Wizi Uliofanywa na Genge la Vikongwe
IMEANDIKWA NA THE BOLD
************************************************************************
Simulizi: Wizi Uliofanywa na Genge la Vikongwe
Flying Squad, kitengo maalumu cha polisi nchini Uingereza ambacho kwa jina lingine kinajulikana kama SCD7 (Serious Crime Directorate 7) kitengo kinachohusika na uchunguzi wa matukio makubwa uhalifu na yaliyotumia weledi wa hali ya juu, kitengo hiki mpaka leo hii ikiwa inakaribia miaka miwili kiko katika msako mkali wa kumtafuta muhalifu wasiyemjua jina na wamembatiza jina la ‘Basil’.
Basil anatafutwa kwa kupanga na kutekeleza tukio la ujambazi lililotumia weledi wa hali ya juu na moja ya matukio ya ujambazi yaliyo wezesha kuibiwa vitu vyenye thamani ya hali ya juu kabisa katika historia ya nchi ya Uingereza.
Tukio hili alilitekeleza na wenzake wapatao saba ambao wote wametambuliwa na kujulikana isipokuwa Basil pekee amabaye ndiye alikuwa kiongozi wa mpango huu (mastermind) hajajulikana ni nani (Identity) na wala hajajulikana anaishi wapi.
Kitu pekee kinachojulikana kuhusu Basil ni kwamba alikuwa na ufahamu wa hali ya juu na ‘access’ ya sehemu ambapo tukio hili lilikuwa linaenda kutekelezwa. Sehemu yenyewe ni Hatton Garden.
Katikakati ya jiji la London, upo mtaa unaitwa Hatton Garden. Hii ni moja kati ya sehemu yenye utajiri mkubwa duniani kutokana na kuwa na moja kati ya mitaa duniani inayoongoza kwa biashara ya madini na Vito vya thamani.
Huu ndio mtaa unaoongoza nchini Uingereza kwa kuwa na wauzaji na wanunuzi wengi wa almasi (diamond dealers) na madini mengine yenye thamani kubwa kama dhahabu na platinum.
Katika mtaa huu ipo kampuni maarufu inayomiliki kuba kadhaa (vaults) kwa ajili ya wafanya biashara kuhifadhi vitu vyao vya thamani hasa madini ya almasi na dhahabu. Kampuni hii inajulikana kama Hatton Garden Safe Deposits Ltd.
Moja ya vault za kampuni hii yenye kutumiwa sana na wafanyabiashara iko jengo namba 89-90, ambalo ni jengo lenye ghorofa saba na vault yenyewe iko chini kabisa ya jengo (basement).
Vault hii inapendewa kutumiwa na wafanyabiashara wengi katika mtaa wa Hatton Garden kutokana na usalama wake wa hali ya juu.
Kama nilivyoeleza, Jengo hili lina ghorofa saba. Katika Jengo hili kuna wapangaji wengine wapatao 60 ambao wengi wao ni wafanya biashatmra za madini. Vault yenyewe iko chini ya jengo.
Mbele ya jengo kuna mlango wa kuingilia. Mlango huu unatumia funguo kufungua na kufunga. Kila mpangaji kwenye jengo hili ana ufunguo mmoja wa kumuwezesha kufungua mlango huu.
Pia ukishafungua mlango huu unakutana na mlango mwingine wa kioo ambao unafunguliwa kwa kutumia neno la siri (PIN code) ambayo wapangaji wote ndani ya jengo wanayo.
Baada ya hapo unakutana na lifti kwaajili ya kumpeleka mtu floor ambayo makazi yake yapo. Lakini lifti hii imetengenezwa katika namna kwamba haishuki mpaka chini kwenye ‘basement’ ya jengo.
Yani kwamba, mtu anaweza kutumia lifti kupanda nayo juu kwenda kwenye floor yeyote na pia anaweza kushuka nayo kutoka juu mpaka ghorofa ya chini (ground floor) lakini lifti haiwezi kushuka kwenda chini ya jengo, yaani kwenye basement. (Kumbuka vault ipo huko chini kwenye basement).
Pembeni ya lifti kuna mlango ambao ukiufungua unakutana na ngazi zinazoshuka chini kwenda kwenye basement. Mlango huu unafunguliwa kwa funguo maalumu ambayo moja anakuwa nayo mtu kutoka kampuni ya ulinzi ya H.G.S.D na funguo moja anayo mtu wa usafi pekee.
Ukishachuka chini kwenye ngazi na kufika chini kwenye basement mkono wa kushoto unakutana na mlango mwingine ambao unatumia funguo maalumu ambayo anakuwa nayo mlinzi wa H.G.S.D pekee. Ukishafungua mlango huu unakuwa na sekunde 60 kuingiza tarakimu za siri katika keypad iliyoko ukutani ili kuzima (deactivation) alamu ya tahadhari (intruder alert). Alarm hii inakaa kimya kwa sekunde 60 pekee na kama tarakimu hizo za siri hazitoingizwa kwenye keypad iliyoko ukutani, basi itapiga kelele na pia kutuma ujumbe maalumu wa simu kwa jeshi la polisi la London.
Baada ya kufungua mlango huu kuna geti dogo la chuma ambalo linafunguliwa kwa kutumia namba za siri (PIN code) alafu unakutana na kichumba kidogo cha mlizi ambapo pembeni yake kuna mlango mwingine wa chuma ambao huu unafunguliwa kwa kuusukuma tu kisha unakuwa uko mbele ya mlango wa Vault yenyewe.
Vault yenyewe inafunguliwa kwa kuingiza namba kwa mpangilio maalumu (combination) na kisha kuzungusha ringi lake.
Hapa unakuwa uko ndani ya vault yenye viboksi takribani 966 zenye madini, fedha taslimu, Vito vya thamani vyote hivi vikiwa na thamani ya mamia ya mabilioni.
Hii ndio vault ambayo Basil alikuwa amepanga kuiba. Licha ya kiwango hiki kikubwa cha ulinzi na teknolojia hii kubwa ya ulinzi, lakini thamani kubwa ya ‘mzigo’ uliopo ndani ya vault ukamfanya Basil aweke mkakati wa kuiba vault hii.
The Team
Ili kufanikisha lengo hili aling’amua wazi kuwa hawezi kufanya tukio hili peke yake. Alihitaji wabobezi wengine wa kushirikiana nao ili kufanikisha kutengeneza mkakati wa kuiba katika hii vault.
Ndipo hapa akawasiliana na mzee wa miaka 76 aliyeitwa Brian Reader. Huyu alikuwa ni mwizi nguli mstaafu aliyekuwa na weledi wa hali ya juu kuhusu upangaji wa mikakati ya ujambazi.
Huyu alikuwa moja ya washiriki katika tukio la ujambazi la kihistoria la wizi wa Bank ya Lloyd tawi la London mwaka 1971. Tukio ambalo majambazi walichimba shimo chini kwa chini mpaka ndani ya bank na kuiba fedha na vitu vyenye thamani ya mabilioni.
Pia mzee brian aliwahi kushiriki tukio lingine kubwa mwaka 1983 la kuiba mzigo wa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa uwanja wa ndege akishirikia a na jambazi maarufu jijini London aliyeitwa Kenny Noya.
Tukio hili lilimsababishia kufungwa miaka tisa jela na alipotoka ndipo akaamua “kustaafu” ujambazi.
Lakini Basil ambaye inakadiriwa anaweza kuwa na miaka 50, alimfuta mzee huyu na kumsisitiza juu ya mpango huo. Hasa hasa alikuwa akimgusia kuwa, anajua kama amestaafu lakini anaomba ashirikiane naye kufanya “Tukio Moja La Mwisho”, litakalowaweka kwenye vitabu vya historia na pia kujipatia mabilioni ya kuwawezesha kuishi uzee mwema.
Baada ya takribani miezi miwili ya kunshawishi hatimaye mwezi February, 2015 Mzee Brian ambaye wenzake walipenda kumuita “The Old man” akakubali kushiriki kuandaa mkakati wa kufanikisha tukio hilo.
Na akamuweka wazi kuwa ili kufanikisha tukio hilo wanahitaji timu ya watu. Watu wenye weledi wa hali ya juu na uzoefu katika kufanya matukio makubwa ya ujambazi. Na akamueleza kuwa anataka awashawishi marafiki na wezi wenzake wa siku nyingi ili kufanikisha tukio hilo.
Ndipo hapa ambapo mzee Brian akawasiliana na wezi wenzake na ambao pia ni marafiki zake wa siku nyingi.
Timu hii ambayo Mzew Brian aliitengeneza ilikuwa na watu wafuatao.
Terry Perkins, miaka 67. Huyu alikuwa ni moja ya wezi weledi kabisa katika jiji la london. Perkins anakumbukwa sana kwa ushiriki wake katika tukio la wizi kwenye gari la kusafirisha fedha la kampuni ya Security Express mwaka 1983 ambapo waliondoka na dola milioni 9.
Perkins alishiriki matukio mengine mengi ya ujambazi lakini tukio lililompeleka jela lilikuwa ni kitendo chake cha kumtishia kumteka na kumuua meneja wa benki aliyekuwa anamtakatishia fedha zake baada ya kuanza kumzunguka na kutaka kumtapeli.
Kitendo hiki kilimfanya Perkins kuhukumiwa miaka 22 gerezani, lakini akafanikiwa kutoroka gerezani na kwenda kuishi Hispania na kurejea Uingereza miaka 17 baadae akiwa amebadili jina.
Wa pili aliitwa Jones, miaka 60. Huyu alikuwa mwizi mzoefu na alichukulia wizi kama ni wito wake wa maisha (destiny).
Jones alikuwa akitumia muda wake wote kujisomea kuhusu mbinu za wizi kwenye mitandao, namna ya kutoboa kuta za vault, namna ya kutoacha alama kwenye eneo la tukio (forensic evidence).
Pia huyu ndiye alikuwa mtu mwenye nguvu zaidi za mwili na aliye fiti zaidi ya wenzake wote.
Watatu aliitwa Carl Wood, miaka 58. Huyu alikuwa ni mwizi nguli na alikuwa na weledi mkubwa wa kudili na ‘system’. Carl mwenye umbo jembamba na mrefu hakuwa kama wezi wengine. Alijiweka kama mfanyabiashara muhimu. Alipendelea kuvaa suti kwa unadhifu mkubwa. Pia alikuwa na viongozi kadhaa wa jeshi la polisi amewaweka mfukoni.
Wanne aliitwa John Collins, miaka 75. Wenyewe walipenda kumuita “Kenny”.
Huyu alikuwa ni “mwizi mjanja mjanja” (“mtoto wa mjini”). Alikuwa anaufahamu mkubwa ya mji wa London na watu wake. Mojawapo ya shughuli zake za ‘kuzugia’ ilikuwa ni kununua kwa watu saa za gharama na kisha anaenda kuziboresha kidogo na baada ya wiki kadhaa anawauzia wale wale waliomuuzia mwanzo pasipo wenyewe kujua.
Pamoja na hawa,MzeBriane Brian alifanikiwa kuwashawishi watu wawili wakiokuwa wafanyakazi kwenye jengo lenye Vault, akawashawishi wajiunge nao kwenye mpango huo.
Watu hawa walikuwa ni Hugh Doyle mwenye miaka 48 na William Lincoln mwenye miaka 60. Hawa walikuwa ni mafundi bomba katika jengo husika.
Sababu ya Mzee Brian Reader kuwashirikisha watu hawa kwenye mpango huu ilikuwa ni kuzingatia kwamba kwa kuwa wao ni wazew basi watu hawa wawili wahusike zaidi kubeba vifaa vya kwenda kufanyia kazi na kubeba “mzigo” pindi wakimaliza kazi.
Mpaka hapo timu ilikuwa imekamilika. Kwahiyo jumka timu hii ya wazee hawa ilikuwa na watu 8. Mzee Brian Reader (“The old man”), Mzee Perkins (aliyetorokaga jela kifungo cha miaka 22), Mzee Jones (yule mwenye kuamini wizi ni ‘destiny’ yake, Mzee Carl (yule nadhifu na mwenye connection kwenye ‘system’), Mzee Collins “Kenny” (mjanja mjanja), pamoja na mafundi bomba wale wawili (Doyle na Lincoln), na mwenyewe Basil (the mastermind).
Mwezi mmoja baadae yaani March, 2015 wakaanza kusuka mikakati juu ya namna ya kuingia ndani ya vault pasipo kugunduliwa. Vikafanyika vikao usiku na mchana, zikatafutwa ramani za jengo husika. Zikatafutwa ratiba za shifti za walinzi wa jengo pamoja na taarifa teknolojia zote zinazotumika kulinda jengo hilo.
Baada ya mwezi mmoja mkakati ukawa umekamilika. Wakawa na mpango kamilo wa namna gani watakavyo ingia katika vault. Kilichokuwa kimebakia ni kuteua siku ambayo wataweza kutekeleza tukio hilo. Na kwa haraka tu walogundua kwamba kampuni ya H.G.S.D huwapa mapumziko wafanyakazi wake wote mpaka walinzi katika kipindi cha sikukuu yeyote ile.
Hii ilidhihirisha ni namna gani walikuwa wanajiamini kupitiliza juu ya teknolojia yao ya ulinzi katika vault zao.
Habari njema zaidi kwa Wazee hawa ilikuwa ni pale walipogundua kwamba kwa mwaka huo 2015 sikukuu inayojulikana kama ‘Bank Holiday’ nchini Uingereza kwa mwaka huo 2015 inaungana na sikukuu ya Pasaka.
Sikukuu hii ya ‘bank holiday’ huadhimishwa mara moja kila mwaka katika nchi nyingi za jumuiya ya madola ambapo wafanyakazi wa mabenki na sekta nyingine hupumzika kwa siku mbili.
Kwa mwaka 2015 sikukuu hii ilidondokea siku ya Jumatano tarehe 1, April. Hivyo hii ilimaanisha kuwa Jumatano na Alhamisi zingekuwa ni maadhimisho ya sikukuu ya bank holiday, Ijumaa itakuwa ni Ijumaa Kuu, na Jumamosi siku ya mapumziko na Jimapili itakuwa pasaka yenyewe na Jumatatu itakuwa ni Jumatatu ya Pasaka.
Hii ilimaanisha kuwa kulikuwa na siku sita za mapumziko ambazo wafanyakazi watakuwa majumbani. Huu ulikuwa ni mwanya mzuri ambao wazee hawa waliuona ili waweze kuyekeleza tukio lao. Hivyo wakakata shauri kwamba tukio lao watalitekeleza kuanzia siku ya Jumatano Tatehe 1, April 2015.
Siku ya Jumatano asubuhi tarehe 1 april, 2015 mafundi bomba wale wawili (Doyle na Lincoln)ambao walikuwa wafanyakazi katika jengo hili na majengo ya jirani na ambao walikuwa wameshawishiwa na Mzee Brian Reader na kukubali kujiunga na genge hili la wazee hawa kutekeleza tukio, walipewa maelekezo na mzee Brian kufanya jambo la msingi sana.
Walienda kwenye jengo la jirani na jengo lenye vault wakijifanya kama kuna mabomba wameenda kuyarekebisha.
Wakafanikiwa mpaka kuingia sehemu ya chini ya jengo yenye mfumo wa mabomba ya gesi ya matumizi ya nyumbani ambayo mabomba hayo yanaelekea kwenye vymba vya jengo hilo na majengo ya jirani.
Walichokifanya mabwana hawa ni kufanya uharibifu wa makusudi kwa mabomba kadhaa ya gesi na kuzichuna baadhi ya nyaya za umeme na kuondoka.
Kutokana na uharibifu walioufanya ulisababisha gesi ianze kuvuja.
Muda si mrefu ukatokea mlipuko mkubwa wa moto kutokana ma uvujaji huo wa gesi. Hii ilisababisha polisi na zima moto kuwaondoa wakazi wote (evacuation) waliokuwa wanakaa kwenye jengo lililowaka moto ma majengo ya jirani likiwemo jengo lenye vault, wakiwataka watafute sehemu nyingine za kukaa au waende kukaa kwa ndugu au marafiki zao mpaka pale ambapo zima moto watakapofanikiwa kugundua chanzo cha moto huo na kukidhibiti.
Hii ilimaanisha kuwa kwa siku hizo za sikukuu majengo hayo ya karibu pamoja na jengo lenye vault hayatakuwa na wakazi isipokuwa kwenye jengo la jirani na jengo lenye vault kutakuwa na zima moto pekee wakiwa na pilika za kujua chanzo cha moto. Lakini kwenye majengo mengine likiwepo jengo lenye vault yatakuwa tupu kabisa bila wakazi wake.
Kwahiyo jioni ya siku hiyo Mzee Brian na genge la wazee wenzake wakaingia kazini.
Kama nilivyo eleza awali kwamba ‘mchora ramani’ wa tukio hili aliitwa Basil, ingawa jina hili alitungwa tu na polisi kwani hawamjui ni nani na wala hawajui jina lake halisi. Lakini inaonekana alikuwa ni mtu mwenyw ‘access’ na hili jengo.
Hivyo majira ya saa mbili usiku Basil akiwa amevalia nadhifu kabisa alifika mbele ya jengo hili na kufungua mlango wa mbele kwa kutumia funguo na kisha kuingia ndani. Mpaka leo hii haijulikani Basil alipata wapi funguo za jengo.
Wenzake waliosalia walikuwa nyuma ya jengo ambapo baada ya yeye kuingia ndani aliwafungulia mlango wa nyuma na wote wakaingia ndani.
Kama nilivyoeleza awali kwamba lifti katika jengo hiki ilitengenezwa katika mfumo kwamba haiwezi kushuka chini kwenye basement Bali ilikuwa inaishia ‘ground floor’.
Badala ya hili kuwa kikwazo, wazee hawa walichukulia hili kama fursa kwao.
Baada ya wote kuingia ndani wakapandisha ngazi mpaka ghorofa ya pili. Walipofika ghorofa ya pili wakabonyeza kitutufe cha kuiita lifti kuja juu ghorofa ya pili. Lifti ikapanda juu mpaka ghorofa ya pili. Ilipofika wakaharibu nyaya na mtambo wa lifti kifanya ibaki hapo hapo ghorofa ya pili isishuke au kupanda juu au kwa ufupi lifti ikawa imeharibika haifanyi kazi but imeganda ghorofa ya pili.
Baada ya hapo wakashuka tena mpaka ground floor.
Hapa nieleze kidogo.
Mfumo wa lifti (elevator) ulivyo, ni kwamba kwenye kile kijichumba unachoingia baada ya milango ya lifti kufunguka ni kama kiberenge au kijikontena ambacho kina panda juu au chini kutegemea na unakoelekea. Sasa kiberenge/kikontena hiki kinauwezo wa kupanda juu au chini kwasababu kimewekwa kwenye eneo la jengo lililotengenezwa kwa kuacha uwazi/shimo kuanzia chini ya jengo mpaka juu. Kwahiyo ndio kusema kwamba, kama kiberenge kile kikiondolewa na ukifungua mlango wa lifti utakutana na uwazi/shimo refu linaloanzia chini ya f
Ghorofa mpaka juu. Uwazi/shimo hili linaitwa ‘elevator shaft’.
Sasa, nimeeleza hapa kwamba wazee hawa walipanda mpaka ghorofa ya pili na kuita lifti ije juu kisha wakaiharibu igande hapo isishuke wala kupanda kisha wenyewe wakashuka tena ground floor.
Sasa waliposhuka geound floor wakafungua mlango wa lifti na baada ya kuufungua mlango wa kifti wakakutna na shimo (elevator shaft) kuelekea chini kwenye basement kwa vile ‘kiberenge’ cha lifti kiliganda juu ghorofa ta pili.
Na hili ndilo lilikuwa lengo lao.
Kumbuka nimeeleza kuwa lifti ilitengenezwa kwa mfumo ambao ulikuwa haina uwezo wa kushuka chini kwenye basement, kwahiyo walifanya hivi kwa makusudi ili wapate upenyo wa kushuka chini kwenye basement.
Kwahiyo, baada ya kufungua mlango wa lifti na kukuta shimo ambalo lilikuwa na urefu wa kimo kama cha binadamu wawili (futi 12) ndipo hapa Basil ambaye ndiye alikuwa kijna zaidi ilibidi aruke kwa ustadi mpaka chini kwenye basement.
Wakati Basil akiwa tayari amefanikiwa kufikakwenye basement kwa kuruka, wenzake wakapandisha tena ghorofa la kwanza.
Hapa napo panahitaji kupaelewa kwa umakini.
Katika majengo yote ya ghorofa huwa zinawekwa njia/ngazi (stairs) maalumu kwa ajili ya mtu kupita pale inapotokea hali ya taharuki, na hasa taharuki ya moto. Njia/ngazi hizi zinaitwa ‘Emergency fire exit’.
Katika jengo hili ngazi hii ilijengwa katika namna ambayo kama mtu akipita anatokea chini kabisa ya jengo (kwenye basement) lakini anakuwa hayuko ndani ya basement kwani kunakuwa na mlango wa lifti unao mtenganisha yeye na ndani ya basement, na mlango huu wa lifti unaoukuta hapo haufunguki kwa kuwa lifi haifiki huku kama nilivyoekeza. Kwahiyo hapa unakuta mlango wa lifti (ambao haufunguki) na mlango mwingine mbele yako ambao unaweza kuufungua na kutoka nje.
Lakini kitu ambacho wengi walikuwa hawajui na wazee hawa walikigundua baada ya kufanya utafiti kipindi wanapanga mikakati yao ni kwamba, mlango huu wa lifti ulikuwa una funguka kwa ndani. Na hii ilitengenezwa hivi makusudi na wenye jengo ili kusaidia kufanya usafi au marekebisho kwenye shimo la lifti (elevator shaft).
Kwahiyo wazee wale walipopanda mpaka ghorofa ya kwanza wakatumia njia ya dharura (emergency fire exit) na kushuka nayo mpaka chini ya jengo na kufika nje ya basement (mbele la mlango wa lift kwenye basement) na Basil ambaye tayari yupo ndani ya basement akawafungulia mlango wa lifti (nimeeleza mlango huu ilikuwa unafunguka kutokwa ndani). Pia kumbuka hapa hakuna shimo la lifti ka kwenda chini (elevator shaft) kwa kuwa ndio mwisho wa jengo ila kuna shimo/uwazi kwenda juu.
Kwahiyo baada ya Basil kuwafungulia tayari wote wakawa wako ndani ya basement. Kisha wakafungua ule mlango wa kioo nilioueleza mwanzoni, na baada ya kufungua hapa unakuwa uko mbele ya mlango wa Vault yenyewe, ambao ukiufungua tu unakuwa uko ndani ya chumba cha vault.
Lakini kama nilivyoeleza awali kwamba ukifungua tu mlango wa kioo unakuwa na sekunde 60 kuingiza tarakimu za siri ukutani kwenye keypad ili kuifanya alarm isitoe mlio kuashiria uvamizi (intruder alart) na kutuma meseji kwenda polisi.
Kwa kuwa hawakuwa na tarakimu hizo za siri, Basil akaifungua haraka haraka hiyo keypad ukutani na kukata nyaya kadhaa kwa ufundi ili kuifanya alarm hiyo isifanye kazi. Hii ikifanikiwa kwa 50% pekee kwani ni kweli alarm haikulia lakini meseji ilitumwa kwenda polisi.
Polisi wakawasiliana na kampuni ya H.G.S.D ambao wakatuma MTU kwenda kwenye jengo na alipofika kwenye jengo na kukuta mlango wa mbele haujavunjwa, akachungulia ndani milango pia haijavunjwa (kumbuka wazee walitumia mbinu nyingine kuingia sio kuvunja milango) na wala hakuona purukushani yeyote akawapigia simu polisi na kuwaeleza kwa kifupi tu “false alarm” (kwamba ni matatizo tu ya kiufundi ila Vault iko salama.
Hakujua kabisa kwamba wanaume wako ndani wanashughulika.
Baada ya Basil kukata nyaya za alarm, mioyo yao ikatulia wakajua wako salama.
Sasa walikuwa mbele ya vault na kizingiti pekee kichobakia mbele yao kilikuwa ni mlango wa vault. Mlango huu ulikuwa wa Chuma na ni mnene sana ukiwa na sentimita 50 na ulihitaji uingize mfululizo wa tarakimu za siri (combination) ili uweze kuufungua.
Hapa ilikuwa ni dhahiri kabisa kuwa wasingeweza kuufungua mlango huu, hivyo njia pekee ambayo walikuja wakiwa wamejiandaa kifanya ilikuwa ni kutoboa ukuta. Walikuwa wamekuja na mashine kabisa ya kutobolea (drill) ambayo ilikuwa na ncha ya almasi.
Walikuja na Mashine hii maalumu yenye ncha ya almasi kwasababu ukuta wa vault pia ulikuwa na unene mkubwa (sentimita 50) na ulijengwa kwa tofali nzito.
Hivyo kazi ya kuanza kutoboa ikaanza. Iliwachukua takribani masaa matatu kutoboa matundu matatu ya mduara yanayo ingiliana (overlaping circles).
Baada ya kutoboa wakakutana na jambo ambalo hawakulitegemea kabisa. Mbele ya ukuta (ndani ya vault) kulikuwa na mgongo wa kabati la visanduku vya watu kuhifadhia Mali zao. Kabati hili lilitengenezwa kwa kkunganishwa moja kwa moja kwenye ukuta hivyo haijalishi unalisukuma vipi haliwezi kudondoka.
Wazee wakachoka. Hili hawakulitegemea na hawakujiandaa nalo. Wakabishana sana kuhusu wafanye nini lakini mwishowe wakakubaliana waondoke kwenda kufikiri zaidi wanakabiliana vipi na changamoto hiyo. Kumbuka hii ilikuwa ni “weekend ndefu” karibia siku sita za mapumziko, hivyo hawakuwa na wasiwasi kwani wafanyakazi wa vault hawaji mpaka sikukuu zipite.
Hivyo wakaondoka eneo la tukio na kurejea makwao.
Kesho yake wakakutana na kufanya kikao kujadili namna ya kulisukuma lile kabati ndani ya vault ili waweze kuingia.
Baada ya majadiliano marefu wakaafikiana kuwa watumie Mashine ya mtetemo/msukumo yenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kufannikisha hilo.
Wakamuagiza Mzee Jones kwenda kununua Mashine hiyo, na akanunua Mashine murua kabisa yenye uwezo wa kusukuma kitu chanye uzito hadi wa tani kumi (10 ton hydraulic ram).
Usiku wake wakarejea tena kwenye vault, kazi ikaendelea.
Iliwachukua dakika kumi pekee kutumia Mashine waliyokuja nayo kuweza kudondosha kabati iloyokuwa inawazibia njia ya kuingia.
Baada ya kudondosha kabati hiyo. Mzee Carl wood (yule nadhifu) ambaye ndiye alikuwa mwembamba kuliko wote pamoja na mzew Jones ambaye alikuwa na stamina na fiti zaidi ya wore wakajipenyeza kwenye uwazi waliotoboa na kuingia ndani ya vault.
Wakatumia siku nzima iliyofuata (jumamosi) kufungua visanduku vya kuhifadhia mali ndani ya vault.
Ndani ya vault vault kulikuwa na jumka ya visanduku 966 na mpaka kufikia jumapili walifanikiwa kufungua visanduku 396 na ilikuwa inatosha.
Walifanikiwa kuchukua kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu, alamsi na fedha taslimu vyote vikiwa na thamani ya zaidi dola milioni 200 za marekani.
Kwahiyo wakafunga mzigo na kuondoka kwenda kugawana mzigo na kuka pasaka na familia yao jumapili hiyo.
Tukio lilikuwa limefanikiwa kwa asilima 100.
* * * * * * * * * * * * * * * * * * * * * * * * *
Jumanne baada ya wafanya kazi kuja kazini ndipo walipogundua kuwa vault imevunjwa na kuibiwa.
Taarifa ikatumwa polisi na upelelezi ukaanza mara moja. Lakini kwa miezi minne ya upelelezi polisi hawakufanikiwa kung’amua lolote kuhusu kesi hiyo.
Ndipo hapa ambapo kesi ikahamishiwa kitengo maalumu cha weledi wa hali ya juu ndani ya jeshi la polisi nchini uingereza, kitengo kinachojulikana kama Flying Squad.
Baada ya miezi minne ya uchunguzi huku wakitumia picha za CCTV camera za jengo lililopo mkabala na jengo lenye vault iliyoibiwa wakafanikiwa kupata picha y ya gari iliyoonekana kupaki katibu na jesngo la vault usiku wa siku ya tukio na walifuatilia gari hii ilikuwa inamilikiwa na Mzee Collins “kenny” (yule mtoto wa mjini mjanja mjanja) na hii ilipekekea mwezi january mwaka huu 2016, mzee Collins kukamatwa na baada ya mahojiano marefu kwa wiki kadhaa akakiri kuhusika na tukio hilo na kuwataja wenzake.
Baadae wenzake wote walikamatwa na mwezi march mwaka huu wakafikishwa mahakamani na mwezi june wote wakahukumiwa miaka sita jela.
Lakini mastermind mwenyewe wa tukio hili ambaye hajulikani jina lake halisi mpaka leo na polisi wamembatiza jina la Basil, hajulikani alipo mpaka leo hii na vitu vyote vilivyoibwa vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 400 za Tanzania havijapatikana.
Tukio hili linaingia kwenye vitabu vya historia kama tukio la ujambazi lenye thamani kubwa zaidi, lakini historian kubwa zaidi ni kwamba lilitekelezwa na wazee vikongwe.
Kipindi bado wahusika wa tukio hili hawajakamatwa, zilizagaa habari katika mitaa ya London kuwa kutokana na weledi na akili kubwa iliyotumika kutekeleza tukio hili, iliaminika kuwa tukio hili lazima lilitekelezwa na majambazi sugu ambao yawezekana wamewahi kutumikia kwenye vikosi maalumu vya kijeshi kama SAS au Navy SEALs… Ulimwengu ulishikwa na butwaa siku wahusika wamekamatwa na kutangazwa kwamba ni vikongwe vyenye miaka zaidi ya 70 na wengine 60.
Mwisho.
Imeandikwa na Habibu Anga “The Bold”
Also, read other stories from SIMULIZI;