikataka kucheka yaani amembamiza na kitako cha bunduki amepasuka halafu anamwambia eti ajitahidi kutabasamu. Nikaichukua kamera yake ndogo iliyokuwa pale ndani. Nikampiga picha yule mama aliyekuwa amepasuka vibaya sana!! Na vile alikuwa ni mwarabu basi zile damu zilimfanya aonekane kama kuku aliyechinjwa!!

“Baisar yupo wapi? Na Latipha yupo wapi. Nahitaji uongee Kiswahili kilichonyooka!! Ole wako sasa uende kinyume” Geza alimuuliza yule mama kwa ghadhabu..

“Au usinipe jibu nitalitafuta mimi mwenyewe nikikuruhusu kunijibu utanipotezea muda we na huyu Dogo hamna tofauti kabisa katika kujibu maswali!!” alimkatisha yule mama alipotaka kujielezea. Na baada ya hapo alimuacha yule mama akiwa pale ameketi damu ikiwa imemchafua vibaya sana. Akatembea kidogo kisha akasimama na kugeuka.

“Yaani ulitaka kufyatua risasi ili utuue si ndo maana yake au?…. halafu nilisahau kabisa kama ulitaka kutuua dah! Yaani zingekuwemo risasi swasa hivi sisi wawili maiti halafu wewe unacheka si ndo hivyo madam!… anyway hayo tuachane nayo kwanza wanadamu tumeumbiwa kufanya makosa hivyo tunatakiwa kuwa tunasameheana. Maana najua hata wewe utanisamehe tu wakati ukifika!!” Geza akasita kidogo wakati huo ilikuwa ni saa kumi na moja jioni!!

Geza alinieleza kuwa huo ulikuwa wakati muafaka kabisa wa kutoka ili kusikiliza ni kitu gani kilikuwa kinaendelea mtaani.

Alimchukua yule mwanamke na kumfungia katika chumba kimojawapo akafunga kwa nje kisha tukaondoka. Hatukuondoka na gari safari hii tulitembea kwa miguu hadi tulipofika internet café Geza akasema tuingie hapo. Geza akachukua ile kamera na kisha kuchomeka waya na kuitafuta ile picha ambayo nilimpiga yule mama akiwa amepauka.

“Kesho kinanuka mjini hapatakalika!! Yaani mpaka aseme poo!! Hivi na wewe ulicheza hiyo michezo ya kusema poo!! Au ulikuwa haujazaliwa” Geza alinieleza kwa sauti ya chini wakati huo akiituma picha mahali alipojua yeye mwenyewe, mimi nikawa mtazamaji tu!!.

Alipomaliza akaifuta ile picha kisha tukaondoka!!

Kweli kilikuwa kizungumkuti palipopambazuka, ile picha ya mwanamke wa kiarabu akiwa amepasuka vibaya na kutapakaa damu ilisambaa kila kona, magazeti yakaandika na runinga zikaonyesha!! Habari kubwa zaidi iliyotapakaa ni kutekwa kwa mke wa Baisar na kisha kupewa mateso makali sana.

Mtekaji akatajwa kwa anuani ya barua pepe aliyotumia kutuma picha zile. [email protected] , ilifurahisha sana kuitamka!! Hata magazeti yaliandika katika mfumo wa kukiri kuwa mtekaji alikuwa ana masihara sana.

Sisi tuliipata taarifa ile tukiwa pamoja na mke wa Baisar. Geza akaanzisha visa vyake upya.

“Yaani Alipotekwa Latipha wetu hakuna aliyeandika na wapo wengi tu wametekwa hakuna anayeandika, kwa sababu wao ni masikini basi habari yao haina mashiko hata kidogo!! Eti umetekwa wewe kila mtu anataka kujua upo wapi? Mimi napenda waukute mwili wako huko ufukweni ukiwa umekufa au we unaonaje eeh! Iwe hivyo ili waandike vizuri kabisa?” Geza alimuuliza yule mama huku akitabasamu kana kwamba lile ni swali la kawaida kabisa. Mama yule alijitahidi sana kujitetea lakini Geza wala hakuonyesha dalili ya kushawishika.

“We mwanamke, lengo la kukuchukua wewe ni moja tu. Nisikilize kwa makini sana, naomba uelezee mambo yote ambayo jamii haijui kuhusu Baisar. Sasa ole wako usijibu ama ukaanza kuzungusha maneno.”

“Nasema keli, keli tupu. Baisar nausa dawa kulevya, Baisar nauza toto kike, Baisar naiba, Baisar na… na…. hivyo tu” alijibu yule mwanamke.

Geza akatabasamu kisha akamuuliza ni kitu gani kilitokea hadi Baisar akamchukua Latipha!!

Yule mama akababaika kidogo kisha akasema kuwa hamjui Latipha. Geza akiwa katika utulivu mkubwa akauendea mfuko fulani akatoka na picha na kumrushia yule mama.

“Huyo ndiye Latipha bila shaka umewahi kumuona.”

“Nimewai ona hii.” Alijibu!!

“Elezea nini kinaendelea kwa huyu mwanamke!! Kupatikana kwa mwanamke huu ndiyo nafasi yako ya kutoka salama katika mikono yangu la si hivyo nakuua na nitakuua kwa mateso sana mama. Utakufa kwa mateso makubwa sana”

Yule mwanamke alitulia kwa sekunde 30 ama zaidi kisha akaelezea jambo ambalo lilitushangaza sana.

Licha ya kwamba Kiswahili chake kilikuwa kibovu sana lakini bado aliweza kueleweka.

Baisar licha tu ya kuuza madawa ya kulevya alikuwa na tabia ya kuwatumia wanawake. Wanapasuliwa matumbo dawa zinaingiza humo kisha safari ya kwenda kwa mteja alipo. Mara nyingi sana inakuwa kwa wale wateja wa nje ya nchi.

Baisar hufanya tabia ya kuwalaghai wasichana na kuwanao katika mahusiano na baada ya hapo huwaingiza katika utumwa huu. Utumwa mbaya kabisa.

Maelezo ya yule mama yakanifanya niione sura ya Latipha mbele yangu. Mke wangu wa ndoa kabisa anafanyiwa mambo ya kinyama namna hii.

Looh!! Nikajisikia kumtamani sana huyo Baisar ili niweze kumwadabisha kwa yote mabaya ambayo huenda alifanya kwa mke wangu. Lakini nilijiapiza kuwa kama huyu bwana alithubutu kumpasua mke wqangu na kumuimngiza katika hiyo biashara basi ama zangu ama zake!!

Geza aliishia tu kunitazama asiseme neno lolote!!

Lakini ile simulizi ilikuwa imemfanya awe na simanzi kubwa sana.

“Dogo kesho tutaenda kuonana na huyu bwege!!” Geza aliniambia huku akisimama na kutembea kwenda huku na kule.

GEZA aliposema tuondoke sikujua atafanya nini kuhusiana na Yule mwanamama wa kiarabu pale ndani.

Wakati tunaondoka akanivuta kisha akaninong’oneza.

“Unakumbuka nilimwambia Yule bwege kuwa ninazijua njia themanini na nne za kuua…..” akanisubiri nijibu, nikatikisa kichwa kumuunga mkono!! Akaendelea.

“Pia nafahamu njia kama nane au kumi hivi za…. Zaa…” hakuendelea kuzunguka.

Ghafla akageuka na kufanya kitendo ambacho siwezi hata kukielezea ukanielewa lakini lilikuwa pigo fulani aaargh! Natamani basi ningekuwa najua kuelezea walau nikueleze nawe ujue. Lakini kikubwa ni kwamba Yule mama alipiga kelele kidogo kisha akanyamaza kimya!!

Geza akanigeukia kisha akaimalizia ile kauli yake aliyoiacha ikielea angani!!

“Nafahamu njia nane za kumfanya mtu asisikilize mnachozungumza kwa muda!!” akaniambia huku akitabasamu.

Kweli Yule mama hakuwa akisikia lolote lile tena!! Alikuwa amepoteza fahamu.

Tukaondoka Geza akaufunga mlango huku akijiamini kabisa!!

Ama kwa hakika Geza alikuwa ni funga kazi.

“Nilikwambia kuwa leo tunaenda kwa bwana Baisar kumsalimia!!”

“Nakumbuka bro!!” nilimjibu huku moyo wangu ukiwa hauna amani kabisa, yaani mtu tumemteka mke wake halafu leo hii eti tunaenda kumsalimia. Lakini ile kukumbuka kuwa Geza yu makini katika mipango yake hofu yangu i8kapungua na kuamini kuwa kila kitu kitaenda sawa kabisa.

“hahahahahah! (Geza akacheka) eti bro, nani bro wako, we vipi wewe we umeoa kabisa unaniita mimi bro wakati sijaoa hebu acha kukataa ukubwa bro!!” Geza alizungumza huku akicheka sana, nikakiri katika akili yangu kuwa Yule bwana alikuwa na matatizo ya akili… kauli hii ikanifunga sana kwa sababu awali nilishakiri kuwa Geza alikuwa na akili sana kunizidi.

Sasa kama ana matatizo ya akili mimi nitakuwa na nini??

Sikuuliza nikabaki kimya kisha na mimi nikatabasamu!!

Tabia za Geza zilikuwa zimeanza kunikolea!!! Nikawa naufurahia uwepo wake jirani yangu.

Tulifika hadi duka moja kubwa sana la spea za magari. Awali nikadhani kuwa Geza anaenda kutazama spea za gari lake akaniambia niingie pale dukani kisha niulizie tairi za Toyota.

Nikatii amri nikaenda kuulizia nikatajiwa bei nikaenda kumweleza Geza.

Akaniuliza iwapo kuna mtu mnene mfupi ana ndevu nyeupe nimemkuta humo ndani!!

Nikajibu kuwa nimeona mtu kama huyo!!

“Safi sana tunaanzia hapa yaani atakonda yeye na ukoo wake” Geza alizungumza peke yake huku akitupa ngumi hewani katika ishara ya kushangilia.

“Twende!” aliniambia nikamfuata.

Hii ilikuwa mara ya kwanza Geza kunikumbusha kumfuata!!!

Tukaingia hadi mahali walipokuwa wanasafisha picha, Geza akatangulia nami nikafuata kwa nyuma. Akaingia na kuisafisha ile picha inayomuonyesha mke wa Baisar akivuja damu baada ya kuwa amemtandika vibaya na kitako cha bunduki!!!

Yule bwana msafisha picha alikodoa macho sana alipoiona ile picha aliyotakiwa kusafisha.

Nikamgeukia geza nikakuta anatabasamu!!! Tulipogonganisha macho, akakwepesha na kumtazama Yule anayetusafishia!!!

“Ebwana huyu mama unamfahamu!!” hatimaye Geza alimuuliza yule jamaa aliyekuwa amehamaki mdomoni mwake bado alionyesha tabasamu Geza..

“Am…a… hapana bro!” alijibu huku akisuasua.

Geza akacheka sana kisha akazungumza.

“We jamaa wa wapi wewe sasa, upo mjini humjui huyu mwanamke, si mke wa Baisar huyu au…. Ok! Tuprintie sisi tuondoke!! Kama haumjui shauri zako” alimaliza kuzungumza kisha akashusha sauti yake akawa kama anamnong’oneza Yule bwana.

“Yaani huyu mama kakutana na wahuni huko wamemuadabisha aisee hizi picha ukienda kuuza gazetini zinalipa balaa….”

Hakusubiri ajibiwe. Akaingiza mada nyingine!!

Tukapatiwa picha yetu tukaondoka!! Tulipotoka nje nikaona ni vyema nimshauri jambo Geza nilihisi kama kuna umakini fulani alikuwa ameupoteza.

“Sasa Geza we huoni kama jamaa atatuharibia mipango yetu!!”

“Hapana hatatuharibia ila atanogesha zaidi!! We ngoja!! Haka kamchezo ukijua tu kukacheza utafurahia sana” akanijibu kisha akataka kuishia hapo lakini akajikuta akiendelea tena.

“Dogo!! Yule boya hana kifua kabisa, ninavyoongea na wewe hapa tayari keshaanza kuwatangazia wenzake hiyo habari pale ofisini kwao. Halafu sasa alivyokuwa mjinga amejifanya ameifuta ile picha wakati hajaifuta anadhani Geza mimi sijui maana ya Delete… Yes … No…. kabofya Delete halafu kabofya No (Geza akacheka sana)…. Najua dogo unajiuliza maswali mengi ila utayapata majibu lakini niamini mimi Baisar atakonda mpaka kanzu itampwaya, yaani atakonda hadi kichwa kile kibalaghashia hakitakaa vizuri!!!” Geza alimaliza kuzungumza. Mimi nikawa msikilizaji tu!!

https://2c44d75308dfc189e316821bbf7f9432.safeframe.googlesyndication.com/safeframe/1-0-40/html/container.html

Tulipotoka pale tukaenda mahali alipojua yeye mwenyewe!! Alikuwa ametembea na begi lake. Safari hii hakuniaga kwa maneno bali ishara akanambia nimsubiri pale nje.

Akaingia mahali akachukua muda mrefu sana baadaye akatoka akiwa amebadilika sasa alikuwa Yule Khajat bint Hemed!!

Geza alikuwa amejitanda manguo yake ya kike!!

Akafika na kunipita nikamfuata nyuma hadi akaifikia bajaji akapanda nami nikapanda!!

“Tupeleke Mbezi Afrikana (Anaongea kwa kubana pua kikekike)”

Dereva akaondoa hadi tukafika Geza alipoelekeza.

Tukashuka na kisha moja kwa moja tukaelekea mahali Geza alipokuwa ameahidi!!

Nyumbani kwa Baisar!!

Tulifika na kupokelewa na mlinzi getini!!

Geza hakuzungumza sana badala yake akamuachia Yule mlinzi bahasha iliyokuwa na ile picha kisha akataka kuondoka Yule mlinzi akataka kuhoji huku akizuia asitoke getini!!

“We mbaba vipi kwani?” Geza katika sauti yake ya kike!!

“Mmeleta huu mzigo kwa nani? Na hamjajitambulisha majina yenu!!” alichimba mkwara. Mkwara ukanitetemesha nikaona mambo yanataka kuharibika.

“Khalfani hili jibaba vipi au nikuonyeshe njia nyingine tena…” aliniuliza. Nilitamani kucheka kwa ile sauti yake lakini eneo halikuruhusu.

Yule mlinzi akamsogelea Geza akiamini kwamba kweli ni mwanamke!!

Hilo likawa kosa kubwa sana.

Alipigwa ngumi moja kali usoni!! Nikamwona jinsi anavyolegea na kutua chini.

“Dah! Jela bwana sijui nirudi tena?? Kutamu kweli” Geza sasa akaongea sauti yake ya kiume!!!

Na hapo tukafungua geti ili tutoke!!

Ile tunapiga hatua mbele ili kutoka, mara gari ya polisi ikasimama kwa fujo na kutimua vumbi vibaya mno mbele ya nyumba ya Baisar!!

Binafsi sikuwa nimejipanga kukabiliana na jambo lile hata kidogo!!

Sijui kwa Geza!!

Nikaanza kutetemeka!!!

Baada ya ile gari kusimama wale askari walikimbia na kuanza kubisha hodi katika geti la nyumba iliyokuwa inafuata.

Nilimsikia Geza akishusha pumzi kwa nguvu sana, nikatambua kuwa Geza alikuwa ametetemeshwa pia kutokana na tukio lile.

“Dogo tupotee bila papara… tembea kama hakijatokea kitu. Wamejichanganya geti hao….” Alinisemesha kisha akaanza kuondoka taratibu nami nikawa pembeni yake tukaondoka hadi tukapotelea mbali upesi Geza akanisihi nisiambatane naye kila mmoja apite kivyake kisha tutakutana nyumban. Hakusubiri jibu langu akatoweka nami nikatoweka.

Huo ukawa mwanzo wa kujua nini maana ya mkuki kwa nguruwe kwa mwanadamu mchungu!!!


Geza ulole!! Nikiwa naye bega kwa bega alikuwa ameamua kumfunza adabu Baisar hii ikiwa ni kulipa visasi viwili na kisha kuujua ukweli ni upi.

Baada ya kukoswa koswa na lile tukio la kukamatwa na askari, siku zilizofuata mtaalamu wa kuchora tayari alikuwa amemohoji Yule bwana aliyetusafishia picha wakafanikiwa kuichora picha ya Geza Ulole. Ikasambaa magazetini, Yule mlinzi aliyepigwa ngumi moja na kupoteza fahamu naye akahojiwa na kuchora picha ya Geza ulole akiwa ni mwanamke akiwa amevaa hijabu.

Bahati iliyoje picha yangu mimi hakuna mahali ilipochorwa!!

Bila shaka wao walimtilia maanani zaidi Geza na sio mimi.

Jambo hili kila mmoja alilifurahia!!

Lakini sasa tulikuwa tunacheka sana na hapo nikaijua maana ya Geza kumfanya Yule bwana aikariri sura yake.

Geza wa sasa hakuwa na ndevu hata moja na kichwani hakuwa na nywele hata moja kama awali.

Geza akaitazama picha iliyochorwa magazetini na kujihakikishia kuwa hakuwa akifanana na Yule mtu!!

Hapo safari ikaanza rasmi!!

Baada ya siku tano za kumteka Yule mama huku akiwa amehifadhiwa katika namna ambayo hawezi kujulikana popote hatimaye Geza alinyanyua simu na kumpigia Baisar!!.

He! Kumbe mkwara wa Geza haukuwa kwangu tu, Geza alikuwa anaweza kumchimba mkwara kila mtu.

Kule Mwanza mtu kama huyu wanamuita Mtabe!!!

Baada ya simu kuita kwa muda mrefu ilipokelewa na binti!! Geza akaweka spika za nje!!

“Mpe mwenye simu tafadhali….” Alizungumzakwa utulivu.

“Nani veve kani” sauti ikahoji.

Geza akafanya kosa la maksudi!!

Akiwa na simu bado sikioni alimgeukia mke wa Baisar na kumuuliza.

“Samahani kwa kiarabu wanasemaje kuwa mimi ni Mtekaji!!” Yule mwanamke akajibu kuwa hajui. Geza akaendelea, “Na nikitaka kusema mpe huyo mjinga simu nasemaje vile ujue nimeanza kusahau kiarabu sijui kihindi kile!!” Geza aliendelea kufanya makosa ya maksudi. Yaani alizungumza kwa sauti ya juu ili wale wa upande wa pili wamsikie

Mchakato ukawa unasikika upande wa pili, sijui Yule dada aliyeuliza veve nani alianguka au vipi. Maana purukushani zilikuwa kubwa sana.

Geza akawa anacheka!!

“Nani we nani nasema…” ikasikika sauti kutoka upande wa pili. Geza akanyanyua mabega yake juu katika namna ya majivuno. Kisha akajibu.

“Mimi mume wa… mume wa…” akasita akamgeukia Yule mwanamke na kumuuliza, “Unaitwa nani mpenzi wangu?”

“Mozah Balaghash!!” alijibu Yule mama…. Hapohapo Geza akarejea kwenye simu bila kujalisha kuwa upande wa pili kuna chochote ulikuwa unauliza.

“Ni mimi mume wa Mozah!” akajitambulisha Geza kisha akaleta ule ukichaa wake ambao mimi nilikuwa nimeuzoea tayari.

“Kwani wewe nani mwenzangu unanipigia simu usiku huu nipo na mke wangu Mozah tunakula raha zetu. Ni kwanini mnakuwa hamtambui nini maana ya usiku eeh!!” Geza akahoji. Wakati ni yeye alikuwa amepiga simu.

Hakika Geza alikuwa amepagawisha!!

Upande wa pili ukabaki kuhangaika bila neno lililonyooka.

“Yaani upo na mke wangu mwanaharamu wewe, nasema hivi ninakuja kukuua mimi mwenyewe kwa mkono wangu” jamaa akachimba mkwara.

Geza naye akajibu kwa mkwara!!

“Hiyo mikono yako kuliko kuniua mimi kwa nini isije kufanya kazi ya kubeba maiti ya huyu mke wangu maana nina mpango wa kumuua baada ya kukata simu hii.” Ule mkwara ukamwingia Yule bwana, akabaki kujiumauma……

Na mara Geza Ulole akabadilika kabisa.

“Sikiliza wewe mpuuzi, muuaji, mnyanyasaji, unayewakosea heshima mama na dada zetu…. Wakati huu nakuhakikishia kuwa hautakuwa na pa kuchomokea. Najua unanijua vizuri sana lakini nataka unijue zaidi ya unijuavyo, sijui nini maana ya kutisha nakuhakikishia kuwa safari hii ni aidha uikimbie nchi ama la uyatangaze maovu yako mbele ya watu upatwe na fedheha lakini uwe huru!! Lakini ukiendelea kubaki katika nchi hii bila kujisalimisha mbele ya sheria nakuhakikishia kuwa hautaweza kuondoka tena badala yake yataondoka maiti yako. Una pesa sawa! Umezifanya kuwa fimbo kwa wanyonge, biashara ya madawa ya kulevya umeona haikutoshi, unachukua wake zetu utakavyo kisa una pesa, Baisar…. Baisar ikiwa vyema basi zigawe pesa zako kwa ndugu zako kwa sababu haziendi kukusaidia katika vita hii. Halafu nimesema vita nimekumbuka kitu, huwezi amini hamna kitu sipendi kama kupigana vita kwa siku nyingi sana. Mi nataka vita fupi tu. Siku tano zinatosha kabisa, vita vya kupigana miaka kumi walifanya wazee wetu!!

Sasa uamuzi upo mikononi mwako, nikiona magazeti ninayoyaamini kuwa hayayumbishwi na pesa zako yameandika kuwa umekiri kuwa una danguro na unauza wasichana wasikini bila hiari yao, unawachana matumbo yao na kuweka madawa ya kulevya kwa masilahi yako mwenyewe…. Hapo nitakusamehe.

Lakini vinginevyo!! Nitaanza na huyu mkeo ambaye lenu moja, kisha utafuata tena kwa mateso makali. Huwa sina tabia ya kujisifia!!

Ole wako kesho nisikie polisi wana haya mazungumzo kati yetu!!

Ili huyu mwanamke asije kuoza huko nakufanyia msaada mmoja, miguu yake yote miwili utaikuta koko beach, vilivyosalia utavikuta bagamoyo stendi ya mabasi!!!

Uwe na usiku mwema bosi tutachekiana kesho kama vipi!!” lile likawa neno la mwisho akaikata simu!!

Aisee!! Hata kama ningekuwa ni mimi ndo Baisar pale lazima haja kubwa na ndogo zing’ang’ane kutoka kwa wakati mmoja!!

Geza alikuwa na mkwara madhubuti!!

Mkwara ulioshiba haswa!!

Baada ya kukata ile simu akamgeukia mke wa Baisar aliyejitambulisha kwa jina la Moza!

“Niliyomwambia mumeo sijamtania… aah! Ok tuzungumze kirafiki kabisa, ikiwa mumeo atavunja masharti, unapendelea hiyo miguu niliyosema nitakukata niiweke eneo gani pale koko beach ili iwe rahisi kwake kuiona….. na huko bagamoyo kama una kauenyeji kidogo, nikiweka tumbo lako pale stendi vipi itakuwa rahisi kuonekana au?” Geza alimuuliza Yule mama safari hii nilishindwa kujikaza nisicheke!!

Yaani Geza dah!! Halafu ye wala hacheki hata kidogo zaidi ya lile tabasamu lake la kila siku!!

Yule mama hakujibu kitu akaanza kulia huku anazungumza kiarabu.

Ebwanaeeh! Eti hilo likawa kosa.

Geza akasimama wima, akaanza kuzunguka huku na kule kisha akaanza kuaniambia mimi.

“Dogo…dogo yani… aah! Umemsikia huyo mama alivyoongea hapo kiarabu yaani anasema mimi na wewe mama zetu Malaya…. Dogo unamuangalia tu… eeh! Unamuangalia anatutukana!! Mi namuua namuua nasema!!” Geza alitaka apite ili amsulubu Yule mama, nikalazimika kumzuia kwa sababu ningemwachia pale huenda angeua kweli.

Sasa Geza na kiarabu wapi na wapi!! Kama sio uonevu!! Nilijiwazia.

“Mimi jatukana ntu jatukana kabisa…jatukana jama!! Jatukana!!” Yule mama akawa anajitetea.

Sauti yake ya huruma ikaniumiza sana nikageuka na kumtazama, alikuwa na umri sawa tu na mama yangu!!!

Nikaendelea kumdhibiti Geza!! Japokuwa nilijua Yule bwana hakawii kunigeuzia kibao mimi!!!

Lakini ilikuwa heri kujaribu tu!!

ITAENDELEA

Fedheha Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment