Kiguu na Njia Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
*********************************************************************************
Simulizi : Kiguu Na Njia
Sehemu Ya Kwanza (1)
yeyote mwenye
umri wa baba akilia, iwe sirini au hadharani. Kitendo cha mwanamume kutokwa na machozi, iwe kwasababu ya maumivu au majonzi, hakikupata kukubalika katika jamii yetu.
Nakumbuka nilipokuwa mtoto mdogo, wa miaka mitatu au minne hivi, nilipojikwaa na kuumia au kupigana na wenzangu nikalia. Baba alikuwa akinicharaza bakora huku akisema, “Mwanaume gani wewe unalia? Mwanaume halii!”
Babu yangu pia, mzee Karimanzila, aliwahi kunicheka sana kwa suala hilo la kulia. Siku hiyo mtego nilioutega mwituni ulikuwa umemnasa kanga mkubwa sana. Rafiki yangu mmoja tuliyekuwa naye porini aliniita kwa sauti kubwa kuniarifu juu ya kanga huyo. Lakini nilipofika kwenye mtego huo nilimkuta Katato, ambaye alituzidi sana kwa umri na umbile, akimfungua kanga huyo kwa madai kuwa ni mtego wake. Tulibishana naye sana. Kwa kunikomoa Katato alimwachia kanga wangu, ambaye aliruka na kutokomea zake mwituni. Nilijaribu kupigana naye lakini akanizidi nguvu na kunitia ngeu katika paji la uso. Nililia njia nzima hadi kijijini. Babu
aliposikia habari hizo aliniita na kunidhihaki kwa kusema, “Ukiona mwanaume analia ujue na roho ya kike. Angestahili kuvaa gauni badala ya kaptula.”
“Lakini yule alikuwa kanga wangu wa kwanza. Nimekwishanasa njiwa, hondohondo na kware. Leo
nimebahatika kumnasa kanga. Ningefurahi sana kumchinja na kumla!” Nilimjibu babu.
Babu alitabasamu kidogo kisha akasema, “Kanga elfu moja utawala. Tatizo ni hayo machozi. Machozi ya mwanaume yanatakiwa kuwa adimu sana. Leo jioni uje nikusimulie kisa cha mwanaume aliyepokonywa mke kwa ajili ya machozi.”
Nilizipenda sana hadithi na simulizi za babu. Kwa ujumla, kijiji kizima na hata vile vya jirani vilipendelea sana kuja kwetu kumsikiliza babu akisimulia matukio mbalimbali yaliyomkuta katika maisha yake. Hadithi zake zilijaa miujiza na maajabu kiasi kwamba baadhi ya watu walidiriki kumwita ‘mwongo’ au ‘anatia chumvi’. Lakini yeye aliwacheka watu wa aina hiyo na kuwaambia, “Hamjaiona dunia. Dunia yenu ni kijiji hiki pekee. Mimi nimeizunguka. Nimefika upande wa pili wa dunia!”
Hiyo ilikuwa kauli yake ya mara kwa mara, kauli ambayo iliongeza utamu wa simulizi zake. Hakika babu mwenyewe alikuwa hadithi, tena hadithi ya kusisimua kuliko zile simulizi zake. Inadaiwa kuwa, utotoni, akiwa na umri wangu, alitoweka kijijini hapo kama mzuka. Alitafutwa kwa siku kadhaa bila mafanikio. Watu walidhani kuwa ameliwa na simba au mamba. Lakini alipoibuka miaka kadhaa, baadaye, akiwa na simulizi tele za ‘kuizunguka dunia,’ watu walibadilika na kuamini kuwa alichukuliwa na mashetani ya chini ya bahari.
Pamoja na kuzipenda hadithi zake, pamoja na kiu ya kusikia kisa hicho cha ‘machozi ya mwanamume’ bado hasira dhidi ya kanga wangu aliyepeperushwa kwa
makusudi na maumivu toka kwenye ngeu ya paji la uso kwa mara ya kwanza vilinifanya nikatae kwenda kumsikiliza. Hivyo, kumwona baba akilia lilikuwa jambo jipya kabisa katika maisha yangu. Alikuwa kaketi juu ya gogo, mikono yake yote miwili ikiwa imekishika kichwa chake huku macho yake yakitazama mbele yake, ingawa ilikuwa dhairi kuwa haoni kitu chochote kutokana na wingi wa machozi. Nilijikaza na kumsogelea kwa nia ya kumuuliza kulikoni. Lakini mara nilipomfikia ushujaa ulinitoka. Nikajikuta nikiambulia kukaa ubavuni mwake, juu ya gogo lilelile. Kwa mshangao wangu, baba alifanya kitu ambacho hakupata kukifanya huko nyuma.?
Alinikumbatia kwa mkono wake mmoja huku mkono wake wa
pili ukifuta machozi ambayo yalimiminika kwa wingi zaidi. “Mwanangu!” nilimsikia akiniita kwa sauti ndogo
yenye kigugumizi.
Sikumbuki kama niliitikia au la.
Wala yeye hakuzungumza neno jingine.
Nilipopata nafasi nilijichopoa toka katika mikono yake na kuingia ndani kwa dhamiri kuu mbili. Dhamiri ya kwanza ilikuwa kuficha machozi, ambayo mie pia yalianza kunilengalenga. Dhamiri ya pili ikiwa kumpata mama ili anifafanulie kisa na mkasa wa hali hiyo.
Mama hakuwepo. Wala hakuwepo mtu wa kumuuliza kwani mimi nilikuwa mtoto pekee katika familia hiyo. Na nilipatikana kwa shida baada ya mama na baba kuhangaika kwa waganga kwa zaidi ya miaka kumi. Hatimaye, walimpata mganga mmoja aliyebobea, ambaye alimtibu mama kwa kuchanganya mitishamba aina ya Mhusu na Mnywanya ambayo
mama alitakiwa kunywa kwa siku mbili. Siku chache baadaye alitangaza kuwa yu mjamzito. Hapo mganga alimbadilishia dawa na kumnywesha mti uliotajwa kuwa Sagamba mara kwa mara hadi nilipozaliwa.
Miaka mingine kumi tayari ilikuwa imepita bila dalili za kupatikana mdogo wangu. Mganga wake alishakufa na hakupata kumwonyesha mtu yeyote miti ile. Hivyo, mimi nilikuwa kama mboni ya jicho kwa baba na mama, ingawa hawakutaka kamwe nijisikie hivyo.
Wakati nikihangaika bila mafanikio kuwaza na kuwazua namna ya kumnyamazisha baba, mara nilimwona mama akirudi nyumbani, huku kafuatana na babu. Kumbe yeye pia alikuwa amehangaika sana kumtuliza baba na kumuuliza kulikoni bila mafanikio. Ndipo lilipomjia wazo la kutembea mwendo wa zaidi ya dakika ishirini hadi kwa babu ambaye kwa bahati alikuwa nyumbani.
Kama kawaida yake, tofauti na watu wengine wote kijijini hapo, babu alikuwa amevaa kaptula yake nyeupe, shati jeupe, soksi nyeupe na viatu vyeusi. Akiwa miongoni mwa watu wengi waliovaa lubega za kaniki, miguu yao ikikanyaga chini, siku zote babu alionekana mtu wa aina ya pekee.
“Kuna nini?” babu alimuuliza mwanawe akiwa ameketi pale nilipoketi mimi muda mfupi uliopita. “Kuna nini?” alirudia na kuongeza, “Nasikia tangu umetoka kuonana na Mwami umerudi unalia. Kuna nini?”
Baba hakujibu mara moja. Alimtazama baba yake kwa muda kabla hajainuka taratibu na kumshika babu mkono. “Ni mambo mazito yaliyonipata leo. Twende faragha nikusimulie, ingawa nimekula kiapo cha kutotoa siri hii nje.”
Walikwenda pembeni, mahala ambapo masikio yangu na ya mama yasingeweza kusikia wanachozungumza. Hapo waliteta kwa muda mrefu, baba akizungumza babu akisikiliza. Baadaye, nilimwona babu akicheka na kuzungumza kwa muda kabla hawajarudi na kuketi tena kwenye gogo. Mama alipoona wametulia, aliingia ndani na kuwaletea kibuyu cha togwa ya mahindi. Waliinywa taratibu huku wakiwa kimya.
Nadhani togwa hii ilikuwa kali kwani baada ya muda mfupi nilimwona baba akichangamka huku babu akizungumza kwa sauti ya juu kidogo.
Sikubahatika kupata mtiririko wa maongezi yao. Lakini mawili matatu niliyoweza kudonoa katika matamshi yao yalinifanya nipate hisia kuwa nilihusika kwa njia moja au nyingine na majonzi yao. Imani hiyo ilijengeka zaidi pale nilipomsikia babu akisema kwa sauti ya juu kidogo, “Mjukuu wangu mie! Nadhani mwanangu hunifahamu hata kidogo. Haiwezekani!”
Baba: Lakini wamesema itakuwa siri. Huenda hata mimi mwenyewe hawatanishirikisha.
Babu: Nasema haiwezekani. Enzi za utukufu na uhuru wa kufanya chochote wanachotaka zimepita zamani. Wakithubutu nitahakikisha wananyongwa.
Baba: Watanyongwa kabla au baada?
Babu: Hawawezi kuthubutu!
Mmoja wao alinitupia jicho. Wakabaini kuwa nafuatilia maongezi yao. Wakapunguza zaidi sauti zao na kuendelea kunywa.
Usiku huo babu alinichukua nikalale kwake. “Twende zetu mjukuu wangu. Leo nina hadithi nyingi za kukusimulia, hadithi za kweli ambazo sijapata kumsimulia mtu yeyote.”
Nikiwa na hakika kuwa kwa kiasi fulani mwaliko huo ulitokana na kisa au mkasa nisioufahamu, wa hapo nyumbani, niliafiki kufuatana na babu hadi kwake. Bibi alinipokea kwa furaha huku akiniita ‘mume’ wake. Akanipa kata kubwa iliyojaa togwa tamu, tofauti kabisa na ile waliyokunywa babu na baba. Baada ya hapo nilipewa ugali na pande kubwa la nyama ya nyati. Babu alikuwa mwindaji, bibi akiwa mkulima.
Nyumba yao katu haikupata kupungukiwa na chakula. Nilikula hadi nikavimbiwa, kabla sijatandikiwa mkeka na bibi kunipa moja ya kaniki zake nitumie kama shuka. “Tutazungumza kesho, leo pumzika mapema.” Babu?
aliniambia alipoona dalili za usingizi katika macho yangu.
* * *?
Hakuna mtu aliyeujua umri wa babu, ikiwa pamoja na yeye mwenyewe. Ilikadiriwa tu kuwa alizaliwa miaka ya 1850 au baadaye kidogo, kwani wakati huo zilikuwepo habari nyingi za nchi kuvamiwa na watu weupe wenye mianzi inayotoa moshi wenye uwezo wa kuua tembo hata akiwa mbali. Watu hao walidaiwa kutembea hovyo katika misitu na kushangaa kwa kila walichokiona.
Miongoni mwa watu hao alitajwa sana mtu mmoja anayeitwa Hanning Speke na mwenzie Richard Burton. Hawa walitembea hadi maeneo yetu ya Buha na kupita na kushangazwa sana pale walipoliona ziwa kubwa la Tanganyika ambalo lilitenganishwa au kuunganisha nchi yetu na zile
za Kongo na Burundi. Inasemekana pia kuwa walitembea porini kwa miezi kadhaa hadi walipofika ziwa Lweru, ambalo walilibadili jina na kuliita Victoria huko katika nchi ya Wahaya na Wasukuma.
Wakati huohuo zilikuwepo habari za mtu mwingine aliyeitwa David Livingstone aliyeweka makazi yake Ujiji na akafia nchini Zambia. Wasaidizi wake maarufu, Susu na Chuma wanaelezewa kuwa waliibeba maiti yake hadi upande wa pili wa nchi, pwani ya Bahari ya Hindi ambako ilisafirishwa hadi kwao Ulaya.
Niliyajua yote hayo kutokana na simulizi za babu mwenyewe. Katika enzi hizo alikuwa tayari ana akili zake, nguvu za kutosha na uwezo wa kuanzisha mji wake mwenyewe, ingawa alikuwa hajaoa. Na ni wakati huo aliopatwa na ule mkasa wa aina yake, mkasa ulioacha gumzo hadi leo, na aliporudi, kimiujiza vilevile kama alivyoondoka, akiwa na simulizi za ajabuajabu, gumzo likaongezeka.
Moja ya maajabu aliyokuja nayo ni mavazi. Nguo zake zilikuwa sawa na zile zilizodaiwa kuvaliwa na watu weupe. Na siku zote alihakikisha kuwa ni safi.
Ajabu ya pili aliyoileta babu ni taarifa kuwa watu weupe kumbe siyo kabila moja bali ni watu wa makabila mbalimbali, wanaotoka nchi mbalimbali na kuzungumza lugha mbalimbali. Alizitaja nchi kama Uingereza, Ujerumani, Sweden, Ureno na nyinginezo kuwa ni nchi tofauti, zenye utawala tofauti na lugha tofauti kabisa.
Ajabu ya tatu, na pengine kubwa zaidi ni pale alipodai kuwa alikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali za makabila hayo, kama Kiingereza, Kijerumani na Kisweden. Kwa hilo watu walielekea kutomwamini. Lakini pale Wabelgiji
walipovamia Buha, na kuzunga wakitokea Kongo, miaka ya 1916, babu alidhihirisha uwezo wake wa lugha kwa kuzungumza na mmoja wa makamanda wao waliopotea njia na kujikuta wamefika kijijini kwetu. Wageni hao walishangaa sana kumkuta mtu anayezungumza Kiingereza ambayo ni lugha ya jirani zao katikati ya pori kama hilo. Walijaribu kumshawishi babu afuatane nao ili awe mkalimani wao lakini alikataa katakata kwa kusema, “Nimekaa kwao na kukataa kuwa mtumwa wao, vipi nikubali kuwa mtumwa wao katika nchi yangu mwenyewe?”
Umaarufu wa babu kwa lugha uliongezeka maradufu miaka mitano baadaye, pale Uingereza ilipochukua madaraka ya utawala wa Tanganyika toka kwa Mjerumani ambaye alikuwa pia ameupokonya toka kwa Wabelgiji katika eneo hilo la Buha. Mwaka 1931 chifu, ambaye tulimwita Mwami wa Heru juu alifariki. Amri toka kwa Gavana G. S. Symes ilimtaka DC kuteua ‘Mwami’ mpya. DC akaamua kupata mawazo ya wananchi kabla ya uteuzi wake. Ujumbe wake ulipofika kijijini kwetu na kumkuta mzee mmoja aliyevaa kama wao, akizungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha kabisa mara moja babu alipendekezwa kuwa Mwami. Lakini kwa mshangao wa wengi babu alikataa cheo hicho katakata. Kwa maelezo yake alidai cheo hicho ni kidogo sana kwa upeo wake na kwamba thamani yake ni sawa na kilemba cha ukoka.
Hicho kilikuwa kitendawili kingine cha babu kwa jamii yetu na kwa Waingereza wenyewe. Kwa kuwa walimhitaji sana, walao kuwa karibu na uongozi ndipo walipomwomba babu amruhusu walao baba akawe babarike, yaani mmoja wa wasaidizi wa Mwami. Babu alimruhusu.
Uamuzi wa babu kukataa cheo hicho ulipelekea DC
kuteua machifu wengine wa Heru Juu, Kalinzi, Bushingo na Buhambwe kutoka katika makabila ya mbali kama Mmanyema aliyetoka Tabora na mwalimu Mfipa aliyetoka Sumbawanga kuwa machifu wa eneo letu kwa nyakati tofauti.
Simulizi, visa na mikasa ya babu haikuwa na mwisho. Kila siku alikuwa na kitu kipya cha kusimulia, ambacho ama kilishangaza ama hakikuaminika miongoni mwa wasikilizaji wake.
Kwa mfano, alizungumza juu ya vitu kama nyumba ndogo ambazo watu huko Ulaya huzitumia kwa kusafiri umbali mrefu bila kutuma miguu yao wala kuchoka. Pia, alisema kulikuwa na kijumba ambacho alikitaja kuwa kinaitwa gari.
“Uchawi?” mtu mmoja alipata kumuuliza.
“Hapana,” babu alimjibu. “Hayo ni maendeleo tu ya Sayansi na Teknolojia.”
“Sayansi na Teknolojia ndio nini?” “Ni aina fulani ya elimu na ujuzi.”
Hadithi nyingine ya babu inayofanana na hiyo ni ile ya madai yake kuwa kuna vyombo vingine vikubwa zaidi ya gari ambavyo huruka angani, toka mji hadi mji, au nchi hadi nchi, kwa muda mfupi zaidi, vikiwa vimebeba abiria. Alivitaja vitu hivyo kuwa ni sawa na ndege mkubwa aliyeumbwa na binadamu.
“Huo sasa ndio uchawi wenyewe!” mzee mmoja aliyekuwa akimsikiliza alipata kumwambia. “Nikiwa mdogo mie pia nilipata kuchukuliwa katika ungo na babu yangu hadi pwani ya Tanga. Lakini safari hizo tulizifanya usiku tu, tukiwa tumejifunika sehemu za siri pekee. Kwa bahati mbaya, mpaka nakufa babu hakupata kuniambia siri ya uwezo ule.”
Babu alicheka sana kabla ya kumjibu mzee mwenzake
huyo akisema, “Nafasi ya uchawi inazidi kuwa ndogo katika dunia ya leo ya Sayansi na Teknolojia. Nani atakubali kusafiri usiku tu, tena bila nguo; wala kuiona mashine ya ndege hiyo?” Utamu wa aina mbalimbali za vyakula, urahisi wa maisha, barabara za juu na chini ya ardhi, magari, ndege na meli kubwa, matibabu ya kisasa na mambo mengine tele ni miongoni mwa simulizi nyingi ambazo wasikilizaji wake?
walizifurahia sana.
* * *?
Naam, huyo ndiye babu yangu, mzee Kionambali Mtukwao, kama alivyofahamika katika eneo lote hilo la wilaya ya Kasulu na vitongoji vyake. Ni babu huyu ambaye siku hiyo niliamka nikiwa nimelala chini, kando ya kitanda chake cha kamba, kilichotandikwa ngozi ya ng’ombe na blanketi nzito iliyoanza kuchakaa, ndani ya nyumba yake ya tembe. Niliamka alfajiri, lakini tayari babu alikwishaamka kitambo na kukoka moto nje ya nyumba. Bibi pia alikwishaamka na kuelekea mtoni kuchota maji.
Nikatoka nje na kumsalimu babu. Aliitikia kwa furaha kisha aliniamuru kumkamata jogoo mmoja mweupe na kumchinja ili awe kifungua kinywa cha siku hiyo. Ilikuwa kazi rahisi niliyoipenda sana. Kwa kuwarushia punje mbili tatu za mahindi, huku nikipiga mluzi, kuku wote ambao walishaanza kutawanyika huko na huko vichakani walirejea. Nikaendelea kurusha mahindi kwa karibu zaidi. Dakika mbili baadaye jogoo niliyemtaka alikuwa miguuni mwangu. Nikamdaka mara moja na kisha kumchinja. Bibi aliporudi alianza kumshughulikia mara moja.
Nikaenda mtoni ambako nilioga maji baridi yaliyouchangamsha mwili wangu. Nikasafisha meno yangu kwa mti wa mdaa ambao pia ni dawa ya kinywa na meno. Niliporudi bibi alikuwa akimalizia kutenga ugali wa muhogo kwa kitoweo cha kuku wa kuchomwa. Mimi na babu tuliketi mkao wa kula na kuanza kumshambulia jogoo yule ambaye muda mfupi alikuwa akiwika kama mfalme wa mji huo.
Pamoja na utamu wa kuku, pamoja na simulizi nyingi za babu, shahuku yangu kubwa ilikuwa kufahamu kile ambacho kilimfanya baba atokwe na machozi hadharani. Nikijua kuwa ni jambo hilo lililomfanya babu anichukue jana na pengine hata jogoo huyu amechinjwa kuhusiana na kisa au mkasa huo nilistahimili kwa muda nikimsubiri babu azungumze. Lakini babu alikuwa kimya. Chakula kilipokwisha nilitoa vyungu na kuvipeleka ndani. Niliporejea nilimsogelea babu na kumwambia taratibu, “Nadhani ulikuwa na jambo la kuniambia babu.” Babu alitabasamu na kuruhusu meno yake yote kuonekana, tofauti na wazee wengi wa umri wake ambao walibakiwa na magego machache tu vinywani mwao. “Mbona una haraka mjukuu wangu? Tuna mengi sana ya kuzungumza. Tusubiri kidogo bibi yako aende shamba. Nataka tuzungumze kama wanaume wawili, si mtu na mjukuu wake.”?
Kauli ambayo iliniongezea shahuku.
Mara bibi alipochukua jembe lake na kuelekea shambani babu alianza simulizi zake. Ajabu ni kwamba alianza kwa kunirushia maswali badala ya mimi kumrushia yeye.?
Babu: Unajua wenzetu walioendelea zaidi huko Ulaya maisha yao ni bora zaidi yetu?
Mimi: Najua, umesema hivyo mara nyingi.
Babu: Umepata kujiuliza nilifikaje huko na kutembea?
nchi zote hizo?
Mimi: Niliwahi kukuuliza. Unasema ulienda Ulaya kwa
Babu: ni kwlei. Nilienda kwa ajali.
Babu: mtu kwao mjukuu wangu. Maisha yangu yote ya
ugenini sikupata kujisikia.?
Babu alisitia kidogo akitafakari jambo. Nikatumia mwanya huo kutumbukiza swali langu badala ya kuwa mtu wa kuulizwa, “Kwa hiyo babu, pamoja na raha zote hizo kwa nini ulirudi? Au kurudi kwako pia ilikwua ajali nyingine?”
Babu: Hapana nilirudi kwa hiari.
Mimi: Kwa nini?
Babu: Mtukwao mjukuu wangu. Maisha yangu yote ya ugenini sikupata kujisikia nyumbani. Baadhi ya mila na desturi zao haziendani kabisa na zetu. Mvulana mkubwa kabisa anamkumbatia mama yake na kumbusu mdomoni! Msichana wa makamo anamvalia baba yake nguo fupi na pengine kumkalia mapajani!
Alisita kabla hajaendelea, “Halafu waliniudhi kwa jambo moja kubwa.
Mimi: lipi hilo?
Babu: La kudharau utamaduni na mila zetu na kuamini zao ndio sahihi. Kwa mfano makabila mengi ya Kiafrika yalimkataza mwanamke mwenye mimba kula mayai au maini kwa visingizo mbalimbali. Lakini walikuwa na sababu kubwa za msingi kabisa.
Mimi: Zipi hizo kama sio uchoyo na uroho?
Babu: (Akicheka) Uchoyo? Kwa kweli ulikuwa ukarimu wa hali ya juu sana. Unajua mwanamke mwenye mimba akila mayai mengi wakati wa ujauzito wake atanenepa yeye na mtoto aliye tumboni pia?
Mimi: Hilo najua.
Babu: Basi kwa hekima za wazee wetu walibuni hila ya kuwatishia hivyo. Ukweli ni kwamba walihofia mtoto akinenepa sana tumboni asingezaliwa. Hatukuwa na vifaa vya upasuaji kama wao. Na hatukutaka kuhatarisha maisha ya mama na mtoto; wazee wetu walikua na hekima sana.
Mimi: kweli uzee ni dawa…!
Babu alisita tena, kama mtu aliyejisikia kichefuchefu kwa mambo yale. Halafu akaendelea, “Si hayo tu. Hata nchi na mazingira yao hayafikii kabisa ya kwetu. Ndiyo, wana barabara kubwa na magari. Ndiyo, wana majengo mapana na bustani za kuvutia. Lakini hawana ardhi nzuri, misitu ya asili, mbuga za kuvutia, wanyama na ndege wa kusisimua kama sisi. Wengi wao hawana mito wala maziwa wenye samaki wengi kama yetu. Hata hali ya hewa kwao ni taabu tupu. Zipo nchi zenye baridi kwa mwaka mzima. Ziko zile zenye vipindi vya baridi kali na joto la kutisha katika mwaka mmoja. Sisi tumejaliwa sana.” Nilimwona babu akitabasamu kidogo na kisha kuangua kicheko. Nikamwuliza kulikoni. “Nitakuambia jambo moja,” alisema akiendelea kutabasamu. “Lakini naomba iwe siri kati yetu. Moja ya mambo yaliyonifanya nitamani sana kurejea nyumbani ni uhuru wa kujisaidia porini. Miaka yote niliyokuwa huko vyoo viko ndani ya nyumba. Ukipanda meli choo, ukipanda treni choo, ukipanda ndege choo. Hata mara moja hupati fursa walao kujisaidia haja ndogo porini, uone faraja ya maji yaliyochujwa na mwili wako yakipokelewa na nyasi za kijani na baadaye kumezwa na ardhi yenye kitovu chako.” Sikuweza kujizuia. Nikaangua kicheko kirefu. “Hapa tunazungumza kama mtu na rafiki yake.?
Nitakuambia sababu ya pili iliyonifanya niamue kurejea nyumbani.” Babu aliendelea.
“Lakini babu,” nilidakia, “Shida yangu kubwa ni kujua baba alikuwa analia nini jana. Hayo mengine tutayazungumza baadaye.”
“Tunaelekea hukohuko,” babu alisema. “Ungependa
kujua sababu nyingine iliyonirejesha huku?” aliongeza swali. “Nadhani ningependa kujua.”
“Nina tatizo kubwa. Sijui kusoma wala kuandika.” Babu
alitamka ghafla.
Tamko ambalo lilinipiga kwa mshangao kama radi. Babu hajui kusoma wala kuandika! Pamoja na kujua lugha mbalimbali za dunia! Pamoja na kutembea huko na huko. Nilihisi huo ulikuwa utani mwingine wa babu na mjukuu wake. “Naona huniamini. Sikubahatika kwenda shule. Baba?
yako vilevile hajui kusoma wala kuandika. Ninachotaka kufanya ni kuhakikisha wewe unapata kile ambacho wazazi wako hatukubahatika kupata. Tunataka upate elimu. Dunia inatawaliwa na kuongozwa na wenye elimu. Siri zote za dunia zimefichwa na kuhifadhiwa katika vitabu.” Aliongeza.
Wakati nikiitafakari taarifa hiyo ya kushangaza nikapambazukiwa na jambo moja. Ili kuhakikisha nikamuuliza babu, “Niambie ukweli babu. Ulikataa cheo cha uchifu kwa ajili ya kutojua kusoma na kuandika?”
“Mjukuu, naona una akili nyingi,” Babu alisema. “Ni kweli kabisa. Chifu gani ambaye atalazimika kupeleka barua kwa mtu mwingine ili asomewe? Ningekubali, ningeumbuka.”
“Hizo lugha ulizijuaje bila kusoma?”
“Uzoefu. Huwezi kuishi na mtu miaka kumi bila kujua lugha yake. Labda uwe na kichwa cha boga.”
“Na kwa nini hukujifunza kusoma na kuandika?” “Umri.”
“Umri?”
“Umri ulishapita. Ningeweza wapi mzee mzima kuketi na vitoto vya miaka sita kufundishwa a e i o u. Tena wanaokufundisha wakiwa watoto au wajukuu wako?”
Kwa kiasi fulani, nilimhurumia babu. Si kwa kukosa elimu ya vitabuni, bali kwa jitihada alizofanya za kujiweka wazi kiasi hicho mbele yangu hata akatoa siri ambayo naamini hakupata kumwambia mtu mwingine.
“Hawakukulazimisha?” nilimuuliza.
“Nini? Wanilazimishe kusoma? Baadhi yao pia walikuwepo wachache wasiojua kusoma wala kuandika. Wawili watatu walijaribu kunilazimisha kwa kuwatuma watoto wao wanifundishe. Lakini nilijifanya naumwa macho, kwa hila nikajitia vitunguu machoni na kutokwa na machozi kila kitabu au daftari lilipofunguliwa mbele yangu. Wakaniacha nilivyo.”
“Ni hilo la kutojua kusoma hasa lililokurejesha nyumbani?” niliuliza.
“Hilo ni moja wapo. Nisingerudi ningefia hukohuko nikiwa mpishi au mfagizi wao milele. Lakini kuna sababu nyingine”
“Ipi hiyo?”
Babu alikohoa kidogo kabla hajasema, “Ujinga ni mzigo mjukuu wangu. Wale watu waliojifanya wafadhili wangu, kumbe mimi ndiye niliyekuwa mfadhili wao. Walinitegemea mimi ili kupata mkate wao wa kila siku.
“Kwa vipi?”
Kwa sauti ya huzuni kiasi babu alieleza, “Wale jamaa kumbe walikuwa wakinifanyia maonyesho na kupokea fedha lukuki kwa jina langu. Unajua watu wa nchi nyingi Ulaya bado hawajapata kumwona mtu mweusi? Wengine ni wajinga kama wengi wetu tulivyo wajinga kwa kutopata kumwona mtu mweupe.”
“Kwahiyo walinigeuza biashara. Zile safari nyingi za hapa na pale, toka nchi hadi nchi, kumbe zilikuwa za kunifanyia maonyesho. Watu walitoa pesa nyingi ili wamwone ‘nyani mweusi’ anayekula kwa uma na kuzungumza Kiingereza. Kuna wakati niliombwa kuimba, au kualikwa kucheza muziki na wasichana wa Kizungu. Picha nyingi zilipigwa na kuuzwa kwenye vyombo vya habari.”
“Nikiwa nchini Sweden, katika mji mmoja uitwao Jonkoping niliajiriwa na familia moja ya watu ambao walikuwa wakiendesha shamba la wanyama. Wengi kati ya wanyama hao walikuwa wa porini ambao walikamatwa wangali wadogo na kufundishwa ama kuishi na binadamu. Wale wakali kama simba, chui na vifaru walifungiwa katika maeneo maalumu.”
“Ajira yangu kama nilivyoambiwa awali ilikuwa kusaidia kuwatunza wanyama hao. Niliingizwa katika mikataba ambayo sikuielewa na kushawishiwa kuweka dole gumba kwenye karatasi zao kama sahihi. Niliiona kazi rahisi na kuziona mia tatu kila wiki nilizokuwa nikilipwa kama za bure. Lakini nilishangaa pale nilipoanza kuvalishwa mavazi yaliyoandaliwa kitaalamu na kuonekana kama nyani dume. Hayo yalianza pale nyani aliyekuwa shambani humo alipofariki kwa uzee, wamiliki wakaifanya habari hiyo siri kwa hofu ya kupoteza wateja wao waliokuwa wakimiminika kila siku kumtazama nyani huyo anavyoruka toka tawi hadi tawi la miti iliyooteshwa shambani humo.”
“Nikaelekezwa kujifanya nyani yule. Kwa kuwa nilikuwa hodari sana wa kupanda miti, kuachia tawi moja na kudaka jingine halikuwa jambo geni kwangu. Niliwafurahisha sana watazamaji, hasa watoto. Nadhani niliwafurahisha zaidi kwa kuwa nilikuwa binadamu nikisoma hisia zao na hivyo kufanya
mengi ambayo hawakuyatarajia.”
“Waajiri wangu walifurahi sana. Muda wote walikuwa na kamera za video ambazo walizitumia kunukuu kila kitendo changu. Baadaye wateja walipoondoka waliendelea kunipiga picha hata wakati navua mavazi yale ya kinyani na kuvaa ya kibinadamu. Mara kwa mara walinihoji vilevile, kwa lugha zote nilizoweza kuzungumza na kunukuu maongezi yangu kwa vinasa sauti.”
“Ikaja siku ya balaa. Wakati nikiruka toka tawi hadi tawi la mti uliokuwa juu ya zizi la simba dume ilitokea bahati mbaya nikateleza na kudondokea ndani ya zizi hilo kando kidogo ya simba yule. Nadhani nilipiga ukelele wa hofu, kwani nilijua nimefika mwisho wa maisha yangu. Nilitetemeka zaidi pale simba huyo alipoanza kuninyatia taratibu akinguruma. Wakati nikijiandaa kwa vita ya kuipigania roho yangu nilishangaa kuona simba huyo akiweka kinywa chake kando ya sikio langu na kuninong’oneza, “Usiogope, mimi ni binadamu kama wewe!”
“Kweli? Wewe mtu wa wapi?” nilinong’ona vilevile. “Mimi ni Mmarekani. Nipo hapa mwaka wa tatu.” Alisema.
“Nilipigwa na butwaa. Lakini walioduwaa zaidi ni watazamaji ambao kwao kitendo cha simba kuteta na nyani kilikuwa muujiza wa pekee. Walitegemea kuona nikiliwa hadharani, badala yake nanong’ona na simba!”
“Toka siku hiyo shamba hilo likawa linafurika wateja. Walitoka miji ya mbali na hata nchi za jirani kuja kushuhudia maajabu ya ‘nyani’ na ‘simba’ waliojenga urafiki.”
Lakini kwangu hiyo ilikuwa siku ambayo niliamua kuacha kazi hiyo. Pamoja na kulipwa fedha nyingi, nilikichukulia kitendo hicho kama udhalilishaji mkubwa.
Hivyo, mara tu nilipopata mshahara wangu wa mwezi huo, ambao uliongezwa mara dufu, nilitoweka.”
Nilicheka sana. Kwangu ilikuwa habari ya kusisimua sana. Ilinisisimuazaidikumsikiababu,kwamarayakwanza,akisimulia tukio lililomuhusu kwa kirefu kiasi hicho. Mara nyingi yeye alikuwa mtu wa simulizi na kujibu maswali kwa mkatomkato. Nilikuwa na kila sababu ya kumhurumia babu. Kwa upande mwingine, maelezo yake yalizidi kunithibitishia jambo moja kubwa; umuhimu wa elimu. Lakini mara nikakumbuka kuwa babu alikuwa hajafikia au kugusia kiini cha maelezo hayo. Sababu ya kulala kwangu kwake na kuchinjwa kwa jogoo wake bora kuliko wote; kwa kila hali kulihusiana na
majonzi aliyokuwa nayo babu. Nikamkumbusha hilo.
“Nakumbuka vizuri sana,” Babu aliniambia. “Lakini,” aliongeza. “Kama nilivyosema awali unahitaji kuwa na kifua. Taarifa nitakayokupa huenda ikakutisha au kukuogofya. Lakini unatakiwa kupokea kama mwanamume na kuichukulia kwa upande wa pili kama msukumo wa ufunguo mpya wa maisha yako.”
Niliona kama babu anazidi kunichanganya. Nikamtumbulia macho ya mshangao na kumtegea sikio kwa makini.
“Inabidi uondoke kijijini hapa mara moja,” babu
aliniambia ghafla.
Kati ya yote niliyotarajia, hilo la kuondoka halikuwemo katika mawazo yangu, “Nani? Mimi!”
Babu akakubali. “Kwa nini?” “Wanataka kukuua.”
Sikuyaamini masikio yangu, “Wanataka kuniua mimi, watu gani hao?”
“Wanakijiji. Wakazi wa eneo hili.”
Bado sikumwelewa babu. Nilihisi huo ulikuwa utani wake mwingine, pengine kwa nia ya kupima ujabari wangu. Ili kumthibitishia hivyo niliangua kicheko na kumwambia taratibu, “Babu acha utani huo. Unanichulia kifo.”
Lakini macho ya babu yalikuwa hayana utani wala mzaha wa aina yoyote alipoongeza, “Wanataka kukutoa kafara. Lazima uondoke haraka iwezekanavyo.”
* * *
Kwa takribanimiakamitatuiliyopita eneo letulilikumbwa na ukame. Mazao yaliyopatikana yalikuwa machache sana. Mimea mingi ilinyauka, hata baadhi ya vyanzo vya maji vilianza kukauka. Mbaya zaidi ni pale ilipoonekana wazi kuwa mwaka huo pia hakukuwa na dalili ya mvua.
Zaidi ya tatizo hilo la ukame lilikuwepo tatizo jingine kubwa zaidi, tatizo la ugonjwa wa malale. Eneo kubwa la mapori na misitu iliyovizunguka vijiji vyetu ilikuwa na mbung’o wengi sana ambao walidaiwa kusababisha malale. Mbung’o hao walianza hata kuvamia mifugo iliyokuwemo zizini na hivyo kusababisha maradhi ya usingizi na hatimaye vifo vya ng’ombe wengi. Wala haikuwa mifugo pekee. Zaidi ya watu wanane kijijini hapo walikuwa wamekwishakufa kwa malale huku wengine wasiopungua ishirini, wakiugua ugonjwa huo ambao haukusikia dawa.
Kwa mujibu wa babu, Mwami, wasaidizi wake na wazee wenye busara kijijini hapo waliketi vikao vingi kujadili namna ya kupambana na matatizo hayo bila mafanikio. Hali
hiyo ilisababisha wachukue uamuzi wa kuomba msaada wa bingwa wa ramli katika eneo hilo. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo miungu ilikuwa imekasirika kwa kusahauliwa kwa muda mrefu. Hivyo, ilidai kafara ya damu ya mtu ili iwafukuze mbung’o na kuamuru mvua inyeshe kama kawaida.
Kwa maelezo ya mtaalamu huyo, kafara huyo alitakiwa azikwe hai, usiku wa manane; katikati ya msitu mnene wenye mbung’o wengi. Aidha, mtu huyo alitakiwa awe msichana au mvulana anayetoka kwa baba na mama mwenye mtoto mmoja. Ni hapo nilipoingia mimi. Katika eneo lote hilo wazazi wangu walikuwa watu pekee wenye mtoto mmoja. Kwa bahati, baba alikuwa mmoja kati ya babarike walioteuliwa kufanya mawasiliano na mtabiri yule. Vinginevyo, zoezi hilo lingefanywa kwa siri. Mwami na viongozi wengine walimweka kitako na kumtaka apige moyo konde na kumtoa mwanae wa pekee ili
kuiokoa nchi na maafa zaidi.
Ni hilo lililomfanya baba arudi nyumbani huku akibubujikwa na machozi. Alikuwa katika mtihani mkubwa wa kuchagua kati ya mwanae wa pekee na ukombozi wa nchi yake ili iondokane na maafa.
* * *
“Nadhani sasa umeona umuhimu wa kuondoka kwako hapa haraka,” babu aliniambia mara baada ya maelezo yake. “Ni sawa na kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Utakuwa ukikimbia kifo, wakati huohuo ukiifuata elimu.” Alifafanua.
Nilimsikiliza babu kwa makini. Hata hivyo, moyo wangu ulikuwa mzito sana kwa ukubwa wa suala zito lililokuwa kichwani mwangu. Kwamba watu walikuwa wamekaa vikao na kufikia hatua ya kuamua kunizika nikiwa hai ili wapate mvua!
Haikuniingia kabisa akilini. Ndiyo, siku za nyuma nimewahi kusikia hadithi za aina hiyo. Hadithi za watu, hasa watoto, kutolewa kafara. Lakini sikupata hata mara moja kumfahamu mtu yeyote au mtoto wa mtu yeyote aliyepata kutolewa kafara. Pengine kafara hizo zilitolewa kwa siri? Pengine hilo ndio jibu la hadithi za kutolewa kwa baadhi ya watu kijijini hapo miaka ya nyuma?
Tishio la maisha yangu lilikuwa kubwa. Tishio la kulazimika kuondoka kwangu lilikuwa kubwa zaidi. Mimi, ambaye sijapata kutoka nje ya vijiji viwili vitatu vinavyotuzunguka katika eneo hilo, nitakwenda wapi? Na nitarudi kweli? Nilihisi chozi likinitoka na kuteleza hadi kidevuni kwangu. Nikalifuta harakaharaka kuchelea babu asilione. Aliliona. Lakini, kwa mara ya kwanza, hakunishutumu kwa kitendo hicho cha Mwananume kulia.
“Najua hiki ni kipindi kigumu sana kwako, mjukuu wangu. Lakini wewe ni mwanamume. Ulitarajia nini katika maisha yako? Uzaliwe hapa, ukulie hapa, ufie hapa? Bahati ya mwanamume iko miguuni mwake. Lazima utoke. Lazima ukatafute elimu ili ubadili maisha yako. Chukulia tishio la maisha yako kama changamoto inayokupa msukumo wa kuondoka hapa haraka zaidi, si vinginevyo.” Babu alinihubiria. Aliongeza kuwa siku zote alikuwa na nia ya kuhakikisha naondoka hapo kijijini kwenda nchi za mbali kutafuta elimu ya maisha mapya. Lakini wakati ulikuwa haujajiri. “Wakati huo
sasa umefika. Huna budi kuacha kijiji na kuikabili dunia.” “Nitakwenda wapi?” niliuliza ghafla. Hisia fulani rohoni
mwangu zikinishangaza. Nilihisi kama ambaye nilikuwa tayari nimeridhika na maelezo yake na kuanza kujenga shahuku ya kuifanya safari hiyo mara moja.
“Swali zuri sana,” babu alinijibu. “Ni swali ambalo nilikwishalifikiria kwa muda mrefu na kulipatia ufumbuzi. Utaelekea kaskazini, katika nchi ya Wahaya. Huko Wazungu wanaotangaza dini yao, tayari wamejenga shule na wanapokea watoto na kuwafundisha kusoma na kuandika.”
Nitafikia kwa nani? Nitakula nini? Nikiugua atanisaidia nani? Ni miongoni mwa maswali lukuki ambayo yalijaa katika kichwa changu. Nilitamani kumuuliza hayo babu, lakini nilisita kwa kujua kuwa angeyapuuza mara moja. Si alikwishaniambia kuwa bahati ya mwanamume iko miguuni mwake? Nikapiga moyo konde na kufikia uamuzi. Lazima niondoke.
Babu aliusoma uamuzi wangu katika macho yangu. Akatabasamu. Kisha akasema, “Wewe ni mwanamume. Siku zote nilijua kuwa mwanangu amezaa dume la simba. Kazi iliyobaki sasa ni maandalizi ya safari yako. Si unafahamu kuwa tunataka iwe siri?”
* * *
Kuagana na wazazi wangu lilikuwa jukumu zito kuliko nilivyodhania, hasa ukizingatia kuwa zoezi hilo lilikuwa la ghafla sana na lilifanyika kwa siri sana. Mara tu baada ya maafikiano yangu na babu tulirejea nyumbani ambako babu alimweleza mwanae uamuzi wangu. Baba hakuwa na hiari ingawa aliipokea habari hiyo kwa majonzi makubwa.
Tatizo kubwa lilikuwa kwa mama. Kwanza, hakuamini masikio yake. Kulikuwa na mpango wa mtoto wake wa pekee kutolewa kafara kwa siri. Hilo la kuondoka kwangu pia kwake lilikuwa pigo jingine. Mama alichukulia safari yangu sawa na kifo changu. Aliangua kilio cha kwikwi, huku akisema, “Sikubali mwanangu aondoke. Sikubali kabisa.”
Babu na baba walimsihi aache kulia na kisha kumfahamisha umuhimu wa kuondoka kwangu. “Ataokoa maisha yake na atapata elimu.” Walimwambia.
“Nani atampikia chakula? Akiugua nani anajua dawa zake? Akifa huko tutajuaje?” Mama aliendelea kulalamika. “Sikubali! Labda niondoke na mwanangu!”
Ilichukua muda mrefu kumshawishi mama. Aliporidhika alinitemea mate kwenye paji la uso kuniombea baraka, “Mwanangu, Mtukwao, nenda salama, urudi salama. Kumbuka wazazi wako tupo na tunakupenda sana. Usitusahau asilani.” Alisema huku akiwa ameweka mkono wake wa kushoto kifuani mwangu.
Nilishindwa kujizuia. Machozi yalinitoka. Hakuna aliyenishutumu.
2SURA PILI
Porini… Simba.
afari ilianza alfajiri sana, yapata saa tisa au kumi hivi. Nyasi na majani yalijaa umande mwingi ambao ulifanya tulowe chapachapa, dakika
chache tu baada ya safari. Kiza pia kilikuwa kimetanda huko na huko kuongeza ugumu wa safari. Kwa kweli, mimi sikujua kama tunaelekea upande upi; mashariki au magharibi, kaskazini au kusini. Nilichofanya ni kumfuata babu ambaye alikuwa mbele yangu, akitembea kwa ule mwendo wake mkali, wa hatua ndefundefu ambao mara nyingine ulifanya nitembee huku nikikimbia ili niwe naye sambamba. Babu alikuwa amejitolea kunisindikiza hadi atakaponiacha katika mikono salama. Uamuzi wake, kwa kuzingatia umri wake na urefu wa safari, ulipingwa sana na baba. Lakini haikuwepo njia nyingine. Babu alionya kuwa umri wangu haukuniruhusu kusafiri maporini peke yangu. Hali kadhalika, alichelea kuwa kama baba angetoweka kijijini hapo pamoja na mimi ingekuwa dhahiri kuwa amenitorosha, jambo ambalo lingemletea matatizo makubwa na wanakijiji wenzake. Zaidi, kwa kuwa babu alijua lugha mbalimbali za kigeni aliamini kuwa wamisheni wenye shule wangemsikiliza kwa makini zaidi na kunipokea, kwani shule nyingi alisema
zimejengwa kwa ajili ya watoto wa Machifu.
“Lakini kuna sababu nyingine. Kwa umri wangu huu huenda mjukuu wangu atakaporudi hatanikuta nikiwa hai, wakati bado nina mengi ya kumfundisha. Hivyo, katika safari yetu ndefu nitapata wasaa wa kumrithisha hiki na kile ambacho kitamfaa katika maisha yake.” Babu aliongeza hoja ambayo si baba wala mama aliyeipinga.
Usiku huo wa kuamkia safari sikupata usingizi. Kichwa changu kilijaa maswali mengi pasi ya jibu hata moja. Kiwingu cha hofu kilitanda katika fikra zangu kiasi kwamba hata nilipopata lepe dogo la usingizi, ulikuwa wa mang’amung’amu; ukiambatana na ndoto za kutisha. Hali hii ilisababisha nikurupuke mara kwa mara na kukodolea macho kiza kilichotanda chumbani humo.
Kitu kingine kilichonikosesha raha ni mlio wa bundi. Katikati ya usiku bundi mmoja alitua juu ya paa la nyumba yetu na kuanzisha kile kilio chake chenye sauti mbaya ya kutisha. Hakuna mtu ambaye hakujua kuwa bundi kukesha katika mji wako akilia ni dalili mbaya. Mara nyingi huashiria msiba au nuksi itakayoipata familia hiyo. Hivyo, wakati babu aliponiamsha na kuninong’oneza ‘tuondoke’ hata kabla jogoo hajawika nilianza safari nikiwa na moyo mzito sana.
‘Kwa heri Buha…. Kwa heri Kasulu… Kwa heri Heru…’ nilihisi moyo wangu ukinong’ona wakati nikichukua furushi langu dogo, lenye ngozi, kipande cha kaniki na akiba ya chakula njiani. Nje ya nyumba babu alikata fimbo mbili toka kwenye matawi ya miti na kunipa moja. Sikuhitaji kuambiwa kazi ya fimbo hizo. Zilitumiwa kupiga majani ya mbele yako kwa ajili ya kupunguza umande. Fimbo hizo hazikufua dafu kutokana na ukubwa wa pori ambalo katika sehemu fulanifulani nyasi zilitumeza kabisa.
Tulimsikia jogoo wa kwanza akiwika toka mbali baada ya mwendo wa dakika zipatazo arobaini hivi. Muda mfupi baadaye jogoo wengine walianza kuwika toka huko na huko wakiashiria mapambazuko. Hawa walifuatiwa na milio ya ndege wa alfajiri toka katika matawi ya miti mbalimbali. Muda mfupi baadaye dalili ya mapambazuko zilijidhihirisha zaidi. Hali ya hewa ilibadilika kwa namna fulani na kiza kuonekana kama kimetamalaki zaidi. Kisha, mashariki ilianza kubadilika na miale yenye rangi ya dhahabu kuanza kuchomoza toka nyuma ya vilima na mti toka mbali.
“Kumekucha,” babu alisema taratibu.
Nadhani hakutarajia jibu. Hivyo, sikumjibu chochote. Nilichofanya ni kuongeza hatua zangu ili kuwa naye karibu zaidi.
Jua lilichomoza kwa maringo, hatua baada ya hatua. Tahamaki miale yake murua yenye rangi ya dhahabu ilianza kupenya na kuifikia miili yetu ambayo ilikuwa taabani kwa baridi. Taratibu joto la miale hiyo lilikausha umande katika miili yetu na kuifariji. Nilijihisi nikichangamka si mwilini tu, bali pamoja na moyoni pia.
Nadhani babu alichangamka pia kwani nilimwona akitabasamu na baadaye kusema taratibu, “Jua ni Mfalme, unajua kuwa nchi nyingine huko Ulaya waliabudu jua na kulichukulia kama Mfalme wao?”
Sikumwelewa. Wakati bado natafakari kauli yake hiyo aliongeza nyingine, “Unajua huko Ulaya kuna nchi ambazo huwa hawalioni jua kwa karibu mwaka mzima?”
Babu alinichanganya zaidi.
“Sasa wanaishije bila jua?” nilimuuliza.
“Wanaishi kwa kuvaa makoti makubwa na
kujifunika mablanketi mazito. Mchana na usiku wanakoka moto majumbani mwao kutafuta joto.” Alieleza. Kwajinsinilivyomfahamubabunilijuabaadayakuchangamshwa na jua hilo amepata nguvu na kuanza hadithi zake zisizo na mwisho. Nilikuwa nimechoka. Nilikuwa tayari najisikia njaa. Nilichelea kumjibu kungemfanya aongeze hadithi nyingine. Nikakaa kimya nikifikiria namna ya kumwomba tupumzike kidogo.
Kana kwamba alikuwa akiyasoma mawazo yangu babu mwenyewe alishauri tupumzike. Nilishukuru kimoyomoyo.
Nikamwonyesha babu mbuyu mkubwa wenye kivuli mwanana na kumtaka tukapumzike pale. Babu alitikisa kichwa kukataa. “Mbuyu sio mti mzuri sana wa kukaa chini yake. Unajua mbuyu unaishi maisha marefu pengine kuliko miti yote duniani? Mara nyingi mizimu na mashetani pia hufanya mibuyu makazi yao. Jitahidi kuiepuka.” Babu alinieleza na kunishauri.
Haikuwa hadithi mpya kwangu. Mara kwa mara tulikuwa tukionywa kucheza chini ya mibuyu na hasa kuingia katika mapango makubwa ambayo huchimbika katika mashina ya mibuyu mikongwe zaidi. Tunaambiwa humo wanaishi majini au mashetani katika sura mbalimbali. Pia tunaambiwa kwamba baadhi ya viumbe hai huonekana katika sura ya nyoka, ndege au wanyama wengine.
Tulitembea zaidi ya dakika tano nyingine kabla hatujafikia eneo lililozagaa mivule mingi na kufanya kuwe na kivuli kikubwa. Tuliketi juu ya magogo ya miti iliyokufa na kuifungua akiba yetu ya chakula. Tulikuwa na mihogo ya kuchemsha, ndizi, nyama kavu ya nyati na ugali wa lowe. Tulikula kimyakimya, ndege wadogo wakitumbuiza kwa
nyimbo zao tamu toka kwenye matawi ya miti hiyo. Baadhi ya ndege hao, tetere na kitororo, waliruka juu yetu mara kwa mara kama wanaotushangaa kwa kuwepo kwetu pale. Muda mfupi baadaye kundi kubwa la tumbiri lilivamia miti hiyo na kuanza kuruka toka tawi hadi tawi juu ya vichwa vyetu kwa namna ya kutudhihaki
“Dalili njema.” Babu alisema. “Safari yetu itakuwa nzuri,” aliongeza.
Nikaona huo ulikuwa wasaa muafaka wa kutoa dukuduku langu. “Lakini babu,” nilimwambia. “Mbona usiku wa leo bundi amekesha akilia juu ya paa la nyumba yetu? Si wanasema bundi kulia juu ya nyumba usiku ni ishara ya balaa?”
Babu alitafakari hilo kwa makini. Baadaye alisema, “Bundi ni ndege wa usiku. Haoni mchana ndio maana kutwa nzima hushinda amelala. Usiku hutoka na kuanza mawindo yake. Anapenda kula panya na ndege wengine wadogowadogo. Kuna imani nyingi juu ya bundi katika makabila na mataifa mbalimbali. Kwa mfano, wakati huku kwetu wengi tunamchukulia bundi kama nuksi, nchi nyingine huko Ulaya bundi akikesha analia kwenye nyumba yao wenyeji hufurahi sana na hata kufanya sherehe. Wao wanakichukulia kitendo hicho kama dalili ya neema.”
Ilikuwa habari mpya kwangu, “Umejuaje yote hayo babu?” nilimuuliza.
“Kutembea mjukuu wangu, wanasema, ‘kutembea ni shule.’ Halafu kuna wale waliosema. ‘kuishi kwingi ni kuona mengi. Mimi nimetembea sana, halafu nimekula chumvi nyingi.”
Kwa muda tuliendelea kula kimyakimya. Tulipotosheka tulifunga vibuyu vyetu ambavyo bibi alituandalia maziwa ya ng’ombe kwa ajili yangu na togwa kwa ajili ya babu. Tukanywa taratibu huku tukiwa tayari tumewapuuza ndege waliokuwa wakicheza juu ya vichwa vyetu. Nadhani baadaye nao pia walitupuuza kwani walishika hamsini zao na kuendelea na shughuli zao kana kwamba hatupo.
Babu alishauri tupumzike kidogo chini ya mti huo, uamuzi ambao niliupokea kwa mikono miwili. Nikajinyoosha chali, juu ya majani makavu na kuyafumba macho yangu kwa matarajio ya kupumzika kidogo. Kwa mshangao usingizi mtamu ukanipitia. Ama babu pia alilala, ama aliamua kuniacha nilale kwani nilipofumbua macho tena ilikuwa jioni, jua likielekea kuzama. Babu alikuwa kaketi palepale akinitazama.
“Umepumzika vya kutosha,” Babu aliniambia. “Tuendelee na safari. Leo ningependa tulale karibu na Makere, kesho jioni tuamkie Mto Malagharasi na kulala Nyakisogo ili ikiwezekana keshokutwa tufike Kibondo.”
* * *
Laiti babu angejua ratiba aliyopanga ingetibuliwa mara moja, bila shaka asingefuata njia hiyo tuliyokuwa tukiifuata.
Ratiba yake iliharibika kesho yake tu, wakatitukiukaribia Mto Malagharasi. Tulikuwa tumejipumzisha chini ya mti, baada ya kula na kunywa maji safi toka katika kimojawapo cha vijito vingi vilivyokuwa vimetapakaa katika eneo hilo, vijito ambavyo kwa ajili ya ukame vingi vilianza kuonyesha dalili ya kukauka.
Mara tulisikia mlio wa bunduki, ukifuatiwa na vilio na kelele za watu wanaolia au kukimbia kwa hofu. Babu
aliniamuru kupanda mti mara moja kwa nia ya kujificha. Yeye pia akapanda mti huo. Tulienda hadi kwenye matawi ya juu na kutulia huku tukiangalia purukushani toka mbali. Tuliwaona watu wapatao kumi wakiwa wamefungwa mikono wawiliwawili, wakiongozwa na watu waliovaa kaptula za kaki na viatu vizito. Hawa walishika marungu. Nyuma yao kulikuwa na watu weupe wawili waliobeba bunduki.
Watu hao walipofika chini ya mti na kuona mizigo yetu hawakuangaika kututafuta. Walitupa macho yao juu na kutuona tulivyoning’inia kwenye matawi kama nyani.
“Shuka chini.” Mmoja wao aliamuru kwa sauti kubwa.
Nilimtazama babu kwa hofu. Nikamwona akianza kushuka taratibu. Nikamfuata.Tulipofika chini tuliamriwa kukaa chini pamoja na wale mateka wengine, amri ambayo babu alikataa.
“Nyie nani?” aliwauliza watu hao ambao walikuwa bado wameduwaa kwa kitendo chake cha kugomea amri yao.
“Huoni kama sisi ni askari?” wale askari weusi walijibu. Mmoja wao aliongeza, “Wale pale ni maafisa wa kodi.” Alielekeza kidole chake kwa Wazungu waliokuwa wakitazama zoezi hilo kana kwamba haliwahusu.
“Enhe! Mkiwa askari kwangu mnataka nini?” babu aliwahoji tena.
“Tunakamata watu wote wanaoishi juu ya miti kama tumbili,” mwingine alijibu.
Babu: Kwa nini?
Askari: kwasababu watu wanaoishi juu ya miti ni wale ambao hawajalipa kodi.
Tuonyeshe kipande chako cha kodi.
Hadi hapo nilijua mambo yameharibika. Babu alikuwa
mbishi sana katika suala la kodi. Kama nakumbuka vizuri hakupata kulipa kodi hata mara moja. Kila ulipofika msimu wa kodi yeye alibadilika na kuwa mkali kama pilipili. Ilifikia hatua askari wa kodi walimkwepa na kumkimbia kwa ukali na ubishi mwingi aliokuwa akiutoa kiasi cha wao kujiona wapumbavu mbele yake.
Nilimwona babu akitabasamu. Kisha aliuliza, “Kodi hiyo nimlipe nani?”
Askari: Unailipa serikali ya Uingereza. Ni amri halali ya Malkia. Wale pale ni wawakilishi wa Gavana.
Babu alicheka tena. “Majuzi,” alisema “Walipita Waarabu wakikamata watumwa na kuwauza kwa kisingizio cha kodi. Baadaye walikuja Wabelgiji na kuanza kudai kodi. Siku chache baadaye tukawaona Wajerumani. Wao pia walitudai kodi kwa jeuri na ukatili mkubwa. Leo tunaambiwa ni zamu ya Waingereza. Na nyie weusi kama mimi, ndio mko mbele kunidai kodi! Vichwa vyenu vinafanya kazi kweli nyie?” Askari hao waliduwaa. Mmoja alikasirika na kuinua rungu lake tayari kumtwanga nalo babu kichwani. Mmoja wa askari wa Kizungu, aliyeelekea kuvutiwa na mdahalo huo alimzuia askari huyo na kisha yeye mwenyewe kumkabili
babu, “Weye iko nani?” alihoji kwa Kiswahili chake kibovu.
Askari huyo alipigwa na butwaa pale babu alipomjibu kwa Kiingereza fasaha, “Mimi ni raia wa nchi hii. Nimekaa kwenu nikawalipa kodi. Nimerudi kwetu mnataka niwalipe kodi! Tena mnadai kwa mtutu wa bunduki kama majambazi! Sijawahi na wala haitanitokea kamwe kumlipa kodi mgeni!”
Wazungu wale walipigwa na butwaa, kitendo ambacho yule askari mweusi, mwenye jazba, alikitafsiri kitendo hicho
kuwa ni kashfa kwa maafisa hao. Bila subira wala simile aliinua rungu ili ampige nalo babu kichwani. Lilikuwa kosa ambalo askari huyo atalijutia milele kwani babu alimkwepa na hapohapo kumpiga ngumi tatu za usoni ambazo zilimfanya askari huyo ateme mate yenye damu na jino lake moja. Pua yake pia ilitokwa na damu nzito. Askari wa pili alipotaka kuingilia kati Wazungu wale walimzuia. Badala yake walimkodolea babu macho ya mshangao mkubwa zaidi. Kwa umri wake, hawakuamini kuwa babu angeweza kuwa mwepesi na mwenye nguvu kiasi kile.
“Wewe ni nani?” walimuuliza tena taratibu. “Naitwa Kionambali, Mtukwao.”
“Unatoka wapi, unakwenda wapi?”
“Natoka Buha. Nakwenda nchi ya Wahaya.”
“Unajua kutolipa kodi ni kosa kubwa? Unajua kumshambulia mtumishi wa Malkia ni kosa kubwa zaidi?”
Babu hakujibu.
“Unajua adhabu ya makosa yako? Kwa umri wako huo unajua kuwa tukikupeleka jela utafia huko na kupigwa viboko vitano kila siku ya uhai wako gerezani?”
Babu hakujibu vilevile.
“Mfungeni mikono,” mzungu huyo alitoa amri. Babu alipotaka kuanzisha vurumai jingine mzungu huyo aliinua bunduki na kufyatua risasi moja hewani. “Risasi ya pili hapana kwenda hewani. Takwenda moja kwa moja katika kifua yako.” Alionya.
Babu alinywea na kuruhusu mikono yake yote miwili ifungwe kwa pamoja.
“Twende,” Mzungu huyo alimsukuma babu kwa tako la bunduki yake.
Babu aligeuka kunitazama. Kisha alimgeukia Mzungu yule na kumuuliza “Mjukuu wangu nitamwacha na nani?
“Hapana kazi yetu,” Mzungu alimjibu kikatili. “Taishi kwenye miti kama nyama. Takula matunda ya porini kama ndege. Kama nachoka tarudi nyumbani yenu.”
Babu alipojaribu kubisha tena yule askari aliyeumizwa aliitumia fursa hiyo. Alimpiga babu kichwani kwa rungu lake kwa nguvu zake zote. Babu alipepesuka na kuanguka chini. Damu nyingi zilimtoka kisogoni.
Sikuweza kuvumilia. Nilikurupuka na kumvamia yule askari kwa nia ya kumpiga tumboni. Aliniwahi. Akanipiga makofi makali na kunisukuma. Nilipepesuka na kumfuata tena. Safari hii alinipokea kwa rungu la kichwa ambalo lilinifanya nipoteze fahamu na kudondoka chini kama mzoga
* * *
Sikumbuki nilipoteza fahamu kwa muda gani.
Nadhani ilikuwa zaidi ya saa sita. Ninachokumbuka ni pale nilipokurupuka baada ya kupatwa na hisia za hatari. Kitu kama kishindo au mlio fulani ndio ulionizindua ghafla. Kweli. Mara nilipoinuka niliona kitu au mnyama fulani mkubwa akiruka na kukimbia. Tukio hilo lilifuatiwa na kicheko au kilio cha kuogofaya.
Fisi!
Wala hakuwa fisi mmoja. Milio yao iliashiria kuwepo kwa fisi wengi katika eneo hilo. Bila shaka walikuwa wakininyemelea kwa matumaini kuwa ningekata roho ili waule mzoga wangu!
Nilipatwa na hofu kubwa. Fisi ni mnyama mwoga lakini mwenye nguvu nyingi. Taya na meno yake pia yana nguvu sana kwani mifupa uliomshinda yeye hakuna mnyama mwingine
anayeuweza. Fisi huenda kushambulia wanyama wadogo au wagonjwa, ingawa mara nyingi uwa yuko nyuma ya simba akisubiri aue mnyama, amle ili yeye aambulie mabaki. Fisi ni mnyama mvumilivu pia. Anaweza kumfuatilia, mnyama au binadamu mgonjwa hata kwa siku tatu atakapoishiwa nguvu ili amle.
Sikuwa tayari kufanya mzaha na fisi. Mara moja nilitafuta mti uliokuwa karibu na kuuparamia. Pamoja na kiza totoro kutanda huko na huko niliufahamu mtu huo kuwa ni uleule ambao muda mfupi mimi na babu tuliutumia kujificha. Nikapanda hadi mahala penye tawi zuri ambapo niliweza kulala chali, nikajipumzisha. Ni hapo nilipopata wasaa wa kusikiliza maumivu makali niliyokuwa nayo toka kichwani, pale rungu la askari yule liliponipiga barabara.
Aidha, ni wakati huo nilipoweza kutafakari kwa kina masaibu yaliyonipata. Sikujua babu amepelekwa wapi. Sikujua kama alikuwa hai au tayari ameuawa. Sikuwa na hakika kama nitamwona tena mzee yule mwenye mengi ambayo nilitegemea hadi mwisho wa safari yetu awe amenichotea kiasi fulani, mzee niliyemchukulia kama fimbo au kitendawili ambacho kimetoweka kabla ya kuteguliwa.
Machozi yalinitoka.
Nikajifikiria mimi mwenyewe jana tu niliishi raha mustarehe kwa baba na mama leo nimekuwa yatima katikati ya msitu mkubwa wenye hatari zote. Sikujui ninapokwenda wala ninapotoka. Hata kama ningeweza kurudi nyumbani hatari ya kifo bado inanisubiri. Kuendelea na safari niliona ni kifo vilevile. Sikuwa mwerevu wa kutembea porini. Sikuwa na chakula. Zaidi ya yote sikujua njia. Sikujua kama nilipaswa kuelekea kushotoa au kulia, nyuma au mbele.
Machozi yalinitoka.
Sikuthubutu usingizi unipitie. Hofu ya kudondoka toka juu ya mti huo ni moja ya sababu zilizoninyima usingizi. Milio ya kuogofya ya ama wanyama wa porini ama ndege na wadudu wengine ni sababu ya pili. Lakini sababu kubwa zaidi iliyochangia kupaisha usingizi wangu ilikuwa mawazo tele yaliyojaa kichwani mwangu. Kwa kweli mawazo hayo yalinizidi kimo na hata umri. Iwapo ilinipasa kurudi au la iwapo ningeweza kuijua njia ya kurudi au la! Na kadhalika na kadhalika.
Hofu yangu iliongezeka maradufu, nusura nipige kelele pale nilipopata hisia za kitu kama mnyama au nyoka anayepanda taratibu juu ya mti huo. Huku nikitetemeka niliyakaza macho yangu kwa nguvu zote ili niweze kuona kitu hicho. Hofu yangu kubwa ilikuwa ya chui, mnyama ambaye anapenda sana kujificha juu ya mti wakati akiwinda. Aina fulani ya chatu pia wana tabia ya kuparamia miti na kujipumzisha juu ya matawi. Nilihisi maisha yangu yamefikia ukiongoni, kwani yeyote kati yao, angenishambulia ama kwa hofu ya kunikuta huku ama kwa njaa.
Kitu hicho kiliendelea kupanda juu, taratibu na kimyakimya kama kivuli. Nilianza kupapasa huku na huko kwa matarajio ya kupata tawi la mti lililokatika ili nilitumie kujitetea katika kupigania roho yangu. Sikupata. Akili fulani ikanishauri nijitetee kwa kukitisha kiumbe hicho kwa sauti. Nikakohoa kwa nguvu. Kwa mshango wangu kiumbe huyo alikohoa kwa sauti ya binadamu. Sikuyaamini masikio yangu. Nikakohoa tena.
Kitendo hicho kilifuatiwa na sauti ya binadamu iliyoita taratibu, “Mtukwao?”
Ilikuwa sauti niliyoifahamu fika, sauti ambayo
sikutarajia kuisikia tena katika maisha yangu! “Babu,” niliita kwa sauti ya chini vilevile. “Naam,” alinijibu.
Nilitamani kupiga ukelele wa furaha. “Umerudi?
Wamekuachia?”
Nilimsikia babu akicheka kabla hajasema, “Wale ni watoto wadogo. Msitu huu ni wetu na ni mkubwa sana kwao. Umejaa miti na miti. Kwao kila mti ni mti. Kwangu mie kuna miti na mitishamba. Liko jani dogo tu, ambalo nimelichuma na kulitafuna, wakawa hawanioni wala hawanikumbuki tena. Nimewaacha wakihangaika ovyo, wasipoangalia hata njia ya kurudi walikotoka hawataiona.”
Zamani kidogo nilikuwa nikishangazwa na vitendo na simulizi za babu. Lakini baada ya kuishi nae kwa muda mrefu nilikoma kushangazwa naye. kila alilofanya, kila alilosema, nililichukulia kama lilivyo. Kwa mfano, sikuwa na uhakika iwapo ujio wake huo kweli ulitokana na ujuzi wake wa mitishamba au wa watekaji wake walikuwa wamwachie kutokana na ukubwa wa umri wake. Kwa kweli, sikujishughulisha kutafuta ukweli. Sikuwa na nafasi. Moyo wangu ulikuwa umefura kwa furaha ya kumwona tena. Matumaini ya kuendelea na safari yetu.
Nilitamani kushuka chini, ili nikutane naye na kumkumbatia. Lakini kana kwamba anayasoma mawazo yangu nilimsikia akisema, “Lala kama uko mahala pazuri. Kesho tutaanza safari mapema sana. Wale wajinga tayari wametuchelewesha sana.”
Sikuweza kulala.
* * *
Safari ilianza mapema kama ilivyokusudiwa. Tulishuka kwenye mti huo alfajiri sana, wakati kiza bado kimetanda. Tukakata miti ya kupunguzia umande na kujitoma tena katika vichochoro, katikati ya pori. Nilimfuata babu mgongoni mwake kiasi nikitetemeka kwa baridi kwa kweli sikujua tunaelekea upande gani wa dunia.
Aidha sikujua kama tunakwenda mbele au tunarudi nyuma.
Ilikuwa safari ngumu kuliko ilivyoanza. Akiba yetu ya chakula na maji ya kunywa ilikuwa imetoweka. Bila shaka vifurushi vile vikiwa vimeporwa na fisi au mbweha ambao walikesha chini ya mti ule tuliolala wakirandaranda huku na huko kwa matarajio waliyoyafahamu wao. Hata blanketi langu na nguo za babu za kubadili pia zilikuwa zimetoweka lakini kilichomsikitisha zaidi babu ni rupia zake kumi zilizokuwa ndani ya mzigo huo. Zilikuwa zimepotea pia.
Pamoja na kuficha hisia, zake niliweza kumsoma babu kuwa hana raha kabisa. Ile hamasa ya safari tuliyoanza nayo ilikuwa imetoweka tangu alipozitafuta pesa zake bila mafanikio. Hata hivyo hakutamka neno lolote la kunung’unika zaidi ya kunihimiza niongeze mwendo kila alipogeuka na kubaini kuwa ameniacha hatua nyingi nyuma.
“Tutakula nini?” Nilimchokoza kwa nia ya kuanzisha maongezi.
“Msitu huu unawalisha ndege wasio na mikono na wanyama wasio na akili za kutosha. Itashindwa kutulisha mimi na wewe?” Alinijibu kwa swali jingine.
Wakati jua linachomoza tulikuwa tuko mbali sana. Jua lilileta neema kwa kutuzawadia nuru. Pia lilituondolea umande toka kwenye matawi ya miti yaliyotufunika. Lakini
neema hiyo haikudumu. Muda mfupi baadaye jua liligeuka kero. Lilisababisha joto kali kiasi cha kufanya miili yetu iliyokuwa ikitetemeka kwa baridi, muda mfupi baadaye ilianza kuloa kwa jasho. Nadhani jua pia lilileta njaa na uchovu. Nilitamani kumwambia babu tupumzike. Nikasita. Nilimwona kama mtu aliyekuwa mbali kimawazo ambaye hangefurahia kubughudhiwa kwa wakati huo.
Hata hivyo, tulipofika kwenye mti mmoja wenye matunda ya porini, ambayo sikubahatika kuufahamu jina babu alisimama. Akanyoosha mkono na kuangua tunda moja lililoiva akalila. Nilifuata mfano wake. Matunda ya karibu yalipopungua niliamua kuyafuata hukohuko juu ya mti.
Tulikula kefu yetu. Kisha tukaendelea na safari. Huku mbele tulipata kijito chenye maji murua ambayo tuliyatumia kwa kunywa na baadaye kuoga. Tulipumzika chini ya kivuli cha miti mingi iliyoneemeka kando ya kijito hicho kwa muda kabla ya kuendelea na safari yetu.
Sikumbuki tulitembea maporini humo kwa siku ngapi. Wala sikumbuki idadi kamili ya matukio tuliyopambana nayo na yepi yalikuwa ya kutisha, yepi ya kuchekesha na yepi ya kusisimua. Nilichokumbuka ni kwamba ilikuwa safari ndefu, ngumu na ambayo iliambatana na kila aina ya visa na matukio. Baadhi ya matukio hayo yalikuwa ya kusisimua yaliyonipa ari ya kuendelea na safari.
Kwa mfano, lilikuwepo tukio la kukutana ana kwa ana na simba dume. Siku hiyo babu aliapa kuwa lazima tule nyama badala ya matunda na mizizi kama ndege. Alitafuta vichochoro vya wanyama na kujificha kando ya kimojawapo huku mkononi akiwa na pande kubwa la gogo. Haikuchukua muda mrefu kabla hajapita nguruwe mwitu katika uchochoro huo. Babu
hakuwa amejitayarisha vizuri. Hivyo, aliporusha gogo lake kwa nia ya kupiga kichwa cha mnyama huyo, alikosea shaba. Gogo lilianguka kando ya kichwa hicho. Nguruwe alikurupuka na kutimua mbio kali. Nilishangaa kuona babu akiokota gogo lake na kujificha palepale akitazama kwa makini upande alikoelekea mnyama yule.
Babu aliusoma mshangao wangu. Akacheka kidogo kabla ya kusema, “Atarudi njia hiihii. Nguruwe ni mnyama wa ajabu. Nadhani ana ubongo mdogo kuliko wanyama wengine wote. Huko mbele atachoka. Atakapojipumzisha usingizi mzito utamchukua. Akiwa amelala ataota ndoto ya tukio hili la leo. Ataliona kama la miaka mingi sana. Ataona kwamba aliwahi kupita njia fulani. Akakurupushwa na kitu fulani. Atakuwa hakumbuki ni kitu gani. Hivyo, atakapoamka ataamua kurudi njia ileile ili akaone kitu gani kilichomkurupusha. Hivyo ndivyo ambavyo wawindaji huwapata nguruwe kwa urahisi. Wanachokihitaji ni subira tu.”
Nilitamani kucheka. Lakini kwa kuhofia sauti ya nguruwe ingefichua maficho yetu, nilikaa kimya nikiutafakari ubongo wa nguruwe.
Kweli! Haikupita muda mrefu tulimwona nguruwe yuleyule akirudi njia ileile kwa kasi ileile. Nilimwona babu akiwa ameshangaa. Bila shaka alitarajia nguruwe yule aje taratibu, alitazama huko na huko kutafuta kulichomkurupusha mwaka jana. Safari hii babu alikuwa amejiandaa. Pigo la gongo lake lilitua barabaraba juu ya kichwa cha nguruwe. Nguruwe akapepesuka na kisha alianguka chali huku akirusha miguu yake huko na huko katika harakati za kuzuia uhai wake ulikuwa ukitoweka.
Mara jambo la ajabu likatokea. Hata kabla nguruwe huyo hajakata roho, mnyama mwingine mkubwa zaidi mwenye
shada la manyoya mabegani mwake alichupa na kutua juu ya nguruwe huyo!
“Simba!” babu alisema kwa nguvu. Mara moja mkono wake ukaelekea kiunoni mwake. Palipokuwa na kisu chake.
Inaelekea, kama babu, simba huyo hakuwa na ndoto ya kukutana na binadamu mahala hapo, muda huo. Ni wazi kuwa yeye ndiye aliyekuwa amemkurupusha nguruwe huko alikokimbilia kabla hajalala na kuota ndoto zake ambazo zingemfanya arudi njia hiyo. Simba alimkazia babu macho ya mshangao ambayo pia yalibeba dalili za hofu. Babu naye alimkazia simba macho yake. Akimtazama jicho kwa jicho. Mara nilimwona simba akiepuka macho ya babu kwa kuinama chini, kisha alipiga hatua za taratibu, moja baada ya nyingine akiliacha windo lake na kutokomea porini.
Mara alipoondoka babu naye aliniashiria kuondoka mara moja. Anaweza kurudi na akirudi hatakuwa na simile tena.” Babu aliniambia wakati tukiondoka harakaharaka.
“Simba amekukimbia!” Nilimwuliza babu hali ya kutetemeka mwili ilipoanza kunitoka.
“Binadamu ni mfalme wa dunia hii.” Babu alinieleza. “Pamoja na ukweli kuwa sisi ni dhaifu kuliko viumbe wengi duniani, bado tunauwezo na utukufu fulani juu ya viumbe wengine. Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, tuna uwezo wa kutawala hata majini na mashetani. Simba yule alishindwa kustahimili. Nuru yenye madaraka yaliyotoka katika macho yangu ilikuwa silaha tosha.”
Niliyatafakari maelezo yake kwa muda mrefu. Jambo hilo nahisi babu alilichukulia kuwa natilia mashaka maelezo yake. Hivyo, akanigeukia na kuniambia, “Zaidi ya utukufu huu tuliopewa na Muumba nina hii.” Toka kifuani mwake
alichomoa hirizi ndogo nyeusi iliyokuwa ikining’inia kifuani mwake siku zote.
“Hii ndio hasa inayotulinda,” alisema. “Niliirithi kwa babu yangu ambaye naye aliirithi kwa babu yake. Haijapata kutuangusha kamwe. Ilinipeleka Ughaibuni na ikanirudisha hapa salama.”
Tukio la pili ambalo pia sitalisahau ni lile la kujikuta tukiingia katika kundi la tembo wasipungua arobaini waliokuwa katika kitu kama tafrija au halaiki ya aina fulani.
Ilikuwa majira ya saa tisa au kumi za jioni. Mimi nilikuwa taabani kwa uchovu na njaa. Mayai mabichi ya kanga tuliyokula na matunda ya pori hayakukidhi haja yangu. Nilitamani sana kula ugali wa muhogo na kisamvu kisha nipooze koo kwa togwa tamu. Nadhani babu pia alikuwa amechoka. Alikuwa mkimya kuliko kawaida yake na alitembea taratibu kinyume na mazoea yake. Nilimwona akitazama huko na huko kama anayetafuta ama chakula ama mahala pa kupumzika. Wakati huo tulikuwa ndani kabisa ya msitu mnene wenye miti mingi mikubwa kwa midogo ambayo ilifanya nuru iwe hafifu na jua tulione kwa nadra sana. Mara tukasikia mlio wa waaa… waaa… waaa… uliosikika kwa sauti kubwa. Mlio huo ulifuatiwa na sauti kama hizo toka pande mbalimbali za msitu huo.
Tembo!
Wakati nikiwaza hilo niliona tembo watatu wakiwa wamesimama mbele yetu wakituangalia. Niligeuka kutaka kukimbia. Nyuma yetu walitokea tembo wengine huku mikonga yao ikielea huku na huku, pua zao zikichezacheza kama waliojaribu kuipata harufu yetu halisi. Mara tembo mkubwa zaidi alianza kusagasaga miguu yake ardhini huku akitumia
mkoa wake kukatakata matawi ya miti na kukanyagakanyaga kwa hasira.
Kamababuasingenivutamkonokwanguvunakuniashiria kukimbilia mti mkubwa uliokuwa karibu na kuupanda, pengine tembo huyo angenifuata na kunikanyagakanyaga huku nikiwa nimeduwaa kwa hofu na taharuki iliyonishika. Kwa jinsi nilivyokuwa nikitetemeka, miguu na mikono yangu ikawa imeishiwa nguvu kabisa. Sijui nilipata wapi uwezo wa kuparamia mti huo na kuupanda hadi juu, babu akinifuatia. Tulipofika mahala salama, ambapo tembo hao wasingeweza kutufikia, tuliketi na kuwatazama.
Wakati huo, zaidi ya tembo ishirini walikwishakusanyika chini ya mti huo wakipiga kelele kwa sauti zao mbaya, za kutisha. Yule tembo mkubwa alitufuata mbio na alipoufikia mti wetu alijaribu kuung’oa kwa mkonga wake lakini mti ulikuwa mkubwa mno. Mkonga wake haukuweza kuuzunguka ili aweza kuuongo’a. Alipokata tamaa, alianza kuupiga kwa pembe zake kubwa. Pia hazikufua dafu. Akaamua kumalizia hasira zake kwa kung’oa miti midogomidogo ya jirani na kuturushia. Haikufika.
Nilikuwa bado natetemeka mwili mzima hivyo nilimshangaa kumsikia babu akiangua kicheko ambacho kilifuatiwa na maneno ambayo katika mazingira tofauti na hayo, yangeweza kunichekesha pia. “Kweli ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi.”
“Una maana gani?” Baadaye nilimuuliza kwa sauti ya mnong’ono.
“Si unaona tembo hawa,” alinijibu. “Ni mkubwa kuliko wanyama wote wa nchi kavu. Baadhi yao wana ukubwa wa
nyumba ndogo na uzito upatao hadi kilo mia nne au zaidi. Lakini ubongo wao ni mdogo tofauti na maumbile yao. Wameshindwa kung’oa mti huu. Sasa wanashambulia miti midogomidogo isiyo na hatia. Kama sio ufinyu wa akili ni nini?”
Sikumjibu babu. Hali haikuniruhusu.
Tembo walipochoka waliamua kukaa chini ya mtu huo kana kwamba wanatusubiri hapohapo. Tukalazimika kulala juu ya mti huohuo na njaa yetu na kiu zetu.
Mimi sikulala.
Tembo waliondoka alfajiri sana kuendelea na safari zao.
Mie na babu pia tuliondoka na kushika hamsini zetu.
Ndiyo, ilikuwa safari ya kutisha iliyojaa visa na mikasa. Lakini kwa upande mwingine ilikuwa safari ya kusisimua ambayo kwangu ilitosha kuwa darasa mahususi ambalo si aghalabu sana kila mtu kukutana nalo. Ni safari ambayo ilinipa fursa na wasaha wa kuona mengi na kujifunza mengi.
Kwa mfano, tukiachana na tishio la simba na tembo, nilibahatika pia kukutana na burudani toka kwa ndege na wanyama wengine. Tuliweza kuingia na kutoka katika uwanda mpana uliojaa twiga na pundamilia kana kwamba wako zizini. Wakati pundamilia wanavutia kwa miramba yao iliyozunguka mwili mzima walitukimbia kidogokidogo kama mbuzi amkimbiavyo binadamu, twiga na mashingo yao marefu walitupuuza kana kwamba hatupo. Twiga walitumia shingo zao hizo kula majani na miche iliyochipukia juu kabisa ya matawi na miti. Miili yao mikubwa, miguu na shingo ndefu pamoja na rangi ya kuvutia yenye mabaka ya udongo kwa njano mpauko zaidi ule mwendo wao usio na haraka viliwafanya twiga waonekane kama wanaoringa na kujivunia umbile lao.
“Kama simba ni mfalme wa msituni basi twiga ni malkia wa mwituni.” Babu alisema baada ya kuona nilivyowakodolea macho yao kwa husuda kwa muda mrefu. “Nani kama twiga?” Kabla ya twiga hao, nilikuwa nimevutiwa sana na ndege ambao tuliwakuta eneo moja lenye mabwawa mengi. Babu aliniambia kuwa eneo hilo linaitwa Moyowosi nje kidogo ya
Kibondo.
Kando ya mkondo mmoja wa mto huo tuliwaona heroe, wenye miguu na shingo ndefu mfano wa twiga na mdomo ulipinda pia. Na ndege hao wekundu walipenda kuwinda ndani ya maji. Pia tuliwaona ndege waliofanana na jogoo ambao babu alinielekeza kuwa waliitwa jogoo mwitu Kwembe – Kisunzu ambao wanamkia mfupi na manyoya yaliyoota katikati ya paji la uso kwa mpangilio kama panga la jogoo. Hondohondo, kibeti, kisi, kiguudani kiparara na ndege wengine ainaaina pia tuliwaona katika safari hiyo. Kila mmoja alikuwa na rangi yake, mlio wake na tabia zake.
Jambo jingine lililonifuraisha katika safari hiyo ngumu ni jinsi babu alivyotumia kila fursa kunielimisha juu ya kile alichokiita, “mitishamba”. Alinionyesha majani haya na yale na kunieleza matumizi na manufaa kwa binadamu.
“Unaona mti hule? Unaitwa Mguluka. Ule ni mti muhimu sana. Jitahidi kuukariri. Unatibu magonjwa mengi sana hata yale sugu. Unatibu ngiri, degedege na magonjwa ya kina mama. Unachukua magamba au mizizi yake na kuichemsha kisha unainywa kwa siku saba, kwisha.”
Babu alinionyesha miti aliyoitaja kama mvumbasa, mshashu, muuka, mzungwa, ulenge, ungwia na mlonge kuwa ni matibabu muafaka kwa maradhi mbalimbali. “Si hiyo tu.”
Babu alinieleza, “Kabla hatujafika mwisho wa safari hii pia, nitakuonyesha pia mnyembe, uwe na mingineyo ambayo si tu kuw inatibu bali pia hurefusha maisha ya mtumiaji.”
Kuna wakati babu alinishtua ghafla, “Angalia! Usikanyage jani hilo. Ukilikanyaga kama uko porini peke yako, utapotea siku nzima bila kuona njia ya kurudi nyumbani! Litazame uzuri jani hilo na ulikariri!”
Wakati mwingine babu alisikiliza mlio wa ndege au mnyama fulani na kuniamulu kubadili mwelekeo kuwa huko mbele kuna hatari fulani, “Ama simba wanawinda au wameua wanyama ama sokwe mtu wametanda.” Alionya.
SURA YA TATU
Ile Palee, Nchi Wahaya
ulifika nchi ya Wahaya bila kutegemea. Mimi binafsi nilikuwa nimechoka kwa mwendo wa muda mrefu, kulala sehemu za ajabuajabu na
kula chochote kilichoweza kulika, jioni hiyo nilikuwa nikitembea kwa kujivutavuta, kama mzigo. Tulikuwa tukishuka toka juu ya kilima tulichopanda mchana wa jua kali, niliposikia ukelele wa furaha toka kwa mmoja wa watu tuliokuwa nao. Kelele hizo zilipokelewa na watu wengine zikifuatiwa na vicheko vya furaha.
Nilipoinua uso wangu kutazama huko wanakotazama wengine nilipigwa na butwaa. Takriban dunia nzima mbele ya macho yetu iligeuka kuwa uwanda mkubwa, mweupe unaomeremeta hadi upeo wangu kuona. Sikuelewa ninachokitazama hadi pale babu aliponishika bega na kuniambia, “Tumefika!” huku akitabasamu.
Sikumwelewa, “Tumefika wapi? Na kile nini
kinachomeremeta kiasi kile?” nilimuuliza.
“Yale ni maji. Lile ni ziwa Lweru, ambalo siku hizi nasikia linaitwa Victoria. Tumefika salama mwisho wa safari yetu. Ile pale nchi ya Wahaya.”
Ziwa! Ndio kwanza nikaelewa kile ambacho nimekuwa
nikikisikia juu ya maziwa na bahari. Katika safari yetu hiyo ndefu nilipata kuiona mito mingi, mikubwa, na kuivuka kwa mitumbwi. Kamwe sikupata kufikiria kuwa ziwa lingeweza kuwa kubwa na lenye maji mengi kiasi hiki! Niliduwaa kwa muda mrefu, nikiwa nimelitumbulia macho ziwa hilo kwa shahuku. Nilihisi uchovu ulikuwa umeniteka mwili mzima ukitoweka na nguvu mpya na ari mpya kuchukua nafasi yake katika nafasi yangu.
Msafara wetu huo ulioanza kwa upweke mkubwa kati yangu na babu, sasa ulikuwa wa kundi la watu wasiopungua kumi na wawili. Watu hao, Mwarabu mmoja mwenye ndevu nyingi nyeupe na upara kichwani, ambaye baadaye tuliambiwa kuwa anaitwa Sheikh Seif, alitajwa kama mfanyabiashara wa chumvi na pembe za ndovu. Mtu mmoja kati yao, mrefu sana, mweusi sana, tuliambiwa kuwa ni Mnubi toka Uganda na kwamba alikuwa msaidizi wake mkubwa kibiashara. Wengine, mmoja, akiwa Muha aliyelowea Kagera, wawili Wamanyema wa Kongo na waliobaki wakiwa Wanyamwezi wa Tabora walikuwa wapagazi wake, walioajiriwa kwa safari hiyo pekee.
Tulikutana na watu hao katika kijiji kidogo kilichoitwa Kakonko. Siku hiyo babu alishauri tutafute eneo lenye watu ili tuombe msaada wa chakula cha binadamu zaidi, baada ya kukinaishwa na matunda na nyama za kuchomwa ambazo tulizila bila ugali wala chumvi. Mzee mmoja kijijini hapo alitudokeza juu ya kuwepo kwa wageni wengine kama sisi, waliokuwa wakitokea kwenye biashara ya kubadilishana nguo na shanga kwa chumvi za magadi iliyokuwa ikipatikana katika mabwawa ya maji huko Uvinza, Kigoma.
Tulitambulishwa na watu hao na mara moja wale Wahaya wakaanza kumtania babu kwa kumwita ‘mtani’.
“Msiwe na wasiwasi,” mmoja wao alisema. “Hawa Wamanyema hawawezi kuwala mbele yetu. Tutawafikisha kwetu salama na kuwapatia vibarua kwenye mashamba yetu.”
Babu naye hakuwa mgeni kwa matani, “Nyama yenu chungu hailiki,” aliwajibu. “Wakijaribu tu kuionja watavimbiwa na matumbo yao kufura kama ya tembo. Halafu, huko kwenu hatuendi kutafuta kibarua. Tunakwenda kutafuta vibarua, waje wafanye kazi ya kurina asali katika misitu yetu.”
Wamanyema wale walicheka sana, Wahaya walicheka pia. Hata Mwarabu, ambaye alicheka kwa nadra sana safari hiyo alitabasamu na kuruhusu pengo moja la meno ya juu kuonekana. Mmanyema mmoja, aliyeonekana kuvutiwa zaidi na mimi kuliko babu, alinivuta kando na kuninong’oneza, “Msimchekee sana yule Mwarabu. Mnajua alikuwa akifanya biashara gani zamani? Hata kabla sijamjibu aliongeza, “Biashara ya watumwa. Hapo ulipo bila shaka anakutamani sana. Kwa jinsi ulivyo kijana, mwenye afya nzuri na wajihi wa kupendeza, enzi zake angekuuza kwa faida kubwa sana kuliko babu yako. Tena kwa jinsi alivyokuwa katika enzi hizi, kama angekukamata wewe na babu yako angempiga babu yako rungu la kichwa na kumwacha aliwe na tai, wewe angekupeleka hadi Bagamoyo au Zanzibar ambako angekupeleka mnadani, huku ukiwa umefungwa mnyororo mikononi na miguuni.
Sikujua kama bwana huyo alitaka niichukulie vipi taarifa hiyo, nicheka au nilie? Nilimkodoea macho, jambo alilolitafsiri kuwa ni kuvutiwa na simulizi zake. Hivyo, akaongeza, “Siku hizi amekwisha. Tangu biashara ya utumwa ilipopigwa marufuku amekuwa mtu wa kuuza shanga na chumvi, sio binadamu.
Nilimtazama Mwarabu huyo. Kweli aikuwa akinitazama pia. Lakini macho yake hayakutoa tafsiri yoyote ya ama
kunitamani ama kunipangia bei. Alikuwa bado anatabasamu, tabasamu la kibinadamu!
Tulilala kijijini hapo siku mbili. Kwa kiwango fulani tulilala vizuri na kula vizuri. Hivyo, safari ilipoanza tena nilikuwa mchangamfu, tayari kwa safari.
Wenzetu hao walikuwa na mizigo mikubwa. Walikuwa na pembe nne, kubwa sana, za ndovu, ambazo walizibeba kwa kupokezana. Walikuwa pia na viroba vinne vya chumvi, makapu mawili ya chakula na gudulia la maji. Tuliamua kuwasaidia. Mimi nilikabidhiwa kapu moja la chakula, babu akabeba lile gudulia la maji.
Msafara ukiwa mkubwa kidogo, haukupungukiwa simulizi za uongo na kweli. Utani, michapo na pengine nyimbo za kikabila ziliibuka mara kwa mara kiasi cha kufanya niichukulie safari hiyo kama tukio la kuvinjari tu katika nchi yangu. Tulivuka mito na vijito, tulipenya msitu na misitu, tuliwaona ndege na wanyama wa kila aina. Ndiyo, kuna nyakati tulichoka na kukata tamaa kutokana na njaa, mbu, uchovu na kero nyingine za porini. Lakini, kwa namna moja au nyingine, kero hizi ziliondokea kuwa kama sehemu ya burudani, kwani hakuna raha isiyo na karaha. Hadi tunaliona ziwa likimeremeta mbele yetu, kana kwamba linatulaki kwa vicheko na tabasamu, nilipata hisia kuwa safari yetu ilikuwa ya kheri na mafanikio yalikuwa yakitusubiri.
Muda mfupi baadaye tulifika pwani ya ziwa, katika kijiji cha wavuvi kilichokuwa kando kidogo ya kijiji cha Kashozi. Ilionyesha kuwa Mwarabu huyo na msafara wake walikuwa wenyeji katika kijiji hicho, kwani tulipokelewa juujuu na kuandaliwa chakula murua, ndizi zilizopikwa vizuri kwa samaki wakubwa aina ya sato. Baadaye tulipewa rubisi ambayo mimi
nilionja kidogo tu, kabla ya kuonyeshwa sehemu ya kulala.
Usingizi ulinipokea juujuu, wengine wanaita usingizi wa kifo, kwani nililala zaidi ya masaa kumi na mawili, bila kushtuka, kuzinduka wala kuota ndoto yoyote ile. Nilipofumbua macho ilikuwa kesho yake, saa mbili au tatu za asubuhi. Wavuvi walikuwa wakitoka ziwani, mitumbwi yao ikiwa imejaa samaki aina ya sato na sangara.
Nilimwona babu akiwa kando ya ziwa, akizungumza na mmoja wa wenyeji wetu, mzee mpole, ambaye baadaye niliambiwa kuwa anaitwa Buberwa, rafiki wa karibu wa ‘Mtume wa karagwe’ mwalimu Ibrahimu Kazigu.
* * *?
Ujio wa kigeni katika mkoa wa Kagera haukuwa lelemama. Kwanza kabisa, Wahaya walikuwa na mungu wao ambaye walimwamini na waliamini kabisa kuwa aliwatatulia matatizo yao. Mungu huyu alijulikana katika majina mbalimbali kama Ruhenga; Mweza wa yote, Mutonzi; Muumba, Nyakubao; Aliyepo, Nyakumerera; Wa milele na kadhalika. Jina kubwa zaidi lililojumisha miungu hio likiwa lile la Mugasha; Mungu wa mvua, Mlinzi wa mito, ziwa, wavuvi na samaki.
Wahaya walikuwa hawatoi zaka wala sadaka. Hali kadhalika, walikuwa hawatoi kafara. Siku zote waliamini kuwa mungu wao alikuwa na kila kitu, kamwe asingehitaji chochote kutoka kwa viumbe wake.
Dini za kigeni zinaweza kuelezewa kuwa ziliingia Kagera kwa kupitia mlango wa nyuma. Mnamo mwaka 1878 mapadri wa kwanza wa kikatoliki walifika Zanzibar wakitokea Algiers, Aljeria. Mapadri hao walitawanyika hadi kufika Uganda kwa Kabaka Mutesa, aliyekuwa mfalme wa himaya ya Buganda,
kumwomba msaada. Mapadri hao walipata upinzani mkubwa sana toka kwa Waislamu ambao walikwishatangulia nchini humo na kumsilimisha Kabaka mwenyewe, pamoja na Wakristu wa madhehebu ya ki-prostetanti ambao pia walikuwa wametangulia. Hata hivyo, Mutesa aliridhia maombi yao na kuwapa mashua iliyowafikisha Bukoba April 1880.
Kumbe Mutesa alikuwa akiwala kisogo. Wakati akijitia kuwasaidia alikuwa pia akitangaza taarifa kwa watemi wa Kagera ambao wengi wao walikuwa wakiwajibika kwake, akiwaagiza kutowapa ushirikiano wamisionari hao. Iliwachukua wamisionari hao miaka kumi na miwili kuweza kuanzisha kazi yao ya kutawanya ‘neno la bwana,’ katika eneo hilo.
Katika eneo hilo la Karagwe watemi Kahigi na Kyobya walikuwa wameshiriki sana kugomea jitihada hizo za kuanzisha kanisa katoliki. Hali kadhalika, upinzani kati ya utawala wa Wadachi waliokuwa madarakani na Waingereza ambao waliwang’oa Wadachi madarakani ulichangia sana katika vita dhidi ya madhehebu ya kikristo. Itakumbukwa kuwa mtemi mmoja wa enzi hizo, aliyejulikana kwa jina la Ntare, alitolewa mhanga katika changamoto hiyo kwa kushtakiwa kwa Wadachi kuwa alikuwa akiwakaribisha Waingereza. Mtemi huyo alihukumiwa kifo na kunyongwa mwaka 1916.
Mwaka huohuo wakati Mwami Ntare ananyongwa mtu mmoja aliyekuja itwa Ibrahimu Kazigu alibatizwa, akiwa na umri wa miaka kumi na mitano. Wana Karagwe wanamwelezea bwana huyu kuwa ni mfano wa mtume Paul, kwani alikubali kuacha kila alichokuwa nacho na kujitolea kulitumikia kanisa. Bwana huyu alitumikia kanisa kwa zaidi ya miaka thelathini na miwili akihubiri, kuanzisha makanisa, kuanzisha shule
na kubatiza. Mapadri walipokuja kuanzisha misheni eneo hilo, kule Bugere, mwaka 1934 walikuta tayari Karagwe ina waumini wapatao elfu mbili na wanafunzi, wake kwa waume takribani mia nane.
Ni mtu huyu, Kazigu ambaye babu alinikabidhi kwake kupitia kwa mwenyeji wetu Buberwa, ambaye aliondokea kuwa rafiki mkubwa kwa babu. Kitendo cha kuambiwa kuwa tumesafiri safari ndefu, toka nchi ya mbali, kwa ajili ya kuja kufuata ‘neno’ na elimu kilimfanya Ibrahimu Kazigu aliyekuwa hapo Kashozi wiki mbili baadaye kukutana na wamisionari, anipokee kwa mikono miwili. Akanitia mikono kichwani na kunibariki. Jumapili iliyofuata nilibatizwa na kupewa jina la Petro, badala ya langu la zamani la Mtukwao ambalo niliambiwa kuwa ni la kipagani. Kisha nikakabidhiwa katika shule maalumu ambazo zilikuwa zikipokea watoto yatima na wale waliokombolewa kutoka utumwani hasa wakitokea Kongo, Rwanda Uganda.
Babu hakushiriki sherehe za ubatizo wangu. Alitoroka usiku wa kuamkia siku ya ubatizo kwani ‘mtume’ Ibahimu Kazigu alikuwa amemtaka yeye pia kubatizwa kwa maelezo kuwa ‘ameona mwanga, hastahili tena kukaa gizani.’ Lakini babu hakuwa tayari. Alishindwa kumkatalia Ibrahimu kimachomacho kwa ajili ya kuchelea kuharibu jitihada alizofikia juu yangu. Ndipo akaamua kutoroka. Lakini haikuwa kabla ya kuchanjiana damu na rafiki yake Buberwa, hatua ambayo ilihitimisha urafiki wao na kuwafanya ‘ndugu wa damu.’
Tuliagana na babu kwa siri, katika uchochoro wenye kiza, hivyo sikuweza kuyaona macho yake kuona kama anachosema yalikuwa yakitoka mdomoni au moyoni. Alisema maneno machache yaliyojaa pongezi kwa uvumilivu wangu
wa kuweza kuikamilisha safari ile ngumu. Pia alishukuru kwa jinsi jitihada hizo zilivyoweza kuzaa matunda kwa urahisi kuliko alivyotegemea.
“Nakuacha mikononi mwa rafiki yangu wa damu na mtu wa Mungu. Sina shaka kuwa utaishi salama na utapata elimu itakayokupa nafasi katika dunia hii,” babu alisema na kuongeza, “Sina cha kukupa mjukuu wangu. Kitu pekee nitakachokuachia ni hiki.” Alivua hirizi iliyokuwa shingoni mwake na kunivisha. “Hii ni hirizi ya bahati. Ilinde nayo itakulinda maishani mwako. Kamwe usiiweke mbali nawe.”
Nilijikuta nikilengwalengwa na machozi. “Babu hii ni hirizi yako. Imekulinda maisha yako yote. Ukinipa mimi huoni kama maisha yako yatakuwa hatarini?” nilimwambia.
“Hapana mjukuu,” babu alinijibu. “Mie hirizi hii niliirithi kwa baba, ambaye aliirithi kwa baba yake. Ni hirizi ya familia. Wewe unaingia katika safari ndefu ya maisha. Unaihitaji kuliko mimi na baba yako tunavyoihitaji sasa.”
Nikaipokea na kuivaa.
“Halafu uifiche sana,” babu alionya. “Hawa watu wa kanisa kwao kila kitu chetu cha asili kwao ni dhambi. Wakiiona wataipokonya na kuichoma moto. Ifanye siri yako, siri ya moyo wako.”
Baada ya maneno hayo babu alinitemea mate katika paji la uso na kunitakia kheri. Kisha akageuka na kutoweka gizani.
Nilishindwa kujizuia. Machozi yalinitoka.
Laiti ningejua kuwa agano hilo lilikuwa la mwisho, kwamba nisingemwona tena babu yangu, nisingekubali kuachana naye kirahisi kiasi kile.
“A!”
“Ahaaaaaaaaa!” “E!”
“Eheeeeeee!” “I!”
“Ihiiiiiiiii!” “Oh!”
“Ohoooooo!” “U!”
“Uhuuuuuuuu!”
“a,” inaandikwa kama punje ya harage….’e’ iko kama ndizi iliyovimba juu…. ‘I’ ni kama msumari… ‘o’ ni kama yai…. ‘u’ ni kama shimo. Mnanielewa?”
“Ndiyoooo!”
Mtukwao, bin Karimanzira bin Kionambali nilikuwa nimeanza shule. Hapana! Sikuwa tena Mtukwao, wala Karimanzira. Nilikuwa na jina jipya, Petro Kionambali. Ndivyo nilivyoandikishwa. Ndivyo nilivyokuwa nikiitwa na walimu na wanafunzi wenzangu katika maisha na mazingira hayo mapya.
Tuliishi katika mabweni, tukiwa wavulana wapatao sitini au sabini hivi. Wengi wetu tulikuwa watu wa makabila tofauti, utamaduni tofauti na hata maumbile tofauti. Tulitofautiana pia katika umri. Wakati mimi nilijiona mdogo kwa umri wangu wa miaka kumi na mitatu, walikuwepo kaka zetu wenye umri wa miaka kumi na saba katika darasa hilohilo la kwanza. Wengine walikuwa wadogo kabisa kwa miaka yao kumi hadi minane.
Tulifundishwa kusoma na kuandika. Lakini mkazo mkubwa hata kabla hatujaanza kusoma na kuandika ulikuwa wa mafundisho ya dini. Tulifundishwa upendo, kusali pamoja
na kuimba nyimbo za kumsifu bwana. Tulifundishwa kila kitu juu ya mungu wa Izrael, aliyemtuma mwanawe wa pekee, ili azaliwe kama binadamu katika zizi la kondoo, ateswe, asulubiwe na kufufuka siku ya tatu baada ya kifo chake kwa ajili ya kutukomboa na dhambi zetu. Zaidi, tuliambiwa kuwa tayari siku zote, kwani haikujulikana siku wala saa ambayo angerudi tena duniani na kuwachukua ‘wateule’ wake na wale wasio wake kutupwa jehanamu ambako wangeungua kwa moto mkali wa milele.
Nikijua kuwa nilikuwa nimetembea safari ndefu na ngumu kuifuata fursa hiyo ya kupata elimu nilitilia maanani kila nilichofundishwa na kuzingatia kila fundisho la dini. Jambo hilo lilinifanya baada ya siku chache tu niwe mmoja wa wanafunzi hodari sana shuleni hapo. Walimu walinipenda, wanafunzi walinisikiliza. Hivyo, haikuwa ajabu pale, ulipofika mwisho wa mwaka huo nilipoteuliwa kuwa kiranja wa darasa langu.
Mafunzo ya dini pia niliyazingatia sana. Sikuwa na sababu wala wasaa wa kuiba, sikuwa na haja ya kumtukana mtu wala kumzulia uongo. Kama kuna dhambi pekee, ambayo siku zote ilinisuta moyoni basi ilikuwa ile ya kundelea kuthamini na kuivaa kwa siri hirizi yangu niliyoachiwa na babu. Sikuwa tayari kuitoa kwa shemasi au kasisi ili ichomwe moto. Nilichukulia ile kama kiungo pekee baina yangu na familia yangu, kiungo ambacho kukitoa ingekuwa sawa na kuukata mzizi wa mwisho; kati yangu na asili yangu.
Elimu niliyoipata katika nchi hiyo ya Wahaya haikuwa ile ya darasani wala ya dini pekee. Nilipata elimu ya mitaani ambayo kwa kweli ilinisaidia sana. Kwa mfano, wakati shule hazikufundisha lugha ya Kihaya, huko mitaani nilifundishwa.
Ndani ya mwaka mmoja tu nilikuwa tayari nikisikia na kuzungumza Kihaya kwa ufasaha kama Muhaya yeyote yule.
Shule hatukufundishwa kuogelea. Lakini mimi katika kipindi hichohicho cha mwaka mmoja tayari nilikuwa hodari wa kucheza na maji kama samaki. Niliweza kuelea juu ya maji kama boya au kupiga mbizi kama sangara. Hali kadhalika, nilijifunza kupiga makasia na kuvuta aina kwa aina za samaki. Kwa kushika maji au kuangalia mwenendo wa mawingu angani nilijua ni wakati gani ziwa lingechafuka kwa upepo mkali, wakati gani limepungua.
Kwa kiasi kikubwa ‘utundu’ wangu ziwani ulichangiwa na mapenzi makubwa niliyokuwa nayo kwa ziwa hilo toka pale nilipoliona kwa mara ya kwanza. Nililichukulia kama hazina ya pekee tuliyojaaliwa na Muumba kwa kuzingatia kuwa nchi nyingine badala ya maji hayo mengi wao wamejaliwa majangwa yaliyojaa mchanga na joto kali. Nililichukulia ziwa hilo kama hazina ndani ya hazina. Wingi wa samaki waliojaa katika ziwa hilo, aina waliokuwa wakiishi ndani au kando mwa ziwa hilo ulikuwa ushahidi tosha wa utajiri huo.
Mtu aliyechangia kunipa elimu na ujuzi mwingi juu ya ziwa hakuwa mwingine zaidi ya mzee Buberwa, baba yangu wa kufikia. Kila nilipopata likizo nilikuwa nikienda kwake ambako nilishirikishwa katika uvuvi na kuweza kujipatia si ujuzi tu bali pamoja na vijisenti vya matumizi kutokana na mchango wangu katika uvuvi. Mtoto wake mkubwa, Muleju, aliondokea kuwa rafiki yangu mkubwa na ndiye aliyenipa darasa la awali la kuogelea. Madarasa yaliyofuata nilijifunza mwenyewe kutokana na ujasiri na jitihada zangu.
Buberwa alikuwa mzee aliyependa sana utani. Hakuchoka kuniambia mara kwa mara, “Mwanangu
tumekupeleka shule kuchukua elimu. Hatukukupeleka pale kujifunza utawa na upadri. Chukua elimu yako, usichukue upadri wao. Nataka ukimaliza shule nikupe msichana mrembo wa Kihaya, umuoe na kurudi naye kwenu. Watu wa huko wajue Mungu alivyopendelea nchi ya Wahaya si kwa samaki na maji pekee, bali pamoja na wajihi murua wa wakazi wake.” Kuoa! Nililichukulia kama jambo ambalo lingenitokea baada ya karne nyingine zijazo. Sikupata kumjibu kwa hilo. Naye nadhani hakutegemea jibu langu. Ilikuwa kama mtu anayenikumbusha jambo fulani, mara kwa mara, ili lisije
likanitoka akilini.
Nimezungumza mengi juu ya raha za ziwani, raha za kula samaki watamu, raha za kuelea juu ya maji, raha ya kupata fedha kutokana na mauzo hayo. Pengine haitakuwa haki kama sitataja chochote pia juu ya karaha zake pia.
Wanasema, wavuvi wengi kwamba ukiwa ziwani ujue kuwa unatembea na ‘kifo mkononi.’ Madai ambayo niliyadhibitisha kwa vitendo kwa uhai wangu wa ziwani hapo.
Tukio la kwanza lilikuwa lile la kupotea ziwani. Siku hiyo tulikwenda kuvua samaki usiku. Ghafla, ulizuka upepo mkubwa ulioambatana na mvua nzito ambayo ilifanya karabai tulilokuwa tukilitumia kwa ajili ya mwanga lizimike. Upepo huo ulisababisha mawimbi makubwa yaliyofanya mara kwa mara maji yaingie ndani ya mtumbwi. Huku nikitetemeka nilipewa kazi ya kuondoa maji hayo yaliyoingia huku wenzangu wawili waliobakia wakijitahidi kupiga makasia kurudi ufukweni. Zilikuwa jitihada zisizo na matunda. Kwanza, kutokana na kiza kilichotanda hakuna aliyefahamu nyumbani ni upande upi. Pia, kasi ya maji kuingia katika mtumbwi ilikuwa kubwa kuliko ile ya kuyaondoa. Muda mfupi baadaye wenzangu walikata
tamaa ya kupiga makasia bila kujua kama wanakwenda mbele au wanarudi nyuma. Wakajiunga nami katika jukumu la kuondoa maji katika mtumbwi. Haikusaidia. Muda mfupi baadaye mtumbwi wetu ulizama na kupinduka. Tukaogelea na kupanda juu ya mgongo wake huku tukipiga kelele kuomba msaada.
Katika purukushani hizo mwenzetu mmoja alipotea. Nadhani alichoka kuendelea kuung’ang’ania mgongo wa mtumbwi ambao ulikuwa ukiyumba na kutupwa huku na kule kwa mawimbi hayo. Mimi na Muleju tuliendelea kung’ang’ania hadi alfajiri, upepo huo ulipopoa.
Tulishinda ziwani humo, juu ya mgongo wa mtumbwi huo tukiwa hatuna la kufanya. Makasia yetu yalikuwa yamechukuliwa na mawimbi na uwezo wa kuufunua mtumbwi huo hatukuwa nao.
Siku ya kwanza na usiku wake ukapita. Siku ya pili, jioni sana, tukiwa tayari taabani kwa njaa na uchovu, tuliona mtumbwi wa wavuvi ukitujia. Hawa walituzoa na kutupakia kwenye mtumbwi wao kisha wakajitahidi kuubinua mtumbwi wetu na kuondoa maji yaliyokuwemo. Wawili kati yao waliingia katika mtumbwi huo na kuupiga makasia kuelekea ufukoni. Ufukwe huo uliondokea kuwa kisiwa kidogo cha Bumbire, mbali sana kutoka Kashozi tulikoanzia safari.
Tulipumzika kisiwani humo kwa siku tatu zaidi, kabla ya kurejea nyumbani ambako walikwishakaa matanga wakiamini kuwa nilikwishakufa. Tuliopona tulifanyiwa sherehe ndogo, mwenzetu aliyepotea aliombolezwa kwa taratibu za kimila.
Nikiwa na hakika kuwa kilichoniokoa katika mkasa ule ilikuwa ile hirizi yangu niliyopewa na babu, ambayo muda wote ilikuwa kifuani mwangu, niliibusu na kuikumbatia kwa
furaha, “Nitakulinda daima, ili nawe unilinde,” niliinong’oneza. Katika hali ya kawaida, tukio hilo lingetosha kabisa niliogope ziwa hilo kama simba mla watu. Lakini, kwa jinsi ziwa lilivyokwishaniingia akilini niliichukulia tukio zima kama jambo la kawaida tu, katika pilikapilka za maisha. Nikaendelea
na shughuli zangu bila hofu wala wasiwasi wowote.
Tukio lililofuata, ambalo pia sikulitegemea kiasi lilikuwa kama la kuchekesha. Nilikuwa nikiogelea kando ya ziwa, baada ya kazi ya kutwa nzima za mchana huo. Nadhani nilikuwa nimeogelea kwa muda mrefu kiasi, kwani nilijihisi uchovu mwingi. Mara nikaona kitu kama gogo likielea juu ya maji mbele yangu. Nikalifuata na kuparamia juu yake ili nipumzike kidogo. Nilishangaa kuona gogo hilo likizama ghafla na kisha likiibuka hatua chache mbele yangu na kufunua domo lake kubwa ama kupiga mwayo ama kunifokea.
Mamba!
Nilikuwa nimeparamia mgongo wa mamba. Kwa kujua kuwa mamba hana uwezo wa kumnasa mtu katika maji mengi niliogelea harakaharaka kupanda ziwani. Zilipogeuka nilimwona mamba yule akiogelea kurudi ufukoni. Ama alikuwa ameshiba sana, ama alishtuka mie kukimbia.
Hilo na lile la kukoswakoswa na kiboko mmoja aliyefanikiwa kupindua mtumbwi wetu ni miongoni mwa matukio mengi, ya kutisha yaliyoambatana na maisha yangu katika ziwa hilo.
Kwa kupona hatari baada ya hatari, huku nikiendelea kupata mafanikio kimaisha na kitaaluma niliamini kabisa kuwa hirizi yangu ilikuwa ikitimiza wajibu wake. Mara kwa mara niliibusu na kuinong’oneza, “Nitakulinda daima ili nawe unilinde.”
SURA YA NNE
Hirizi yazua jambo.
ana mkasa iliyosababisha safari yangu kielimu ikome baada ya miaka mitano tu.
Wakati huo nilikwishashuhudia watu wote waliovuka miaka kumi na minane akihesabiwa katika kile kilichoitwa sensa ya kwanza nchini Tanganyika. Tukio hilo lililofanyika Julai mosi, mwaka 1931. Mimi sikuhesabiwa kwa ajili ya umri na hata kama ningekuwa na umri nisingehesabiwa, kwani Makarani wa kazi hiyo walikuwa wakihesabu wakuu wa kaya pekee na kisha kwenda kutengeneza hesabu zao. Jambo hilo lilileta manung’uniko kuwa kazi hiyo haikufanyika kwa ufanisi.
Pia, wakati huo nilikuwa nikidonoadonoa maneno kadhaa yaliyoandikwa katika gazeti la Kiingereza lililoitwa Tanganyika Standard, ambalo lilikuwa limeanzishwa huko Dar es Salaam mwaka uleule wa hesabu ya watu.
Ni kupitia gazeti hilo nilipofahamu kuwa Gavana wa nchi wakati huo aliitwa H.A MacMichael akiwa amemrithi
G.S Symes ambaye naye alimrithi D.C Cameron. Wote hao walikuwa wamemfuatia Gavana wa kwanza wa Uingereza nchini aliyeitwa H.A Byatt, aliyepewa wadhifa huo mara baada ya Wajerumani kupokonywa nchi ya Tanganyika mwaka 1920.
Naikumbuka vizuri sana siku ya balaa. Ilikuwa tarehe
4 Novemba, 1934. Kule Dar es Salaam kulikuwa na kikao muhimu cha watawala kilichoitwa Kamati ya Ushauri wa Elimu kwa Mwafrika. Kamati hiyo ilipinga wazo la wanafunzi wa Kiafrika kuchangia mitaala na madarasa ya Wazungu au Waasia kwa madai kuwa uwezo wa watoto wa Kiafrika kuelewa wanachofundishwa ulikuwa duni sana ukilinganishwa na Wazungu na Wahindi. Hata hivyo, mjumbe mmoja, aliyeitwa Martin Kayamba, alipinga vikali madai hayo. Alisema, “Huwezo wa mtoto wa Kiafrika haukuwa na tofauti yoyote na ule wa Wazungu au Wahindi bali tatizo pekee lililosababisha hisia hizo zijitokeze ni watoto hao kutopewa nafasi sawa na wengine.”
Habari ambazo shuleni hapo, miongoni mwa walimu na wanafunzi, zilikuwa kubwa sana. Kayamba alisifiwa na kupongezwa sana kwa kitendo chake cha kuwapa wakoloni ukweli.
Kwa utoto wetu tuliamini kauli yake ingekuwa mwisho wa kutengwa na mwanzo wa kuruhusiwa kusoma pamoja na watoto wa Wazungu na Wahindi ambao walikuwa na shule bora mara kadhaa zaidi yetu. Tulikuwa katika vijikundi vidogovidogo tukijadiliana juu ya hilo baada ya masomo ya kutwa nzima tulipozinduliwa na kelele za baadhi yetu ambao walikuwa tayari wakikimbilia nyuma ya shule wakibeba mifuko na mabakuli.
“Senene!” mmoja wetu alitamka. Mara alikurupuka na kupiga mbio kuwafuata wengine.
Ulikuwa msimu wa senene. Mara nyingi msimu huo uliambatana na ule wa kumbikumbi ambao ni jamii ya mchwa ambao huota mbawa na kuruka kwa makundi makubwa angani kwa muda mfupi. Baadaye kuishiwa uwezo wa kuruka
na kudondoka ardhini huku mbawa zao zikinyofoka.
Wakishapoteza uwezo wa kuruka kumbikumbi huzagaa ardhini wakitafuta namna ya kurudi katika vichuguu vyao. Wengi huishia kuwa kitoweo cha binadamu na ndege. Kati ya wachache ambao hubaatika kunusurika mmoja wao hugeuka Malkia ambaye hutaga maelfu kwa maelfu ya mayai hivyo kuanzisha upya kizazi chao. Hao ni kumbikumbi.
Senene, ambao ni jamii ya panzi, ni maarufu zaidi kwa wakazi wa eneo hilo jirani. Wao wana tabia ya nzige, ingawa hawana madhara makubwa kama ndugu zao hao ambao wanaweza kugeuza pori kuwa jangwa kwa muda mfupi sana.
Senene, ni chakula maarufu zaidi, na kwangu mimi walivutia zaidi. Hivyo, kama wenzangu wote sikuweza kujizuia. Nilikimbia huko na huko na kuwakamata wengi tu ambao niliwajaza katika mfuko ili kesho niweze kuwaanika na kisha kuwahifadhi kwa matumizi ya baadaye.
Na baada ya pilikapilika hizo, wakati tukiwa katika sala ya mwisho kabla ya kulala nilipohisi upungufu fulani katika mwili wangu. Nimepoteza nini? Nilijiuliza huku nikijipapasa. Haikunichukua muda kubaini kuwa hirizi yangu, ambayo tunapokuwa darasani nilikuwa na tabia ya kuhifadhi mfukoni, ilikuwa imetoweka! Bila shaka ilidondoka katika zile purukushani za kunasa senene.
Hirizi yangu! Niliwaza kwa uchungu, nikihisi nguvu zote zikiniisha mwilini. Ibada iliyokuwa ikiendelea haikuniingia akilini. Nilitamani kutoka nikaitafute lakini tayari ulikuwa usiku mwingi, kwanza nisingeiona, pili nisingeruhusiwa kutoka.
Usiku huo usingizi ulinikata kabisa. Alfajiri sana, kabla ya mtu yeyote kuamka mimi tayari nilikuwa nje nikijaribu
kupita kila mahala nilipohisi kuwa ningeweza kuidondosha. Sikuipata.
“Unatafuta nini?” nilisikia sauti ya mtu ikizungumza nyuma yangu. Nilipogeuka nilimwona Byabato, mwanafunzi mfupi, mnene, ambaye kwa kweli hakupata kuwa rafiki yangu.
“Natafuta kalamu yangu,” nilidanganya.
“Kalamu! Utaiona kweli saa hizi? Kwa nini usingoje jua lichomoze?”
“Siyo kazi yako!” nilimwambia
Byabato alinitazama kwa mshangao. Mara nikamwona yeye pia anaanza kutafuta kitu huko na huko kama mimi. Ilikuwa zamu yangu kushangaa.
“Unatafuta nini?” nikamuuliza.
Naye akanipa jibu lilelile ambalo mimi nilimpa dakika mbili zilizopita, “Siyo kazi yako!”
Kihoro kilinipanda. Kwa jinsi nilivyomfahamu Byabato nilijua kuwa kama angeipata hirizi ile asingesita kubaini kuwa ndiyo nilikuwa naitafuta. Na kwa tabia yake asingekuwa mtu wa kuniwekea siri. Ingemchukua dakika chache sana kuitangazia shule na dunia nzima kuwa nilikuwa na hirizi. Sikuwa na namna ya kumzuia. Nilichofanya nilijaribu kumpoteza kwa kutafuta sehemu ambayo nilikuwa na hakika kuwa sikuifikia. Lakini, kwa mshangao wangu yeye alielekea upande wa pili, ambako ndiko hasa nilikopita katika nyendo zangu.
Nilishukuru pale kengele ya kujiandaa kuingia madarasani ilipolia kabla sijaipata wala kumwona Byabato akiiokota. Nikaondoka kinyonge na kurejea bwenini kujiandaa.
Nilikuja kuiona tena hirizi hiyo saa nane za mchana. Kuiona, siyo kuipata rafiki yangu! Kwani ilikuwa mikononi mwa Padri Backhove aliyekuwa ametembelea eneo hilo ili
kukagua maendeleo ya shule na maendeleo ya wanafunzi na waumini wengine kiimani.
Ilikuwa baada ya mlo wa mchana, ambao mimi niliula kidogo sana, kengele ya dharura ilipigwa na wote tukakusanyika katika ukumbi wa ibada. Padri alianza kwa kutoa nasaha au somo refu juu ya raha inayotusubiri huko mbinguni na mateso makali ya moto wa milele unaowasubiri huko jehanamu wote ambao watakwenda kinyume na amri kumi za Mungu. “Mungu wetu ni mwenye wivu,” aliongeza Padri. “Moja ya amri zake kumi, alizozileta kwa mkono wa mtumishi wake Musa pale kwenye mlima Sinai inasema waziwazi, ‘Usiitumikie miungu mingine ila mimi’ Sawa?”
“Sawa,” wote tuliitikia.
“Mungu wetu ni msafi,” Padri Backhove aliendelea, “Anapenda wote tuwe wasafi wa miili na mioyo yetu. Sawa?”
“Sawa.”
“Kumfuata bwana maana yake ni kukana dhambi. Kukana mila na desturi zetu zote potofu na kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Maisha safi kimwili na kiroho. Mkristo wa kweli hatakiwi kuamini uchawi. Hatakiwi kuabudu sanamu… Hatakiwi kuvaa hirizi… sawa?”
Mara lilipotajwa neno ‘hirizi’ nilijua wapi mahubiri hayo yanaelekea. Nilihisi miguu yangu ikiishiwa nguvu na mwili wangu ukitetemeka. Sikuwa na uwezo wa kusikia tena chochote ambacho padri aliendelea kusema hadi pale nilipomwona akiwa ameishika hirizi yangu na kuining’iniza mbele yetu, huku akisema, “… Nauliza kwa mara ya pili nani kati yenu aliyeidondosha hii?”
Wote tulitazamana. Macho yangu yalikutana na yale ya Byabato ambayo yalinitazama kwa namna ya kunisuta
na kunidhihaki. Macho yaliyokuwa yakisema, “Unajua kuwa najua kuwa ni yako!”
“Nitauliza kwa mara ya tatu,” Padri aliendelea. “Nani kati yenu aliyedondosha hirizi hii jana?”
Macho ya Byabato yalikuwa yameganda juu ya macho yangu, yakinicheka. Sikuweza kustahimili zaidi. Niliinua mkono wangu juu na kisha kusimama huku nikijibu taratibu, “Ni yangu, Padri.”
Si Padri wala wanafunzi wenzangu walioamini masikio yao. Kwa darasa langu, kwa shule nzima na hata jamii nzima ya eneo hilo mimi nilikuwa mfano bora zaidi kimasomo na kikanisa. Nilikuwa hata nikiwasaidia mashemasi katika huduma ndogo ndogo za kanisa.
“Ni yako?” Padri aliniuliza tena, kana kwamba alitaka nibadili kauli na kuikana hirizi yangu. Sikuwa tayari kwa hilo. “Unajua kuwa mwili wako ni hekalu la Mungu? Aliniuliza?
Padri.
“Najua!”
“Kwa nini basi unavaa uchafu? Kwa nini unahifadhi
dhambi na kuishi nayo? Hutaki kuingia katika ufalme wa Mungu?”
Sikumjibu.
“Sio neno,” Padri aliendelea. “Leo Bwana amefanya muujiza kwa ajili yako. Ameifichua hirizi hii chafu, ambayo umeivaa kwa muda mrefu, ili ujitakase upya. Tutawasha moto hapo nje, utaichoma hirizi hii kwa mkono wako mwenyewe. Kisha tutakuombea na kukubariki kwa kitendo hicho cha kuachana na upagani milele.”
Tulitolewa nje. Zikaletwa kuni, moto ukawashwa.
Huku wenzangu wakiimba pambio mbalimbali, mimi na Padri
Backhove tulisimama mbele ya kadamnasi hiyo, mikononi mwake akiwa na Biblia na hirizi yangu.
“Wakati nikianza kusali, ichukue hirizi hii uitupe ndani ya moto ukitamka maneno yafuatayo ‘Shetani nakuteketeza sasa na milele, kwa jina la Yesu’ Umeelewa?”
Niliitikia kwa kichwa.
Nyimbo zilipamba moto. Sauti ya Padri akisoma sala ilisikika waziwazi. Lakini mkono wangu uliokuwa na hirizi uliishiwa nguvu huku nikitetemeka mwili mzima. Niliishikilia kwa zaidi ya dakika mbili, nikiining’iniza juu ya miale murua ya moto huo lakini vidole vyangu vilielekea kunigomea. Hisia zangu zilikwenda mbali sana toka hapo. Zilisafiri hadi usiku ule tulipoagana na babu uchochoroni. Masikio yangu yalisafiri pia. Yalikuwa pamoja nami huko uchochoroni, gizani, yakimsikia babu akisema; Hii ni hirizi ya bahati. Ilinde nayo itakulinda maishani mwako. Sauti hiyo ilikuwa wazi wazi kabisa masikioni mwangu.
“Ichome!” Padri alikatiza sala na kuniambia kwa ukali. “Siwezi!” Nilimjibu.
“Huwezi nini?” aliniuliza kwa mshangao. “Tupa uchafu huo ndani ya moto!” nilishindwa kabisa kuviamini vidole vyangu kufanya hivyo. Mara nikageuka na kuanza kuondoka. Padri hakuyaamini macho yake. Akanifuata na kujaribu kunishika. Nikamsukuma.
Padri Backhove alikuwa mtu mnene na mzito sana. Lakini hakuwa na nguvu nyingi. Nilimsukuma kidogo tu, lakini akaanguka chali, kama gunia. Sehemu ya kanzu yake ndefu, iliyofika miguuni iliangukia ndani ya moto huo na kuanza kuungua.
“Nakufa!” Padri alipiga kelele akijiviringisha huku na
kule katika jitihada za kujizoa ainuke toka mavumbini hapo.
Nilishikwa na hofu kubwa. Wakati wenzangu wakihangaika kuzima moto katika mwili wa padri, wengine wakijaribu kuinua mwili wake wenye zaidi ya kilo mia na sitini mimi nilianza kukimbia kwa nguvu zangu zote huku nikihisi sauti za watu wanaonifuata wakizomea nyuma yangu. Sikugeuka wala kusimama hadi nilipofika vichakani, mbali sana, ambako niliamini mtu yeyote asiye na uwezo wa kukimbia kama mimi na ujuzi wa mambo ya porini kama mimi, asingeweza kunipata.
* * *?
Nilijipumzisha kwa muda chini ya kivuli cha mti aina ya mvule, ulioonekana kupevuka sana. Nikaketi na kuegemea shina lake huku nikiitumia akili yangu kutafakari mustakabali wa maisha yangu baada ya tukio lile. Moyo wangu ulijaa kiza, hofu kubwa ikiwa imetanda katika nafsi yangu kwa kufikiria tu uzito wa mkasa ule.
Sikuwa na hakika kama padre Backhove alikuwa hai au la kwa moto na mweleka ule. Hata hivyo, hakika niliyokuwa nayo ni kwamba alikuwa ameathirika sana kimwili na kisaikolojia. Kwa vyovyote vile kama angenitia mkononi adhabu ambayo ningeipata isingekuwa kifani. Wazo ambalo lilinifanya nisahau kabisa ndoto ya kurudi shuleni pale na kuomba msamaha.
Zaidi ya hayo, hata kama ningerudi na kusamehewa ningeishi maisha gani shuleni pale bila kuwa kituko na kichekesho kwa kila mtu kwa miaka nenda miaka rudi? Sikuwa radhi kwa hilo.
Halafu, hata kama ungetokea muujiza nirejee shule na yote mengine yasahauliwe, jambo moja tu lisingeweza kusahauliwa kamwe. Hirizi. Kwa vyovyote vile msamaha wangu
na kutakasika kwangu kungeendana na kuiteketeza hirizi ile hadharani, hirizi ambayo ni urithi wangu pekee! Kiungo cha mwisho kati yangu na familia yangu!
Mara nikaikumbuka hirizi hiyo! Iko wapi? Nilijiuliza nikitia mkono wangu mfukoni kuitafuta. Haikuwemo. Nilikagua mifuko yangu yote na kujipapasa mwili mzima, wapi. Hirizi yangu ilikuwa imepotea, bila shaka katika zile purukushani za kukimbia!
Nilihisi nikiishiwa nguvu. Kwa muda nilipoteza mapigo kadhaa ya moyo, huku macho yakiingia kiza. Hirizi yangu ambayo ilikuwa kila kitu maishani mwangu. Hirizi ambayo ilisababisha nipoteze kila kitu maishani mwangu! Imepotea!
Wanasema binadamu katika uhai wake, anaweza kufa kidogo! Kama madai hayo ni ya kweli basi mimi Petro Kionambali, siku hiyo, chini ya mti ule wa mvule nilikufa kidogo.
Na hata pale uhai uliponirejea sikuwa mtu yuleyule tena. Sikuwa na pa kwenda. Nisingeweza kurudi Kashozi kwa mzee Buberwa na kumsimulia kuwa nimeshindwa shule wa ajili ya hirizi. Kadhalika, nisingeweza kurudi kwetu Buha na kumwambia babu na wazazi wangu kuwa nimeacha shule kwa ajili ya hirizi ambayo haipo tena. Shule nako kusingeendeka. Iko wapi hirizi tuichome? Ningeulizwa kabla ya mengine yote. Imepotea! Lingekuwa jibu langu. Nani ambaye angeniamini? Zaidi nani ambaye angenithamini? Haikuwepo namna.
Ghafla nikajiona yatima. Hapana, nilikuwa mwana
mpotevu, asiye na mbele wala nyuma.
Nikainuka na kujitazama. Tayari nilikuwa kijana mrefu kuliko watu wote katika familia yangu. Nilikuwa mwembamba lakini mkakamavu. Mikono yangu ilikuwa na nguvu, miguu
yangu ikiwa na uwezo. Zaidi ya kaptula, shati na viatu nilivyovaa sikuwa na chochote mkononi wala mfukoni mwangu. Nilikuwa masikini. Lakini nilijiamini. Afya yangu, elimu yangu na ari yangu vilifanya niamue jambo moja; sirudi kwetu wala sirudi shule. Nitapiga mguu, kutafuta maisha upya. Hata kama nitafika mwisho wa dunia!
* * *?
Nilipiga mguu kuelekea Kanazi. Nilifika usiku sana. Kwa kuhofia kuwa habari zangu zilishafika hapo nililala porini, juu ya mti. Alfajiri nilianza tena safari. Kiguu na njia hadi Muhutwe. Hapo niliomba hifadhi kwa wavuvi waliokuwa wamejenga vibanda vyao pwani. Hawakuwa na hiyana, ingawa mavazi ya shule niliyoyavaa yalifanya wanishuku kuwa nimetoroka shule. Sikukosa uwongo wa kuwaambia hata mashaka juu yangu yakaisha.
Katika elimu yangu fupi shuleni nilikuwa nimepata ufahamu wa kutosha wa Jiografia. Baada ya kughairi kurudi kwetu au kwenda kwa mzee Buberwa niliamua kwenda nchi ya Wasukuma. Mengi yalikuwa yakizungumzwa juu ya nchi hiyo ambayo nilitamani kuyaona kwa macho.
Zilikuwepo hadithi za Msukuma aliyeitwa Ng’wanamalundi ambaye alisemekana kuwa mganga aliyewashinda wachawi wote kwa kutumia ngoma zake. Mtu huyo wa miujiza alisemekana pia kuwa alikuwa na macho yenye nguvu za ajabu, ambayo yaliweza kukausha miti na hata binadamu aliowakazia macho, jambo lililopelekea awe akitembea huku akiwa amejifunga kitambaa usoni kufunika macho yake. Mtu huyo alidaiwa kuwa katika moja ya hafla zake alipata kukausha msitu mkubwa na mamia ya watu waliokuwa mbele
yake. Jambo hilo liliifanya serikali ya mkoloni imkamate na kumhukumu kunyongwa. Lakini hakuna aliyethubutu, kwani kabla ya hukumu hiyo kutekelezwa alifungwa katika kimojawapo cha visiwa vidogovidogo vilivyo baharini katika pwani ya Bahari ya Hindi, huko Dar es Salaam. Hata hivyo, ilielezwa kuwa Ng’wanamalundi huyo kila jioni alionekana katika vilabu vya pombe Dar es Salaam akiwa amevuka bahari kwa kutembea juu ya maji. Wakoloni wakalazimika kumwachia.
Sifa nyingine ya nchi ya Wasukuma ni zile hadithi kuwa kulikuwa na milima ya mawe, ama majini ama nchi kavu. Baadhi ya milima hiyo ilielezewa kuwa ilikuwa katika maumbile ya binadamu, ikiwa imesimama miaka nenda rudi kama inayosubiri mwujiza fulani utokee, ili ipate uhai na kuanza kutembea kama binadamu wengine.
Nchi hiyo pia ilikuwa ikisifiwa sana kwa ukubwa wa ardhi na wingi wa rutuba yake. Kilimo cha mazao ya chakula na yale ya biashara kama pamba na katani kilielezewa kuwa hakikupata kumtupa mtu. Kwa bahati mbaya, mimi sikupata kuwa mkulima wa haja. Wala sikuona kama ningeweza kuwa na ustahimilivu wa kulima leo kusubiri mavuno miezi au miaka kadhaa baadaye. Mimi nilikuwa mtu wa maji. Mtu wa kutupa nyavu na kuzitupa huku tayari zimejaa samaki! Hivyo, sababu kubwa iliyonipa msukumo wa kutamani kufika huko hasa lilikuwa ziwa. Jiografia yangu ilionyesha kuwa Wahaya na Wasukuma walichangia ziwa hili. Wakati Wahaya wakiwa Magharibi wakilitumia kwa shughuli zilezile.
Kwa kuzingatia hali yangu ya kutokuwa na kazi wala ujuzi wowote wa kuweza kupata ajira nyingine nililichukulia ziwa hili kuwa mkombozi wangu pekee. Nilitegemea ziwa
liniajiri, linilee, kwani taaluma ya uvuvi niliyoipata katika likizo zangu ilitosha kabisa kunipatia ajira hiyo.
Ni kwa mtazamo huo ndipo nilipojikuta nikijiunga na vikundi mbalimbali vya uvuvi kwa lengo la kujipatia fedha. Siku zote za uvuvi wangu nilifuata ziwa kuelekea upande wa kushoto kwangu badala ya upande wa kulia. Kama ningeelekea kushoto, ningelazimika kufika Uganda na baadaye Kenya, kabla ya kuingia Tarime, Musoma, Bunda hadi kufika Mwanza. Ingekuwa safari ndefu isiyo na sababu yoyote.
Mimi nilielekea kulia. Nilivua katika pwani na visiwa mbalimbali kama Bambire, Iroba, Rubondo na Nyamiende. Ilikuwa safari ndefu na ngumu sana. Takribani mwaka mzima uliishia njiani. Ama nilikwamishwa na ukosefu wa majahazi yanayoelekea huko nilikokuwa nikielekea, ama upepo mkali wa siku kadhaa ziwani ulifunga kabisa njia. Msimu wa masika ulioambatana na mvua kubwa za radi na mingurumo ya kutisha ni miongoni mwa sababu nyingine iliyonichelewesha njiani. Nililazimika kusubiri kwa zaidi ya miezi minne katika kijiji fulani huko Biharamulo.
Urefu huo wa safari ulikuwa na faida moja. Kwanza, ulinipa fursa ya kupata ukomavu na uvumilivu mkubwa katika pilikapilika za ziwani na nchi kavu. Ningeweza kuvumilia mvua ya siku mbili au tatu ikinipiga mwilini, niliweza kustahimili jua kali linalochoma kama mkaa wa moto. Niliweza pia kuipuuza njaa kwa muda mrefu. Zaidi, mwili wangu ulijenga uwezo mkubwa wa kuyashinda maradhi madogomadogo kama homa au tumbo bila haja ya kutumia dawa za madukani au mitishamba tele niliyopata kuelekezwa na babu.
Faida nyingine kubwa niliyoipata kutokana na urefu wa safari hiyo ilikuwa udugu. Nilikutana na watu mbalimbali,
nikashirikiana nao kwa hili na lile na kujikuta nimepata ndugu na marafiki tele, ambao kila nilipoondoka kuendelea na safari yangu walisikitika sana, lakini haikuwa kabla ya kunitakia kheri na baraka za safari.
Nilikosa raha kiasi pale tulipofika kisiwa cha Kome tukikaribia kabisa Mwanza. Rafiki zangu hao walishauri tubadili mwelekeo na kwenda kwanza Ukerewe. Tulifika Nansio. Tukafanya shughuli zetu za uvuvi hapa na pale, katika kijiji hiki na kile hadi tukajikuta tumeingia katika kisiwa kingine kidogo kiitwacho Ukara.
Ulipata kuona au kusikia juu ya mawe yanayocheza muziki? Kama hujapata hata kusikia mwenzio niliyaona kwa macho yangu katika kisiwa hicho cha Ukara. Kisiwa hicho kina mawe yaliyokaa kiajabu ajabu. Mtu anaweza kufikiria kuwa yalipangwa na binadamu, kwani baadhi yako juu ya mengine, yakiwa yamegusana kwa sehemu ndogo sana lakini hayadondoki si kwa mawimbi wala dhoruba la ziwani. Nilikuwa nikiyakodolea macho mara kwa mara mawe yale hadi mwenzangu mmoja aliposema, “Unashangaa kuyaona yalivyokaa, jee ukiyaona yanacheza?”
Nilidhani ni mzaha. Tulipobishana jamaa hawa walinipeleka katika kijiji cha Kome, ambako tulipata mwenyeji aliyetupelekeka eneo la Kululibha yalipo mawe haya ya ajabu. Mwenyeji wetu alitoa amri kwa lugha yake ya Kikara. Mara mawe hayo yakaanza kucheza kama watoto mapacha moja juu ya jingine. Hadi leo sijui ni kitu gani kinachotokea hadi mawe hayo yamtii binadamu.
Lakini huo si muujiza pekee wa Ukara. Pale kijijini kuna kisu chenye makali pande mbili. Unapotokea uhalifu wa aina yoyote watuhumiwa hupelekwa kwa mtaalamu na kuamriwa
kukalia kisu hicho. Lakini si kwa mhalifu. Yeye hukatwa mara moja, hata awe amevaa nguo nzito kiasi gani. Kwa yale niliyoyaona, ya mawe kucheza, sikuwa na ubishi wowote kwa jambo hilo.
Maajabu mengine ambayo niliyaona kwa macho yangu, ni mti mmoja kijijini Chilabi huko Ukara. Mti huo ulipigwa na radi ukang’oka. Wenyeji wakaanza kujipanga ili waupasue mbao na kuni. Wakati kabla kazi hiyo haijaanza, mti huo ukiwa umesimama na kuota tena palepale ulipokuwa awali. Hata hivyo, haukuwa na majani. Mti huo upo hadi leo. Niliutazama, nikaupapasa. Unaonekana mkavu lakini unaishi.
Maajabu hayo yalifanya tulipoanza tena safari ya Mwanza niwe nimechangamka zaidi.
SURA YA TANO
Nawa Chifu Wa Wasukuma
akati huo nchi ya Wasukuma ilikuwa eneo kubwa kuliko yote nchini Tanganyika, lililojumuisha wilaya za Shinyanga, Maswa,
Mwanza, Kwimba na Geita. Wilaya tatu za mwisho zikiwa zinapatikana na ziwa Vitoria.
Isipokuwa kwa tofauti ndogo za kimatamshi baina ya Wasukuma na Wanyamwezi ambao walienea zaidi maeneo ya Tabora, wakazi hawa walichukuliwa kama kabila moja ambalo liliongozwa kwa idadi ya watu. Eneo hili lililokadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 20,000 miaka ya 1945 na 1950 lilikisiwa na kuwa na watu wapatao milioni moja hivi.
Kabla ya wahamiaji wengi walioingia eneo hili kwa sababu zile na hizi makabila mengine ya asili katika eneo hilo yalikuwa pamoja na jirani zao wa sasa Wanyamwezi, ndugu zao Wanyantunzu na Wasukuma wenyewe.
Zaidi ya mandhari ya kuvutia ya ziwa, eneo hili lilifurika utajiri wa asili. Licha ya ardhi ya kandokando mwa ziwa kuwa na rutuba tele iliyokubali mazao mbalimbali, mbuga kama zile za Serengeti, zaidi ya kuvutia macho zilijaa wanyama wa kila aina. Aidha, licha ya mibuyu mikubwa yenye umri wa miaka nenda rudi ilikuwepo misitu mikubwa iliyobeba miti ya asili
aina mbalimbali ambayo baadhi ilipanda juu kwa takriban mita mia moja.
Kama ilivyo kwa Wahaya, Wasukuma na Wanyamwezi waliunganishwa na watawala na kijadi, ambao wengi wao walikuwa na asili ya wa Hima waliotokea Uganda baada ya kuwashinda maarifa ya utawala wale wa kibantu waliokuwepo. Watawala hawa ambao waliitwa Watemi, wasaidizi wao waliitwa Banagwa, walikuwa na nguvu nyingi za kiuchumi kutokana na kodi walizokuwa wakitoza raia wao na maeneo makubwa ya ardhi walizomiliki. Kiutawala, pia walikuwa na mamlaka makubwa kiasi kwamba kutoa hukumu ya kifo na ikatekelezwa lilikuwa jambo la kawaida.
Hayo na mengine mengi niliyajua siku mbili tatu tu baada ya kufika Nyamagana ambako kwa namna ya ajabu nilipata hifadhi katika himaya ya Chifu Masanja mwana Kasanga.
Hadi leo sijui kama tukio hilo lilikuwa mwendelezo wa bahati iliyotokana na hirizi au la baada ya hirizi kupotea. Ilikuwa ndio kwanza tumemaliza safari yetu, ambayo ilituchukua muda mrefu. Tulikuwa wanne, mimi, mzee mmoja na vijana wawili walionizidi kidogo umri.
Nilikutana na wavuvi hao katika kisiwa cha Kome ambako walikuwa wakivua samaki aina ya sato na kuwakausha kwa moto. Nilikaa nao kwa zaidi ya wiki moja kabla hawajaamua kurudi Nyamagana ambako walinielekeza kuwa ndiko yalikokuwa makazi yao.
Mara tulipofika nchi kavu na kuvuta mtumbwi ule, tulijikuta tumezungukwa na vijana wapatao kumi waliovaa nguo za aina moja na kufunga vitambaa vyekundu kichwani. kila mmoja alikuwa na mkuki mkono mmoja, rungu mkono
wa pili. Tuliamriwa kuketi chini, juu ya mchanga na kuanza kuulizwa maswali kwa lugha za Kiswahili na Kisukuma.
Mimi, nikiwa sijui Kisukuma, sura yangu ikiwa ngeni mbele ya watu hao ambao baadaye nilifaahamishwa walikuwa vijana wa Chifu, nilijikuta nikiwa mtuhumiwa namba moja mara hiyohiyo.
“Tuambie wewe ni nani… Unatoka wapi… Na unakwenda wapi…” aliamuru mmoja wao huku wenyeji wangu wakiruhusiwa kurejea makwao.
Waliniuliza kwa Kisukuma. Lafudhi yao haikutofautiana sana na Kiha au Kihaya. Niliwaelewa lakini sikuweza kuwajibu kwa lugha yao. Niliamua kuwajibu kwa Kiswahili “Mimi ni mimi. Sijui niendako wala nitokako.”
Walishindwa kuona mzaha katika jibu langu. Mmoja wao, mfupi, mnene mwenye tumbo kubwa zaidi ya umbile lake lilivyoruhusu alionyesha kukasirika sana. “Mnaona?” alisema “Huyu ni mrugaruga, mfungeni kamba twende naye.”
“Twende wapi?” nilihoji hofu ikianza kuniingia “Halafu nyie ni nani kwanza?”
“Unaona?” alifoka tena yule mnene ambaye alionekana kiongozi wao. “Anatuuliza sisi ni nani, mfungeni kamba.” Aliamuru tena.
Amri yake ilitekelezwa. Nilifungwa kamba za mkononi na kiunoni. Mmoja wao alishika ile ya kiunoni na kunivuta kama mbuzi. Ili kukwepa kuburuzwa nilikaza mwendo na kuwa nao sambamba.
Tulipita hapa na pale. Watu wengi waliwaona wakija, hasa vijana wa kiume, walitimka mbio na kutokomea maporini. Ajabu ni kwamba baada ya kunipata mimi hawakuonyesha nia ya kukamata mtu mwingine.
Katika maongezi yao, ingawa walipenda sana kuzungumza kisukuma, nilibaini kuwa mmoja wao alikuwa ‘akida’ ambaye ni mwakilishi wa serikali katika kaya mbili tatu za eneo hilo. Wale wengine walikuwa wasaidizi wa ‘Mwanangwa’ aliye msaidizi wa Chifu. Aidha, nilibaini kuwa jukumu walilopewa na chifu lilikuwa la kukamatwa kijana au vijana wenye umri wangu na kuwakabidhi kwake. Hakuna kati yao aliyefahamu Chifu alimhitaji kijana huyo kwa lipi, nilibaini kupitia maongezi yao.
Laiti wangefahamu hofu iliyonishika kwa taarifa hiyo, nina hakika kuwa watekaji wangu hao wangenihurumia na kuniacha niendelee na hamsini zangu badala ya kunipeleka kwa mtemi huyo. Hawakujua kuwa nilitoroka nyumbani kuja Uhayani kwa ajili ya Watemi haohao ambao walitaka kunitoa kafara ili kuleta mvua! Hivyo, ni dhahiri kuwa hawakujua pia kujihusisha na mtu yeyote mwenye madaraka au mamlaka ya Utemi au Uchifu kwa namna yoyote ile, kwani lolote lingeweza kutukia.
Nilitetemeka! Machozi yalinilengalenga. Kwa bahati nilikuwa nyuma yao, hawakuiona hali yangu. Nikaamua kujikaza huku nikianza kubuni njia za kutoroka mara itakapotokea fursa yoyote ile.
Wakati huo kichwa changu kilikuwa kikijiuliza maswali mengi kuliko majibu. Inawezekana kuwa mganga mwingine ametabiri shida ya mvua na kupendekeza kafara ya binadamu ambaye ameondokea kuwa mimi tena? Au watu weupe huko kwao wamenzisha vita nyingine kubwa kama ile iliyoitwa vita kuu, ya mwaka 1914 hadi 1918 ambayo waliwakamata babu zetu kwenda kuwasaidia bila khiari yao? Au ameibuka Mtemi Milambo mpya, aliyewachachafya sana Waarabu na
kuwakomboa mateka wao hadi alipofariki 1884, ambaye Mwingereza ameona hana jinsi ya kumshinda bila vijana wenye asili yake? Au kazi ya ujenzi wa reli ya kati, uliokamilika mwaka 1914 imeibuka tena hivyo wanahitajika manamba wenye damu changa?
Nilijiuliza mengi. Hadi tunafika katika himaya ya Mtemi au Chifu Masanja mwana Kasanga, sikuwa na jibu lolote zaidi ya mzigo wa hofu, mshangao na mashaka tele kichwani.
Mapokezi niliyoyapata katika himaya hiyo yalikuwa muujiza mwingine. Nilipelekwa moja kwa moja katika nyumba ambayo baadaye nilifahamu kuwa ilikuwa ya mke mkubwa wa Chifu. Mmoja kati ya wake zake kumi, ambao kila mmoja alijengewa nyumba yake na kuishi na wasaidizi wake, wake kwa waume, jambo lililoufanya mji huo wa Chifu kuwa kama kijiji kidogo chenye watu wapatao mia mbili hivi. Ng’ombe mia saba, mbuzi elfu moja, kuku, bata na njiwa wasio na hesabu walifanya kijiji hicho kiwe kama mji mdogo ndani ya mji.
Mama Chifu, mtu mnene wa maungo, ambaye mvi zilianza kumeza sehemu kubwa ya nywele zake fupi, alinitazama kwa makini kwa dakika mbili au tatu. Akatikisa kichwa. “Mara akawageukia wale walionikamata na kuwauliza, “Kwa nini mmemfunga kamba?” hakusubiri jibu lao, “Mfungueni mara moja,” aliamuru, amri ambayo ilitekelezwa mara moja.
“Chifu amepumzika,” mama huyo aliongeza. “Hapendi kuamshwa katika usingizi wake wa mchana. Kijana huyu amefika. Mwache aoge, ale, alale. Kesho ataonana na Chifu.”
Watekaji wangu waliondoka zao. Wasaidizi wa mama huyo wakapokea jukumu hilo. Nilitayarishiwa maji ya moto, ambayo sikupata kuyaoga kwa muda mrefu. Nilipotoka kuoga nilipewa ugali mkubwa kwa kuku mzima. Niliula karibu wote.
Nikaushushia kwa kibuyu cha maziwa ambayo pia nilikuwa na hamu nayo. Baadaye nilionyeshwa chumba cha kulala ambacho kilikuwa na kitanda chenye godoro la sufi. Kama haya ni maandalizi ya kunitoa kafara, kwa fadhila hii niko radhi! Niliwaza wakati nikijibwaga kitandani na kuchukuliwa na usingizi mnono uliofanya nisahau shida za mkesha, uchovu na malazi mabaya ya muda mrefu katika safari yangu hiyo.
* * *?
Sikuonana na Chifu hadi baada ya siku tatu. Zikiwa siku za kula vizuri, kulala vizuri na kupumzika, huku tayari nimepewa nguo na viatu vipya, nywele zangu zikiwa zimekatwa vizuri, nilimwona Chifu akinitazama kwa makini kabla ya kutikisa kichwa kama alivyofanya mkewe na kisha kutabasamu.
Nilikuwa nimepelekwa kukutana naye katika ‘Ikulu’ yake, chumba kikubwa chenye viti vipatavyo mia moja vilivyoelekea kwenye kiti chake cha enzi, ambacho kilichongwa kwa mbao za mpingu na fundi anayejua kila aina ya nakshi. Sehemu kubwa ya kiti hicho kilimeremeta kwa aina fulani ya mawe ambayo baadaye nilikuja kufahamu kuwa ni almasi.
Chifu alikuwa amekikalia kiti hicho, mimi nikiwa nimesimama wima mbele yake. Tulikuwa wawili tu chumbani humo baada ya walinzi ambao huwa wako nyuma yake siku zote kuamriwa kuondoka.
“Karibu mwanangu!” Chifu alitamka baada ya kunitazama kwa muda mrefu. “Karibu katika himaya ya Masanja mwana Kasanga, Msukuma halisi aliyewashinda wavamizi na wahamiaji wote. Jisikie uko nyumbani.”
Nilitikisa kichwa kumkubalia ingawa nilikuwa sijamwelewa.
“Hata hivyo, ningependa kukufahamu vizuri, wewe ni nani, kabila gani, ulikuwa ukitokea wapi na kwenda wapi kabla vijana wangu hawajakuleta hapa?” Chifu aliniamuru. Sauti yake ilionyesha upole na upendo kama ya mkewe. Ikanitia moyo.
Nilieleza ukweli juu ya kwetu, Buha, ambako nilizaliwa na kukulia. Kwa hofu kuwa ule mweleka ulikuwa umemwua padri Backhove na kwamba habari za kifo chake zilikwishawafikia huku, nilidanganya juu ya maisha yangu ya elimu. Nilimwambia Chifu kuwa ingawa nilifuata elimu huko kwa Wahaya niliishia kuvua samaki katika ziwa kwa kukosa mtu wa kunisomesha.
Kwa mshangao wangu habari hiyo ilimfurahisha sana Chifu. Alipotabasamu, akacheka kabla hajakohoa kwa kupaliwa na kicheko chake. Baadaye alisema, “Mungu amekuleta nyumbani, upate elimu uliyokuwa ukiitafuta. Utasoma shule ya watoto wa Machifu. Kama ubongo wako unachemka barabara utafika hadi Ulaya. Utakuwa Cheyo lakini Cheyo ataendelea kuwa Cheyo.
Sikumwelewa. Nikamtumbulia macho ya mshangao na kutoamini, macho yaliyojaa maswali ambayo Chifu aliyaona na akaamua kuyajibu, “Nitakuibia siri moja. Nataka ibakie siri, kati yangu na wewe tu. Unaweza kutunza siri?”
Nilikubali.
“Pamoja na umri huu,” Chifu alisema. “Pamoja na kuwa na wake tele hadi leo nimejaliwa kupata mtoto mmoja tu, wa kiume. Anaitwa Cheyo. Tena ana umri kama wako.” Alisita kidogo kabla hajaongeza, “Himaya yangu iko mashakani. Nikifa himaya itapotea mali zangu zitaparanganyika. Hivyo, walipokuja wazungu kutaka kumchukua mwanangu huyu wa
pekee ili wampeleke nchi ya mbali akapate elimu, naona tukio hilo litaiweka mashakani zaidi himaya yangu. Nani atarithi Ufalme wangu?”
“Na hata kama akirudi, akiwa amepoteza maadili ya utawala na mila za kabila langu na kuambulia tamaduni za mila za wageni nitakuwa nimejiweka katika nafasi gani?” Chifu alihoji na kuishia kujijibu mwenyewe, “Hapana. Nimekataa. Cheyo ni mwanangu. Nitamlea na kumfundisha mwenyewe. Sitaki kuchekwa na Machifu wenzangu wenye watoto lukuki.” Alisita kwa muda akiwa amejiinamia. Alipoinuka alinikazia macho, “Mwanangu,” akasema “Ni hapo unapoingia katika familia. Kama kweli unataka elimu, kama kweli unaweza, nitakupeleka wewe badala yake. Utatumia jina langu na hadhi yangu. Utalelewa kwa upendo na amani maisha yako yote,
kama mtoto wangu wa damu.”
Alinikazia tena macho, kwa muda mrefu kama anayejaribu kuusoma moyo wangu. Kisha akaniuliza taratibu, “Unasemaje?”
Niseme nini? Kwanza sikulitegemea swali hilo. Lakini sikutegemea kabisa kuwa matokeo ya kutekwa kwangu majuzi yangekuwa habari njema kama hiyo. Shule! Ni kitu nilichoondokea kukipenda kuliko chochote kile katika uhai wangu. Jambo lililofanya nishindwe kuamini iwapo nilichokuwa nimesikia ilikuwa ukweli au niko ndotoni. Niseme nini? Sikuwa na la kusema zaidi ya kuhisi machozi ya furaha yakinitoka na kuteleza juu ya mashavu yangu. Nilijaribu kuyafuta kwa mkono wangu ambao pia ulikuwa ukitetemeka.
Chifu hakuhitaji sauti yangu kupata jibu langu. Alielewa. Akainuka na kunikumbatia. “Hutajutia uamuzi wako. Naapa…” alininong’oneza.
Siku mbili tatu zilizofuata zilikuwa za maandalizi ya safari. Niliandaliwa vizuri sana kwa kufundishwa historia ya ukoo na majina ya mababu zao, ambao walikuwa wangu pia. Nilitakiwa kukariri majina hayo pamoja na mambo mengine tele ya kifamilia, kiukoo na kikabila. Haikuwa kazi rahisi.
Kiafya niliandaliwa pia. Ilikuwa nile mayai sita, kuku mmoja, ugali au ndizi za kutosha na kunywa kibuyu kimoja cha maziwa kila siku. “Ili ukifika pale ufanane na mtoto wa Chifu,” mzee Masanja alisisitiza. Amri hiyo iliambatana na kulala mapema, kuoga mara mbili kutwa, kuchana nywele zangu na kujipaka mafuta ya mgando mwili mzima. Hilo liliambatana na kununuliwa nguo za maana, viatu vya bei, mfuko wa safari na noti ya shilingi kumi ambayo Chifu alisema ni ya ‘kulinda mfuko.’
Matokeo ya kazi hiyo yalimshangaza kila mtu, ikiwa pamoja na mimi mwenyewe. Liliibuka dume lililopanda juu, lenye maungo yenye nguvu na afya tele, dume ambalo ile sura ya hofu na mashaka ilitoweka, nafasi yake ikachukuliwa na sura ya ucheshi, iliyojaa matumaini. Sura ya Mtanganyika halisi, aliyependwa na kupendeza kwa kila aliyemtia machoni. Sura ya Mtukwao au Petro mwana wa Karimanzira, mjukuu wa Kionambali. Hapana, sasa nilikuwa Cheyo mwana Masanja mwana Kasanga!
Nilikuwa mimi yuleyule, lakini mpya! Msomi mtarajiwa! Pamoja na maandalizi hayo ya kusisimua, kitu kimoja kilikuwa kikisumbua sana akili yangu. Toka nilipokuja katika familia hiyo na kupewa nafasi ya kuwa mwana familia na fursa ya kupata elimu sikuwa nimebahatika kukutana ana kwa ana na mrithi halali wa familia, ambaye nafasi yake ya elimu nilielekea kuipokonya. Ningependa sana kumwona mtu huyu.
Nijue ni mtu wa aina gani kitabia na kimaumbile. Lakini zaidi ningependa kujua msimamo na fikra zake juu ya uamuzi wa baba yake wa kumnyima fursa ya elimu ili awe mrithi na Chifu wa baadaye wa eneo hili.
Nilipata kumuuliza Chifu juu ya hilo, iwapo mwanawe ameridhia maamuzi hayo au la, lakini, kwa mshangao nilimwona Chifu akionyesha dalili za kukasirika kabla hajanijibu kwa mkato, “Yule ni mwanangu. Atafuata matakwa yangu,” jibu ambalo lilinitia mashaka zaidi.
Nilipopata wasaa nilimuuliza bi mkubwa juu ya jambo hilo. “Ni kweli mwanao hataki shule. Ni kweli atafurahi akisikia kuwa nakwenda kule kutumia jina lake na nafasi yake kujipatia elimu? Halafu yuko wapi mbona hajaonekana?”
Mama Chifu alinifumbua macho kidogo. Alisema, “Cheyo alikuwa anapenda shule. Hiyo sio siri. Lakini anatupenda zaidi wazazi wake. Hawezi kututupa kwa ajili ya kujua kusoma na kuandika. Alikubaliana na baba yake na ameachana na ndoto zote za kwenda shule. Amejiandaa kuja kuchukua nafasi yake mara Mungu atakapomchukua baba yake.”
“Yuko wapi?” nilimuuliza.
Nilimwona mama akisita kidogo. Baadaye alisema, “Nitakuibia siri. Chifu amemficha, hadi suala hili litakapokwisha.”
“Amemficha wapi?” nilisisitiza.
“Amemsafirisha. Yuko Misungwi kwa wajomba zake. Watamrudisha hapa mara wewe utakapoondoka na kuingia shule ili Wazungu waache kutuma matarishi wa kumtaka Chifu apeleke mtoto wake shule.”
Kiasi nilifarijika, walao kwa kuelewa ukweli.
Hata hivyo, usiku wa kuamkia safari yangu mashaka
yangu yaliibuka pale mmoja wa wajomba hao wa Misungwi alipofika kwa Chifu akiwa na taarifa ambayo ilimchanganya Chifu mwenyewe na kila mtu katika familia hiyo. Kwamba Cheyo alikuwa ametoweka kwa wajomba zake na hajulikani aliko!
Chifu aliduwaa. Alimtolea shemeji huyo macho makali, yaliyojaa hasira. “Kwa nini hamkumwangalia?” alifoka. “Mtafuteni, arudi hapa!” aliamuru.
ITAENDELEA
Kiguu na Njia Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;