KIJASUSI

Ep 02: Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili

SIMULIZI Mifereji ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki wala Ukatili
Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi : Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili 

Sehemu ya Pili (2)

Baada ya harakati zao za OAS kupigwa marufuku Spaggiari akabakia na kinyongo kikubwa sana dhidi ya Rais De Gaulle. Hivyo basi mwaka huo huo wa 1961 akasafiri mpaka nchini Hispania kwenda kuonana na mmoja wa waanzilishi wa kikundi cha OAS mzee aliyeitwa Jenerali Pierre Lagaillarde. Sababu kubwa ya kumfuata ni kwamba Spaggiari alikuwa anahitaji apewe ruhusu ya kumdungua kwa risasi Rais De Gaulle ili kulipiza kisasi kwa “kuwasaliti” OAS na ‘raia’ wa Ufaransa kwa kuunga mkono Algeria kupewa Uhuru.

Jenerali Pierre akamwambia kuwa ampe ‘ramani’ yake jinsi alivyopanga ni namna gani atampiga risasi Rais De Gaulle.

Bila kusita Spaggiari akamueleza mpango wake, kuwa msafara wa Rais De Gaulle huwa unapita katika mji mdogo wa Hyerès na huwa wanapita mbele ya duka la mama yake Spaggiari (mama yake Spaggiari alikuwa ni mfanyabiashara wa mavazi ya ndani ya akina mama (langarie)). Hivyo Spaggiari akamueleza Jenerali Pierre kuwa atakaa juu ya paa la duka la mama yake na atakaa na bunduki ya wadunguaji na Msafara wa Rais ukupita atampiga risasi Rais De Guelle.

Jenerali Pierre akakubaliana naye kuwa arudi ufaransa na akatekeleze mpango huo lakini akampa onyo kuwa siku hiyo atayotakaa juu ya paa la duka la mama yake, asifyatue risasi kabla hajapata amri ya moja kwa moja kutoka kwake (direct command). Spaggiari akakubali na kurejea ufaransa.

Siku ya siku ikafika, Spaggiari akakaa juu ya paa la duka la mama yake, msafara wa Rais ukapita mbele ya duka, Spaggiari akasubiri ‘direct command’ kutoka kwa Jenereli Pierre ili amfyatulie risasi Rais De Guelle, akasubiri na kusubiri, amri haikuja na msafara wa Rais ulitokomea mbali na macho yake.

Wiki chache baadae Spaggiarri akakamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na vikundi vya ‘kigaidi’. Spaggiarri akagundua kuwa Jenerali Pierre ‘alimuuza’.

Mahakama ikamuhukumu kifungo cha miaka minne jela. Spaggiari akatumikia miaka yote.

Siku ya kutoka jela ni mke wake Audi pekee aliyemkuta nje ya geti la jela akimsubiri waende nyumbani. Spaggiari akamuapia mkewe kuwa hataki tena kujihusisha na harakati zozote wala siasa. Kuanzia sasa kitu pekee anachokitaka ni kuwa mume bora kwake.

Spaggiarri hakuwa anatania, akafungua ofisi yake ya upigaji picha katika jiji la Nice. Akafanya kazi kwa bidii usiku na mchana na ndani ya miaka michache akaibukia kuwa ndiye mpiga picha bora zaidi katika jiji la Nice, na harusi zote za hadhi ya juu ni Spaggiari ndiye alipiga picha, matukio yote muhimu ya kiserikali na binafsi, tenda ya kupiga picha alipewa Spaggiari. Punde si punde Spaggiari akawa moja ya watu mashuhuri zaidi katika jiji la Nice, na akafahamiana na kila mtu muhimu kwenye jiji la Nice. Mpiga picha Spaggiari akawa moja ya raia wanaoheshimika zaidi jijini Nice.

Lakini licha ya mafanikio na heshima yote, kana kwamba uhalifu umeandikwa kwenye vinasaba vyake, roho ya Spaggiari ilitaka zaidi! Sio pesa zaidi, sio umaarufu zaidi, hapana roho ya Spaggiari ilitamani kuiba! Kufanya tukio moja kubwa kuudhihirishia ulimwengu umahiri wake katika wizi.

Roho ya Spaggiari iliwasha kwa kiu ya kutaka kuiba, na alijua bayana roho yake haitotulia mpaka pale atakapo tekeleza walau tukio moja maridadi la wizi. Na ili kujiridhisha Spaggiari akaamua kuwa atafanya tukio la wizi ambalo litasimuliwa vizazi na vizazi.

Turejee kwenye Kikao cha “Mpiga Picha” Spaggiari na wenzake

Baada ya wote waliokuwepo kwenye kikao hicho kusikia historia hiyo ya Spaggiari walishikwa na bumbuwazi. Wote waliduwaa kwani baadhi yao waliwahi kusikia minong’oni mtaani kuwa mpiga picha Spaggiari ni ‘mtundu mtundu’ lakini hawakutegemea kama huo ‘utundu’ wake aliwahi kuhusika kwenye maisha ya hatari kama jinsi ambavyo wamesimuliwa kwenye kikao hicho.

Kwa ufupi kwa historia hiyo fupi, Spaggiari alivuna heshima kutoka kwa watu wote ambao walikuwa wamehudhuria kikao hicho lakini swali moja likabaki hewani, je mpango wake ni upi juu ya utekelezaji wa kuiba benki hiyo ya Société Générale, naye Spaggiari akawajibu kuwa hicho ndicho alichowaitia hapo kuwa wakae chini wote watoke na mpango kabambe wa kuiba katika benki hiyo na yeye yuko tayari kusikia mawazo yao kwanza.

Baadhi ya waliokuwepo kwenye kikao kile hasa wale wanachama watano kutoka ukoo wa Mafia wa usisili, wakatoa maoni yao. Wakasema kuwa kama anaweza kuwapa uhakika kuwa katika tarehe fulani mahususi benki hiyo itakuwa na kiwango kikubwa cha fedha basi wao wanaweza wakasaidia wapate silaha na kuweka mpango madhubuti wa kuivamia hiyo bank na kupora hela. Baada ya wanachama hao wa Mafia kutoa maoni hayo Spaggiari akawapa jibu la kuwashangaza sana, kuwa hakubaliani na mkakati huo kwasababu anataka kwamba tukio hilo watakalotekeleza anataka waweke mpango wa kutumia akili zaidi badala ya kutumia mabavu na silaha.

Baada ya maoni hayo kukataliwa wengine nao wakatoa maoni kwamba labda wamteke mtoto au mke wa meneja wa benki kisha watumie kigezo hicho kumshawishi meneja awasaidie kuiba katika benki yake. Wazo hili nalo lilipingwa na Spaggiari na akawaeleza kuwa hataki ukatili wowote utumike katika kutekeleza tukio hili. Mzee mmoja veterani wa kikundi cha OAS ambaye alikuwepo yeye akasema kuwa anatamani afahamu siku ambayo benki yoyote kubwa inakuwa na kiwango kikubwa cha fedha kisha wailipue ili kuikomesha serikali kwa ‘kusaliti’ kikundi chao cha OAS. Spaggiari akamjibu kwa kifupi tu kuwa kama akitaka afanye tukio lolote kwa ufanisi anatakiwa aweke hisia za chuki pembeni. Hivyo wazo lake hilo la kulipua benki kwa kisasi alikuwa analipinga.

Wale jamaa watano wanachama wa ukoo wa kihalifu wa Mafia, ambao walisafiri kutoka Itali kuja kuhudhuria kikao hicho wakainuka wote kwa pamoja na kumwambia Spaggiari kuwa wanaondoka. Wanahisi kuwa licha ya kuwa ni kweli kama walivyosikia kwenye kikao hicho kuwa amewahi kushiriki katika mipango ya hatari katika maisha yake lakini wanahisi kuwa kwasasa Spaggiari ana ndoto za mchana na hayuko kwenye uhalisia kwasababu kama anakataa maoni yote yaliyotolewa hawaoni uwezekano wowote wa kikao hicho kuzaa mkakati wenye uhalisia wa kutekeleza tukio la ujambazi.

Spaggiari akawasisitiza kuwa wakae chini wasikilize maoni mengine yakiwemo maoni yake lakini wanachama hao wa Mafia wakamwambaia kuwa hawako tayari kuendelea na kikao hicho kwani wanadhani mkakati wowote utakaowekwa hapo utakuwa ni kana kwamba wanaenda kujitoa sadaka kwani haiingii akilini watu muwe na dhamira ya kuiba benki alafu msitumie silaha. Mafia hao wakainuka, wakaaga na kuondoka.

Kwahiyo Spaggiari akabakia na watu 15 pekee kwenye kikao hicho wengi wao wakiwa ni wanachama wa zamani wa kikundi cha OAS. Na alivyowaangalia nyuso zao aligundua dhahiri kuwa ndani ya dakika chache kama hatowapa mpango wowote wa kuwashawishi kuhusu hilo tukio nao wangeweza kuinuka na kuondoka.

Spaggiari akaenda mpaka kwenye kabati la pembeni lililopo kwenye sebule hiyo na kutoka na boksi dogo la saizi ya kati na kulibeba kwa mikono miwili mpaka kwenye meza iliyokuwepo katikati ya sebule na kisha akawaomba wote wainuke na kusogea karibu na meza.

Baada ya wote kusogea karibu na meza Spaggiari akatoa makaratasi kadhaa kutoka kwenye lile box na kayatandaza juu ya meza.

Mifereji Ya Dhahabu:  Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment