Konstebo Nguzu Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
*********************************************************************************
Simulizi: Konstebo Nguzu
Sehemu ya Kwanza (1)
“Nimekosa magoli zaidi ya 9000 katika maisha yangu, nimepoteza mechi zaidi ya 300 katika maisha yangu, niliaminiwa mara 26 kuwa nitaipa timu yangu ushindi lakini nikashindwa. Nilishindwa tena na tena na tena katika maisha yangu NDIO MAANA NIKAFANIKIWA- Michael Jordan, mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu.”
HALI haikuwa shwari katika kota za polisi maeneo ya Mabatini jijini Mwanza, shida ya maji ilisababisha baadhi ya maaskari kwenda kazini pasi na kuiloweka miili yao panapo maji. Umeme nao uliwalazimu wengi wao kuzipiga saluti huku nguo zao zikiwa hazijanyooshwa.
Hii haikuwa shida sana kwa kundi kubwa.
Majira ya saa tatu kasorobo gari la maji liliwasili, lilikuwa ni agizo la serikali baada ya vilio kuwa vingi kutoka kwa wafanyakazi hawa watiifu.
Akina mama wakatoka nje na kuikimbilia ile gari na kujikuta wameunda foleni ya kutisha huku kila mmoja akimuhimiza mwenzake asiruhusu mtu kuingia mbele yake kwani kila mmoja ana haraka na anayahitaji sana hayo maji.
Kama ilivyo ada, panapo shida ustaarabu husafiri kwenda mbali.
Akinamama watu wazima walikuwa wakipigana vikumbo haswa, huyu anamsukuma mwenzake aliyesukumwa naye anasukuma.
Ilikuwa ni vita ya kimyakimya.
Mwanamke mmoja mkimya alikuwa anatokwa jasho kutokana na kusimama muda mrefu katika ile foleni. Alikuwa akiitumia kanga yake kujipangusa lile jasho huku moyoni akilaumu sana kampuni inayohusika na usambazaji maji jijini humo kutokana na kushindwa kurekebisha tatioz hili lililoendelea kudumu hadi kwa siku kumi.
Wakati anapanga foleni mbele yake walimtangulia watu wasiopungua thelethini, lakini sasa walibaki takribani saba. Akapata ahueni na tumaini jipya likazaliwa katika moyo wake wa subira.
Macho yake yakiwa yanatazama mbele muda wote mara akagutushwa na mguso wa kusisitizwa katika bega lake. Akageuka…
“Naomba unijazie hizi ndoo mbili foleni yako ikifika.” Sauti kavu ya kike ikamweleza, akashindwa kuelewa kuwa lilikuwa ombi ama amri.
“Mama, nenda ukapange foleni tafadhali.” Akajibu kwa mkato kisha akapiga hatua mbele baada ya foleni kusogea.
“Kwani ukinijazia utapungukiwa nini, watu wengine wana roho mbaya kama nini… ndoo mbili tu!” Mama mtaka kutekewa maji akabwatuka.
“Kha! we shangazi vipi, we mwenzetu ushakoga unanukia pafyumu hapa, sie twanuka jasho halafu unataka urahisi tu. Ebwaneee kapange foleni huko…” Sasa mwanadada akajibu jeuri.
“Na nitachota kabla yako, malaya mgeni wewe…” Akabwatuka huku akiondoka zake kama aendaye kupanga foleni.
Yule binti akatamani kuendeleza shari lakini mmoja kati ya wanawake waliosikia mtafaruku huu akamwonya kuachana na ile shari.
Akatii!
Baada ya dakika mbili anamwona yule mama akiongoza njia kuelekea katika bomba…..
Macho yakamtoka pima asiamini kuwa ni kweli yule mama mnukia manukato anachota kabla yake, hasira zikajijenga katika moyo na kichwa chake.
Kweli akateka ndoo mbili. Akajitwika moja kichwani na nyingine ikaning’inia katika mkono wake wa kuume. Kisha kusudi kabisa akajipitisha mbele ya hasimu wake ambaye alikuwa akisota bado katika foleni.
“Kinyamkera utangoja mpaka miguu izame tumboni…” Neno chafu likamtoka yule mama.
Uvumilivu ukampiga chenga mwanadada akachomoka katika foleni akamvamia yule mama, ndoo ikamtoka kichwani na ile ya mkononi ikatua chini.
Ukafuata ugomvi mkubwa kati ya mama mtu mzima na mwanadada. Mwanadada alikuwa hodari akamrarua vyema yule mama mtu mzima huku akimpa zawadi ya kapu la matusi.
“Wewe Janeth wewe…. mke wa Inspekta huyo. Mungu wangu eeh! umefanya nini sasa… ungevumilia Janeth. Tumeshamzoea huyu hapa kota mbona sisi… ndo tabia zake.”
Janeth akabaki kuduwaa, yaani kuwa mke wa inspekta ndo awe na tabia kama hizo. Janeth hakuwa akielewa sawa juu ya hivyo vyeo, kwake ikawa kama ndoto tu.
Baada ya saa moja kupita askari wawili wakafika kota za polisi mabatini wakamkamata Janeth ambaye alikuwa akiishi peke yake kwa wakati huo baada ya kaka yake ambaye ni askari kusafiri na mkewe kwenda kijijini.
Akawekwa rumande kwa siku nne!
Ilikuwa ni mara yake ya kwanza, hivyo aliteseka mwili na akili.
Alitoka akiwa amekonda mno.
Akapewa onyo kali juu ya kosa lake la kumshambulia mke wa Inspekta.
KILA aliyekuwa nje alimwona Janeth alivyokuwa anapepesuka, kijana mmoja akawahi kumpokea tofauti na wengine waliobaki kusikitika bila kutoa msaada.
Akamfikisha hadi ndani, akatoka nje na kumletea maji ya kuoga, kisha akamkaribisha chai.
Baada ya huduma hizi Janeth akachangamka kidogo. Wakazungumza mawili matatu kisha kijana akajitambulisha wakati anataka kuaga.
“Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu”
“Lipi jina lako, Konstebo ama Martin. Maana umeanza Martin ukasita kisha ukaanza na Konstebo….” Janeth akahoji.
Martin akatokwa na tabasamu hafifu kisha akamfafanulia Janeth kuwa Konstebo sio jina bali ni cheo katika jeshi la polisi.
Hakumweleza kuwa ni cheo cha chini kupindukia…
JIJINI Dar es salaam hali ya hewa ilikuwa tulivu lakini joto halikutoroka liliendelea kuweka kambi jijini humo.
Joto hili halikuyaathiri maji ya bahari ya hindi, hivyo watu walijazana katika fukwe mbalimbali kwa ajili ya kupambana na joto hili linalokera.
Katika ufukwe maarufu wa Koko mamia walikuwa wamejitosa katika maji wakijaribu kuzisahau shida zao kwa kuogelea.
Kijana mmoja alikuwa pembezoni akitazama watu wanavyoshindana kuyakata mkaji kwa mbwembwe. Alifurahia kutazama zaidi kuliko na yeye kujumuika katika maji yale.
Si kwamba alikuwa hajui kuogelea la! Maamuzi tu…
Na vile alikuwa mgeni jijini Dar hakutaka kuleta ujuaji aje aibiwe nguo zake aishie kudhalilika kwa kutembea nusu uchi na nguo za kuogelea barabarani.
Wakati anaendelea kutazama waogeleaji hakuacha kuangaza fahari nyingine ya macho.
Mabinti warembo wa Dar es salaam!
Alikiri kuwa hayakuwa maneno matupu, ni kweli ni warembo mno. Urembo ambao unaweza kusababisha mwanaume kukiuka viapo vyake….
Katika kutazama vivutio hivi likapita kundi la watu watatu. Mwanaume mmoja na wanawake wawili…..
Akaisikia sauti ambayo haikuwa ngeni sana katika masikio yake. Akasimama wima na kuanza kufuatilia kundi lile ili aweze kuona ni nani anayezungumza sauti ile.
Akaongeza mwendo na kulifikia lile kundi. Kishya akapiga moyo konde na kuwasemesha….
Wakasimama!
“Samahani…. kuna sauti naifananisha kati yenu.” Akarusha kete yake.
Wakacheka!
“Ehee! sauti yako dada, si ngeni kabisa katika masikio yangu. Sijui kama tumewahi kuonana…”
“He! kaka, wenzako wanafananisha sura wewe unafananisha sauti, utajuaje labda uliisikia kwenye Televisheni ama huduma kwa wateja…” Akajibu kwa nyodo kiasi.
“Au ndo yaleyale anayoyasema mama yenu… mnafanana misauti hiyo hatari…”
“Eti kaka labda ulimsikia Zubeda ukadhani ndo mimi…” akajazia dada yule mrefu na aliyeumbika vyema hasa hasa miguu yake.
“Mimi naitwa Nguzu, Martin Nguzu. Sijui kama umewahi kulisikia jina hili.” Akajaribu kujitambulisha huenda atakumbukwa.
“Samahani kaka, sijawahi kusikia hilo jina hakika.” Alijibu kiupole.
“Labda umewahi kukaa Mwanza. Huku Shamaliwa, Igoma ama Nyegezi…” Alizidi kutafuta uthibitisho.
“Mh! kaka huyo mtu unamdai ama maana si kwa kulazimisha huko. Huu ni msako haswa…” Dada wa pembeni akachombeza.
“Hebu ngoja, kwanini tuandikie mate….” Dada aliyefananishwa akasema kisha akachukua simu yake akabofya na kuweka sikioni.
“Eh! Da Zuu kuna mtu kakufananisha huku….” Aliongea huku anacheka.
“Anaitwa Zungu sijui nani…”
“Naitwa Nguzu…” alirekebisha upesi Martin.
“Anaitwa Nguzu, hebu ongea naye bwana. Maana alivyotuganda looh!” Akampasia simu Martin Nguzu.
“Habari, naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu…” Akafanya utambulisho kama alivyowahi kufanya jijini Mwanza kwa mwanadada aitwaye Janeth lakini huyu wa sasa ni Zubeda.
Maongezi yalichukua takribani dakika moja kabla simu haijarejea mikononi mwa dada aliyefananishwa.
“Ndiye..” akashusha pumzi martin huku akitabasamu.
“Kumbe ni askari looh! ningeshangaa mlugaluga tu aje kuhangaika na watu asiowajua.” Hatimaye yule mwanaume akazungumza. Mwanaume aliyekuwa pamoja na mabinti hao.
“Amesema nikupatie nambari yangu umtumie sasa hivi anipigie.” tabasamu halikujipa likizo katika midomo yake pindi alipokuwa akiyatamka hayo.
Ikawa hivyo. namba ikatumwa lakini hakupigiwa simu…
Usiku wa saa nne simu yake ikaita…
Alikuwa ni Janeth ambaye kwa sasa anajulikana kwa jina la Zubeda.
Ni miaka mitatu ilikuwa imepita tangu waonane mara moja tu jijini Mwanza. Wamekutana tena jijini Dar es salaam!
Maisha ya Martin yalikuwa tulivu bila ubaya na mtu.
Huenda yangedumu katika utulivu huu kwa miaka mingine mingi, lakini kukutana na Janeth aitwaye Zubeda kwa sasa ikawa ni safari nyingine ya kutisha!
“Nimejifunza katika maisha yangu kuwa walimwengu watasahau vyote ulivyosema, pia watasahau vyote ulivyofanya lakini kamwe hawatasahau ULIVYOWAFANYA WAJISIKIE aidha vibaya ama vizuri….”
Honi ya gari ilisikika mlinzi akafungua kizingiti kidogo kilichopo getini akaisoma nambari na kutambua kuwa ilikuwa nambari ya bosi wake. Upesi akalifungua geti vyema gari ikaingia ndani.
Tofauti na siku zote, siku hii gari lilipita hadi nyuma ya nyumba. Mlinzi hakufuatilia kwa sababu tayari alimuona bosi wake kupitia kioo cha mbele.
Gari lilizimwa kisha akashuka mwanadada ambaye hakuhitaji kukuonyesha mali zake nyingi ili uweze kumweka katika kundi la wanadada wapambanaji wa mjini ambao wamefanikiwa kuzikusanya noti na kuizoea harufu yake.
Alikuwa amevalia sketi fupi iliyoruhusu mapaja yake kuonekana japo kwa kuibiaibia, mkononi alishikilia simu mbili ambazo kwa bei ya harakaharaka unajenga nyumba kijijini kwenu kwa kutumia tofali za kuchoma na kuezeka kwa bati zenye hali nzuri na zinabaki senti kadhaa za kununulia jenereta dogo litakalofanya nyumba yako iwe kivutio kwa watoto mpaka wazazi wa hicho kijiji unachoishi nyakati za usiku.
Kwa mwendo wa madaha akaufungua mlango wa nyuma, akashuka kijana ambaye hawakuwa wakiendana hata kidogo. Huyu alikuwa mrefu wa haja mweusi na ambaye alionekana kuwa mwingi wa mazoezi kwa jinsi umbile la kifua chake lilivyogawanyika.
“Nguzu, hapa nd’o ninapojilaza walau siku ziende…” Alizungumza mwanadada ambaye Nguzu alipaswa kumtambua kama Zubeda na kusahau kabisa kama aliwahi kulijua jina la Janeth maishani mwake.
Nguzu alikuwa amejiandaa kisaikolojia kuanzia awali kuwa yule Janeth wa Mwanza aliyeswekwa rumande kwa sababu ya kumzongazonga mke wa inspekta atakuwa amebadilika mno. Lakini hakudhani kuwa angeweza kuwa anaishi katika nyumba nzuri kiasi kile, kuendesha gari zuri namna ile.
Umbo lake nalo lilikuwa limenoga, hakuwa yule kimbaumbau wa Mwanza mabatini.
Mate ya matamanio yakamruka Nguzu.
Akatamani gari, akatamani nyumba na maisha mazuri kwa ujumla.
Lakini angeyapata kwa wepesi gani ilihali alikuwa amegotea katika cheo cha ukonstebo katika jeshi la polisi na hapo alikuwa na majukumu lukuki yaliyojua kuutafuna vyema mshahara wake mdogo kila ulipokuwa unaingia.
Alipoingiza mguu wake sebuleni akazidi kughafirika, maisha ya Zubeda yalikuwa yanamkera si kwa sababu ni mabaya la! alikuwa na maisha mazuri kupindukia.
Akajaribu kuanza kujifananisha naye walau kidogo, Zubeda anamiliki luninga bapa yeye anamiliki ile modeli ya zamani yenye kisogo mfanowe mlima kilele cha mlima Kilimanjaro.
Nguzu akasonya na kupuuzia uwiano aliotaka kuuweka.
“Huenda ameolewa na kibopa hapa mjini! Acha matamanio Nguzu!” alijionya Nguzu na hapo akamuuliza Zubeda juu ya masuala ya mahusiano.
Upesi Zubeda akajibu kuwa hajaolewa na hatarajii kuolewa hivi karibuni.
Matamanio ya Nguzu yakarejea upya!.
“Njoo uione nyumba yangu Martin, Konstebo Martin Nguzu!” Zubeda akaiga namna Nguzu alivyokuwa akijitambulisha.
Nguzu akatokwa na cheko la haja!
Wakapita huku na kule hadi wakakifikia chumba cha Zubeda. Hapa ndipo Nguzu akahisi kuwa Zubeda ni mwongo tu hakuwa akiishi peke yake, na hii ni baada ya kuiona sare ya jeshi la polisi katika chumba kile.
“Hivi wanawake wataacha lini uongo wao jamani! kwani akiniambia kama ameolewa mimi nitapoteza fahamu ama?” Alijiuliza huku hamu ya kukisaili chumba ikimwisha.
“Zubeda una uhakika haujaolewa?” Kwa ghadhabu kiasi fulani akahoji.
“Eeh! sijaolewa vipi unataka kunitolea mahari.” akajibu na kutupa utani juu yake.
“Na hizo sare..” Akahoji huku akikodoa macho ya kumsuta Zubeda.
“Ooh! sijakueleza kumbe, unapaswa kunipigia saluti Konstebo Martin Nguzu, mimi ni koplo Zubeda Msangi.” alijibu kiuchangamfu sana.
Nguzu akabaki mdomo wazi, moyo ukaingiwa uchungu asiamini kuwa yule binti ambaye miaka kadhaa nyuma hakuwa akijua hata nini maana ya Konstebo leo hii ni Koplo. Cheo kimoja juu yake.
“Nadhani mwakani naweza kuwa ssajenti kama Mungu akipenda!” Alimalizia Zubeda.
Mungu akipenda?? akajiuliza Nguzu, ina maana Mungu haoni kuwa mimi ninahitaji zaidi kuliko huyu mwanamke au? akajiuliza katika nafsi yake na asipate majibu mjarabu.
Zubeda akatoa picha mbalimbali na kumwonyesha Nguzu, siku akiwa anaapa na picha kadhaa akiwa mafunzoni.
Nguzu akapwaya!
Kumbe kweli!! Akagutuka
Akapigia mstari kuwa hana hadhi yoyote mbele ya Zubeda.
Kikubwa alichomzidi ni kwamba yeye alikuwa mwanaume na Zubeda mwanamke, lakini hata akijitoa ufahamu kuhusu hilo bado Zubeda naye angejitapa kuwa yeye ni mwanamke na Nguzu hajawahi wala hatakuja kuwa mwanamke.
Nimepatikana leo! Alikiri Nguzu huku kijasho chembamba kikiulowanisha mgongo wake.
Bahati iliyoje kiyoyozi kilikuwa kinapepea, la sivyo kile kijasho cha usoni kile kinachoibuka ghafla mtu akiwa katika taharuki kingemuumbua Nguzu.
Zubeda alijitahidi kadri alivyoweza kumfanya Nguzu ajisikie yu huru lakini haikuwa heri katika moyo wa Nguzu.
Lakini jitihada za Zubeda kuujenga ukaribu baina yake na Nguzu hatimaye ile safari yao ambayo ilianzia jijini Mwanza ikafikia palipotarajiwa.
Ilikuwa ni siku nyingine ya kukutana kwao, walianza kwa kukumbushiana juu ya lile sakata la shida ya maji kota za polisi jijini Mwanza wakaunganisha na sekeseke la Zubeda kukabana na mke wa Inspekta. Wakafikia lile tukio la Nguzu kujitolea kumsaidia Zubeda kuanzia maji ya kuoga na baadaye chai.
Sasa Zubeda akamtaka Nguzu amtengenezee tena chai, Nguzu akafanya zaidi ya chai akampikia Zubeda ugali wa dona, nyama na mboga za majani.
Pishi likamnogea Zubeda akajikuta anataka tena na tena……
Mwishowe mapishi yakawa mapishi.
Uhusiano wa kimapenzi ukaibuka.
Lakini ulikuwa uhusiano wa kisasa uliotawaliwa na lugha za kisiasa.
Uliojaa masharti lukuki.
“Martin, sina la kukuficha safari yangu hadi hapa nilipo imetawaliwa na mikato mingi. Hadi sasa ninajihusisha kimapenzi na mume wa mtu, sio kwamba ninampenda kwa dhati ila nitakosa adabu nikisema kuwa simuheshimu. Ninamuheshimu sana moyo wangu unanishuhudia katika hili. Ujue niliwapuuzia vijana vijana hawa ama niwaite watoto, wao wanachoweza kukufanyia kwa ustadi mkubwa ni kukuburudisha mwili tu lakini kwenye masuala ya maisha wanakudumaza. Halafu wanabana sana yaani, ikitokea amekulipia kodi basi anataka kila siku aje kuifaidi kodi yake chumbani… looh!” Martin Nguzu akajikuta anatokwa na kicheko kwa jinsi Zubeda alivyokuwa analalamika.
Ni kweli lakini haikuwa masihara!
“N’do hivyo Martin yaani inafikia hatua unajuta, na vile damu inachemka anaweza akakuvunja mgongo. Nikaona hapana siwezi, nikajiweka kwa kile kibabu kina pesa na kuja hapa ni mara moja moja….. Jiulize Martin, kibabu kimenitafutia cheti cha fomfoo kwa jina hili la Zubeda, kimepambana nimeenda jeshini, kimepambana sijapitia msoto jeshini na hatimaye nimepata kazi. Kwanini nikidharau….. nakuapia kwa mizimu yote Martin, katu sijawahi kujihusisha na mapenzi na mwanaume mwingine tangu nianze kuwa na Inspekta. Wewe unakuwa wa kwanza tafadhali nakuomba sana usije ukaniharibia, usijekuwa kama vijana wenzako wanaopenda ngono kama walitangaziwa kuwa ukifanya sana unaongeza umri wa kuishi…..” Akamalizia kwa utani kisha akampiga busu baridi kabisa Konstebo Nguzu katika papi za midomo yake.
Konstebo akajiona yu daraja moja na inspekta ama ikibidi hata mkuu wa majeshi.
Busu pekee!
Mahusiano yakaanza.
Hawakuliona giza lililokuwa linawanyemelea.
Wakapumbazwa na mwanga wa mwishomwisho wa mshumaa!.
Mbaya zaidi Nguzu hakutaka japo kulijua jina la inspekta ambaye anammiliki Zubeda.
Penzi likanoga Nguzu akambatiza Zubeda jina maridadi la kimahaba. Jina linalotamkika kwa sauti tulivu ya kiume na kuleta hamasa panapo faragha.
Akamuita Zuu!
MUHARIRI wa gazeti la SIRI KALI alikuwa akiiendesha gari yake kwa mwendo wa kasi isiyohatarisha maisha yake ili awahi nyumbani. Kuna kitu alihitaji sana kupata uhakika kama kinaenda sawa na anavyodhania.
Ilikuwa kawaieda yake kutopenda kuwa mtu wa kuacha mambo juu juu kama ilivyokawaida ya wengine. Tangu akiwa shuleni alitambulika kwa waalimu wote kutokana na usumbufu wake, alikuwa hakubali kitu kimpite asikielewe kisha akae kimya tu.
Aliwasumbua sana waalimu kiasi kwamba ada yake ilikuwa inakwenda kihalali kabisa.
Tabia yake hii ikaendelea hata katika utu uzima wake akiwa kazini, aliifanya kazi yake kiustadi pasi na kubahatisha na pale alipohisi kuna utata aliwahi kutafuta uhakika kwa wanaojua zaidi yake.
Kutokana na gazeti alilokuwa anafanyia kazi kujihusisha sana na masuala ya siasa muhariri huyu alijiundia urafiki na na vitabu vya siasa ya afrika na dunia kwa ujumla lakini hakuwa mbali na masuala yahusuyo jeshi la polisi ambalo aligundua kuwa lipo jirani sana na siasa kuliko majeshi ya nchi za bara la ulaya ama Amerika.
Utendaji kazi wake wa kiwango cha juu ukamsababisha apewe jina ambalo hakuwahi kulisikia waziwazi zaidi ya tetesi pekee.
Wafanyakazi wenzake wakamuita Juma kimbelembele badala ya jina lake la kuzaliwa Juma Kiwele.
Hakujali maisha yakaendelea.
Alipofika nyumbani akabadili nguo zake na kisha bila kupumzika akamuaga mkewe akaondoa hadi mtaa wa tatu, akaimalizia safari yake kwa mzee wa kale ambaye alikuwa na rundo la magazeti ya miaka ya nyuma. Kuna kitu aliwahi kukiona akahitaji kukiona tena kiuhakika.
Mzee akamwachia ukumbi, akafukunyua kwa juhudi bila papara hatimaye akalipata gazeti la mwaka 1982. Kuna waraka ulikuwa umechapishwa.
“Kwa macho yangu nilitazama mwanangu wa kwanza akiuwawa mbele ya macho yangu, niheri angefyatuliwa risasi moja na kupoteza uhai. Alinyanyasika kabla ya kupoteza uhai, walimkata sikio lake ili akiri kuwa tumehifadhi bunduki ndani ya nyumba yetu, walimvunja magoti yake ili akiri kuwa sisi si raia wa Tanzania. Roho iliniuma sana haswa nilipokumbuka zile harakati za kugombea uhuru angali nikiwa kijana mbichi sana, nilipigana kufa na kupona kwa ajiri ya nchi yangu leo hii mwanangu anavunjwa miguu ili akiri kisichokuwa na ukweli. Sikuwa na la kufanya, akapoteza maisha wakatangaza kuwa alijaribu kutoroka akatandikwa risasi akapoteza damu nyingi kabla ya kugeuka maiti. Haikutosha hii, wakamwendea mke wangu kipenzi, bahati nzuri kwake hakupitia mateso bali alipoteza maisha baada ya kugundua kuwa mwanaye angali mfu!
Sikuwahi kuwa na bunduki lakini sasa ninayo, sikuwahi kuwa na roho mbaya lakini niliyonayo ninakaribiana na ibilisi, ninapoandika waraka huu bila kujalisha kuwa utachapishwa ama la nitakayoyafanya naomba nisilaumiwe na ninajua kuwa ipo siku nitakufa. Mkibahatika kuyaona maitiyangu na myape adhabu kwa kushindwa kuwa na moyo wa kusamehe!
Wakati mnayaadhibu maiti yangu mjiulize kila mmoja kwa nafsi yake.
Je? ungelikuwa wewe ungelistahimili uliyoyashuhudia??
Walidhani mimi ni mfu kwa mabaya waliyoutenda mwili wangu, lakini Mungu akawa upande wangu nikabaki hai…
Florian Ngengekuzenza Nguzu, 1982.”
Waraka ule wa aina yake ukakomea pale, na baada ya hapo ukimya ukatanda mpaka miaka mitatu baadaye ambapo liliibuka kundi lililotikisa nchi, ujambazi ukakithiri utekaji na mambo yote ya kutishia amani.
Waraka ule ukiwa umesahaulika mmoja kati ya watekaji anakamatwa anabanwa na kusema kuwa kiongozi wake anaitwa Nguzu Ngengekuzenza lakini katu hajawahi kumtia machoni.
Msako unapita lakini hakuna walichoambulia. Hakuna aliyetambua ni wapi mzee yule alikuwa amejificha….
Mtindo wa matukio aliokuwa akiutumia Ngengekuzenza ambaye alisadikika kuwa mkuu wa oparesheni hiyo isiyokuwa na jina ulikuwa mtindo wa akili nyingi kuliko nguvu. Wakilinda huku analipua kule, wakiachia hapa anaingia mzima mzima.
Lakini hakuna aliyewahi kumtia machoni.
Mnamo mwaka 1988, Ngengekuzenza anakutwa amepoteza maisha mtaroni bila kuwa na jeraha wala ujumbe wowote.
Maswali mengi yakabaki bila majibu. Wengine wakisema hili hawa wanalipinga bila kuwa na hoja za msingi.
Muhariri akamaliza kupitia alichotaka kupitia kisha akapitia majina yote ya askari waliokuwa wamehamishiwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es salaam.
Konstebo Martin Nguzu!
Jina hili likamkuna sana Juma, akawa anatamani sana kuonana na askari huyu amuulize mawili matatu iwapo ana uhusiano wowote na mzee yule wa miaka ya themanini aliyetikisa nchi na kisha kukutwa amepoteza maisha bila jeraha lolote.
“Nitamtafuta taratibu tu..” alijisemea wakati akiyaweka sawa magazeti yale mengi ili aweze kuaga na kuondoka.
“Kama ni yeye nitaandika makala ambayo itanipa Tunzo ya mwandishi bora. Kupata Tunzo na ujana huu mbona ni fahari sana. Nitawakomesha ofisini watanitungia jina jipya kwa soni itakayowakumba” Alijisemea huku akiwa wima na tabasamu pana usoni.
“Babu kuna gazeti moja ninatoka nalo.”
“Ukumbuke tu kurudisha na kulitunza vyema mjukuu wangu Juma.” Babu akamsihi.
Juma akaaga na kutoweka. Hakuelekea nyumbani badala yake alifuata uelekea tofauti ili ausogelee mwanga kuhusiana na martin Nguzu.
Alisahau kuwa mwanga haumwepushi mtu kupotea njia, mamia kwa mamia hupotea njia mchana kweupe na jua likuwa linaimulika dunia.
“Siku mbili za msingi katika maisha yako ni SIKU YAKO YA KUZALIWA na ile siku utakayogundua NI KWANINI UMEZALIWA….”
KUPENDWA RAHA, tena raha hii huja pale unapoyaona waziwazi mazingira ya penzi lenu kudumu sana.
Mapenzi mengi yanayohusisha watu wengi wasiokuwa na uwezo mzuri kifedha huvunjika mapema kwa sababu ya kutowajibika.
Sasa penzi la Konstebo Nguzu lingevunjikaje?
Zuu haombi kuongezewa salio kwenye simu, halalamiki kununuliwa simu mpya, ukiona anaomba kulipiwa kodi basi huo ujumbe ameutuma bahati mbaya huenda alikuwa anamaanisha ni yeye anataka kumlipia Nguzu kodi ya pango, haombi kununuliwa nguo badala yake analalamika kuwa kabati limejaa mno hana pa kuweka nguo nyingine.
Sasa penzi linavunjikaje hapo, labda wachokane tu!
Nguzu hakuwa na mpango wa kuchoka penzi hili.
Penzi lililomfanya anawiri na kujisahau kabisa kuwa yeye ni Konstebo, kuna kipindi aliwahi kujiona kuwa yungali Mkuu wa majeshi yote ya ardhi na anga nchini Tanzania.
Mapenzi bwana!
Ikiwa imepita miezi takribani minne tangu gundi ya huba iwaunganishe wawili hawa huku lile pepo la wizi wakilihalalisha na kuwa halali.
Konstebo Nguzu alikuwa eneo lake la kazi majira ya asubuhi.
Ilikuwa yapata saa mbili na dakika chache asubuhi katika kituo cha polisi Magomeni usalama, mgahawa ulikuwa umesheheni tayari wateja ambao asilimia kubwa walikuwa ni askari wa kituo kile. Nguzu akiwa mmoja kati yao
Si kwamba raia wema hawakuruhusiwa kutumia mgahawa ule lakini kama ilivyo ada ya Tanzania, raia wanawaogopa askari wao na askari wanapenda kuogopwa.
Watachangamanaje?
Mama muuza alikuwa amejikita katika kuwahudumiwa supu na chai askari waliokuwa wakiwania, kila mmoja akitaka kuhudumiwa wa kwanza ili aingie katika majukumu yanayomuhusu.
Vyeo hadi kwenye chakula cha kulipia? Nguzu alinung’unika katika nafsi yake baada ya kuambiwa ampishe askari mwenzake ahudumiwe kwanza kwa sababu tu alikuwa amemzidi cheo.
Akatii!
Kanuni muhimu kabisa katika jeshi, akawa ameifuata.
Kitendo cha kukatishwa zamu yake kikamfanya anune, kisha akaghairi kunywa supu akaagiza soda baridi akaketi na kuanza kunywa.
Hata kabla soda haijafika robo, akatakiwa kumpisha kiti mkubwa wake mwingine aketi.
Sasa ladha ya soda ikabadilika ghafla na kuwa chungu mithiri ya pombe inavyokuwa kwa mnywaji wa siku ya kwanza.
Akiwa ameegemea ukuta alijitazama begani hakuwa na nyota hata moja mwenzake alikuwa ameanza kuchafuka begani.
“Konstebo!” Sauti ikamtoa katika lindi la mawazo.
Akageuka huku na kule kutazama ikiwa ni yeye anaitwa ama kuna konstebo mwingine jirani na yeye.
Hakuwepo!
“Konstebo!” akaitwa tena kwa cheo chake, cheo cha chini kabisa katika jeshi la polisi. Akaitikia wito, akamwona yule bwana mwenye cheo cha Inspekta akimwonyeshea ishara kuwa kiti kipo wazi aketi.
Akaruka upesi akatua katika kiti.
Kitendo cha kupewa kiti na Inspekta kikarejesha ladha ya soda ile na ubaridi ukapenya vyema kooni.
Akiwa katika utulivu wa hali ya juu bila kuingilia mazungumzo aliyoyakuta alibaki kuinywa soda yake kwa hatua ndogo ndogo.
Lakini alikuwa anatetemeka, na hapa akagundua kuwa kuketi na watu wanaomzidi vyeo lilikuwa jambo lililomuathiri kupindukia.
Masiko yake yalikuwa wazi kusikiliza mazungumzo ya wawili aliowakuta pale.
Ilikuwa ni kuhusu kesi fulani iliyoonekana kuwasumbua vichwa, alitamani kuchangia hoja kidogo lakini akakumbuka kuwa wenzake walisahau ni lini mara ya mwisho kuwa katika cheo chake cha chini.
Akaufunga mdomo.
Lakini kichwani alikuwa anazungumza akijaribu kuwashauri wawili hawa ni kitu gani wanapaswa kufanya kuhusiana na kesi iliyokuwa mikononi mwao.
“Hawa watu nyota zao zote ni bure kabisa, sasa wao wanaona suluhisho ni kumkamata mke wa mshtakiwa. Je kama huyu bwana alimwoa huyu mwanamke ili kumfurahisha mama yake tu.. atajali nini? Mi binafsi sioni kama ni suluhuhisho….” akatokwa na tabasamu jepesi. Inspekta akaliona.
“Vipi Konstebo mbona unatabasamu, ni utamu wa haya mazungumzo ama…”
“Hapana afande, ni utamu wa hii soda, sijatumia siku nyingi sana…” Akajibu kwa utulivu wa hali ya juu.
“Unaitwa nani Konstebo…”
“Konstebo Nguzu, Martin Nguzu afande!”
“Unaitwa nani..” akauliza tena, Konstebo Nguzu akajitambulisha tena kwa ukakamavu.
“Sawa Konstebo Nguzu. Unaweza kutupisha kidogo sasa!” Inspekta alimwamuru, Konstebo Nguzu akajiondokea huku kichwani akiona ni jambo la fahari sana kujihusisha kimapenzi na Koplo Zubeda. Kwani kwa kufanya hivyo anayapooza maumivu yake yote ya kuamrishwa hovyo kila mara.
Amri alizoamini kuwa ni dharau!
Akiwa yu katika fukuto la ghadhabu, simu yake ya mkononi ikaitwa. Akalitazama jina na kupokea upesi.
Walau alikuwa amepigiwa na Koplo Zubeda, mwanamke aliyekuwa anamfariji na kumpa raha, hali iliyomfanya kuzisahau shida zake.
Wakazungumza kwa dakika kadhaa kujuliana hali kisha wakaagana huku wakipeana ahadai kedekede.
Kisha wakaingia kazinui, kila mmoja katika kituo chake.
Nguzu Magomeni na Koplo Zuu Chang’ombe polisi Temeke.
SIMU YA JUMA (Kimbelembele) ilimweka, bado alikuwa kitandani maana hiyo ilikuwa ni siku yake ya mapumziko.
Koplo Mtani, jina lilisomeka. Akapokea upesi.
“Amakweli ukiwa unakitafuta kitu kwa dhati sana unaweza usikipate ila huwa kinajileta wakati umekata tamaa tayari.” Alianzisha maongezi bila kusalimia.
“KUnani tena afande.”
“Leo nimekutana na Nguzu wako. Tena tumeketi meza moja asubuhi kweupe pee! Kumbe ni ka konstebo, kapole halafu kakijana tu. ” Alijibu kwa bashasha Koplo Mtani.
Juma akaketi kitako, na kuuliza maswali mfululizo. Koplo akayajibu yote kiufasaha na kumweleza kuwa siku inayofuata afike kituoni amwonyeshe mtu wake.
Damu ya muhariri wa gazeri la Siri Kali ikachemka, ubinafsi alioanza nao ukaendelea kumtawala hakumwambia mtu ni mpango gani anao dhidi ya Konstebo Martin Nguzu.
Kwanini amshirikishe mtu angali aliamini kuwa anenda kuandika makala pekee??
Amakweli maarifa mengi, mbele kiza!
Maarifa ya muhariri Juma Kihwele (Kimbelembele) hayakumfanya ang’amue kuwa si kila mtembezi hujua uelekeo.
Akatamani siku iliyotajwa ifike upesi.
Masaa akayaona hayasogei, hayawi hayawi mwezi ukaondoka zake baada ya kumaliza utawala wake wa muda, jua likatoka katika usingizi wake na kuisalimia dunia.
Akaianza siku na kauli dogoshi ya Koplo Mtani, ‘Ni ka konstebo , kapole halafu kakijana tu’.
“Ukihisi unaweza kufanya jambo fulani, sawa UPO SAHIHI.
Ukihisi hauwezi kufanya jambo fulani, sawa UPO SAHIHI pia.
Maamuzi ya KUWEZA ama KUTOWEZA yapo katika himaya yako……”
KIMBELEMBELE kilimfanya Juma Kihwele akose usingizi kabisa, alijigeuza huku mara ageuke kule. Alijisemesha kwa sauti ya chini na kucheka mwenyewe.
Mzigo wa kimbelembele kile ulikuwa mzito sana na dhahiri ulionekana kumwelemea. Akaamini kabisa bila kukigawa kidogo kile kimbelembele basi huenda pasingekucha.
Akamuita mkewe chumbani.
“Dear, nimeshindwa kulala mwenzako”
“Ushaanza! hapo unataka kuniambia matukio yenu ya kisiasa huko. Mi siyawezi.” Alijibu mkewe huku akiketi.
“Bora ingekuwa habari za siasa, ya leo kubwa kuliko. Jamani mapenzi haya..” akasita akajikohoza kisha akaendelea.
“Unamfahamu Koplo Zubeda Msangi.”
“Eeh! namfahamu si huyu mama wa hapo mtaa wa pili. Uliyeniambia wakati ule kuwa ni nyumba ndogo ya Inspekta nani vile.”
“Eewala! Inspekta Kobo.” Akahitimisha kwa madoido muhariri Juma Kihwele wa gazeti la SIRI KALI.
“Kafanya nini tena maana we nawe na kazi yako. Kuna habari kaandikwa ama…” Akahoji kwa utulivu akionekana kuwa bado hajavutiwa na simulizi hiyo ya mumewe.
“Bora angekuwa ameandikwa… Sikia ipo hivi, nilikuwa namfuatilia kijana mmoja hivi ni askari. Kuna vitu kadhaa nahitaji kujua kuhusu yeye. Huwezi amini katika kumfuatilia nikamwona anakuja hadi nyumbani kwa Koplo. Kama kawaida yangu nikitaka kujua jambo sichoki, nikaendelea kusubiri hadi walipotoka. Kwa kifupi Koplo Zubeda Msangi anajihusisha kimapenzi na hako kakijana kapole Konstebo Martin Nguzu ambaye nahitaji kufahamu mambo kadhaa kuhusu yeye.” Akamaliza na kumtazama mkewe.
Bado hakuonekana kuvutika!
“Ubaya ni kwamba huyo sijui Konstebo sijui Inspekta wote siwajui vizuri. Nd’o nashindwa kuelewa unashindwa kulala kwa nini haswa. Kisa Zubeda anajihusisha na mtu mwingine amakiasa nini. Nifafanulie basi….”
“Mke wangu, katika kazi yetu ya uandishi kuna mambo mengi. Kuna baadhi ya fursa huja zenyewe machoni, hapa unabaki kupima mzani nani anakupa pesa nyingi. Je? ni bosi wako ofisini ama ni huyo muhusika wa hii habari…”
“Kwa hiyo unataka kuigeuza biashara hiyo habari? Na wewe ulipolala na yule dada wa mapokezi nani aligeuza biashara lile tukio lako ama wewe tu nd’o wayaona mabaya ya wenzako….. nilijua umeniitia mambo ya maana kweli mume wangu. Huo muda ningekuwa nimemfundisha Mariam kuhesabu moja hadi kumi na ameelewa kabisa. Yani we sijui upoje tu…” Akasimama na kutoka nje akiuacha mlango wazi.
Juma akabaki kimya kabisa, mkewe alikuwa amemgusa pabaya mno. Hakutaka kuikumbuka kabisa siku aliyofumaniwa na mkewe juu ya suala hilo la kujihusisha kimapenzi na msichana wa ofisini kwao. Ni kweli haikuandikwa popote, lakini hii haikuwa sababu nzito ya yeye kuachana na hili aliloligundua.
Ukimya huu haukumaanisha kuwa Juma aliamua kuachana na jambo hili. Akaona mtu sahihi wa kumshirikisha ni Koplo Mtani ambaye alimfahamu fika kuwa alikuwa ni mojawapo kati ya askari wasiokuwa waadilifu, rushwa ilikuwa rafiki yake wa karibu mno.
Kuisubiri asubuhi aliona ni kosa la jinai.
Akanyanyua simu na kumpigia kisha akamshirikisha hatua kwa hatua huku akiweka sharti la kutomtaja Inspekta anayejihusisha kimapenzi na Zubeda…
Licha ya kuwa mahiri sana katika kazi yake, lakini aliwapuuza wakongwe waliotangulia mbele ya haki waliponena kuwa hakuna siri ya watu wawili.
Juma Kimbelembele alikuwa ameisambaza na ipo kwa watu wawili naye akiwa wa tatu.
Kumshirikisha jambo lile Koplo Mtani kukampa ahueni, akajigeuza mara kadhaa akasinzia huku akiwaza kuigeuza habari hii mtaji. Aliamini fika kuwa hatakosa milioni kadhaa kibindoni ikiwa atazipanga karata zake vyema.
Wakati yeye anasinzia salama akiwa amejipunguzia uzito kiasi fulani katika mawazo yake. Upande mwingine nd’o kwanza palikuwa panakucha.
MAPENZI RAHA, nilikuelezeni awali. Lakini huwa raha iso’ kifani wakutanapo wawili wanaopendana kwa dhati. Halafu wasipishane sana umri na mitazamo katika uwanja huo wa mahusiano ya kimapenzi.
Muunganiko kati ya Konstebo Nguzu pamoja na Koplo Zuu ulikuwa wa aina yake, waswahili wanasema upele ulikuwa umepata wakunaji.
Siku hii hakuingia kazini mapema, aliwasiliana na mwenzake aliyekuwa na askari mwenzake aweze kumwakilisha katika majukumu yake hadi majira ya saa sita mchana.
Ikawa hivyo!
Nguzu akaamkia nyumbani kwa Zuu, wawili hawa walioshibana wakaanzia kupata kifungua kinywa kilichoandaliwa na Zuu mwenyewe.
Walikula kisha wakalishana huku wakisifiana mambo kadha wa kadha. Baada ya kula wakashushia maji ya matunda.
Kilichofuata ni Zuu kumshika mkono na kumkongoja chumbani Konstebo Nguzu, haikuwa mara yao ya kwanza kuingia katika chumba hiki. Awali Nguzu alikuwa akiogopa sana kufumaniwa lakini mazoea yakajenga kibanda cha kudumu katika mwili wake, kisha kwa sifa mazoea yakajibadili jina yakawa tabia.
Chumbani wakagida mvinyo wa bei ghali, kisha wakakubaliana waende kuogeshana bafuni.
Simu ya Nguzu ikaita ikawakatili uhondo wao.
“Jamali ananipigia, ngoja nimsikilize.” Alimweleza Zuu kabla hajapokea ile simu.
Zuu akaelewa.
Baada ya kuongea kwa sekunde chache akakata simu, taharuki kiasi ikamvaa usoni.
“Nahitajika kituoni muda huu, mkuu wa kituo ananihitaji ni amri.” alizungumza konstebo Nguzu huku akiwa amemkazia macho ya matamanio koplo Zubeda Msangi (Zuu).
Uzuri Zuu naye alikuwa ni askari alijua vyema maana ya amri. Kwa unyonge akakubali matokeo.
Akamuaga Nguzu kwa kumbusu katika papi za midomo yake. Machozi yakamtoka Zuu na asijue ni kwa nini yanamtoka wakati Nguzu akimuaga.
Wakakubaliana kuonana jioni ya siku hiyo wamalizie walichopanga kufanya asubuhi hiyo.
Wakabusiana tena kwa mara ya pili.
Nguzu akatoweka, uzuri alikuwa amebeba sare zake za kazi na alikuwa amezivaa tayari.
Akachukua usafiri wa pikipiki moja kwa moja kuelekea kituoni.
UKIMWONA mtu mzima yu katika kilio pasi na sababu za msingi basi ana matatizo ya ziada katika akili zake, ama la ana tabia ya kulialia tangu utoto wake.
Lakini ukimwona mwanaume aliyekabiliana na majambazi kwa kutumia silaha, akawasambaratimba licha ya kupigwa risasi kadhaa zilizouvunja mguu wake. Ukimkuta huyu analia peke yake, kaa mbali kidogo kwanza uumize kichwa, si kilio cha kawaida asilani.
Inspekta Kobo alikuwa analia kama mtoto mdogo ofisini kwake.
Alikuwa na miaka arobaini na nane, heshima ya kuwa inspekta pekee haikutosha kuthamini mchango wake katika jeshi la polisi. Wakati wa ujana wake alitambulika kwa jina la Vandame kwa jinsi alivyokuwa akiyapenda mapambano, kwake tukio la ujambazi likitokea nd’o alikuwa anafurahi kwenda kukabiliana nao. Tena alipenda sana wakiwa na silaha.
Na hapo alikuwa na cheo cha chini bado, juhudi zake zikampandisha juu na hatimaye anazeeka akiwa Inspekta.
Haikutosha lakini walau.
Mlango wake uligongwa, akajifuta machozi upesi na kisha akamkaribisha aliyehitaji kuingia.
Mlango ukafunguliwa akausikia mshindo wa ukakamavu kisha ikafuata saluti.
Akaipokea kinyonge sana!
“Konstebo Martin, Martin Nguzu afande nimeitikia wito wako afande!” Kikakamavu mgeni akajitambulisha.
“Keti” akamsihi.
Nguzu akajitua katika kiti kilichokuwa jirani yake.
“Una umri gani konstebo?”
“Miaka ishirini na saba afande!”
“Ninaitwa Mathew Koboko, ama inspekta Kobo. Naamini hatujawahi kuonana, zaidi ya yote mimi sijawahi kukuona.” akatulia akamtazama Nguzu. Nguzu akatikisa kichwa kukubali.
“Nina miaka arobaini na nane sasa, umri umenitupa mkono, siko imara sana nilivunjika mguu nikiwa nalitumikia jeshi, mkono wangu wa kuume pia unatetemeka mara kwa mara kwa sababu ya kutumia sana bunduki, mgongo wangu sio mzima sana nikiketisana naumia, nikitembea sana naumia. Akili yangu pekee nd’o ipo salama. Salama kwa asilimia zote” Akatulia na kumtazama Nguzu usoni. Kisha akamwomba radhi kabla hajapenga kamasi nyepesi zilizokuwa zikimwandama.
“Umeoa Nguzu?”
“Sijaona afande!”
“Mimi nimeoa mtoto wangu wa kwanza unamzidi miaka michache lakini ana mwili mkubwa zaidi yako.” Akatulia na kulazimisha tabasamu kisha akaendelea tena.
“Nimekuita hapa ili nizungumze na wewe. Mimi kama Kobo na wewe kama Nguzu tena ni sawa na kijana wangu, lakini hapa tuzungumze kama wanaume wastaarabu walioketi baa kabla pombe hazijachanganya vichwa vyao. Najua wewe umekunywa pombe lakini sidhani kama umepitisha kiasi…”
“Nipo timamu afande!”
“Lakini umekunywa kidogo sivyo.”
“Hapana afande!” Akakanusha Nguzu.
Inspekta Kobo akasimama taratibu, akayaendea maboksi kadhaa yaliyokuwa pale ofisini, akapekua boksi moja na kutoa chupa akaiweka mbele ya Nguzu.
“Nimekusamehe kwa kunidanganya kwa mara ya kwanza, usinidanganye tena kwa sababu hivi vyuma katika mguu wangu havinizuii kuurusha ukakufikia.” akaiacha ile chupa na kurejea katika kiti chake.
“Haukuishia kunywa pombe pekee, Martin Nguzu umejipulizia marashi niliyoyanunua jijini Paris Ufaransa. Kwa kifupi umetoka nyumbani kwangu bwana mdogo. Nyumba inayonipa mimi faraja….” Akasita na kumwacha Nguzu apagawe kwanza.
Hakika alipagawa, hakuamini kuwa siku yaikeinaanza hivyo. Akatambua kuwa yupo ana kwa ana na mume mwenzake.
“Nilikwambia nimeoa Nguzu, lakini nipo salama zaidi nikiwa na Zubeda. Simtumii kwa sababu ya pote nilipomtoa, najua hajakwambia kiundani ni wapi nimemtoa… hawezi kukueleza kuwa nilimkutaanajiuza nikamnunua na hapo nikawa nimeyanunua maisha yake jumlajumla. Alikuwa amefyatuka akili zake na alikuwa amekata tamaa, nilitumia muda na uwekezaji mkubwa sana kumkomboa kutoka janga lile. Narudia tena ninaye mke ninayempenda hata kama yeye hanipendi, lakini kwa Zubeda ni sehemu ninayokuwa salama zaidi.
Siwezi kukulaumu eti umeniingilia katika anga zangu, kama ningekulaumu hata usingeiona sura yangu bali ni mimi ningeiona sura yako baada ya wewe kukatwa kichwa na vijana wangu. Nimeona niwe mstaarabu kidogo, maana na huu uzee nikiwa mkaidi haina maana ya kuwa mzee sasa.
Nguzu, imetosha kuingia nyumbani kwangu, niache basi nisije kufa na magonjwa ya moyo wakati risasi hazikuweza kuniua. Ujue nimelia sana leo hadi nimejishangaa, nimetambua wazi kuwa ninampenda sana Zubeda. Nawe ninakuomba uwe balozi wangu wa kweli, mtafute Zubeda mwambie mzee Kobo anampenda sana na sijawahi kumuwazia mabaya hata siku moja. Msihi haswa kuwa asinirudishe katikaujana wangu kwa namna yoyote ile. Unaweza kuondoka Konstebo Nguzu Martin Nguzu….” Alimaliza Inspekta Kobo kinyonge.
Nguzu akasimama akiwa anatetemeka sana, jasho likimtoka.
“Nenda nyumbani ukapumzike ukitoka humu ndani, nimekupatia mimi ruhusa hii Nguzu.”
Nguzu akasimama huku akihema juu juu akapiga saluti na kutoweka pale ndani. Inspekta akamsindikiza kwa macho hadi alipotoweka.
Simu yake ilimgutusha kutoka katika dimbwi la mawazo. Ilikuwa ni namba ya Zubeda. Akatambua kuwa tayari mambo yamezidi kuharibika.
Akapokea huku akiwa anatetemeka sana, moyoni mwake akitamani hii iwe ndoto ya mchana.
“Laazizi! ukwapi?” Sauti tulivu kabisa ikahoji.
“Nyumbani vipi kwani?”
“Kuna tatizo Nguzu… tena linaweza kuwa tatizo kubwa sana tukilipuuzia.”
“Ni kuhusu inspekta?” Nguzu akauliza.
“Si bora kingekuwa kile kibabu ninakiweza kile. Kuna mtu anaitwa Juma Kihwele sijui unamfahamu?”
“Hapana jina hilo ni geni kwangu Zuu. Kuna nini? na ni nani huyu?”
“Amenipigia simu anasema yeye ni muhariri na anahitaji tuonane kwa mazungumzo juu ya mimi kujihusisha kimapenzi na Inspekta halafu na sasa nipo na wewe. Sijui ameyatoa wapi haya maneno, Nguzu atatuharibia huyu wakati ambao sio muafaka hata kidogo. Nimekupigia maana hili linatuhusu mimi na wewe, nataka tumuwahi.” Aakaweka kituo. Nguzu akapagawa, wakati anawaza kuwa ni jambo juu ya inspekta linakuja jingine khusu mwandishi.
“Nakusikiliza wewe, tunamuwahi vipi sasa?” akauliza kinyonge mno.
“Njoo nyumbani usiku tupange, kama saa tatu hivi.”
“Hapana Zuu sitaweza kuja hapo usiku wa leo. Huoni kama tutazidi kulikuza tatizo… kwanini tusikutane sehemu ambayo sio hapo kwako?”
“Sawa panga wewe halafu utanifahamisha basi…” Akamaliza na kukata simu.
Nguzu akahisi kuugua, kama sio homa basi ni Malaria kali kupindukia.
Utamu utamu sasa ukageuka uchungu!
Hata kabla hajamweleza Zubeda yaliyojiri katika ofisi ya Inspekta Kobo yanatokea haya mengine ghafla!
Akapanga kukabiliana na hili jambo kabla halijakomaa, akasimama imara akapiga saluti na kujiapiza kuwa hatalala tena na kulialia kama mtoto badala yake atapambana kiume.
Hakujua kuwa wakati yeye akiamua kusimama,kuna ambao walikuwa wakikimbia mbio kali kwa nia ya kumzamisha katika shimo lenye kiza kinene.
“WAKATI mzuri zaidi wa kufanya mabadiliko katika maisha yako ulikuwa ni miaka kumi iliyopita….. WAKATI mwingine mzuri zaidi ni SASA! Usije ukathubutu kusema kuwa umechelewa kufanya mabadiliko katika maisha yako……fanya SASA”
ALIJARIBU kujiaminisha kuwa huenda amesikia vibaya, akazidi kujikunja kitandani ili asinzie vizuri. Lakini mlango ulipiga kelele tena, kuna mtu alikuwa anaugonga.
Akiwa na mawenge ya usingizi aliufikia mlango na kuufungua bila kuuliza ni nani alikuwa anahitaji kuingia. Hakuwa katika fahamu zake taslimu.
“Nani?” aliuliza baada ya kuwa ameufungua mlango na kukutana na kiza kinene.
Badala ya kujibiwa akasukumwa ndani, kisha tochi kali ikayamulika macho yake akashindwa kutambua kunani mbele yake.
Akajaribu kutokwa na pigo la ‘Karate’ aliyojifunza akiwa kambini lakini akaishia kupiga ukuta na kutokwa na ukelele wa maumivu.
Mwanga ule ukapotea na kisha taa ya chumbani kwake ikawashwa. Akayapikicha macho yake na hatimaye aliweza kuona ni nani alikuwa mgeni wake asiyetoa taarifa.
Mkojo ukatoka mbio katika kibofu usiangalie kuwa pale si maliwatoni ama msalani. Ulipofika karibu na mlango wa kutokea ukamstahi.
Haukutoka!
“Nguzu, mbona unawahi sana kulala.” Ilikuwa sauti tulivu kabisa ya Inspekta Kobo ndani ya nyumba anayoishi Konstebo Nguzu.
Konstebo Nguzu aliishiwa hamu zote, akabaki katika hali isiyoeleweka.
Inspekta Kobo akaketi. Nguzu akajilazimisha akapiga saluti.
“Nguzu, ni masaa mangapi yamepita tangu tuzungumze?” aliuliza kwa utulivu uleule. Kabla Nguzu hajajibu yeye aliendelea.
“Umenogewa na mali yangu ama? Yaani kweli nimekuita kwa upole na ustaarabu wa hali ya juu kiasi kile lakini kumbe usiku huu umepanga tena kukutanana Zubeda! Mbona unanifanyia hivyo konstebo….” Alizungumza kwa kulalamika Inspekta.
Nguzu kimya!
“Naomba unitazame machoni wakati unajibu swali hili.” Akasita kisha akaendelea baada ya NGuzu kumtazama.
“Unampenda Zubeda kwa dhati ya moyo ama unampenda kwa sababu ni yule mwanamke ambaye hawezi kukulilia shida badala yake wewe nd’o waweza kumlilia shida?” Swali zito likamponyoka inspekta Kobo.
Nguzu akabaki kimya tena huku akionekana wazi kuzidiwa na uzito wa swali lile na pia alikuwa hajaizoea hali ya inspekta kuwa ndani ya nyumba yake.
“Martine Nguzu kwa kumbukumbu zako unafahamu inachukua muda gani kupanda kutoka cheo kimoja kwenda kingine katika jeshi la polisi?”
“Miaka mitatu..” Sasa alijibu huku amani ikiwa imetoweka.
“Unajua kuwa yaweza kukugharimu miaka walau kumi na nane kufikia cheo changu…. lakini mimi sikutumia miaka kumi na nane kuwa inspekta, nilifanya makubwa sana… nilikuwa nina roho mbaya mno na nilikuwa nikiikamata bunduki nakuwa shetani kamili.” akaupitisha mkono wake na kuichomoa bastola yake kutoka mahali alipokuwa ameihifadhi.
Sasa Martin Nguzu aliweza kuzungumza hata ambayo hajaulizwa. Mara aseme Zubeda ndiye alimlaghai mara aseme hatarudia tena…
“Sina maana mbaya kuiweka bastola hii katika mkono wangu, ninajaribu kukueleza na unielewe vyema. Ningekuwa nimekuvamia hapa kwako kwa sababu unahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya ama ujambazi, muda huu mguu wako mmoja ungekuwa unasubiri muda tu ukakatwe. Lakini sipo hapa kupambana na wewe Nguzu nipo hapa kukusihi tu, kama inawezekana naomba uniachie Zubeda wangu, nasisitiza ninajaribu kukusihi tu na wala sio kukulazimisha. Niachie huyu binti, amepitia mengi magumu nimejaribu kuitafuta furaha yake walau kidogo tu, nimewaumizawengi kwa kutumia bunduki sitaki kuumiza tena kwa kutumia moyo.” akasita na kumwomba Martin maji ya kunywa, bahati nzuri hayakuwa mbali.
“Konstebo mfano mimi najitoa katika maisha ya Zubeda nakuachia wewe, je? utaweza kumjazia mafuta ya gari lake? utaweza kumnunulia nguo za gharama kiasi kile, utaweza kumbadilishia samani za ndani ya nyumba yake? utaweza kuwalipa wafanyakazi wake? Utaweza Nguzu?. Kama jibu ni hapana basi nikikuachia Zubeda kuna watu watakuja kukusaidia majukumu nawe utajikuta unaumia moyo huku ukilia kama mtoto.
Kwanini nikuache uyapitie hayo sasa…. kwanini nikuone upo katika njia mbovu nisikueleze ukweli. Nguzu kama Zubeda anakueleza ukweli, atakuwa amekueleza kuwa ninaenda kwake mara ngapi na ninashiriki naye tendo mara ngapi….. nadhani huwa anahisi mimi nimezeeka, ila sijazeeka Nguzu nipo imara mno tatizo ni moja tu, sio ngono iliyoniweka pale….. sio ngono Nguzu” Akashindwa kuendelea kuzungumza, chozi la mtu mzima likaiangukia sakafu ya Nguzu.
Huruma kali ikamshika Nguzu, akataka kusema neno lakini Inspekta akamzuia na hapo akaaga na kuondoka zake bila kuhitaji hitimisho.
Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa Nguzu, akaitazama saa yake tayari ilikuwa saa nne kasoro dakika chache usiku.
JUMA KIHWELE alikuwa nje akipunga upepo huku akingojea kwa hamu simu kutoka kwa Koplo Zubeda ili waweze kumaliza zoezi lao. Alikuwa nje kwa maksudi makubwa, hakutaka mkewe ajue kuwa ameendelea na ule mpango wa kuitumia ile habari ya Zuu kujihusisha na wanaume wawili kujiingizia kipato jambo ambalo mkewe hakuwa ameliunga mkono kabisa.
Kila mara alitazama simu yake kama kuna ujumbe wowote kutoka kwa Zuu, lakini hadi majira ya saa tatu usiku bado hali ilikuwa ya ukimya. Moyo wa subira ukaanza kuingiwa uchovu akafikiria kumpigia simu na kumchimba mkwara kuwa iwapo hatafanikisha kuonana kwao basi asimlaumu pakikucha.
Akiwa katika kusubiri kule akaliona gari likipaki eneo fulani jirani na upeowa macho yake kisha akashuka mtu ambaye anamfahamu vyema.
Kimbelembele kikachukua nafasi yake. Akataka kuhakikisha kuwa anamfahamu vipi mtu yule.
Inspekta! akastaajabu.
“Jamani si inspekta Kobo huyu.” akajiseme huku akisubiri kuona anaenda uelekeo gani, alipopita naye akafuata nyuma. Moyoni alijua wazi kuwa Zuu atakuwa amemweleza kila kitu inspekta, ile mipango yake ya kuvuna chochote kitu akaiona inapoteza uelekeo.
Macho yake yaliyolizoea giza yakamwona inspekta akienda moja kwa moja nyumbani kwa Martin Nguzu.
“Wanaenda kukubaliana nini hawa viumbe eeh!” alijiuliza hukiu akitamani kujisogeza hadi jirani na ile nyumba aweze kuvuna mawili matatu. Lakini alihofia kufumaniwa kisha kudhalilishwa.
Akarejea ndani ya nyumba yake, alipofika nakuiona kamera yake akapata wazo jipya.
“Hawa wawili wanajihusisha na mwanamke mmoja, kwa namna yoyote ile kuna namna fulani ya kutoelewana itajitokeza. Na kama wakipigana basi nitanasa picha nyingine muhimu kwa ajiri ya gazetini.” Wazo hili jipya likamfanya atoke nje na kamera yake akaenda hadi chini ya mti akaketi huku akiiona vyema nyumba ya Nguzu.
Kiupepo chenye ubaridi wa wastani kikaungana na mawazo tele ya Juma Kihwele na kuunda usingizi.
Jumaakajikutaamesinzia akiwa eneo lile.
Alikuja kushtuka baada ya kusikia makelele… akakurupuka akidhani kuna wizi umetokea mahali.
Macho yake yakakutana na moshi ukifuka katika nyumba ya Nguzu.
Nyumba ilikuwa inatetekea katika namna ya kutisha sana. Moshi mweusi tii uliichafua anga.
Mungu wangu! akahamaki Juma, kisha akaiweka sawa kamera yake na kwenda kupiga picha kadhaa jinsi tukio lilivyokuwa likiendelea.
Moyo wake ulikuwa unadunda sana. aliulaumu usingizi uliompitia chini ya mti na kusababisha asiweze kuona tukio lilitokea katika mazingira ya namna gani.
Akatimua mbio mpaka pale lilipokuwa limeegeshwa gari alilokuja nalo Inspekta. Hapakuwa na kitu.
“Inspekta amemchomea ndani Nguzu?” alijiuliza Juma huku akiwa na kimuhemuhe kipya kuliko kile cha awali cha kugundua kuwa wawili hawa wanajihusishakimapenzi na mwanamke mmoja.
Magari ya zimamoto hayakufika usiku ule… nyumba ikateketea yote na kusalia majivu.
Juma alirejea nyumbani kwake akiwa hayuko sawa kabisa, alimfikiria mkewe na kutaka kumshirikisha juu ya kitu kilichokuwa kimetokea lakini alikumbuka majibu yake wakati anataka kufuatilia mkasa ule yalivyokuwa. Akasita kumshirikisha, hili la sasa lilikuwa zito mno na lingeweza kumtia hatiani angefanya kuliropoka.
“Kwa hiyo kulikuwa na watu ndani?” Mkewe alimuuliza juu ya hiyo nyumba iliyoungua, kwani tayari alikuwa amesikia kwa majirani na alijua wazi mumewe hawezi kupitwa na habari ile.
“Yaani hapa sina moja wala mbili.” alijibu kwa ufupi. Na hakutaka kuzungumzia tena jambo lile akaingia bafuni kuoga kisha akalala.
Kitu cha kwanza asubuhi ni kujua kama habari ile tayari imepata mwanga.
Naam! Ikatangazwa kuwa nyumba imeungua kwa chanzo ambacho bado hakijajulikana na inasadikika kuwa askari mmoja amepoteza maisha akiwa ndani ya nyumba hiyo.
Nambari ya askari yule ikatajwa na kisha jina likatambuliwa baadaye.
Konstebo Nguzu alikuwa katikati ya moto ule na alikuwa ameangamia.
Taarifa hii ya habari ikasikilizwa na masikio ya Koplo Zubeda Msangi aliyekuwa anaendesha gari lake kuelekea nyumbani kwa Nguzu ambaye alikuwa hapatikani katika simu ilihali walipanga kuonana usiku ule.
Zubeda akiwa amevimba kwa hasira alikuwa anaenda kumlaumu waziwazi Nguzu kuwa si mtu anayejali hata chembe.
Kulisikia jina lake likitajwa kuwa hayupo duniani tena, Zubeda akajikuta akikanyaga pedeli ya kuongezea mwendo wa gari badala ya kupunguza mwendo na mara akajikuta akikwepa kitu asichokijua gari ikatumbukia mtaroni, Zubeda ambaye hakuufunga mkanda wake akajibamiza katika kioo na kupoteza fahamu palepale huku damu nyingi ikimtiririka.
Kwa sababu ilikuwa asubuhi, askari waliokuwa barabarani waliwahi sana kumtambua koplo Zubeda ambaye alikuwa ndani ya sare zake za kazi. Simu za upepo zikapigwa upesi kutoa taarifa ile.
ITAENDELEA