KIJASUSI

Ep 05: Konstebo Nguzu

SIMULIZI Konstebo Nguzu
Konstebo Nguzu Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Konstebo Nguzu

Sehemu ya Tano (5)

ZUBEDA hakuamini macho yake pindi alipomshuhudia inspekta Kobo akishushwa garini huku akiwa hajiwezi walau kutembea, nguo yake kwa mbali kabisa ilionekana kumpwaya, na ilikuwa imefubaa huku mabakamabaka yaliyoashiria kugandiana kwa damu yalionekana.

Donge la uchungu likamkaba kooni, akajikuta yungali katika mfadhaiko mkubwa sana.

Hakujua ni kwanini Kobo yu katika hali ile lakini kichwani aliitabiri kuwa haikuwa ya heri hata kidogo.

“Martin…… Inspekta Kobo…” Alimwita kutoka pale alipokuwa ameinama bafuni.

Martin akajikuta akisimama wima na hapo akawa amejitonesha mbavu zilizokuwa katika maumivu makali.

Hakujikunja tena, akanyoosha shingo akakiona kile ambacho Zubeda alikuwa anakiona.

Mpango huu ulikuwa maridhawa kabisa.

“Hatuchomoki!” Zubeda alijikuta akitokwa na kauli ile ya kukata tamaa.

Kauli ile haikuelea sana hewani kabla mlipuko mkubwa haujasikika na palepale askari wawili walio katika sare wakaanguka chini.

Mmoja aliyekuwa amemshika Kobo ili aweze kutembea alimwachia na Kobo akatua chini mzimamzima.

Akatulia!

Hapoikazuka vita mpya, Nguzu na Zubeda wakashindwa kuelewa hii vita inahusisha pande ngapi.

Wakati wanaamini kuwa ni pande mbili pekee sasa wanashangaa kuwa wao hawahusishwi na wakati huohuo vita inaendelea.

Milio ya risasi za kuviziana ikaendelea huku askari wakipokea amri kalikali kutoka kwa kiongozi wao.

Mambo yalikuwa magumu haswa!

Asakari walikuwa wamepagawa, ni kama walikuwa hawajatarajia upinzani wa aina ile kutoka katika nyumba ile aliyokuwa akiishi Zubeda.


HAKUWA katika mavazi yake yaliyowatisha wengi pindi walipomuona, hakuwa katika kiti chake cha kuzunguka huku akipokea taarifa zilizopaswa kumfikia yeye na kisha kutoa maamuzi.

Hakuwa katika nafasi yake ya kuwasiliana na raisi wa jamuhuri wa muungano.

Alikuwa katika fulana yake pamoja na bukta laini, na alikuwa chumbani kwake.

Vyeo vyote aliamua kuviweka kando.

Alichoingia nacho pale chumbani ni thamani ya urafiki.

Hakuwa na roho mbaya, na hilo alilitambua vyema bali alikuwa ni mtu anayesimamia haki na usawa.

Ukimwona ana roho mbaya kwa sababu tu amekushinda kwa kuusema ukweli basi alikuwa tayari kuonekana hivyo.

Aliijua mipaka yake vyema, hakuwa shabiki wa mateso wala vifo vya hovyohovyo.

Alikuwa na weledi wa kutosha na hii haikuwashangaza wenzake baada ya kusikia jina lake likitajwa kuwa atakuwa mkuu wa majeshi ya polisi.

Hata yeye hakushangaa, maana hakupewa cheo kile kwa bahati mbaya.

Alistahili!

Sasa alikuwa hayafikirii yote haya, alikuwa akimfikiria Kobo, ambaye alitokea kuwa rafiki yake sana mpaka mtafaruku ulivyokuja kuwaweka mbali kidogo kisha madaraka yakahakikisha wapo mbali kabisa.

Kwa kufumba ama kufumbua macho IGP hakuacha kuiona sura ya Kobo ikiitaka huruma yake, akayakumbuka maneno ya Kobo juu ya mkewe ambaye yu katika kuzimia.

“Nampenda sana mke wangu, ninapaswa kumuomba msamaha. Kama haitafaa mimi kubaki huru nakusihi rafiki yangu na mkuu wangu nifanyie upendeleo nisining’inie katika kitanzi kabla mke wangu hajazinduka.”

Maneno haya yalimuumiza mno, akajaribu kuelekeza macho huku na kule ili asahau kuhusu Kobo lakini akajikuta akilitazama tukio la Kobo kujitoa muhanga na kumsukuma kando ili asipatwe na risasi iliyomkusudia.

Akajikaza hisia zisimwendeshe lakini chozi likamsaliti.

Akajikuta analia!

Akayakumbuka maneno makali ya Kobo juu yake alipomwambia kuhusu pambazuko baya kupindukia.

“Jitazame yawezekana pambazuko hili likakuandama wewe pindi utakapogundua kuwa sikuwa nyuma ya maovu haya.”

IGP akasimama na kujifuta machozi pamoja na jasho lililoanza kumtoka.

Akachukua simu yake na kumpigia msaidizi wake, ambaye pia alikuwa ni rafikii yake nje ya madaraka hayo.

Akajaribu kumweleza kwa kifupi, akaeleweka na hatimaye wakachukua maamuzi ya kutuma watu watatu wa ziada katika tukio hili kutazama jinsi linavyokwenda.

Walikuwa ni vijana wanaoaminika sana kiuwezo katika mapambano na pia katika umakini.

Walau IGP aliweza kulala vyema baada ya kufanya hatua za mwisho kabisa za kutambua ikiwa Kobo anastahili jela ama la?

Majira ya saa kumi jioni alishtuliwa na simu yake ya mkononi.

Ni nambari aliyompatia msaidizi wake ili lolote litakalotokea waweze kupeana taarifa.

Akaipokea upesi ile simu.

“KIjana mmoja ameuwawa na mwingine amejeruhiwa begani.” Taarifa ile ilimtisha mno IGP.

Alitambua kuwa jambo hili lina uzito lakini hakukadiria uzito ule kufikia huku kwa vijana ngangari kama wale kutetemeshwa.

Akamsihi aongeze vijana na amri iwe moja tu, warejee na majibu.

“Kiongozi kuna kitu kingine cha ziada.” Alisema kisha akamwacha IGP apumue kidogo.

“Ile sauti uliyoniambia imesikika tena. ‘SHUSHA MBUYU KUNA NYOKA…”

“Ni sauti ya nani?” Aliuliza kwa utulivu wa hali ya juu.

“Aliyeisikia ni marehemu tayari. Lakini ni mmoja kati ya timu uliyoipa dhamana ya kwenda kuikagua nyumba ya Kobo.”

“Na ni nani anayeshambulia ikiwa sio hao wapekuzi?”

“Kuna safu nyingine kutoka katika kona za nyumba waliyoenda kuipekua. Kuna vita ya pande zaidi ya mbili mkuu.”

“Ongeza vijana, fanya wanane. Wahakikishe wanaleta majibu.”

“Sawa. Afande…” Alijibu na kukata simu.

Hali ilikuwa mbaya tayari.


INSPEKTA KOBO alianguka mwili wote lakini hakuzimika macho yake. Alitulia kama aliyekwishapoteza uhai tayari.

Aliendelea kutazama mashambulizi yalivyokuwa ya kutisha, kuna jambo alikuwa akilisoma.

Wapinzani waliokuwa wamejificha katika kuta na dari walikuwa wakifanya mashambulizi ya akili sana huku hawa waliomsindikiza kukagua nyumba walikuwa wengi lakini bure kabisa.

Walikuwa ni watu wanaotii sheria tu, wakiambiwa waachie risasi wanamimimina hovyo bila kumaanisha kudhuru!

Akiwa palepale alizungusha macho yake huku na kule, na mara akatua katika madirisha ya nyumba ile.

Akaona kama kivuli kikivuka upesi kwa kuinama chini.

Kivuli kile alikuwa amekizoea sana, kama kisingekuwa chenyewe basi kingekuwa ni pacha ya kile alichokizoea.

Zubeda! Inspekta akatokwa na jina lile huku akiwa bado amenasa pale chini, kulia kwake pakiwa na mwili wa askari aliyetokwa na uhai tayari.

Kwa umakini wa hali ya juu akajisogeza mita kadhaa taratibu hadi akawa jirani kabisa na yule askari. Muda wote macho yake yaliwatazama wale washambuliaji waliojificha.

Alishagundua tayari kuwa washambuliaji walikuwa wanaye mdunguaji wao na alijua vyema kazi ya kudungua maana alikuwa hakosi kila akishambulia.

Faida kuu kwa Kobo ni kwamba huo ulikuwa moja kati ya mchezo wake uliompandisha cheo upesi na mchezo huohuo ulikuwa umemuingiza matatani.

Shabaha!

Kobo akainyakua silaha ya askari mfu pale chini.

Akatabasamu baada ya kuitambua kuwa ni silaha aipendayo.

Akatulia tena kama mfu huku akiangalia ni wapi anapoweza kuanza kushambulia. Alitambuwa wazi kuwa hawezi kushambulia kwa muda mrefu kabla nguvu hazijamwisha na pia kuchabangwa risasi na kupoteza maisha hivyo alihitaji akifanya shambulizi liwe kubwa na lenye maana kubwa.

Akiwa bado katika kuliandaa shambulizi aliisikia simu ya upepo jirani na lile gari waliloingia nalo pale ikiunguruma maneno kadhaa ya kusihi.

Hakuwa na uhakika kama msikilizaji wa ile simu aliamua tu asiijibu ama simu ilikuwa haina msikilizaji.

“Shusha mbuyu kuna nyoka. Shusha sasa hivi ova!”

Sauti ile ilitokea nyuma ya gari ambalo lilikuwa limeharibika vibaya kutokana na milipuko ya risasi.

Mapigo ya moyo yakaongeza kasi, umakini ukatoweka akataka kukurupuka lakini alipokumbuka kuhusu ‘sniper’ aliyejificha mahali fulani aliendelea kutulia.

Punde baada ya amri ile kutoka mita kadhaa hadi kuufikia ukuta mrefu kiasi ulioizunguka nyumba ile akasikia kishindo kikali, na kisha kikasikika kilio.

Kuna mwanaume alikuwa amemezeshwa risasi tayari. Alikisia

Huyu ni nani? alijiuliza kisha akajigeuza na kuilalia ile bunduki na kuendelea kubaki kana kwamba hana uhai.

Alikuwa na uhakika wote kuwa alichokisikia katika simu ni sauti ileile iliyomkosesha shabaha na utulivu mjini Shinyanga na kisha kumletea majanga.

Lakini safari hii ilisikika katika simu ya upepo. Hakufahamu fika ni nani mzungumzaji na alikuwa upande upi.

Na punde baada ya kauli ile shambulizi likafanyika.

Ni nani huyu? likabaki kuwa swali zito kwa Kobo.

Tukio la Kobo kuichukua bunduki hadi kuilalia lilikuwa likifuatiliwa vyema na mdomo wa bunduki iliyokuwa tayari kukohoa risasi.

Kobo hakujua, aliamini kuwa umakini wake ulikuwa wa kiwango cha juu zaidi.

Baada ya shambulizi lile akazisikia hatua zikisogea kwa kujiamini kuja mahali alipokuwa.

Akazivuta pumzi zake kisha akaanza kuzitoa nje taratibu kabisa.

Akakisikia kiatu kigumu kikimkanyaga mguuni.

“Huyu tayari… hamna kitu humu.” bwana aliyekuwa anamkanyaga akatoa jibu lile.

“Chapa risasi kabisa kujihakikishia, hakawii kuwa hai akatuharibia.” Iliamrisha sauti nyingine kwa ukali iliyotawaliwa na madaraka.

Kobo akaanza kuweweseka pale chini, alijilazimisha kuendelea kutulia kana kwamba ni mfu lakini kitendo cha kusikia kuwa anapaswa kuchapawa risasi ili kuhakikisha juu ya uzima ama kifo chake, hii ilikuwa ni sahihihi mbaya kabisa.

Kobo hakumsikia yule aliyeamriwa akijibu kitu chochote, alishindwa kuelewa nini maana ya kimya kile.

Hakutaka kucheza bahati nasibu ya ‘nitakufa ama wataniacha’

Akaamua kutumia nguvu zake za mwisho na njia pekee iliyosalia katika kujitetea.

Akageuka upesi mtutu wa bunduki katika mikono yake tayari kwa kufyatua.

Lakini hakuwa na mwendokasi wake wa zamani, Kobo huyu alikuwa mgonjwa, mzito, asiyeweza kuona vyema.

Hakuwa Kobo anayetisha tena.

Inspekta Kobo alikuwa amechelewa tayari……

“Nayaweza yote kwa Imani na jitihada”

Kama alivyoona ndivyo ilivyotokea, yule bwana akafyatua risasi.

Kobo hakutarajia kama angepata nafasi ya kusikia risasi ile ikivuma pembezoni mwa sikio lake.

Lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Shabaha iliyumba malikiti.

Kobo akapata muda wa kufumbua ili atazame kama ataweza kubiringita tena ili akwepe kwa mara nyingine tena.

Akayahimiza macho yake kutazama….

Macho yakakutana na kitu cha kutisha, haikuwa risasi ya kawaida… hii ya sasa asingeweza kuikwepa asilani.

Ilikuwa pana sana, hata kama angebiringita kwa kasi kuu bado asingeweza kujinasua.

Inspekta Kobo akasalimu amri kwa kuitanguliza mikono yake kukabiliana na kitu kile kikubwa.

Kilipomkaribia zaidi akayafumba macho yake.

Kikatua juu yake, upepo ukakata!

Kobo akarejea katika ulimwengu wa waliopoteza fahamu wasijue namna ya kuzitafuta.


MIILI miwili ilikuwa imebebana bila kukusudia, yote isiyojiweza na bila budi kujibweteka mwili mmoja juu ya mwingine.

Miili hii ilitazamwa kutokea mbali na vikundi viwili visivyokuwa na majina rasmi ya kuvitambulisha.

Kukosa majina hakukumaanisha ule uwepo ni batili.

“Unahisi bado anapumua yule?” Sauti dadisi ya Zubeda ilimuuliza Nguzu.

“Uhakika pekee ninaoweza kuuthibitisha ni kwamba yule bazazi nimemfyatua barabara katika chembe ya moyo wake…” Alijibu huku akiwa bado na umakini wa hali ya juu.

Kundi la pili lilikuwa katika mfadhaiko, wakati likiamini kuwa limeunyakua ushindi na kilichosalia ni kuvikwa taji mara shambulizi linatoka wasipopajua na kumsambaratisha mwenzao aliyekuwa anangojewa waweze kuondoka eneo lile.

Makundi yote mawili yalibaki katika tahadhari hakuna aliyekuwa tayari kwenda kuwatenganisha wawili wale waliolaliana.

Mmoja akiwa ni mwili na mwenza wake akiwa ni mwili na roho pamoja na fahamu zilizokwenda likizo isiyokuwa na muda maalumu.

“Martin…. bila kujalisha kama mzee Kobo atainuka ama la, bila kujali kama tutabaki hai ama la. Naomba unisamehe mimi kwa yote yaliyotokea” Sauti tulivu ya Zubeda ilipenya katika masikio ya Martin Nguzu.

Hakuitoa silaha yake katika lindo lake katika watu wale wawili waliolaliana mmoja akiwa ni Inspekta Kobo.

“Unavyozungumzia kuwa hai ama la kana kwamba ni pipi ambayo unaweza ukaamua kuimung’unga ama la na isikupunguzie lolote. Uhai unayo thamani kubwa sana usiuongelee kijuu juu hivyo” Akamjibu kwa kumnanga.

Koplo Zubeda akabaki kimya huku hatia ikimsulubu na kujiona yu mkosaji mkubwa sana.

Hakukumbuka kujiuliza ni lipi basi kosa lake?

KUTOKEA upande wa pili, tumaini la ghafla katika pori la mfadhaiko liliibuka, aliyeshuhudia akawasihi na wenzake nao waone.

“Oya…yupo hai aisee… namuona anatikisika” Alisema na kuwavuta wenzake kutazama kwa makini, kweli mwenzao alikuwa anajitikisa.

Ile hulka ya wanadamu waonapo jambo wasilolitarajia hujikuta wakiisahau misingi yao yote na kujikuta katika mkumbo wa liwalo na liwe, haikuwa upande huu badala yake ilikuwa upande wa pili.

Zubeda anayesukumwa na hatia ya kupendwa kwa dhati kisha kuja kumsaliti Inspekta Kobo na hatimaye kumweka katika kitanzi kile ilikuwa inamponza.

Konstebo Nguzu naye alihitaji sana kujua ni nini hatma ya Kobo pamoja na makundi yanayoshambulia yana nia gani.

Hakuamini hata kidogo kuwa yawezekana kabisa kuwa eti chanzo ni yeye tu hadi haya yote yanatokea.

Kama ni yeye kwanini wahukumiwe hata wasiokuwa watu wa ukoo wake?

Wakati akiwaza na kuwazua akaikumbuka sura tulivu ya Kobo iliyojaa hekima na busara siku aliyomuita na kumsihi aachane na Zubeda wake!

Huruma kuu ikamvamia.

Hali hizi ziliwafanya wasisimke walipoona ile miili pale chini ikijitikisa.

Nguzu akamuhakikishia Zubeda kuwa aliyejitikisa ni Kobo si yule hayawani aliyejaribu kumfyatua.

Zubeda hakuamini upesi, Nguzu akajitoa muhanga kwenda kumwokoa Kobo, huku nyuma shughuli ya kulinda usalama wake akaiacha mikononi mwa Zubeda.

“Kiumbe yeyote atakayejaribu kunidhuru, fyatua usifikirie mara mbilimbili. Ule muda utakaotumia kufikiri nd’o muda ambao macho yako yatakishuhudia kifo changu. Hiki cha sasa kitakuwa kifo taslimu.” Nguzu alimweleza Zubeda.

Kisha akamkumbatia kwa nguvu sana, akamtazama machoni na kuzungumza kwa sauti tulivu.

“Naitwa Martin Ngengekuzenza Nguzu. Jina langu lina maana kubwa kulikoni uhai wangu… kwa lolote lile nikianguka naomba nifukiwe kwa jina hilo.” Akamaliza na kumbusu Zubeda katika papi za midomo yake.

Akaondoka akimwacha Zubeda akipambana machozi yasiyazibe macho yake.

Alihisi lile ni busu na kumbatizi la mwisho kutoka kwa kijana yule machachari.

Umakini ukarejea baada ya Konstebo Nguzu kuingia ukumbi wa vita, Zubeda askari mkakamavu akaishikilia vyema silaha yake, akavuta pumzi na kushusha akajiandaa kukabili kwa lolote kama alivyoelekezwa.

Umbali wa kutoka mlangoni hadi ulipokuwa mwili wa Kobo haukuwa mita nyingi sana, lakini ilikuwa ni zaidi ya kilometa kadhaa kwa Nguzu kutokana na kutokuwa na uhakika ni wapi anaweza kuwepo adui awezaye kuitoa roho yake mara moja.

Akapiga hatua huku uoga ukishamiri katika moyo wake, alijitia ujasiri kwa maneno aliyoelezwa na mzee Majenga kuwa hatakufa kwa sababu mzimu wa babu yake unaishi naye mpaka atakapoitimiza azma yake.

Hatua takribani kama tano kabla hajaufikia ule mzoga juu ya mwili. Kilio kikubwa kikasikika kutokea katika dirisha ambalo alibaki Zubeda kama mlinzi wake wakati akielekea kumkomboa Kobo.

Upesi Nguzu akaiweka vyema silaha yake lakini hakujua ni wapi afyatue kabla hajaisikia sauti kali nyuma yake ikimwamuru kutulia kama alivyo.

Nguzu alikuwa mikononi mwa watu wabaya!

Nini kimejiri kwa Zubeda?? alibaki akijiuliza wakati huu ambapo alimuhitaji sana mwanamama yule ili kuweza kumkomboa.

Kimya! hapakuwa na shambulizi lolote la kumkomboa.

“Taratibu kabisa angusha silaha yako chini, bila kuinama walau sentimita moja” Sauti ikachimba mkwara zaidi.

Nguzu hakusubiri onyo la pili akaiachia bastola yake itue chini naye abaki na Mungu pekee kama mlinzi wake wa haja.

“Wananiua wapuuzi!” alijisemea

“Sogea mbele kwa hatua za taratibu kabisa. Bila shaka sina haja ya kukumbusha kuwa ukifanya upuuzi wowote ule hautakumbuka chanzo cha kifo chako….” sauti ile tulivu inayojiamini iloiendelea kumwongoza Nguzu.

Nguzu akatii!

Alikuwa kama hayawani ama zuzu asiyejua ‘a’ wala ‘ba’. Kifo pekee nd’o kitu ambacho aliwaza kwa wakati huo.

“Shusha mbuyu mwamba….” Sauti tofauti na ile iliyokuwa inamwongoza ilizungumza kwa kukaripia na kuonyesha uharaka.

Mbuyu? Nguzu akajiuliza asijue ni kitu gani kimemaanishwa katika kauli ile tata.

Hakuwa tayari kuuwawa namna ile bila kuimaliza kazi yake, lakini pia hakuwa walau na akili ya ziada ya kujiokoa.

Utajiokoa vipi ungali jirani na mdomo wa bunduki usiokuwa na huruma ukifunguliwa?

“Mpigie tajiri…” Sauti iliyokuwa ya kwanza kumtetemesha Nguzu ilizungumza.

Baada ya sekunde chache, mazungumzo yalisikika upande uliosikika zaidi ulikuwa upande wa kwanza huku aliyepigiwa simu akisikika kwa mbali sana.

Simu haikukatwa iliachwa hewani na hapo Nguzu akarushiwa swali.

“Unaitwa nani? na upo hapa kwa shughuli gani?”

Nguzu akafikiria kuhusu kuongopa kuhusu jina lake, lakini akachagua kucheza karata nyingine.

“Naitwa Martin, nipo hapa kwa ….”

“Martin nani?” Swali lilitupwa, hadi sasa alikuwa hajaziona nyuso za maadui zake.

“Martin Nguzu!” Akamalizia.

“Acha upuuzi, hatuna muda wa kupoteza,” alijibu kwa hasira kisha akarejea katika simu yake, “Tajiri… huyu mjinga anasema anaitwa Martin Nguzu. Hana faida kwetu…”

“Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu. Sijawahi kufa lakini nakijua kifo. Jaribuni kuniua mara ya pili huenda nikakijua kifo” Nguzu akapigilia hofu na utata mwingine. Alikuwa ameupata ujasiri wa hali ya juu sana.

Wale mabwana wawili hawakuelewa ni kipi anachojiamini angali hana silaha na wakiamua ni sekunde moja tu wanammaliza.

Mazungumzo katika simu yakaendelea huku akibaini sasa kuwa mpiga simu alimuhitaji akiwa hai. Lakini hilo si pekee lililomjengea ujasiri.

Kuna jambo la ziada ambalo lilihesabika kwa sekunde kadhaa kabla halijabadilika na kuwa kindumbwendumbwe!

Ilikuwa ghafla sana, Nguzu akaruka upande wa kushoto bila wale watu kumtarajia kama atafanya hivyo.

Palepale milipuko miwili ya risasi ikasikika.

Mayowe ya hofu na maumivu yakasikika.

“Usithubutu walau kujitikisa, maana nitafyatua jicho lako badala ya bega!” Sauti iliyoongea kwa tabu kabisa ilitoa maelekezo.

Bwana aliyekuwa anazungumza na simu akabaki kutulia tuli asiamini kilichokuwa kinatokea.

Inspekta Kobo kutoka katika usingizi wa kifo alikuwa amechota medali zake za ushujaa palepale chini.

Nguzu pekee ndiye aliyeutambua uhai wake, na aliamua kumuamini walipozungumza kwa ishara za macho.

Ishara ambazo ni wao pekee wangeweza kuelewana kwa sababu wamepitia mafunzo ya kijeshi.

Nguzu akajitokeza na kuiwahi ile silaha ambayo ilimponyoka yule aliyesambaratishwa na Kobo kwa shabaha moja iliyojikita katika kifua chake moja kwa moja.

“Nahitaji ujibu swali uliloniuliza hapo kabla. Ni nini unafanya hapa na unafanya kwa manufaa ya nani? Niko tofauti kidogo na wewe… sichimbi mkwara huwa natenda. Ukichelewa kunijibu nakuvunja miguu…..” Nguzu akiwa anatazama na bwana yule aliyepagawa alizungumza.

Yule bwana akapagawa asiamini anaonana ana kwa ana na Kontebo Martin Nguzu ambaye wanaamini kuwa walimteketeza ndani ya nyumba.

Hakuwa na budi kujieleza vyema kabisa.

Nguzu akashtuka jina la muhusika wa haya lilipotajwa.

Lilikuwa jina refu lakini ubini wa ‘KAZEZE’ ukamwacha katika namna ya kupigwa butwaa.

Jina ambalo lipo katika kitabu cha babu yake, mzee Florian Ngengekuzenza Nguzu, jina lililosheheni chuki, visasi na unyanyasaji.

Jina hili linasikika tena katika maisha yake.

“Ina maana Joseph Kazeze alikiacha kisasi chake kirithiwe na watoto wake ama?” Nguzu alijikuta akiuliza kwa sauti, lakini asipate mtu sahihi wa kumjibu.

“Zu…Zubeda yupo wapi” Inspekta Kobo akiwa ameketi chini aliuliza kwa sauti ya chini sana, bila shaka alikuwa katika maumivu bado.

Swali lile likamshtua sana Nguzu, alikuwa amesahau kabisa kuwa kuna mlipuko ulikuwa umesikika kabla hajadhibitiwa na mabwana wale waliodai kuwa walikuwa wameagizwa na mkuu wa majeshi mstaafu, Jeremiah Stamford Kazeze.

Kukosa kule utulivu kukaondoka na umakini wake.

Yule mtumwa akamvamia Nguzu upesi na teke kali ambalo liliiondoa silaha yake mkononi.

Akarusha teke la pili ambalo lilielekea kupasua fuvu la kichwa cha Nguzu. Nguzu akawahi kuinama.

Wakati anajiandaa kumkabili akajikuta akikabiliana na madonge ya damu.

Kobo alikuwa amejipima tena umakini wake kama upo sawa.

“Usingemuua Inspekta…”

“Angekuua wewe…. amepitia mafunzo ambayo wewe hujawahi hata kuyaona kwenye luninga…. hata hivyo sijamuua labda aamue kufa mwenyewe tu…”

Hatimaye Inspekta alisimama kwa tabu, wakati huo Nguzu alikuwa ametangulia kwenda kuitambua hali ya afya ya Zubeda ambaye bila shaka alishambuliwa.

Hakika alikuwa amepoteza fahamu, risasi ilikuwa imemkwangua begani na kumtupa ukutani.

Halikuwa jeraha kubwa sana, hata alivyoshtuliwa kwa kumwagiwa maji ilikuwa rahisi kwake kusimama na kutambua kila kilichokuwa kinaendelea.

Kigiza kilikuwa kinaanza kuingia wakati watatu hawa wakiwa wamepata fursa ya kuwa mbali na ile nyumba na walikuwa wameweza kujadili kwa ufupi sana juu ya kisa hiki.

Hakuna aliyegusia suala la mapenzi ya kuchangia, walitazama zaidi uhai na amani yao.

Inspekta akashauri wafanye mchakato wa kuwasiliana na IGP waweze kuupata msaada wa upesi sana dhidi ya Kazeze IGP mstaafu waliyeamini fika kuwa yupo nyuma ya yote haya.

Wakati wao wanafikiria namna ya kuwasiliana na IGP…. ni wakati huohuo IGP mstaafu Kazeze alikuwa yu njiani kuelekea nyumbani kwa IGP.

JOTORIDI lilikuwa la wastani lakini hiyo ilikuwa kwa wale wenye amani pekee.

Mashaka ya mwandishi wa habari, Juma Kihwele ‘kimbelembele’ yalisababisha mwili wake utokwe jasho mara zote zlizokuwa akifikiria ni mbinu gani za ziada atazitumia kuweza kuipata tena amani yake na uhuru.

Hapo kabla shuleni alikuwa nguli wa kusaliti wenzake linapokuja suala la mgomo. Hakuwa mtu anayeweza kupigana, kila penye shari yeye alijiweka kando na alikuwa shahidi wa kwanza ulipohitajika ushahidi wa nani ameanzisha ugomvi.

Hali hii ilifanya walimu wampende lakini alichukiwa na wanafunzi.

Mbaya zaidi darasani alikuwa anaongoza, chukia usichukie nd’o ilibaki hivyo.

Baadhi ya wanafunzi ambao walijikuta matatani kutokana na ushahidi wa Juma Kihwele waliishia kumwekea viapo ambavyo kwa macho ya kibinadamu ilionekana wazi kuwa ni maneno ya mkosaji.

Walimweleza kuwa ipo siku atajutia uoga wake, kiherehere chake na hapohapo akili zake za darasani hazitamwokoa.

Aliishia kucheka na kuendelea kuhsika namba za juu darasani.

Baada ya miaka mingi kupita Juma amejichanganya na kujiingiza katika ‘dili’ alilolichukulia kuwa ni pesa nyepesi, sasa yu mikononi mwa watu ambao ili uone jino lake moja ni pale tu atakapokuwaanapiga mwayo. Kinyume na hapo zilikuwa ni ndita na lugha za ukali kila mara.

Juma Kihwele analazimishwa aelezee ana ubini gani na Martin Nguzu ambaye aliendelea kutambulika kama hayati Konstebo Martin Nguzu.

Juma alikuwa ametema kila alichokuwa anakitambua lakini bado hakuonekana kama amesema lolote, hakuwa amepigwa sana, vibao kadhaa na mateke yasiyodhamiria kuvunja lakini kipigo hicho kwa Juma alijihisi anapaswa kuorodheshwa katika kitabu cha rekodi za dunia kama mwanadamu aliyewahi kupigwa kupita wote duniani na bado anapumua.

Juma hakujua maana halisi ya kipigo.

Maelezo ya Juma Kihwele yakalileta mezani jina la Inspekta Kobo na Koplo Zubeda.

Juma akamtaja Zubeda kuwa anajihusisha kimapenzi na Inspekta Kobo na hapohapo alikuwa anajihusisha na Konstebo Nguzu.

Jibu hili likaongeza umakini kwa waliotumwa kumuhoji, majibu yakatumwa na kufika sehemu husika.

IGP Mstaafu Jeremia Kazeze akayatazama majina yale kama maadui zake, yeyote aliye karibu na Nguzu kwake alikuwa ni adui asiyefaa kuishi.

Sumu aliyomezeshwa na babu yake na kisha baba yake ilikuwa imekolea na ilikuwa muda wa kuitema.

lakini urithi si kwa magonjwa tu, hata nidhamu ya akili unaweza ukarithi.

Hayati Florian Ngengekuzenza Nguzu wakati anamsimulia Majenga kwa ajili ya kuandika kumbukumbu ya kizazi chake alimuhesabu Joseph kazeze (babu wa Jeremiah) kama mshamba anayetumia cheo chake kijinga. Ngengekuzenza alijihesabu kama mshindi kwa vita vyote dhidi ya Joseph Kazeze, na kweli alimtandika ipasavyo kwa mbinu chache tu ambazo kwa Joseph Kazeze zilikuwa ngeni na zilizosheheni suluba kubwa.

Sasa wawili hawa walikuwa wamepumzika tayari katika nyumba zao za milele.

Ngengekuzenza Nguzu akijitoa uhai kwa kujinyonga huku Joseph Kazeze akikamilisha safari yake kwa shinikizo la damu. Shinikizo lililosababishwa na mapigo kutoka kwa Ngengekuzenza Nguzu.

Chuki haikuishi katika moyo wa Konstebo Martin Nguzu na hakujua hapo kabla kuwa kuna vita mbayo haikuwahi kukamilika, lakini Jeremiah Kazeze yeye alibaki na chuki kuu.

Akafuata misingi aliyorithishwa ikiwa pamoja na mbinu za ‘kikuda’za kukabiliana na adui zake.

Akavishwa cheo cha IGP na kukitumia kusulubu wowote aliodhani ni maadui.

Akamaliza muda wake huku akiwa hajakutana na jina Nguzu.

Akiwa hana cheo jina lile linamjia ghafla mezani kwake.

Vita mpya inaanza, vita mbayo haikuonekana kama inatisha.

Jeremia Kazeze anatuliza akili yake na kufikiria ni kifo gani kitamfaa zaidi Konstebo Martin Nguzu, kifo ambacho kitakuwa ni kisasi sahihi kwa yale yaliyomtokea babu yake miaka ya nyuma.

Hatimaye anamchagulia adhabu ya kuchomwa moto dunia kisha akakutane na mwingine katika safari yake nje ya dunia.

Mpango mdogo unasukwa kwa akili ileile ndogo, Nguzu anachomewa ndani ya nyumba yake.

Wakati wa utafiti wa kuzifuatilia nyendo za konstebo Nguzu. Wanapata jambo jipya, mahusiano kati ya Nguzu, Zubeda na Inspekta Kobo.

Jeremiah anachekelea na kuamua kumuuzia kesi ile Inspekta Kobo.

Oparesheni inafanyika na jalada linakaribia kufungwa.

Mwishoni mwa mchezo anatokea Juma Kimbelembele akijaribu kuandika makala juu ya yaliyotokea.

Anakuwa amenunua kesi pasi na kujua kuwa ni kesi kubwa.

Upande wa Jeremia Kazeze ukaamini fika kuwa yule bwana kuna uwezekano anafahamu ni wao wanahusika katika kuiteketeza nyumba ya Nguzu.

Upesi akaamuru kundi jingine linalomtii limfuatilie kwa ukaribu kila hatua ambayo atakuwa anapita.

Ni katika kufuatilia huku yanazuka mengine makubwa.

Sasa Juma Kimbelembele yu katika mikono yao.

Anatamani walau kupambana lakini uwezo huo hana. Amelia kama mtoto lakini haijatosha kulainisha sauti za watu wale wanaozungumza kama wauguzi wa wodi ya vichaa walioshindikana.

Kila mara wanafoka!

Ilikuwa siku nyingine tena katika mazingira yaleyale, lakini sura ngeni ilimjia.

Ilikuwa ni ngeni kwa pale ndani na sura hii ilimpa tumaini jipya kwa sababu alikuwa akiifahamu vyema.

Alikuwa ni mkuu wa jeshi la polisi mstaafu.

Jeremia Kazeze.

Juma Kihwele akajihesabia kuwa amekutana hatimaye na mtu ambaye atamuelewa na kumwokoa.

Hakujua kuwa amekutana na anayewatuma wale aliowaona kama mashetani yanayoishi.

“Haujambo?” Jeremiah aliuliza kifedhuli.

“Sija… shkamoo… sijambo..” alijiumauma katika kujibu.

“Martin Nguzu alikufa ama hakufa? na kama hakufa nataka kujua ni nani aliyehusika katika kumwokoa…” Sauti kavu ya Jeremia ilihoji.

“Sijui lolote muheshimi…” kabla hajamaliza kumjaza cheo alipokea kofi kali katika shingo yake.

Yowe la hofu likamponyoka.

“Nahitaji jibu tofauti na sijui.”

“Muheshimiwa mi naapa haki ya…” Hata hii kauli pia haikumalizika kabla hajapokea kofi jingine, hili la sasa liliuchana mdomo wake.

“Umeona biblia ama msaafu humu ndani? Sihitaji viapo nahitaji majibu…”

Juma Kimbelembele sasa alikuwa amepatikana.

Alijaribu kutuliza akili yake na kuchagua jibu la kutoa lakini alihofia kuwa linaweza lisiwe na ushawishi.. Lakini ni heri kuzungumza kuliko kuwa kimya dhidi ya mtu yule aliyekuwa mbele yake.

“Nyumba iliungua mkuu, sikumuona akitoka hai. Alikufa na wanahabari waliandika…”

“Wanahabari ni akina nani hadi unawataja kama utetezi wa hayo unayosema?”

Kimya! hakuwa na la kujibu.

“Una uhakika alikufa?”

“Nyumba iliteketea…” alijibu kinyonge lakini unyonge wake haukumzuia Jeremia kumbutua tena, safari hii kwa kutumia mguu wake.

Juma akajikaza hakupiga kelele kubwa licha ya kuumia.

Jeremia Kazeze akatoa picha kadhaa akamtupia Juma Kihwele akawa anatazama nazo.

“Unafahamu hicho ni nini?”

“Ndio mkuu, nyumba ya hayati Nguzu baada ya kuteketea”

“Ooh! Kila mtu anajua nyumba iliteketea, sijafunga safari kutoka huko mbali kuja kupata uthibitisho kuwa nyumba iliungua….. najua kusoma na ninaona pia… nahitaji kujua wewe na Nguzu ni washirika katika ngazi ipi?”

“Wallah! naapa sina ushirika wowote na marehemu…”

“Unavyosema marehemu kama vile uliuzika mwili wake… sikiliza wewe mtoto. Kama unayaficha unayojua kuhusu Nguzu, hautajificha kuizika miili ya wapendwa wako. Kwa mkeo nitajitahidi ubaki uso pekee ili usije kugoma kuuzika mwili ukisema sio mkeo, ila hutapata hamu ya kukiuona kiwiliwili chake, na ukijitia shujaa kukiona utakuwa unakiota ndotoni kila siku na itakuwa ndoto ya kutisha…”

Akaweka kituo na kutoka nje.

Juma alipojaribu kuzungumza akaishia kujikaza asijikojolee zaidi wakati tayari keshajimwagia kojo muda mrefu tu.

______

JEREMIA KAZEZE mwenye akili kiwango cha babu yake aliona njia pekee ni kuwahi kwa IGP kwa ajili ya kujisafisha na kuyaweka sawa mazingira ikiwa tu jambo lolote litaharibika zaidi.

Aliziona dalili za kuangushwa kama alivyoangushwa babu yake zikimnyemelea….

Ilikuwa yapata majira ya saa mbili usiku.

Haukuwa utaratibu wa Kazeze kumtembelea mara kwa mara IGP, ni yeye aliyependa kutembelewa kwa sababu ya kumzidi kiumri na urithi wa tabia ya kupenda sifa za kijinga alioupata kwa babu yake.

Siku hii ilikuwa tofauti zaidi, tena saa mbili usiku.

Mbaya zaidi hakupiga simu kutoa taarifa.

Alipokelewa bila mashaka, taarifa za walinzi zikapitishwa ndani na ruhusa ikatolewa.

Kazeze akaingia kuonana na IGP.

Tofauti na nyakati nyingine walizowahi kuonana, hii ilikuwa tofauti sana. Kila mmoja alikuwa katika ulimwengu wake.

Licha ya kujilazimisha kuonenekana kuwa wapo sawa ila nafsini hali ilikuwa wazi.

Mgeni alianza kuelezea juu ya ujio wake usiku ule, akaanza kuulizia hatma ya Inspekta Kobo na sakata la kujihusisha na majambazi sugu mkoani Shinyanga.

IGP akamweleza juu juu kuwa hadi wakati huo Kobo alikuwa amekataa kukiri kuwa aliikosa shabaha ile maksudi na anaapa kuwa hajihusishi na kundi lile.

“Nawe umeamini?” Aliuliza kwa mshangao..

IGP akaduwazwa na swali lile, japokuwa haikuwa mara ya kwanza kukerwa na maswali ya yule aliyemtangulia.

Kwanini ananichimba huyu?! Alijiuliza kisha akatabasamu na kujibu, “vijana wangu wanaendelea kumuhoji. Watanipatia majibu ninawaamini sana…”

“Na unafahamu lolote kuhusu mauaji ya askari wetu mtiifu, konstebo Nguzu aliyechomewa ndani ya nyumba?”

“Naam! na nilifika eneo la tukio, vipi kuna jipya?”

“Inspekta Kobo anahusika kumteketeza, inasemekana Nguzu anajua kuhusu Inspekta Kobo kujihusisha na kundi lile, na alikuwa anakaribia kuvujisha siri..”

“Unasema Nguzu anajua kama yupo hai mkuu….”

“Aam! Nguzu alikuwa anajua…” Akarekebisha huku akijaribu kujichekesha.

“Upo ushahidi wowote wa kumweka hatiani Kobo?”

“Kuna mwandishi wa habari alishuhudia kila kitu, kuanzia muda wa kuwasili hadi muda wa tukio?”

“Aisee! aliarifiwa na nani hadi kuweza kuzijua nyendo za askari makini kama Kobo!” Alijibu IGP.

Kitendo cga Kobo kuitwa askari makini kikamkwaza Jeremia Kazeze.

“Unamuita makini na kwa maksudi kabisa ameacha kumsambaratisha jambazi sugu, jana watu nane wameuwawa huko Shinyanga, wawili kati ya hao ni askari wetu na pasi na shaka muhusika ni huyohuyo aliyeachwa apumue na Kobo. Leo hii unaendelea kumvesha nishani ya umakini? Are you damn serious brother?” Alilalama.

“Nimvishe jina gani ambalo litakuridhisha na kuyanyoosha mazungumzo yetu?” IGP akahoji, Jeremia akatambua kuwa kile ni kijembe.

hakujibu.

“Anyway, nina taarifa njema sana zinaweza kusaidia katika kuboresha hizo tuhuma” IGP akazungumza kisha akaiacha kauli ile hewani ili imuingie vyema bwana Jeremia.

Jeremia akahoji kwa kimuhemuhe.

“Ni taarifa gani mkuu…”

“Nimepigiwa simu na mtu anayedai kuwa yeye ni konstebo Martin Nguzu. Na tayari nimeagiza vijana wangu wafuatilie alipo na kumtia nguvuni, bila shaka atatusaidia sana katika kukamilisha upelelezi… tukimuunganisha na huyo mwanahabari wako, sioni Kobo anachomokea wapi….” Alimalizia huku akiwa anamtazama kwa macho ya kuibia Askari mwenzake.

Moyo wa Jeremia ulipiga kwa nguvu sana, hakuamini kile alichokuwa anakisikia, alijiona kile kikombe anachomwandalia Kobo kikigeukia upande wake ndani yake kikiwa na uji wa mto ambao anapaswa kuunywa bila kupooza.

Mbaya zaidi kile kikombe kilikuwa cha bati.

Akatamani kutoa kauli yoyote lakini kauli yenyewe ikagoma kuunganika.

Koo lilikuwa limekauka.

“Nisaidie maji ya kunywa!” Jeremia akamwomba IGP.

IGP akatabasamu kisha akaitazama meza, Jeremia alikua ana kikombe cha maji mbele yake.

Ajabu alikuwa hakioni!

“Kwani Nguzu yupo hai au?” Akatokwa na swali la kizembe.

“Kitu pekee ninachofahamu ni kwamba nyumba yake iliteketezwa, kuhusu uhai nitakuongopea,Vipi kwani?” IGP akazidi kuzungumza kwa utulivu kabisa na hapohapo akiifurahia hali ya kupagawa ya Jeremia Kazeze.

“Kwani Nguzu yupo hai au?” Akatokwa na swali la kizembe.

“Kitu pekee ninachofahamu ni kwamba nyumba yake iliteketezwa, kuhusu uhai nitakuongopea,Vipi kwani?” IGP akazidi kuzungumza kwa utulivu kabisa na hapohapo akiifurahia hali ya kupagawa ya Jeremia Kazeze.

Na hapo IGP akashuhudia tembe za jasho zikiumuka katika mgongo wa pua ya Jeremia.

Uoga!

Anaogopa nini sasa? Ina maana jamaa ana ‘kamisheni’ katika kutekeleza mauaji ya Nguzu?

Kwanini mtu aliyewahi kuwa na cheo cha juu kama huyu ahusike katika mpango mdogo kama ule.

Haya yalipita katika kichwa cha IGP kwa kasi kubwa.

Kwa upande wa IGP mstaafu Jeremia Kazeze alikuwa anajaribu kuutuliza muhimili wake wa kufikiri, alijiona yu katika kupagawa tayari na alihisi IGP ameanza kumgundua kuwa anapagawa.

Akajivika ukakamavu huku akijizuia asitazamane ana kwa ana na IGP kwani aliogopa kupepesda macho yake.

“Nadhani sasa mimi niende” Jeremia alizungtumza kwa kuridhika.

“Mkuu, kwa hiyo huyu Nguzu tunamfanyaje ikiwa kweli anapatikana angali hai wakati sote tunajua amepoteza maisha?” IGP akamtundika swali lililojaa maswali ndani yake.

“Nani? Nguzu…aah!” Jeremia akatetereka. Kichwani mwake akajiona yu katika kumi na nane za IGP na sasa alikuwa anajaribu kucheza naye atakavyo na ikiwa ataghafirika na kumkwatua basi uamuzi ulikuwa ni ‘penati.

“Akikamatwa inabidi hapo sheria tu ichukue mkondo wake… no way out! Lazima Nguzu aadabishwe. Period!” Jeremia akajikaza kishupavu akajibu kama mtu aliyeshtuliwa toka usingizini akaulizwa moja jumlisha moja akajibu nne kwa sauti ya juu, akiamini yu sahihi

IGP akaponyokwa na tabasamu jepesi kabla hajamdhihirishia Jeremia kuwa mojawapo kati ya watu wanaoitwa mabwege basi yeye kama si kiongozi wao basi ni msaidizi.

“Sheria ya kumshtaki kwa kuchomewa nyumba ama tutamuadabisha katika ‘engo’ ipi afande” IGP akatupa bomu jingine dogo lenye mlipuko mkali.

Jeremia akajiona jinsi anavyodhihirisha kuwa yungali fala katika ubora wake. Na kupitia maswali yale ni namna ya kuitwa fala bila tusi hilo kutajwa.

Ilimuuma!

Hakutaka kuendelea kulithibitisha hilo mbele ya bwana yule ambaye alikuwa mdogo kwake kimri.

“Kwa hiyo unataka akikamatwa aachwe tu bila hata kusaidia upelelezi?” Akauliza kwa ghadhabu.

“Hapana mkuu, yule kukamatwa muhimu tena muhimu sana….” IGP akajibu kichangamfu kisha akamalizia, “Ishu hapa ni tunamshtaki kwa lipi? Kudanganya uma kuwa amekufa kumbe hajafa? kujichomea ndani ya nyumba au tunamshtaki kwa kuwa hai?”

Jeremia akagundua anachezewa ngoma iitwayo shere.

Ngoma wanayochezewa wajinga bila kujua wanadhihakiwa.

Akaaga na kuondoka kwa mara nyingine.


SAFARI ya kulifikia gari lake ilikuwa ndefu sana, Jeremiah alijiona katika akili yake anatembea kama kitoto kinachojifunza kutembea, kikijiona kinao uwezo wa kumkimbia mama yake, angali mama anapunguza mwendo maksudi ili kichukue ushindi kitoto kile.

Miguu yake ilikuwa kama inayopambana kutangulia kupiga hatua, wa kulia unataka utangulie na wa kushoto unahitaji nafasi hiyo.

Ikafikia hatua akili yake ikawqa haiwazi kitu kingine zaidi ya kuwaza namna ya kuiamuru miguu yake ipeane heshima stahiki japo kwa dakika hizo chache tu za kulifikia gari lake.

Miguu ikatii!

Akalifikia gari.

Walinzi wakamkabidhi silaha yake ambayo waliichukua kabla hajaingia ndani kwenda kuonana na IGP, akaziona saluti alizopigiwa zikiwa ni kama ishara inayochukiwa na vijana wengi wafanyiwapo.

Macho yake hayakuona saluti ya heshima bali aliwaona vijana kadhaa wakiwa wanamzomea na kumwonyeshea ishara ya kidole cha katikatika katika mpangilio wa vidole kiganjani.

Hasira zikazidi kumchemka, akapanda garini.

Akatoweka huku akikiri kuwqa katika maisha yake yote, hii ilikuwa mara yake ya kwanza kujikuta amewekwa mtu kati na siweze kujing’atua.

Aliendesha kwa mwendo wa wastani, hakuelekea nyumbani kwake na hakujali kuhusu hilo na hakufikiria walau kumpa taarifa mkewe.

Alizoea kumwendesha kama alivyokuwa na tabia ya kuendesha askari waliokuwa chini yake wakati wa cheo chake.

Kitu kama mwiba mdogo kikaichoma akili yake wakati akiendelea kuendesha gari, akawakumbuka haohao askari wenye vyeo vya chini walivyo na hatari wakipewa amri.

Akajiona jinsi watakavyomfunga pingu huku mara kwa mara wakimfokea badala ya kumwelekeza nini cha kufanya.

Wakati huo akiitwa mtuhumiwa.

Na baadaye akaziona kero za kulishwa chakula kibovu, kuhesabiwa kwa kupigwa bila sababu pamoja na kulala sehemu moja na chawa kunguni na kadhalika pindi atakapokuwa mahabusu rasmi.

Mapigo yake ya moyo yakapiga kwa nguvu zaidi, hakutaka haya yamtokee.

Lakini katika yote haya hakusita kutabasamu na kisha kutoa sauti ya chini.

“Ukoo wa Nguzu ni kiboko!”

Pongezi hizi zikamkera na kujikuta akipiga honi bila sababu zozote za msingi.

Safari yake ikaishia nyumbani kwa Veto!

Kiongozi wa kikundi cha vijana waliokuwa wakimtii, wakati na baada ya utawala wake.

Muunganiko huu ni pamoja na wale waliopewa vyema hovyohovyo bila kuwa na sifa, ama ambao watoto wao waliingizwa jeshini kwa kauli moja tu ya aliyekuwa IGP.

Jeremia Kazeze!

Wangemlipa nini zaidi ya kuwa vibaraka, wenzetu waliwaita ‘puppets’.

Hakumpigia simu Veto hapo kabla, tabia ya ujivuni ilimtawala na kujiona kuwa anaweza kwenda kwa IGP bila kupiga simu, ya nini kumpigia simu Veto ambaye nd’o kwanza anapambana aweze kuupata u’inspekta?

Hakupiga!

Alifika bila kujali kuwa ule ni usiku sana, akagonga hodi mara kadhaa, hatimaye akaufungua mlango mkewe ambaye bila shaka alikuwa amelala sebuleni kwa kupitiwa na usingizi ama akimngoja mwenzi wake.

“Shkamoo shem!” Mwanadada yule alitoa salamu.

“Vipi yupo huyu?” Jeremia akaipuuza ile salamu akahoji yaliyomleta.

“Hajarudi hadi muda huu lakini niliwasiliana naye akanieleza kuwa iwe isiwe atakuja nyumbani shem” alijibu kwa nidhamu, bila shaka alikuwa akijua nguvu ya mtu aliyekuwa mbele yake.

“Alisema atakuja saa ngapi na wakati anakupigia alikuwa ameanza kuja ama?”

“Hakusema lolote shemeji… ila alini…”

“Sawa.. nitampigia simu.” Akamkatisha.

“Labda ujaribu wewe, maana nimejaribu sana hapatikani, hadi nimeanza kupata mawazo. vipi kwani mbona sielewi.”

“Ambacho huelewi ni kipi na ni wewe umeongea naye kwenye simu?” Akang’aka.

Mke wa Veto akawa mpole!

Wakabaki kutazamana kama kuku, kuku mmoja akiwa amechoka mwingine akiwa muoga sana.

Ukimya uliotanda kati yao ukasababisha chochote chenye kutoa sauti kiweze kusikika.

Jeremia akasikia mchakacho ndani ya nyumba.

“Upo na nani ndani?” Alihoji kama anayesuta

“Niko.. mwe.. aah! nipo na binamu yangu..”

“Binamu yako yupi?” Akahoji tena sasa akiwa amemkazia macho makali.

tayari alihisi kudanganywa.

Na hapo ikasikika sauti ya kike yenye kila dalili za kuongea kwa shida ya kukabiliwa na usingizi mkali sana.

“Nani kwani… eeh!”

Kabla sauti ile haijamalizika, Jeremia Kazeze ambaye alikuwa amerithi tabia ya kukurupuka kutoka kwa babu yake alimsukuma mke wa Veto na kuingia naye ndani kwa fujo.

Bila kutarajia akaitoa bastola yake asijue ni kwa nini alikuwa ameamua kufanya vile.

Wazo la kuwa yule mwanamke anamwongopea na Veto alikuwa yu ndani lilimfikisha hapo, akaamini kuwa Veto amenunuliwa tayari na upande mwingine.

Hivyo ilikuwa ni vita tayari.

Vita dhidi ya kijana wake mtiifu.

Giza lilikuwa limekikabili chumba, alivyoingia Jeremia mara ghafla taa ikawashwa, akababaika na kutamani angekuwa na macho memngi aweze kuona kila upande.

Mbele yake alikuwa Veto aliye hoi kabisa, kushoto alikuwa anatazamana na Inspekta Kobo ambaye alikuwa anaonyesha hali ya uchovu sana lakini anayetabasamu.

Wakati anajifikiria ni kipi anapaswa kusema akayaona macho makali ya Veto yakimulika kumaanisha kuna kitu nyuma yake, upesi akageuka na silaha yake.

Na pale akakutana na teke kali lililopiga silaha yake ikatua chini, kisha mpiga teke yule akafanya ujuzi wa ziada akazunguka na mguu uleule kisha akambamiza Jeremia katika kichwa chake.

Jeremia kazeze aliyesahau masuala ya mazoezi na kuruhusu mwili wake kuwa legevu wenye manyama uzembe alikuwa amepatikana. Lakini alijaribu naye kurusha ngumi ya hovyo, ikamkosa aliyekusudia, akayumba na kuliacha tumbo lake lililochomoza kitambi kama walivyo askari wengi wa Tanzania.

Tumbo lile likapokea tiba mbadala ya kuzuia kitambi.

Mateke mawili ya upesiupesi yakadunda katika tumbo lile.

Jeremia akatapika maji aliyokunywa nyumbani kwa IGP.

Kinywa kile kikawa kimefanya kosa la jinai kutema maji katika zulia lililokuwa na thamani ya juu, mpigaji akatokwa na ngumi nyoofu lakini ya kushtukiza ikakibamiza kile kinywa, kikaacha kutema maji kikatapika damu nzito.

Jeremia Kazeze akaanguka chini na kutulia magoti.

“Naitwa Martin, konstebo Martin Nguzu! Sikijui cheo kingine zaidi ya ukonstebo nilionao” Utambulisho ukatoka hatimaye. Huku anayejitambulisha akiwa amekunja ngumi za mikono yote miwili na mwili wake ukitetemeka sana.

Jeremia akaamini hiyo ilikuwa siku yake ya kushuhudia muujiza, anazungumza na maiti.

“Sikurithi cheo chochote kutoka kwa babu yangu nisiyermjua kwa sura wala sauti, nilirithi hiki unachokiona mbele yako mheshimiwa, sikurithi kupigiwa saluti wala kupiga saluti kinyonge.

Sikurithi roho ya kuua bila sababu na sikurithi udhaifu wa kufa kizembe.

Ninaishi katika misingi ya Florian Ngengekuzenza Nguzu, unaishi katika misingi ya Joseph Kazeze.

Babu yangu alishinda, aliniachia huu ushindi na katu hautakuja kupotea kirahisi, mliweza kuuteketeza mwili wangu lakini sio rahisi kuupoteza mzimu wa babu yangu.

Unapambana na mzimu, kama upo tayari unaweza kusimama tena ujaribu kuurushia ngumi mzimu!”

Alifoka kwa ghadhabu zote Martin Nguzu.

Jeremia Kazeze akabeua damu.

Angesema nini zaidi ya kuendelea kutema tu damu.

Baada ya Nguzu kumaliza aliyotaka kusema, akasimama Inspekta Kobo.

Pamoja na udhaifu wake uleule, hakuna aliyetarajia kuwa angeweza kuwa imara tena mpaka ambapo angepata tiba ya kutosha.

Naye akambana Jeremia Kazeze kadri alivyoweza, na hapo akataja alipo muandishi Juma Kihwele na familia yake, akalazimishwa kupiga simu na watu wale waachiwe huru mara moja.

Jeremia hakuamini hata kidogo kuwa alikuwa anachezeshwa ngoma ya namna ile na vijana wale.

Hakuwa na la kufanya akatii.

Maelezo ya ziada yakatolewa, simu ikapigwa kwa IGP kuhusu ujio wa Juma Kihwele katika himaya yake.

IGP wakati anapigiwa simu ile alikuwa tayari katika sare zake na alijisikia faraja kwenda kuimaliza vita ile angali ana nyota tele katika bega lake.

Vita ilikuwa inaelekea ukingoni kabisa, Konstebo Martin Nguzu akaingia katika chumba kimojawapo na kumkuta Koplo Zubeda akiwa katika usingizi mzito.

Akamwinamia na kuzungumza naye maneno kadhaa ambayo aliamini fika kuwa hataweza kuyasikia.

Kisha akambusu katika paji lake la uso.

Akaliendea dirisha kubwa la kioo, akaruka na kutoweka akipishana na gari kadhaa za polisi zikiwa zinalikaribia eneo lile.

Wazo la kwanza lililomuondoa ni Zubeda. Asingeweza kuendelkea kuwa naye katika mahusiano mwanamke ambaye ni usingizi wa inspekta Kobo, pia asingekuwa na amani kumwona binti yule katika mahusiano mengine hata kama ataachana na Inspektra.

Pili ni upindishaji wa sheria katika ardhi aliyokuwa ameikanyaga, masuala ya kubebana kwa sababu ya kujulikana aliyafahamu wazi kabisa.

Akakihesabu cheo nchake cha ukonstebo, cheo cha Zubeda ukoplo na Inspekta Kobo. Akajaribu kufananisha na kile cha Jeremiah aliyewahi kuwa mkuu wa majershi ya polisi IGP.

Akaamini fika kuwa lolote linaweza kutokea, aidha kuzimishwa hapohapo na kisha taarifa kubadilishwa kuwa waliuwawa wakikabiliana na polisi, ama la kubadilishiwa kesi kabisa na kuonekana walimteka Jeremia na kumtesa kesi ambayo katu isingeweza kuwaacha bila hatia.

Miaka thelathini ingewahusu pamoja na mateso makali.

Konstebo Martin Nguzu, akayaweka mapenzi kando, akautazama usalama wake.

Kubwa zaidi alikiri kuwa hakuwa yeye yule konstebo mnyonge, huyu alikuwa imara na alikuwa na kazi kubwa zaidi za kufanya kuliko kuendelea kuwapigia saluti watu kama Jeremia Kazeze.

Konstebo Martin Nguzu akazidi kukata mitaa jijini Dar es salaam, hatimaye akaipata nyumba ya kulala wageni.

Akamtazama muhudumu aliyekuwa ana mawenge ya usingizi.

Akaulizia bei ya chumba akatajiwa, akalipia na kushangaa anapewa funguo bila kusajili jina lake.

“Hee! unaniruhusu tu naingia kama unanijua vile.”

“Ah! bro we kalale bwana…”

“Hapana lazima niandikishe la si hivyo nilale bure.” akatilia mkazo.

Huku akiwa amekereka yule binti wa mapokezi akampatia daftari huku akihangaika kuipata kalamu.

Hatimaye Nguzu akaishika vyema kalamu, akautazama mstari wa kuandika jina, akatokwa na tabasamu la ushindi kisha akaandika kwa herufi kubwa kiasi cha kuingilia hadi mstari wa chini.

“KONSTEBO MARTIN NGUZU”

Hakujaza sehemu nyingine zilizosalia.

Akamkabidhi daftari akiwa amelifunika na kuamini fika kuwa kwa jinsi alivyoelemewa na usingizi hataweza kusoma, na hata akisoma ataambulia patupu.

Alivyokifikia chumba, akaitoa bunduki yake. Akatoa risasi na kisha akauvamia ukuta na kuandika kwa kukwangua rangi. Huku akiifurahia hali hii, alijiona hana namna nyingine ya kufanya sherehe zaidi ya hii.

Akauchubua vyema hadi ukasomea alivyotaka.

“NAITWA MARTIN, KONSTEBO MARTIN NGUZU”

Akapiga saluti na kisha akalala vyema.

Alfajiri akatoweka.

Akaelekea popote watu wanapoelekea lakini mwisho wake akiutambua yeye mwenyewe.

MWISHO

Leave a Comment