KIJASUSI

Ep 01: Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili

SIMULIZI Mifereji ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki wala Ukatili
Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi : Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili 

Sehemu ya Kwanza (1)

Wako watu ambao uwepo wao katika ulimwengu wamechangia kwa namna moja au nyingine kuufanya huu ulimwengu uwe jinsi ulivyo. Wako wengine ambao wamechangia kwa kiwango kikubwa kuifanya ‘mifumo’ ya dunia iwe jinsi ilivyo. Mara nyingi watu hawa tunawasoma kwenye vitabu endapo kama waliishi miaka mingi iliyopita na endapo kama bado wako hai huwa ni watu tunao wahusudu na kuwachukulia kama mifano ya kuigwa.

Lakini wako watu ambao ni vigumu kuwahusudu au kuwaandika katika vitabu vya historia kutokana na jinsi ambavyo walichangia kubadilisha mifumo ya kimaisha dunia. Moja wapo ya watu hawa ni Wezi ambao mimi binafsi napenda kuwaita ‘Wezi wa Daraja la kwanza’ (First Class Thieves). Hawa wamekuwa toka enzi za kale na wamekuwa wanaushangaza ulimwengu kwa kiwango cha akili walichotumia na uthubutu walionao katika kutekeleza matukio.

Moja wapo kati ya wezi hawa ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mifumo ya kiusalama ni mtu ambaye ameandika historia katika ulimwengu na hususani taifa la ufaransa kwa kutekeleza tukio kubwa zaidi la ujambazi na lenye thamani kubwa zaidi ambayo mpaka leo hii bado hajatokea mtu mwingine katika nchi ya ufaransa aliyefanikiwa kutekeleza tukio kubwa kama hilo na kwa mafanikio. Yeye binafsi hakuiba ili tu apate kutajirika pekee na kuishi maisha ya anasa bali pia aliiba kwa kuwa aliamini huo ndio wito wake (destiny) na aliiba ili kuudhihirishia ulimwengu kuwa anaweza. Jina lake aliitwa Albert Spaggiarri.

May 1976: Nice, Ufaransa

Alfred Spaggiari moja ya watu mashuhuri kwenye jiji la Nice nchini ufaransa na swahiba mkubwa wa Meya wa jiji la Nice Bw. Jacques Medécin, Spaggiari ambaye shughuli zake alikuwa amebobea kwenye upigaji picha za mitindo na matukio muhimu zaidi ya kiserika na binafsi alikuwa ameitisha kikao kilichohudhuriwa na watu wapatao ishirini katika nyumba yake ya mapumziko ya mwisho wa wiki iliyopo nje kidogo ya jiji la Nice. Kikao hicho hakikuhusu upigaji picha au siasa bali aliitisha kikao hicho cha siri na aliwaalika wahalifu kadhaa ili awashirikishe mpango wa siri aliokuwa nao. Kati ya watu hao 20 watu watano walikuwa ni wawakilishi wa ukoo wa Mafia wa usisili ( Sicilian Mafia) aliowaakika kutoka Italia.

Akiwa anafungua kikao hicho Spaggiari aliwaeleza kuwa amewaita hapo ili awashirikishe kwenye tukio la wizi la kihistoria na ambalo anaamini litakuwa na thamani kubwa sana kiasi kwamba hawataitaji kuiba tena maishani mwao ili kuishi maisha ya hali ya juu waliyoyapenda.

Spaggiari akawaeleza kuwa amedhamiria kuiba katika Kuba (vault) ya benki ya Société Générale. Ambayo ndiyo ilikuwa benki kubwa zaidi katika nchi ya ufaransa kwa kipindi hicho na moja ya benki kubwa zaidi duniani.

Lakini kabla hajaendelea zaidi na ‘hotuba’ yake watu kadhaa waliokuwepo kwenye kikao hicho waliangua kicheko cha dharau na kusema kwamba walidhani kuwa wameitwa kwenye kikao hicho labda ‘celebrity’ Spaggiari alikuwa ana ugomvi na ‘celebrity’ mwenzake kwahiyo alitaka awalipe wakamfanyie ‘umafia’ lakini kamwe hawakutegemea mtu ‘mboga saba’ kama Spaggiari ati atake kuwashirikisha wao kuhusu tukio la ujambazi kwani wanaamini kuwa Spagiari hajui chochote kuhusu uhalifu wala hajui hata “a e i o u” za matukio ya ujambazi.

Spaggiari aka kaa kimya kwa sekunde kadhaa huku macho yake yakiangaza kwa wahudhuriaji wote wa kikao hicho na macho yake yakakutana na mzee mmoja wa makamo aliyekuwepo pia kwenye kikao hicho ambaye walifahamiana vyema na Spaggiari. Spaggiari akampa ishara kuwa awaeleze watu hao waliohudhuria kikao hicho kuwa yeye ni nani, yeye Spaggiari halisi ni nani, awaeleze kiundani wamfahamu Spaggiari zaidi ya yule wanayemsoma kwenye magazeti, zaidi ya Spaggiari ‘mboga saba’ wanaye mjua.

UTAMBULISHO MFUPI WA “MPIGA PICHA” ALBERT SPAGGIARI

Albert Spaggiari alizaliwa Desemba 14, 1932 katika mji mdogo wa Hyerés ambapo mama yake alimiliki duka kubwa la mavazi ya ndani ya wanawake (lingerie).

Akiwa bado yuko katika shule ya upili, katika shule yao Spaggiari alitokea kumpenda msichana ambaye alikuwa ni mtoto wa Mkuu wa shule. Mara nyingi Spaggiari alijikuta anaingia kwenye matatizo na walimu kutokana na kumshushia kipigo kijana mmoja wa kisenegali ambaye alipata ufadhili wa kusoma shuleni hapo lakini naye alionyesha hisia za kumpenda binti huyo. Kutokana na Spaggiari kuingia kwenye matatizo mara kwa mara na walimu hakufanikiwa kumaliza shule kwani alifukuzwa baada ya walimu kuchoshwa na tabia zake.

Licha ya kutokuwepo shuleni Spaggiari aliendeleza uhusiano wake na yule mtoto wa Mkuu wa shule

Katika juhudi za Kutaka kumuonyesha huyo binti kwamba yeye sio hoe hae Spaggiari akamuahidi huyo binti kumnunulia pete ya almasi yenye thamani kubwa sana. Uhalisia ni kwamba Spaggiari hakuwa na hela lakini kutoka moyoni alipania kuitekeleza ahadi huyo ili azidi kumfanya mpenzi wake ampende zaidi.

Hivyo basi Spaggiari akamshawishi rafiki yake mmoja kuwa usiku wa siku moja ana mpango wa kuiba pete ya almasi katika duka mojawapo hapo mjini kwao.. Rafiki yake akakubali na wakapanga siku wakatekeleza tukio lakini kwa masikitiko makubwa wakakamatwa.

Baada ya kukamatwa na kushtakiwa mahakamani, Spagiarri alihukumiwa kwenda jela.

Lakini kutokana na umri wake mdogo wa miaka 17, serikaki na Spagiarri wakakubaliana kuwa akajiunge na jeshi badala ya kukaa jela.

Hivyo basi Spaggiarri akajiunga na jeshi kitengo cha wanajeshi wa kutumia parashuti.

Mwaka 1953 Spaggiari alishiriki katika vita ambayo majeshi ya Ufaransa yaliivamia koloni lao la Indochina (Vietnam ya sasa na maeneo yanayoizunguka). Spaggiari alikuwa ni mwanajeshi hodari na aliwahi kujeruhiwa mara mbili katika mapambano na kutokana na uhodari wake alitunukiwa nishani ya heshima.

Lakini ni kana kwamba wizi ulikuwa ndani ya vinasaba vya Spaggiari kwani akiwa huko huko Vietnam na kabla vita haijaisha yeye pamoja na rafiki yake walivamia duka moja mjini Hanoi na baada ya upelelezi walibainika.

Hii ilipelekea Spaggiari kufukuzwa jeshini na kurudishwa ufaransa na kufunguliwa mashtaka na akahukumiwa miaka mitano.

Spaggiarri akatumikia kifungo na mnamo mwaka 1957 akarudi uraiani.

Baada ya kurudi uraiani Spaggiari akajihusisha na kufanya kazi katika viwanda vya kutengeneza makabati ya kuhifadhi vitu vya siri (Safes) na pia akafanikiwa kupata msichana mrembo aliyeitwa Marcelle Audi ambaye kwa kipindi hicho alikuwa anafanya kazi kama Nesi na akafanikiwa kumuoa.

Baada ya kumuoa waliondoka ufaransa na kuelekea nchini Senegal ambapo kwa kipindi hicho bado lilikuwa ni koloni la Ufaransa na wakaishi mjini Dakar. Kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kukaa sana Senegal kwani mwaka 1960 Senegal ilipata Uhuru na ikawalazimu warejee tena Ufaransa.

Baada ya kurejea Ufaransa Spaggiarri akaanza kujihusisha na vikundi vya uzalendo vya nchi za ulaya ambavyo vilikuwa vinapinga wazungu kuachia makoloni ya Africa.

Kikundi ambacho kilimvutia sana Spaggiarri kiliitwa OAS (Organisation de al’rmée Secrète). Kikundi hiki kilijihusisha na shughuli za kishushushu kusaidia kushawishi serikali ya ufaransa isiachie koloni la Algeria na pia kilifanya shughuli zake kudhoofisha harakati za watu wa Algeria kudai Uhuru. Spaggiari akajiunga na kikundi hiki mwaka 1961.

Rais wa ufarasa wa kipindi hicho (Rais De Gaulle) mwanzoni alikiunga mkono kikundi hiki lakini kadiri muda ulivyoenda na kuonekana wazi kuwa suala la kuipatia Uhuru Algeria haliepukiki, Rais De Gaulle akakipiga marufuku kikundi cha OAS na vikundi vingine vyote vyenye mlengo huo.

Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment